UKITAKA KUMFUATA YESU NI SHARTI UACHE VYOTE!

UKITAKA KUMFUATA YESU NI SHARTI UACHE VYOTE!

Luka 14: 25 “Makutano mengi walipokuwa wakifuatana naye, aligeuka, akawaambia,

26 Kama mtu akija kwangu naye hamchukii baba yake, na mama yake, na mke wake, na wanawe, na ndugu zake waume na wake; naam, na hata nafsi yake mwenyewe, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

27 Mtu ye yote asiyeuchukua msalaba wake na kuja nyuma yangu, hawezi kuwa mwanafunzi wangu.

28 Maana ni nani katika ninyi, kama akitaka kujenga mnara, asiyeketi kwanza na kuhesabu gharama, kwamba anavyo vya kuumalizia?

29 Asije akashindwa kuumaliza baada ya kuupiga msingi, watu wote waonao wakaanza kumdhihaki,

30 wakisema, Mtu huyu alianza kujenga, akawa hana nguvu za kumaliza.

31 Au kuna mfalme gani, akitaka kwenda kupigana na mfalme mwingine, asiyeketi kwanza na kufanya shauri, kwamba yeye pamoja na watu elfu kumi ataweza kukutana na yule anayekuja juu yake na watu elfu ishirini?

32 Na kama akiona hawezi, hutuma ujumbe kutaka sharti za amani, mtu yule akali mbali.

33 Basi, KADHALIKA KILA MMOJA WENU ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”

Bwana Yesu alisema katika mstari wa 26 kuwa asiyemchukia Baba yake na Mama yake, mke wake, mwanawe, na ndugu zake wakiume na wake hawezi kuwa mwanafunzi wake..

Chuki inayozungumziwa hapo sio chuki ile ya dhambi, kwamba umchukie Baba yako au mama yako kwa nia ya kumdhuru, au kumdharau, au kumshushia heshima hapana! Bali chuki inayozungumziwa hapo ni “kuyachukia mapenzi yake ambayo ni kinyume na mapenzi ya Mungu”…Baba anakuambia mwanangu tunapaswa tuende kwa waganga na wewe hali unajua kuwa hayo ni machukizo kwa Mungu, hapo unapaswa uyachukie hayo mapenzi ya Baba yako na kumwambia wazi kwa ujasiri kuwa “Baba mimi siwezi kwenda huko, kwasababu ni Mkristo, namwabudu Mungu aliye mbinguni”..

Mama yako anakwambia ukajiuze tupate pesa, wewe unatakiwa umwambie wazi kuwa “mimi siwezi kufanya hivyo kwasababu ni Mkristo”..Mume wako anakuambia ufanye mambo machafu ambayo ni machukizo kwa Mungu, na anakulazimisha, kutenda dhambi.. hapo unapaswa kumweleza wazi msimamo wako kwamba wewe ni Mkristo, na kama hataki kuishi na wewe, basi anayoruhusa ya kuondoka!…Biblia imeruhusu matengano Katika mazingira kama hayo (soma 1Wakorintho 7:15).

Kuna mtu mmoja alikuwa anazungumza na mimi anasema alikuwa ameokoka tu vizuri yeye na mchumba wake, tena walikuwa wamesimama ipasavyo katika imani, lakini siku ya kwenda kutambulishwa kwao, mama yake Yule mwanamume akamwambia kama hutaacha huo wokovu wako, mimi sio mama yako, na nitakuachia laana..Sasa Yule mwanamume kwa kuwa alikuwa anampenda mama yake zaidi ya Kristo, akaamua kuacha wokovu anakamshawishi na mke wake wote wakaucha wokovu, wakaanza kuwa watu wa ajabu, Yule mwanamume akawa mzinzi na mtu wa kidunia kishinda hata walipokuwa hapo mwanzo..Sasa watu wa namna hiyo Kristo anasema hawafai kwake, na aliposema hawafai alimaanisha kusema kweli hawafai..

Na jambo lingine Bwana alilolisema ni kwamba 33…KADHALIKA KILA MMOJA WENU ASIYEACHA VYOTE ALIVYO NAVYO, hawezi kuwa mwanafunzi wangu”

Pia mtu asiyeacha vyote alivyonavyo…Maana ya kuacha vyote ulivyo navyo ni kuvitoa vile vitu ndani ya moyo wako…kila mtu anafahamu namna ya kukitoa kitu moyoni, hakuna haja ya kuelezea… “unapotoa kitu moyoni, unakuwa unakifuta ndani yako, kinakuwa sio kitu tena kinachokupa raha, kiwepo kisiwepo ni sawa tu” Wakati mwingine hiyo hali inaweza kuambatana na kuviacha vitu kwa nje kabisa wazi wazi…

Ulikuwa ni Tajiri unauacha utajiri wako unamfuata Yesu, maana yake…Hata mali zote zikipukutika katika safari yako ya kumfuata YESU hilo hujali, kwasababu hazipo tena moyoni mwako, Unamhisi Yesu moyoni kuliko utajiri ulionao…Na pia unakuwa humfuati Yesu ili akupe mali au azilinde mali zako, unamfuata kwasababu Moyoni mwako unaona una haja naye…Kuna upendo fulani ambao unamiminika ndani yako ambao hauwezi kuuelezea, Unajikuta tu unampenda tu Yesu bila sababu kama yeye anavyokupenda wewe bila sababu yoyote.

Kadhalika Ulikuwa ni MASKINI, unauacha Umaskini wako unamfuata YESU. Unauondoa umaskini moyoni mwako….Usimfuate Yesu kwasababu hauna gari! Au kwasababu umaskini unakutesa na kukuumiza… Hapo hujajikana nafsi ndugu! Usimfuate Yesu kwasababu unataka utajiri, au unataka heshima katika jamii, au kwasababu unataka kuwakomesha maadui..Unatakiwa Uuache umaskini wako ndipo unamfuata Yesu kiasi kwamba hata katika safari yako ya Imani, ukiongezekewa na kuwa Tajiri wa mambo ya kimwili, hilo kwako halina maana sana!…mali zikiongezeka ni kama vile moyoni mwako hakuna kilichoongezeka…lakini uhusiano wako na Yesu unapoimarika ndipo unajihisi uchangamfu wa Ajabu unakuvaa….Inafikia mahali umasikini na Utajiri kwako ni sawasawa tu! Kama Ayubu, ilifika wakati hata mali zilipoongezeka hakufurahia (Soma Ayubu 31:25)..

Wapo watu ni maskini lakini hata katika huo umaskini wao, hawajawahi kumwomba Mungu katika sala zao utajiri, wameridhika na wana amani ya Ajabu mioyoni mwao..wawe nacho wasiwe nacho, hilo kwao halijalishi maadamu wanaye Yesu, hilo kwao ndio linalojalisha, huo ndio utajiri mkubwa kwao. Hivyo ni lazima kabla ya kumfuata Yesu kuuacha umaskini! Na kumfuata yeye wewe kama wewe.

Na pia baada ya kuacha vyote namna hiyo, kitakachofuatia ni kuchukiwa, kutengwa, kuonekana umerukwa na Akili, kuonekana mjinga katika jamii na kuonekana hufai…Na hivyo pia unapaswa uwe navyo tayari! Bwana Yesu hakutuficha kabisa alituambia ili tukikutana nayo tusiseme mbona hivi mbona vile..Upige gharama kabisa kabla ya kuanza kujenga Mnara! Usije ukafika katikati ukashindwa kumalizia…

Ndivyo ilivyo kwa Bwana Yesu kabla ya kumfuata, piga hesabu kuwa kuna kuchekwa huko mbele, kuna kudharaulika, kuna kupungukiwa wakati mwingine hata kwa kipindi kirefu sana, wakati mwingine hata miaka kadhaa, hata miaka 5, au 10, hata 15, lakini haitadumu hivyo hata milele, kuna kutengwa na kuonekana mjinga, hata kwa miaka kadhaa…piga gharama zote hizo..Kama haupo tayari! Kuonekana mshamba kwa muda mrefu hivyo, au kuonekana mjinga kwa miaka kadhaa, au kudharaulika kwa miaka kadhaa, au kama haupo tayari kukosana na mama yako kuhusiana na Imani yako, au kukosana na Baba yako, au Watoto wako, au mke wako..kama unajua yatakushinda huko mbeleni…Biblia inasema tafuta sharti ya Amani mapema!…Usijiingize mahali ambapo hujajua yatakayokupata mbeleni, ukaja ukakutana na ambayo hukutegemea ukaanza kujuta na kulalamika.

Kwasababu Bwana Yesu anasema:

Luka 12: 51 “Je! Mwadhani ya kwamba nimekuja kuleta amani duniani? Nawaambia, La, sivyo, bali mafarakano.

52 Kwa kuwa tokea sasa katika nyumba moja watakuwamo watu watano wamefarakana, watatu kwa wawili, wawili kwa watatu.

53 Watafarakana baba na mwanawe, na mwana na babaye; mama na binti yake, na binti na mamaye; mkwe mtu na mkwewe, mkwe na mkwe mtu”.

Je! Umejikana nafsi?..Umejitwika msalaba wako na kumfuata Yesu? Fahamu kubwa mtu yeyote anayeingia gharama kubwa kama hizo, Sio bure bure tu, Huyo anapelekwa katika viwango vya juu zaidi vya kuwa karibu na Kristo zaidi ya watu wengine wote, anafanyika kuwa mwanafunzi wake, na zaidi ya yote Bwana atakuja kumpa mara mia, na siku ile ataketi pamoja naye katika kiti chake cha enzi akiwahukumu mataifa..(Mathayo 19:27-30)

Bwana akubariki.

Pia kwa Maombezi, Ushauri, Maswali au Ratiba za Ibada Wasiliana nasi kwa namba

+225693036618/ +225789001312

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP



Mada Nyinginezo:

NJIA YA MSALABA.

NI KWANINI MUNGU HAONEKANI?

BWANA ALIMAANISHA NINI KUSEMA JIKANE MWENYEWE?(MATHAYO 6:24)

KWANINI YESU KRISTO NI MWANA WA DAUDI?

JE? NI HATUA ZIPI MUHIMU ZA KUFUATA BAADA YA KUBATIZWA?

MTI WA MLOZI ALIOONYESHWA NABII YEREMIA 1:12 TAFSIRI YAKE NI NINI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments