HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

HUYU MELKIZEDEKI NI NANI?

Melkizedeki ni nani?


Neno la Mungu linatuambia katika 1Timotheo 3:16 kuwa “bila shaka siri ya utauwa ni kuu.” Au kwa lugha rahisi Neno hili tunaweza kusema “bila shaka siri ya Uungu ni kuu; Hii ikiwa na maana kuwa kuufahamu uungu wa Mungu, si kitu chepesi tu cha kufikirika kibinadamu, bali kipo katika Siri na Siri hiyo ni kubwa sana..Hivyo hiyo inatuhimiza sisi tumwombe Mungu atufunulie ili tuzidi kumjua yeye siku baada ya siku.

Kumbuka Hapa katika hii siri ndipo palipoleta mgawanyiko na mkanganyiko mkubwa kati ya Ukristo na Imani nyingine kama vile uislamu, Na hapa hapa ndipo palipoleta migawanyiko mingine mikubwa katikati ya wakristo wenyewe.

Lakini sisi hatutaingia huko leo, bali kwa ufupi tutamtazama huyu Melkizedeki ni nani, kwa kurejea baadhi ya vifungu vya maandiko. Sasa kumbuka biblia inaweka wazi kabisa, kwamba Kristo alikuwepo kabla hata kabla ya kitu chochote kuwepo duniani.

Yohana 8:57 “Basi Wayahudi wakamwambia, Wewe hujapata bado miaka hamsini, nawe umemwona Ibrahimu?

58 Yesu akawaambia, Amin, amin, nawaambia, Yeye Ibrahimu asijakuwako, mimi niko”.

Unaona Lakini swali tunajiuliza alikuwepoje? Hili ni swali ambalo hata wakristo wengi leo hii tunashindwa kulijibu ipasavyo. Tutasema Yohana 1:1 Inathibitisha hilo kuwa hapo mwanzo kulikuwepo na Neno naye Neno alikuwako kwa Mungu naye Neno alikuwa, ambaye ndio YESU. Hivyo Yesu alikuwepo tangu mwanzo mbinguni na baba yake mpaka ilipofika wakati wa yeye akashuka duniani kuja kutuokoa.

Lakini hatujui kuwa huyu YESU ambaye anaonekana kwa maumbile yale, hakuwepo tangu mwanzo. Safari yake ilianzia AD 1, tutaliona hilo tunavyozidi kusonga mbele.

Kama biblia inavyosema hapo mwanzo kulikuwako “Neno”, Hivyo kwa asili yake NENO sio mtu, Hili ni Neno la kigiriki Logos, likiwa na maana ya WAZO LA MUNGU, /KANUNI au NIA ya Mungu.

Sasa hili Neno kazi yake kubwa ilikuwa ni nini?

Tukisoma:

1Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya NENO LA UZIMA;

2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);

3 hilo tuliloliona na kulisikia, twawahubiri na ninyi; ili nanyi pia mpate kushirikiana nasi: na ushirika wetu ni pamoja na Baba, na pamoja na Mwana wake Yesu Kristo”.

Unaona hapo Hili Neno kumbe limebeba UZIMA ndani yake (Yohana 1:4), ambao uzima huo Mungu alitaka kuudhihirisha kwetu tangu zamani. Hapa mitume wanasema walikuwa wanalisikia tangu zamani, hivyo halikuwa jambo jipya katika masikio yao lakini baadaye sasa wakati ulipofika wakaja kupata neema ya kuliona kwa macho yao wenyewe na kulipapasa siku lilipokuja kufanyika mwili ndani ya YESU KRISTO.

Sasa tumeshaona uzima wowote ni Neno la Mungu (Wazo la Mungu) kwa mwanadamu, Kazi yake kubwa ni kurejesha kilichopotea na kukikomboa. Hivyo katika maandiko Neno hili la uzima halikuanzia kwenye Ule mwili wa YESU KRISTO pekee, hapana bali lilianzia tangu mbali sana, isipokuwa lilifichwa tu machoni pa watu wasilitambue kwasababu SIRI ya utauwa ilikuwa bado haijafichuliwa. Hivyo hili NENO Lilichukua maumbile mengi mengi tofauti kwa lengo tu la kutimiza kusudi lile lile kuleta uzima ndani ya watu.

➔Tunaona lilikuwepo kuanzia Edeni, mwanzoni kabisa mwa safari ya mwanadamu kama Ule mti wa Uzima katika bustani, Lile lilikuwa ni NENO LA MUNGU..lilikuwepo pale kuwapa uzima Adamu na hawa, kuwazuia na mauti, lakini walipoasi wakafukuzwa mbali nalo.

➜Baadaye likaja likachukua umbile lingine tena la MERIKEBU(SAFINA), Lilisimama pale ili kuwakomboa wanadamu na uzao wao usipotee kabisa katika uso wa dunia, akaokoka Nuhu na watu wengine 7.

➜Baadaye likaja kuchukua umbo la mnyama MWANAKONDOO, siku ile Ibrahimu alipokwenda kumtoa mwanawe wa pekee kuwa sadaka ya kuteketezwa likasimama kama dhabihu badala ya Isaka kama Yule kondoo aliyekuwa mlimani kichakani, vyote hivyo vilifanyika kwa mafumbo makubwa sana, kufunua UZIMA hasa udumuo utakaokuja huko mbeleni..

➜Ndio baadaye tunakuja kuona linachukua tena maumbile ya wanadamu likaonekana duniani kwa wakati mchache kutimiza kusudi Fulani ndio sasa hapo tunamwona mtu anayeitwa MELKIZEDEKI. Kama kuhani kumpatanisha Ibrahimu na Mungu kwa kitambo tu. Lakini ukuhani halisi ulikuwa bado haujafunuliwa.

Waebrania 7:1”Kwa maana Melkizedeki huyo, mfalme wa Salemu, kuhani wa Mungu aliye juu, aliyekutana na Ibrahimu alipokuwa akirudi katika kuwapiga hao wafalme, akambariki;

2 ambaye Ibrahimu alimgawia sehemu ya kumi ya vitu vyote; (tafsiri ya jina lake kwanza ni mfalme wa haki, tena, mfalme wa Salemu, maana yake, mfalme wa amani;

3 hana baba, hana mama, hana wazazi, hana mwanzo wa siku zake, wala mwisho wa uhai wake, bali amefananishwana Mwana wa Mungu); huyo adumu kuhani milele……………….

Waebrania 7:15 “Tena hayo tusemayo ni dhahiri sana zaidi, ikiwa ametokea kuhani mwingine mithili ya Melkizedeki;[anazungumziwa YESU KRISTO]

16 asiyekuwa kuhani kwa sheria ya amri iliyo ya jinsi ya mwili, bali kwa nguvu za uzima usio na ukomo;

17 maana ameshuhudiwa kwamba, Wewe u kuhani milele Kwa mfano wa Melkizedeki”.

Mahali pengine tena Neno lilipochukua umbile la kibinadamu, ni pale Shedraka, Meshaki na Abednego walivyotupwa kwenye tanuru la moto Likatokea kwa mfano wa mwana wa Mungu, likawa linazungumza nao kisha likaondoka..Kwasababu lilikuwa bado halijashuka rasmi duniani. Lakini utaona lengo lake ni lile lile kuleta uzima na kuokoa.

Sehemu nyingine lilitokea kama MWAMBA. Kule jangwani wana wa Israeli walipokuwa wanakaribia kufa na kiu lilisimama mbele yao ili kuwaokoa, Na Musa hakulifahamu hilo mpaka alipofanya uzembe ule wa kuupiga ule mwamba mara mbili ndipo alipojua kuwa kumbe alikuwa amesimama mbele ya uzima wenyewe, mbele ya mkombozi mwenyewe.

(1Wakorintho 10:4 “wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; kwa maana waliunywea mwamba wa roho uliowafuata; na mwamba ule ulikuwa ni Kristo”.)

➜Baadaye likaja kujidhihirisha katika maumbile mengi tofauti tofauti mfano kama Hekalu, Sehemu nyingine kama malaika, sehemu nyingine kama nguzo ya moto. Sehemu nyingine kama NYOKA WA SHABA.

(Yohana 3:14 “Na kama vile Musa alivyomwinua yule nyoka jangwani, vivyohivyo Mwana wa Adamu hana budi kuinuliwa;
15 ili kila mtu aaminiye awe na uzima wa milele katika yeye”.)

➜Sehemu nyingine likajidhihirisha kama HEKIMA Ambayo aliwavaa waamuzi na wafalme wa Israeli akianziwa na Sulemani na wengineo waliomfuata, ili tu kutimiza lengo la kuwaokoa na kuwatunza watu wake kupita wafalme wale Mungu aliowachagua hekima yake ikae ndani yao.

Ukisoma Mithali sura ya 8 na ya 9 utaona kabisa jinsi Sulemani anavyoilezea hekima kama kitu chenye uhai na kinazungumza, Pia soma (1Wakorintho 1:24) utaona inamtaja KRISTO kama yeye ndio hiyo Hekima ya Mungu yenyewe.

Sehemu hizo hatuna muda wa kuzielezea moja moja, Lakini nataka uone picha Fulani hapo, NENO LA MUNGU jinsi lilivyopana, Na jinsi lilivyokuwepo tangu mwanzo. Hivyo baadaye sasa wakati ulipofika, Mungu kuufunua utimilifu wote, Mungu kuweka wazi WAZO lake lote kwa mwanadamu, Mungu kuufunua uzima wote na Ukombozi wote, akaona ni vyema sasa aunde mwili maalumu, mahususi, uzaliwe na mwanamke bikira, uitwe jina la YESU (Maana yake YEHOVA-MWOKOZI) ili sasa liweze kukaa na wanadamu milele, lizungumze nao, liwajibu maswali yao, liwafundishe, walipapase, walitegemee hilo, liwaongoze katika njia ya kweli na ya haki na ya uzima hata milele. Hapo ndipo tunaona Lile Neno ndani ya mwili unaoitwa Yesu…ambaye kwa ujumla sasa ndio tunamwita BWANA YESU KRISTO HALELUYA! HALELUYA!. 

Yohana 1:14 “Naye Neno alifanyika mwili, akakaa kwetu; nasi tukauona utukufu wake, utukufu kama wa Mwana pekee atokaye kwa Baba; amejaa neema na kweli”.

Ndio maana mtume Yohana alikuwa anaoujasiri kabisa kusema maneno haya…

1Yohana 1:1 “Lile lililokuwako tangu mwanzo, tulilolisikia, tuliloliona kwa macho yetu, tulilolitazama, na mikono yetu ikalipapasa, kwa habari ya Neno la uzima;
2 (na uzima huo ulidhihirika, nasi tumeona, tena twashuhudia, na kuwahubiri ninyi ule uzima wa milele, uliokuwa kwa Baba, ukadhihirika kwetu);”

Sasa tukirudi kwenye zile kauli za Yesu anaposema kabla Ibrahimu hajawapo mimi nipo, hapo tunaona alikuwa hauongelei ule mwili uliozaliwa na bikira, bali alikuwa anaongelea lile Neno la Mungu ndani yake. Ukilijua hilo hutasema kuwa Mungu anazo nafsi tatu. Wewe na MAWAZO yako au NIA yako hamwezi kuwa vitu viwili tofauti vinavyojitegemea, ni kitu kimoja.Lile Neno ndio Mungu mwenyewe, Yesu Kristo ni Mungu ndani ya Mwili.

Hivyo ndugu tukirudi kwenye kichwa cha Somo je! Huyu Melkizedeki ni nani?. Jibu ni kuwa Huyu Melkizedeki ni Neno la Mungu lililojidhihirisha katika mwili kutimiza kusudi fulani kabla ya wakati wake mtimilifu. Lakini baadaye ndilo liliokuja rasmi kuitwa YESU KRISTO.Hata sasa tunaposema mkaribishe YESU Kristo ndani ya maisha yako, tunamaanisha likaribishe Neno la UZIMA la Mungu ndani ya maisha yako, Kwasababu Neno hilo sasa limefunuliwa ndani ya Kristo Yesu Bwana katika utimilifu wote. Kwahiyo unavyolisikia hili Neno na kulipokea, ni sawa umempokea Yesu Kristo mwenyewe ndani ya maisha yako…

Je! Leo hii bado Upo katika dhambi?, Na hali Tumesharahisishiwa wokovu namna hii bado unauona ni mgumu kuupokea?. Watu wa Agano la Kale japo walilifahamu hili Neno la Mungu kwa sehemu tu kwa kupapasapasa lakini walitii kwa utimilifu wote wakapata wokovu sisi je! Tutapataje kupona tusipouthamini wokovu mkuu namna hii?(Waebrania 2:3). YESU KRISTO ndio  wazo la Mungu, ndio NIA ya Mungu, ndio MUNGU MWENYEWE katika Mwili. Tumfuate yeye tupate kuwa salama, katika safari yetu hii fupi hapa duniani.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP



Mada Zinazoendana:

NEHUSHTANI (NYOKA WA SHABA).

KWANINI YESU KRISTO ALIKUJA DUNIANI?

MJUE SANA YESU KRISTO.

SIRI YA MUNGU.


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

14 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Bahati miremba
Bahati miremba
1 year ago

Namshukuru mungu sana kuangukia iyi ujuwe sababu nilikuwa sijaelewa ili neno vizuru asante sana namungu akubariki sana na akujaze mengi

James fliberth
James fliberth
1 year ago

Ubarikiwe sana mtumishi kwa kujitoleo kufundisha neno la Mungu nasema tena ubarikiwe sana

Anonymous
Anonymous
1 year ago

Mtumishi umenifungulia pakubwa sana Mungu akubariki

CHURCH MAN
CHURCH MAN
2 years ago

Hakika Mungu ana watu wake kajiwekea akiba kama wewe. Wakati dunia imepoteza kabisa kweli ya neno la Mungu kama hii anaibuka mtu kama wewe sasa. Anazifungua akili za watu waelewe kile kitu wanakisikia na hawaelewi.
Barikiwa sana .{utukufu ni kwa Bwana}

Lodrick
Lodrick
3 years ago

Nataman sana kumjua Mungu

Lodrick
Lodrick
3 years ago

Hili neno Lina maana gani” Kwa Bwana siku Mona ni Kama miaka elfu na Miaka elfu ni Kama siku moja”

Lodrick masawe
Lodrick masawe
3 years ago

Bwana Yesu asifiwe! Nna abudu kkt lakn naona nna uhaba wa kuckia neno la Mungu,yaana Kuna wakat nataman kusikia nikihubiriwa au nisikie mahubir nijisikie vizuri,yaan ni Kama mtu mwenye kiu,asa najaribu tafta mahali pa kuabudu tatizo nitajuaje Kama ni sahihi na Kristo anaubiriwa kwa usahihi??

Eliki
Eliki
2 years ago
Reply to  Lodrick masawe

Jaribuu kuwatafuta waadventista wasabato popote ulipo watakusaidia

Hosea marko
Hosea marko
4 years ago

Amen ,,,neno zuri sana,,,,nisaidie namba yako mtumishi

Emmanuel Kifaro
Emmanuel Kifaro
4 years ago

Mtumishi wa Mungu, Salamu katika Jina la Yesu Kristo

Nimesoma ujumbe huu, kwa kweli umenifundisha kitu cha thamani sana katika maisha yangu na utumishi Mungu alioweka ndani yangu. Ninakuombea neema ya Mungu izidi kukufunika na kukuongoza, zaidi sana aendelee kuachilia mafunuo ya Neno lake kupitia kwako ili kuzidi kuujenga mwili wa Kristo.

Barikiwa!