Chakula kigumu mfano wake ni upi kama tunavyosoma katika Waebrania 5:12?

Chakula kigumu mfano wake ni upi kama tunavyosoma katika Waebrania 5:12?

SWALI: Biblia inasema maziwa ni kwa watoto wachanga, lakini chakula kigumu ni cha watu wazima. Mfano wa chakula hichi kigumu ni kipi?

Waebrania 5:12 Kwa maana, iwapasapo kuwa waalimu, (maana wakati mwingi umepita), mnahitaji kufundishwa na mtu mafundisho ya kwanza ya maneno ya Mungu; nanyi mmekuwa mnahitaji maziwa wala si chakula kigumu. 13 Kwa maana kila mtu atumiaye maziwa hajui sana neno la haki, kwa kuwa ni mtoto mchanga. 14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

JIBU:

Kabla ya kufahamu hicho chakula kigumu, ni vema kujua kwanza maziwa ni yapi.

Hivyo ukiendelea kusoma  vifungu vinavyofuata anasema..

Waebrania 6:1 Kwa sababu hiyo, tukiacha kuyanena mafundisho ya kwanza ya Kristo, tukaze mwendo ili tuufikilie utimilifu; tusiweke msingi tena wa kuzitubia kazi zisizo na uhai, na wa kuwa na imani kwa Mungu, 2 na wa mafundisho ya mabatizo, na kuwekea mikono, na kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele. 3 Na hayo tutafanya Mungu akitujalia.

Sasa hayo mafundisho ya kwanza ya Kristo ndio maziwa. Yaani Mafundisho ya toba, imani kwa Mungu, ubatizo, kuwekewa mikono, kufufuliwa wafu, na hukumu ya milele ni mafundisho ya watoto wachanga..kiroho hujulikana kama maziwa..

Kimsingi mtoto akiendelea kunywa maziwa tu peke yake daima, kitakachotokea baadaye ni kudumaa kama sio kufa kabisa, hivyo itafika wakati tu atahitaji chakula kingine ili aendelee kuishi. Vivyo hivyo na sisi, vipo vyakula ambavyo tunapaswa tule, kwa jinsi tunavyoendelea kukua kiroho.

Vifuavyo ndio vyakula vigumu vya kiroho vya watu wazima:

1) Upendo kwa maadui

Mathayo 5:44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu jambo hilo linaenda kinyume na asili ya mwanadamu, linafunua asili ya ndani kabisa ya Kristo, ambayo si rahisi mtu aliyemchanga kiroho, kuielewa, au kulipokea nyakati za mwanzoni, yaani kumwombea  na kumpenda Yule ambaye anaiwinda roho yake au aliyemjeruhi, ..

2) Makusudi ya Mungu katika mateso

Wafilipi  1:29 Maana mmepewa kwa ajili ya Kristo, si kumwamini tu, ila na kuteswa kwa ajili yake;

Kwanini ni chakula kigumu?. Kwasababu mwamini mchanga, mara nyingi atapenda kuambiwa maneno ya faraja, baraka, na mafanikio, awapo kwa Kristo,  lakini mkristo aliyekomaa, anayaona mapenzi ya Mungu pia hata katika majaribu na kuyashangalia.

1Wathesalonike 3:3 mtu asifadhaishwe na dhiki hizi; maana ninyi wenyewe mnajua ya kuwa twawekewa hizo

Soma pia 1Petro 1:6-8, 4:13, Wakolosai 1:24, Luka 6:22-23

3) Upambanuzi wa kiroho

Waebrania 5:14 Lakini chakula kigumu ni cha watu wazima, ambao akili zao, kwa kutumiwa, zimezoezwa kupambanua mema na mabaya

Mkristo aliyekomaa kiroho, anafundishwa na Mungu kutambua na kugawanya vema mambo yote, kujua vilivyo najisi na visivyo najisi, mafundisho ya kweli na yale ya uongo, anafundishwa, busara, ujuzi na hekima hata katika kuhubiri injili kwa makundi yote, bila kuanguka na kunajisika, kwasababu amepewa roho ya upambanuzi ambayo huja kwa kuzoeshwa na Mungu kwa kipindi Fulani cha muda kupitia  Neno lake.

1Wakorintho 9:20 Nalikuwa kama Myahudi kwa Wayahudi, ili niwapate Wayahudi; kwa wale walio chini ya sheria, nalikuwa kama chini ya sheria, (ingawa mimi mwenyewe si chini ya sheria), ili niwapate walio chini ya sheria.

21 Kwa wale wasio na sheria nalikuwa kama sina sheria, (si kwamba sina sheria mbele za Mungu, bali mwenye sheria mbele za Kristo), ili niwapate hao wasio na sheria. 22 Kwa wanyonge nalikuwa mnyonge, ili niwapate wanyonge. Nimekuwa hali zote kwa watu wote, ili kwa njia zote nipate kuwaokoa watu.

Soma pia, 1Wakorintho 8:6-13, Yohana 2:1-12, Mathayo 11:19.

Kwanini ni chakula kigumu? Kwasababu mtu ambaye ni mchanga kiroho, akijihusisha katika viwango hivyo, hupotea na kunajisika kama sio kupotea kabisa. Ndicho kilichowatokea Adamu na Hawa kuuvamia mtu wa ujuzi wa mema na mabaya nje ya ratiba ya Mungu, matokeo yake wakayavuna mabaya, wala sio mema.

4) Kuikubali Fimbo ya Mungu.

Katika wokovu ipo fimbo ya Mungu; Mzazi yoyote huwa hatoi zawadi tu, sikuzote, hacheki na mwanawe siku zote, lakini pia kuna wakati fimbo hutumika, Vivyo hivyo Mungu ni Baba yetu, huadhibu, pale tunapokosea..

Waebrania 12:11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.

Kwanini ni kigumu? Kukubali marekebisho kwa kuadhibiwa kama sehemu ya kutengenezwa na Mungu, si jambo rahisi mtu kulikubali mkristo ambaye hajakomaa. Yeye atakachojua tu, kuwa Mungu ni upendo.

5) Kujikana na kuubeba msalaba.

Luka 9:23 Akawaambia wote, Mtu ye yote akitaka kunifuata, na ajikane mwenyewe, ajitwike msalaba wake kila siku, anifuate.

Kwanini ni chakula kigumu? Aliye mchanga kiroho kukubali kukataa mapenzi , kuingia gharama kuacha vyote na kuyakubali ya Mungu tu, si jambo rahisi kwa mwanafunzi wa ngazi ya chini.

6) Unyenyekevu na kujitoa kwa wengine.

Wafilipi 2:3 Msitende neno lo lote kwa kushindana wala kwa majivuno; bali kwa unyenyekevu, kila mtu na amhesabu mwenziwe kuwa bora kuliko nafsi yake.

4 Kila mtu asiangalie mambo yake mwenyewe, bali kila mtu aangalie mambo ya wengine.

5 Iweni na nia iyo hiyo ndani yenu ambayo ilikuwamo pia ndani ya Kristo Yesu;

6 ambaye yeye mwanzo alikuwa yuna namna ya Mungu, naye hakuona kule kuwa sawa na Mungu kuwa ni kitu cha kushikamana nacho;

7 bali alijifanya kuwa hana utukufu, akatwaa namna ya mtumwa, akawa ana mfano wa wanadamu;

8 tena, alipoonekana ana umbo kama mwanadamu, alijinyenyekeza akawa mtii hata mauti, naam, mauti ya msalaba

Kwanini ni chakula kigumu?.

Mkristo mchanga kiroho, si rahisi kuangalia mambo ya wengine, mfano wa Kristo, si rahisi kujinyenyekeza na kukubali kutembea kama mtumwa ili kuwatumikia wengine.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post

About the author

Devis administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments