Huu ni mfufulizo wa mafunzo maalumu ya wazazi kwa watoto..
Ukiwa kama mzazi, Njia bora ya malezi, sio kumjali mtoto wako, kwa kila kitu sasa.. Hata kama ni haki yake kukipata, Usiwe mwepesi kumfanyia kila jambo leo hata kama una uwezo wa kumfanyia, Usimjali sasa, mjali kwa baadaye. Tumia nguvu hizo kumwekezea kwa baadaye lakini sasa shughulika naye kitabia, kinidhani, ki-utu..Acha hiyo tabia ya kujali-jali utamuharibu mtoto.
Wengi wetu tunashindwa kujua, kuwa ni kanuni ya ki- Mungu mtoto aishi kama mtumwa, hata kama yeye ndio mrithi wa yote.
Wagalatia 4:1 Lakini nasema ya kuwa mrithi, wakati wote awapo mtoto, hana tofauti na mtumwa, angawa ni bwana wa yote; 2 bali yu chini ya mawakili na watunzaji, hata wakati uliokwisha kuamriwa na baba
Mzazi mwenye Akili na maono bora kwa wanawe, haangalii mali zake anazitumiaje kwa mwanawe sasa, bali huangalia tabia gani anamjengea leo, ili kesho aweze simama vema maisha yake, au mali zake.
Embu fikiria vema, yule Baba Tajiri aliyekuwa na wana wawili, ambao kwa siku nyingi waliishi na baba yao bila kuona faida ya utajiri wa baba yao. Mpaka siku moja mmojawao (yule mdogo) uzalendo ukamshinda, akamwambia baba yake nipe sehemu ya mali yangu inayoniangukia, hatimaye akapewa akaondoka, lakini maisha yaliyopo-mgeukia hali ikawa mbaya, mwishowe akazingatia kurudi kwa baba yake. Na baba yake akampokea akamfanyia karamu kubwa. Lakini yule mwana mwingine aliporudi mashambani, na kuona sherehe kubwa kwa ndugu yake, akachukizwa, ndipo akamwambia baba yake “Tazama, mimi nimekutumikia miaka mingapi hii, wala sijakosa amri yako wakati wo wote, Lakini hujanipa mimi mwana-mbuzi, nifanye furaha na rafiki zangu;”
Tusome;
Luka 15:11-31
11 Akasema, Mtu mmoja alikuwa na wana wawili; 12 yule mdogo akamwambia babaye, Baba, nipe sehemu ya mali inayoniangukia. Akawagawia vitu vyake. 13 Hata baada ya siku si nyingi, yule mdogo akakusanya vyote, akasafiri kwenda nchi ya mbali; akatapanya mali zake huko kwa maisha ya uasherati. 14 Alipokuwa amekwisha tumia vyote, njaa kuu iliingia nchi ile, yeye naye akaanza kuhitaji. 15 Akaenda akashikamana na mwenyeji mmoja wa nchi ile; naye alimpeleka shambani kwake kulisha nguruwe. 16 Akawa akitamani kujishibisha kwa maganda waliyokula nguruwe, wala hapana mtu aliyempa kitu. 17 Alipozingatia moyoni mwake, alisema, Ni watumishi wangapi wa baba yangu wanaokula chakula na kusaza, na mimi hapa ninakufa kwa njaa. 18 Nitaondoka, nitakwenda kwa baba yangu na kumwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; 19 sistahili kuitwa mwana wako tena; nifanye kama mmoja wa watumishi wako. 20 Akaondoka, akaenda kwa babaye. Alipokuwa angali mbali, baba yake alimwona, akamwonea huruma, akaenda mbio akamwangukia shingoni, akambusu sana. 21 Yule mwana akamwambia, Baba, nimekosa juu ya mbingu na mbele yako; sistahili kuitwa mwana wako tena. 22 Lakini baba aliwaambia watumwa wake, Lileteni upesi vazi lililo bora, mkamvike; mtieni na pete kidoleni, na viatu miguuni; 23 mleteni ndama yule aliyenona mkamchinje; nasi tule na kufurahi; 24 kwa kuwa huyu mwanangu alikuwa amekufa, naye amefufuka; alikuwa amepotea, naye ameonekana. Wakaanza kushangilia. 25 Basi, yule mwanawe mkubwa alikuwako shamba na alipokuwa akija na kuikaribia nyumba, alisikia sauti ya nyimbo na machezo. 26 Akaita mtumishi mmoja, akamwuliza, Mambo haya, maana yake nini? 27 Akamwambia, Ndugu yako amekuja, na baba yako amemchinja ndama aliyenona, kwa sababu amempata tena, yu mzima. 28 Akakasirika, akakataa kuingia ndani. Basi babaye alitoka nje, akamsihi. 29 AKAMJIBU BABA YAKE, AKASEMA, TAZAMA, MIMI NIMEKUTUMIKIA MIAKA MINGAPI HII, WALA SIJAKOSA AMRI YAKO WAKATI WO WOTE, LAKINI HUJANIPA MIMI MWANA-MBUZI, NIFANYE FURAHA NA RAFIKI ZANGU; 30 lakini, alipokuja huyu mwana wako aliyekula vitu vyako pamoja na makahaba, umemchinjia yeye ndama aliyenona. 31 Akamwambia, Mwanangu, wewe u pamoja nami sikuzote, na vyote nilivyo navyo ni vyako.
Nataka uone sifa ya huyo baba, kwa wanawe, ijapokuwa alikuwa na mali, lakini hakutaka Watoto wake, waishi kwa mali zake, bali waishi kama watumwa wengine. Sio kwamba alikuwa anawatesa, Hapana, alikuwa anawatengeneza ili baadaye wakishajua maisha hasaa ni nini kivitendo, ndipo awaache huru, wapewe vyote na baba yao, wafurahie maisha wayapendayo.
Leo hii imekuwa kinyume chake, utaona mtu ndiye anayetumia nguvu zake, na mali zake, kumdekeza mtoto, kama yai, kumletea wafanyakazi ndani, wawapikie, wawafulie, wawapigie deki, na pasi, wenyewe wakae wakitazama muvi Netflix, na kucheza magemu, kwenye Ipad, na computa,
Akidhani anamlea mtoto, kumbe anamlea mwana-mpotevu. Mtoto akikosea tu, hawezi kuadhibiwa, mzazi anasema sitaki mtoto wangu ateseke kama mimi nilivyoteseka, kwani ni nani kakwambia mtoto akiadhibiwa ni lengo la kuteswa? Watoto hawafundishwi kufunga, hata kwa sehemu (nusu siku), au kupelekwa mikesha mara moja moja wajifunze kanuni za kiroho, wazazi wanasema hawa bado wadogo. Hivi ni kazazi gani tunakilea??
Si lazima kila siku ale mboga saba, si lazima umpe chakula anachokitaka yeye, siku nyingine fululiza ugali maharage, wiki mbili nyumbani, mwache alie, mpaka azoee..Mambo kama hayo unaweza kuona unamtesa mtoto, lakini ndio njia sahihi ya maleza..unamtengeneza mtu imara sio lege-lege.
Likizo inapofika, kuliko kumpeleka beach kwenye mapembea, na masherehe, mpeleke kijijini kwenu, aone mazingira ya asili, ale vyakula vya kule, atumie vyoo vya kule ambavyo sio vya kuflash, aende akakatie ng’ombe majani, aende na wafungaji machungaji akae huko mpaka likizo iishe, ndipo arudi..
Lakini wewe mwenyewe huku nyuma unajua ni nini unafanya, ukimwandalia akiba, nzuri, ili baadaye atakapoelimika kiroho na kimwili, ukimpa vya kwako, au ukimdekeza atakavyo, ataweza kujisimamia mwenyewe, na kuwa mtu mkakamavu thabiti, na Jasiri, mwenye utu na kiongozi awezaye kuishi katika jamii, na kuwajali na walio wanyonge na wenye shida.
Hayo ndio malezi bora ya mtoto. Mfanye leo mtumwa ili kesho awe mfalme, lakini ukichagua kumfanya leo mfalme, jiandae kesho kuwa mtumwa mfano wa mwana- mpotevu.
Mithali 22:6 Mlee mtoto katika njia impasayo, Naye hataiacha, hata atakapokuwa mzee
Bwana akubariki
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
NI NINI KINATOKA KINYWANI MWA MTOTO WAKO?
MRUDI MWANAO NAYE ATAKUSTAREHESHA
NAFASI YAKO WEWE MAMA KWA MTOTO NA WAJUKUU WAKO NI IPI?.
Print this post
Save my name, email, and website in this browser for the next time I comment.
Δ