WAKRISTO WA UONGO.

WAKRISTO WA UONGO.

Je unajua nguvu ya manabii, wachungaji, mitume, waalimu na wainjilisti wa uongo inatoka wapi?

Si kwingine zaidi ya kwa wakristo wa uongo!..

Labda utajiuliza wakristo wa uongo ni wapi?

Wakristo wa uongo ni wale wenye majina ya kikristo, na madhehebu ya kikristo, na wenye kukiri ukristo lakini mioyoni mwao hawana Nia ya uzima wa milele bali vitu vya duniani,

Ni wale ambao sababu kuu ya kuomba ni kupata mali, sababu kuu ya kwenda kanisani ni kupata wapenzi, sababu kuu ya kutoa sadaka ni ili wabarikiwe wawe na vingi katika ulimwengu, lakini hawawezi kufunga na kuomba na kutoa ili Bwana awape utakatifu, hawawezi kutoa sadaka ili Bwana awakirimie vipawa vya rohoni, wala hawawezi kufunga na kuomba ili mahusiano yao na MUNGU yaongezeke.

Huwapendi kusoma Neno kabisa…

Sasa ongezeko la hili kundi la wakristo wa uongo, ndilo linalowapa nguvu na kiburi manabii wa uongo.

Kwani wateja wakubwa wa manabii wa uongo ni wakristo wa uongo…

Kama wakristo wa uongo wasingekuwepo manabii wa uongo wangepotea wote, kwani wangekosa wateja, lakini kwasababu manabii wa uongo wanaona kazi hiyo inalipa na wateja wao wa kwanza ni wakristo na tena hawatumii nguvu nyingi basi ndio wanazidi kuongezeka na kutanuka.

Kwani mali wanazozipata zote zinatoka kwa wakristo wa uongo, ambao wanatoa sadaka ili wapate vya ulimwengu, na hivyo manabii wa uongo wanachukua hiyo nafasi ya kuwadanganyia vitu vya ulimwengu na kuwachukulia mali zao.

Sasa si kwamba manabii wa uongo hawakuwepo miaka ya zamani tofauti na miaka hii…walikuwepo!! tena wengi tu!!…lakini ni kitu gani kilichowafanya wasiwe na nguvu au wasivume katika nyakati hizo kama wanavyovuma sasa katika nyakati hizi??.

Jibu ni rahisi…ni kwasababu nyakati za nyuma, hakukuwa na jopo kubwa la wakristo wa uongo ukilinganisha na sasa…

Nyakati za nyuma, mtu akitangaza maombi ya kupokea mambo ya kidunia hakuna mtu anahudhuria hiyo ibada, kanisani ilikuwa ni mahali pa mifungo na maombi kwaajili ya watu kujengwa roho zao na kuimarisha mahusiano yao na MUNGU, watu walikuwa wanajua kabisa mahusiano yao na MUNGU yakiwa sawa basi hiyo ni zawadi tosha hayo mengine watazidishiwa, hivyo hakukuwa na mtu anayedanganywa, na manabii wa uongo wakawa hawapo, kwasababu wateja hawapo..

Lakini sasa ni kinyume chake, mahali watu wanapoambiwa wafunge na kuomba ili wajazwe Roho Mtakatifu hawaendi, bali mahali wanapoambiwa wafunge na kuomba ili wapate vitu vya ulimwengu, hapo ndipo wanapojaa…unategemea vipi manabii wa uongo wasipate nguvu??…(kwao biashara imefunga, ni msimu wa kuvuna).

Ni majira yao, kwani wateja wameanza kuonekana…wakristo wamebadilika, sasa wanataka vya ulimwengu zaidi ya vya MUNGU, ni msimu wa mavuno..

Kwahiyo kuna shida kubwa katika wakristo wa siku za mwisho, zaidi ya manabii wa siku za mwisho.

Je wewe ni mkristo yupi?

Ni mkristo wa kumtafuta MUNGU ili ujenge nyumba na kuendesha gari au yupi?..

Ni kweli hayo tunayahitaji sana, lakini yamezidi kiasi kwamba sasa yamegeuka kuwa ibada, magari yamegeuka kuwa mungu, nyumba zimegeuka kuwa sifa, na fedha ndio nyimbo za kuabudu.

Ndugu, ukatae ukristo wa uongo, kwasababu ni roho kamili ya shetani….

Kwanza Bwana alisema itatufaidia nini tupate dunia yote halafu tupate hasara za nafsi zetu..

Marko 8:36 “Kwa kuwa itamfaidia mtu nini kuupata ulimwengu wote, akipata hasara ya nafsi yake?”.

Ni heri tumtafute Bwana kwanza kwa lengo la kupata matunda ya roho…

Wagalatia 5:22 “Lakini tunda la Roho ni upendo, furaha, amani, uvumilivu, utu wema, fadhili, uaminifu,

23 upole, kiasi; juu ya mambo kama hayo hakuna sheria”.

Hayo mengine tumeambiwa tutazidishiwa, na hata yasipokuja katika kiwango tunachokitaka pia sio lazima…maadamu tunaye KRISTO huo ni utajiri mkubwa zaidi ya vyote vya ulimwengu.

Hebu jiulize ni lini umefunga, na kutoa sadaka ili tu MUNGU aondoe madhaifu na makosa ndani yako, ili MUNGU akutakase usimtende dhambi, ili MUNGU akuonyeshe mapenzi yake?.

Kama hujawahi kufanya hayo, au yanayofanana na hayo basi kuna shida, hebu badilisha gia, toka katika kundi la wakristo wa uongo bali kuwa bibi harusi wa kweli wa Kristo.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Devis administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments