JE UNAMTHAMINI BWANA?

by Admin | 7 February 2020 08:46 pm02

(Je unamthamini Bwana?) Jina la Bwana libarikiwe…Karibu tujifunze maandiko…

Neno la Mungu ni Mwanga wa njia yetu ielekeayo mbinguni na Taa iongozayo miguu yetu katika safari yetu ya mbinguni. (Zab 119:105).

Jambo la muhimu la kufahamu ni kuwa Mungu wetu aliyetuumba kamwe hawezi kumtumia mtu ambaye hayupo tayari..au moyo wake haupo tayari kumpokea yeye. Wakati mwingine mioyo yetu ya kutokuwa watoaji  inatuzuilia sisi kupokea Baraka kutoka kwa Mungu.

Hebu tujifunze mifano michache ya kwenye biblia jinsi Bwana alivyoweza kuwatumia watu katika kulitimiza kusudi lake..ambapo kwa kupitia mifano hiyo..tunaweza kutoka sehemu moja hadi nyingine kiimani..

Marko 14:12 “Hata siku ya kwanza ya mikate isiyochachwa, walipoichinja pasaka, wanafunzi wake wakamwambia, Ni wapi utakapo tuende tukuandalie uile pasaka?

13 Akatuma wawili katika wanafunzi wake, akawaambia, Nendeni zenu mjini; atakutana nanyi mwanamume amechukua mtungi wa maji; mfuateni;

14 na po pote atakapoingia, mwambieni mwenye nyumba, Mwalimu asema, Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu?

15 Naye mwenyewe atawaonyesha orofa kubwa, imeandikwa tayari; humo tuandalieni.

16 Wanafunzi wakatoka, wakaenda mjini, wakaona kama alivyowaambia, wakaiandaa pasaka”.

Katika Tukio hilo..Tunamwona kuna mtu mmoja ambaye ni mcha Mungu biblia haijamtaja jina lake…Lakini Mtu huyu anaonekana alikuwa ni mtu mwenye uwezo kidogo kutokana na habari hiyo…kwasababu utaona anatajwa kuwa na Mtumwa, na pia anayo nyumba yenye ghorofa…Sasa kwa enzi hizo kumiliki nyuma ya ghorofa tena katikati ya Mji kama ule (Yerusalemu) si rahisi kama wewe sio mtu mwenye uwezo ni sawa na leo umilika nyumba ya ghorofa pale Posta Daresalaam…

Lakini pia kama ukichunguza mtu huyo ni lazima alikuwa anamjua Bwana Yesu sana..na pia alikuwa anafuatilia mafundisho yake na alikuwa anampenda sana…Ingawa pengine hakupata nafasi ya kukutana naye..Lakini pamoja na hayo ndoto yake kubwa ilikuwa ni siku moja akutane naye, amkaribishe kwake…

Sasa pengine alifunga na kuomba kwamba angalia msimu huu wa sikukuu amtembelee kwake…na hivyo akapanga pengine namna ya kumtafuta akakosa…moyoni mwake akiwa na mawazo hayo..wazo likamwingia aandae chumba kabisa kilicho kizuri tena ghorofani ili atakapompata Yesu wakati huo huo aingie kwenye chumba hicho isiwe baada ya kumpata ndipo aanze maandalizi.

Siku chache kabla ya sikukuu…moyo wake pengine ukiwa na shauku ya kumkaribisha Bwana…..Yesu akauona moyo huo maili kadhaa mbali na alipokuwa…kama vile alivyomwona Nathanieli siku ile alipokuwa chini ya mtini alipokwenda kuitwa na Filipo.

Yohana 1: 48 “Nathanaeli akamwambia, Umepataje kunitambua? Yesu akajibu, akamwambia, Kabla Filipo hajakuita, ulipokuwapo chini ya mtini nilikuona”.

Na ndivyo hivyo hivyo Bwana alivyouona moyo wa huyu mtu akiwa nyumbani kwake..tayari amemwandalia yeye chumba…Na kwasababu Roho ya kinabii ilikuwa juu ya Yesu akawaambia wanafunzi wake waende mjini watamkuta mtu kabeba mtungi wamfuate mpaka atakapoingia wamwulize mwenye nyumba

“Ki wapi chumba changu cha wageni, niile pasaka humo, pamoja na wanafunzi wangu”

Hebu tafakari hiyo sentensi… “Ki wapi chumba changu”..na si “ki wapi chumba chako”…Kitendo cha Yule mtu kukiweka tayari kile chumba kwaajili ya Bwana..tayari Bwana ameshakiheshimu na kukiita chumba chake na si cha Yule mtu tena…Hebu tafakari huyo mtu alifurahi kiasi gani kusikia vile??..Chumba kile alichomwandalia Bwana, Bwana amekijia…Ni furaha ya ajabu sana.

Ndugu yangu..Bwana hawezi kuja mahali ambapo hatujamwandalia…na Bwana akija mahali tulipomwandalia anakuja na Baraka. Sio kwamba Bwana alikuwa hana mahali pa kwenda…alikuwa na sehemu nyingi za kwenda lakini aliutazama mji mzima ni nani aliyekuwa na moyo wa kumpenda kwa dhati kuliko wote aende kwake…

Ndio maana sehemu nyingine Bwana Yesu alisema maneno haya…

Luka 4:25 “Lakini, kwa hakika nawaambia, Palikuwa na wajane wengi katika nchi ya Israeli zamani za Eliya, wakati mbingu zilipofungwa miaka mitatu na miezi sita, njaa kuu ikaingia nchi nzima;

26 wala Eliya hakutumwa kwa mmojawapo, ila kwa mjane mmoja wa Sarepta katika nchi ya Sidoni”.

Wajane walikuwepo wengi lakini Eliya hakutumwa isipokuwa kwa mwanamke wa Taifa la mbali..akakaa kwake na nyumba yake ikabarikiwa..mkate haukuwaishia.. Kadhalika kulikuwepo na matajiri wengi pale Yerusalemu lakini Bwana hakwenda hata kwa mmojawao isipokuwa kwa mtu huyu ambaye moyoni mwake alimpenda Bwana kiasi kwamba alikuwa tayari kumwandalia chumba kabla hata ya kumwona wala kumkaribisha.

Bwana anaitazama mioyo yetu ndugu?..Je tunamjali kiasi gani? Tafakari mfano mwingine tena huu wa mwisho..

Marko 11:1 “Hata walipokaribia Yerusalemu karibu na Bethfage na Bethania, kukabili mlima wa Mizeituni, aliwatuma wawili katika wanafunzi wake,

2 akawaambia, Nendeni mpaka kile kijiji kinachowakabili; na katika kuingia ndani yake, mara mtaona mwana-punda amefungwa, asiyepandwa na mtu bado; mfungueni, kamleteni.

3 Na mtu akiwaambia, Mbona mnafanya hivi? Semeni, Bwana anamhitaji na mara atamrudisha tena hapa.

4 Wakaenda zao, wakamwona mwana-punda amefungwa penye mlango, nje katika njia kuu, wakamfungua.

5 Baadhi ya watu waliosimama huko wakawaambia, Mnafanya nini kumfungua mwana-punda?

6 Wakawaambia kama Yesu alivyowaagiza, nao wakawaruhusu.

7 Wakamletea Yesu yule mwana-punda, wakatandika mavazi yao juu yake; akaketi juu yake”.

Katika habari hii, jambo ni lile lile…Hawa watu walikuwa na punda wao amefungwa pale..lakini pengine walishawahi kusikia habari za Yesu na kumwamini..na kutamani wangempatia angalau kitu Fulani…Na Bwana alipoiona mioyo yao…pale pale kwa kuwa yeye ni Nabii akawatuma wanafunzi wake kuwaomba punda yule amtumie kuingia naye Yerusalemu..Na wale wenye punda walipowauliza kwanini mnamfungua? Waliposikia kwamba ni Bwana anamhitaji…wala hawajauliza mara mbili mbili wala kuhoji..Ni wazi kuwa walifurahi mno na kujiona wenye bahati..

Ni wazi kuwa walikuwepo wengi wenye punda pale mjini lakini Bwana Yesu hakwenda kuchukua hata wa mmoja wao…Ni kwanini? Ni kwasababu hakuna chochote ndani yao cha kuuvuta Moyo wa Bwana Yesu uwaelekee wao…Pengine Bwana angeenda kwa mmoja wao na kuomba punda Yule wangeanza kusema…oo kwanza wewe unawapinga wazee wetu wa dini…oo kwanza wewe unajiita Mwana wa Mungu..oo wewe umetoka wapi, huna shughuli maalumu unazunguka tu…wengine wangeanza kumwita hata mwizi…wengine wangeanza kusema huna kazi ya kufanya unataka kuharibu mali za watu…

Vivyo hivyo walikuwepo wenye magari sio punda tu…kwasababu kipindi hicho yalikuwepo magari ya farasi watu wenye uwezo walikuwa wanayatembelea….Lakini hakukuwa na hata mmoja mwenye moyo wa dhati wa kutamani siku moja Bwana angelipanda gari lake…Lakini Bwana anauona moyo wa mtu mmoja anayetamani siku moja Bwana angepanda punda wake…Na Bwana anakwenda kwa Yule mwenye moyo uliomwelekea.

Ndugu yangu..habari hizi ni mifano inayotufundisha dhahiri..Jicho la Bwana linatazama kote kote ulimwenguni kila siku anatazama ni yupi, ni nani, na yuko wapi aliye tayari angalau kutoa chochote kwaajili yake?..Kumbuka yeye hana shida..lakini anaipenda mioyo ya utoaji…anaangalia ni mtaa gani kijiji gani kuna mtu ambaye anatamani angalau kitu chake kile, kingetumiwa na yeye…Anaangalia huku na huko..Anatamani sana kututembelea lakini hawezi kumtembelea mtu ambaye hataki kutembelewa na yeye..

Tafakari tena maneno haya ya kumalizia aliyoyasema juu ya siku ile ya mwisho itakavyokuwa..

Mathayo 25:31 “Hapo atakapokuja Mwana wa Adamu katika utukufu wake, na malaika watakatifu wote pamoja naye, ndipo atakapoketi katika kiti cha utukufu wake;

32 na mataifa yote watakusanyika mbele zake; naye atawabagua kama vile mchungaji abaguavyo kondoo na mbuzi;

33 atawaweka kondoo mkono wake wa kuume, na mbuzi mkono wake wa kushoto.

34 Kisha Mfalme atawaambia wale walioko mkono wake wa kuume, Njoni, mliobarikiwa na Baba yangu, urithini ufalme mliowekewa tayari tangu kuumbwa ulimwengu;

35 kwa maana nalikuwa na njaa, mkanipa chakula; nalikuwa na kiu, mkaninywesha; nalikuwa mgeni, mkanikaribisha;

36 nalikuwa uchi, mkanivika nalikuwa mgonjwa, mkaja kunitazama; nalikuwa kifungoni, mkanijia.

37 Ndipo wenye haki watakapomjibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona una njaa, tukakulisha, au una kiu tukakunywesha?

38 Tena ni lini tulipokuona u mgeni, tukakukaribisha, au u uchi, tukakuvika?

39 Ni lini tena tulipokuona u mgonjwa, au kifungoni, tukakujia?

40 Na Mfalme atajibu, akiwaambia, Amin, nawaambia, kadiri mlivyomtendea mmojawapo wa hao ndugu zangu walio wadogo, mlinitendea mimi.

41 Kisha atawaambia na wale walioko mkono wake wa kushoto, Ondokeni kwangu, mliolaaniwa, mwende katika moto wa milele, aliowekewa tayari Ibilisi na malaika zake;

42 kwa maana nalikuwa na njaa, msinipe chakula; nalikuwa na kiu, msininyweshe;

43 nalikuwa mgeni, msinikaribishe; nalikuwa uchi, msinivike; nalikuwa mgonjwa, na kifungoni, msije kunitazama.

44 Ndipo hao pia watajibu, wakisema, Bwana, ni lini tulipokuona wewe una njaa, au una kiu, au u mgeni, au u uchi, au u mgonjwa, au u kifungoni, tusikuhudumie?”

45 Naye atawajibu, akisema, Amin, nawaambia, Kadiri msivyomtendea mmojawapo wa hao walio wadogo, hamkunitendea mimi.

46 Na hao watakwenda zao kuingia katika adhabu ya milele; bali wenye haki watakwenda katika uzima wa milele.

Usipokubali kujitoa kwa Bwana kamwe usitegemee Baraka wala kupokea kutoka kwake…Naamini maarifa haya yatakusaidia kuchukua hatua ya kumthamini Bwana. (Je unamthamini Bwana?)

Ubarikiwe sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe au piga namba hii +255 789001312


Mada Nyinginezo:

SAKRAMENTI NI NINI, NA JE! IPO KATIKA MAANDIKO?

INGIENI KWA KUPITIA MLANGO ULIO MWEMBAMBA.

USIZITEGEMEE NGUVU ZAKO KUKUSAIDIA!

Ni sahihi kumuita Mariamu mama wa Mungu?

TOFAUTI KATI YA HEKALU, SINAGOGI NA KANISA NI IPI?

USIMPE NGUVU SHETANI.

Je! Ni kweli ubatizo wa maji hatuuhitaji tena?

UKITAKA KUMFUATA YESU NI SHARTI UACHE VYOTE!

Rudi Nyumbani:

DOWNLOAD PDF
WhatsApp

Source URL: https://wingulamashahidi.org/2020/02/07/je-unamthamini-bwana/