Wana wa Israeli walipotoka nchi ya Misri, baada ya miezi kadhaa tu walifika mahali PALIPOITWA KADESH-BARNEA, ilikuwa safari ya mwendo mfupi tu, kabla ya kuingia katika nchi yao ya ahadi. Lakini tunasoma walipofika mahali pale walikutana na kikwazo kikubwa sana. Biblia inaonyesha eneo lile lilikuwa ni eneo kame kuliko maeneo yote, hakukuwa na jani wala mche, wala dalili ya mto kupita maji mahali pale, ni eneo lilokuwa limezungukwa na milima tupu, Na ndipo wana wa Israeli walipofika pale wakaona kuwa hakuna dalili yoyote ya kupata maji mbeleni kwa ajili yao na watoto wao na mifugo yao, wakaona kuwa pengine hawatakuwa na siku 5 za kuishi mbeleni kwa jinsi hali ilivyokuwa mbaya, ndipo wakaanza kumnung’unikia Musa na Mungu kwa nguvu sana, ni kwanini aliwatoa kule Misri katika nchi yenye bustani nzuri na chakula na kuwaleta katika jangwa baya kama lile ili kuwamaliza huko wao na watoto wao?.
Wana wa Israeli walifika mahali wakasahau siku chache tu nyuma Mungu aliwageuzia yale maji yalikuwa machungu kuwa matamu, walisahau miujiza yote waliyofanyiwa na Mungu kule Misri, walisahau nyama zote zilizokuwa zinawafikia za wale kware kutoka mahali wasipopajua, pamoja na Mana iliyoshuka kutoka mbinguni, wakashindwa kumwesabia Mungu kuwa anaweza hata kuwafanyia miujiza ya kuwanyeshea mvua nyingi mahali pale lakini badala yake baada ya kukutana na ukame ule, na kiu kile na mbele yao upo MWAMBA MKUBWA SANA umesisimama ambao kwa kiu kile wasingeweza kuuvuka, ndipo wakaanza kunung’unika kwa nguvu.
Hawakujua kuwa ni Mungu kwa makusudi kabisa aliwaacha waone kiu ili akawanyeshwe maji yaliyo hai, yatakayowafanya wasione kiu tena ya mambo watakayokutana nayo huko mbeleni baada ya pale, lakini wao mawazo yao yalikuwa yanafikiria mambo ya mwilini tu . Huku Wakiutazama huo mwamba mgumu mkubwa uliowafunika mbele yao usio na mahali pa kuzungukia ndio uliwafanya wazidi kujawa na hasira na uchungu, hata kutaka kumpiga Musa kwa mawe.
Hawakujua kuwa ule mwamba ulikuwa ni KRISTO mwenyewe. Hawakujua kuwa Kristo alikuwa amesimama mbele yao kuondoa kiu yao ya mambo maovu, lakini wao kwa kuwa macho yao ya mwilini yalikuwa yanaona ni jiwe tu kubwa sana limewazinga hawana mahali pa kwenda wakawa wanakufuru mbele ya Kristo.
Na ndipo Mungu hakupendezwa nao matokeo yake akamwambia Musa, aupige mwamba ule na utatoa maji. Na kweli Musa alipoupiga ule mwamba ulitoa maji mengi sana, lakini maji yale hayakuwa maji ya rohoni tena, bali yalikuwa ni ya kukata kiu chao tu kwa muda,lakini matatizo yataendelea pale pale.
1 Wakorintho 10 : 1-33
“1 Kwa maana, ndugu zangu, sipendi mkose kufahamu ya kuwa baba zetu walikuwa wote chini ya wingu; wote wakapita kati ya bahari;
2 wote wakabatizwa wawe wa Musa katika wingu na katika bahari;
3 wote wakala chakula kile kile cha roho;
4 wote wakanywa kinywaji kile kile cha roho; KWA MAANA WALIUNYWEA MWAMBA WA ROHO ULIOWAFUATA; NA MWAMBA ULE ULIKUWA NI KRISTO.
5 Lakini wengi sana katika wao, Mungu hakupendezwa nao; maana waliangamizwa jangwani.
6 Basi mambo hayo yalikuwa mifano kwetu, kusudi sisi tusiwe watu wa kutamani mabaya, kama wale nao walivyotamani”.
Na ndio maana tunaona baada ya pale, hata hawakuweza kustahimili zile habari za wapelelezi zilizoletwa na Akina Yoshua matokeo yake Mungu akakasirishwa nao akawarudisha tena kwenye lile jangwa, Biblia inasema wakalizunguka tena kwa muda wa miaka 40 mpaka kile kizazi chote kilichomnung’unikia Mungu kilipopotea na ndio tunakuja kuona tena Mungu akiwarudisha mahali pale pale kwenye ue mwamba wa kwanza,kuwajaribu kwa mara nyingine baada ya muda huo mrefu kupita.
Hakukuwa na njia ya mkato nyingine ya kufika Kaanani, ni Sharti waupitie MWAMBA ULE ULE uliokataliwa. Na kama ilivyo ada eneo lile la Kadesh-barnea ni eneo lisilokuwa na maji, eneo kame kuliko maeneo yote, na mahali ambalo halina kitu chochote, na wana wa Israeli walipofika tena mahali pale, tunaona wakaanza kumnung’unikia tena Musa kama mwanzo na kusema.
“Ingalikuwa heri kama tungalikufa wakati ule ndugu zetu walipokufa mbele za Bwana!
4 Mbona mmewaleta kusanyiko la Bwana hata jangwa hili ili tufe huku, sisi na wanyama wetu?
5 Na mbona mmetupandisha kutoka Misri ili kutuleta hata mahali hapa pabaya? Si mahali pa mbegu, wala tini, wala mizabibu, wala makomamanga; wala hapana maji ya kunywa..”( Hesabu 20: 3-5)
Unaona?. Ni mahali ambapo hata viumbe hai hawakuweza kuishi kwa jinsi palivyokuwa pakame kupindukia na zaidi ya yote upo mwamba mkubwa sana umesimama mbele yao, usiovukika, japo ni mahali palipokuwa karibu sana na nchi yao ya ahadi waliyokuwa wanatazamia kwa muda mrefu.
Hawakujua kuwa kiu chao kitaondolewa na ule mwamba mmoja tu, licha ya kuzunguka huku na huko jangwani kwa muda mrefu lakini hatimaye wanairudia njia ile ile ya mwamba waliokuwa wameukataa. Na safari hii pia tunaona wakinung’unika vile vile, Ndipo Mungu akamwambia Musa nenda kaseme na Mwamba ule. Lakini Musa naye hakuwa makini kwa kuzingatia aliyoambiwa alidhani kuwa anazungumza na jabali hakujua kuwa ni Kristo alikuwa amesimama pale katika Roho kuwaponya watu wake, Lakini yeye akaenda kwa zile desturi za kwanza za kuuchapa mwamba, na huku Mungu alimwambia azungumze na ule Mwamba, akaenda hivyo hivyo kuuchapa maji kweli yalitoka lakini kumbe na yeye alikuwa amejiwekea hukumu mwenyewe.
Hivyo laana ambazo zingepaswa ziwapate wale watu zikamwangukia Musa na Haruni .Hivyo kwa tendo lile tu hawakuweza kuiona nchi ya Ahadi. Hapo ndipo walipojua kuwa ule mwamba haukuwa jabali ni Mungu mwenyewe.
Kristo hadhihakiwi, alikuja Hapa duniani kwa ajili ya kuwaokoa watu wake, yeye kama ule Mwamba imara utoao maji ya uzima wakati wa Kiu lakini mwamba huo huo unaweza kukwamisha wengi na wakati mwingine kuletea mauti kama hatutajua njia ya kuuendea.
Mathayo 21:42 “Yesu akawaambia, Hamkupata kusoma katika maandiko, Jiwe walilolikataa waashi, Hilo limekuwa jiwe kuu la pembeni; Neno hili limetoka kwa Bwana, Nalo ni ajabu machoni petu?
43 Kwa sababu hiyo nawaambia, Ufalme wa Mungu utaondolewa kwenu, nao watapewa taifa lingine lenye kuzaa matunda yake.
44 NAYE AANGUKAYE JUU YA JIWE HILO ATAVUNJIKA-VUNJIKA; naye YE YOTE AMBAYE LITAMWANGUKIA, LITAMSAGA TIKITIKI”.
Ule mwamba ndio ulikuwa njia pekee ya wao kuingia katika nchi yao ya ahadi,lakini wengi wao uliwaangamiza. Uliwaangukia na kuwasaga tikitiki, ni wawili tu ndio walifanikiwa kuingia katika nchi ya Ahadi kati ya mamilioni ya watu. Ule Mwamba ndio uliokuwa geti la kuingia Kaanani..Leo hii na sisi tunasema ni wakristo tuliokatika safari ya kwenda mbinguni, jiwe lile (YESU KRISTO), ndio litupalo maji ya uzima katika safari yetu ya wokovu hapa duniani. Yesu ndiye Lango la kuingia Kaanani (mbinguni)
Lakini na sisi tukiwa watu wa kumnung’unikia Mungu tunapopitia shida, au tunapopungukiwa, au tunapougua, ni kweli Mungu alituokoa na sisi tulibatizwa kama wana wa Israeli walivyobatizwa katika bahari ya shamu, lakini tunaweza tukakosa mbingu kwa mambo kama yale yale ya kunung’unika, kusahau kuwa jana yetu na juzi yetu ilikuwa mikononi mwake, yeye ndiye aliyetufanikisha katika hili katika lile kipindi fulani, lakini leo tunapitia haya madogo tu kwa muda tunamnung’unikia. Tena mbele ya ule mwamba wake mteule Yesu Kristo Bwana wetu aliyetuokoa kwa damu yake ya thamani.
Biblia inatuambia mambo hayo yaliandikwa kwa mifano ili kutuonya sisi. Je! leo unaonyeka wewe mkristo?
Daudi alisema.
Zaburi 18: 1 “Wewe, Bwana, nguvu zangu, nakupenda sana;
2 Bwana ni jabali langu, na boma langu, na mwokozi wangu, Mungu wangu, MWAMBA WANGU ninayemkimbilia, Ngao yangu, na pembe ya wokovu wangu, na ngome yangu.
3 Nitamwita Bwana astahiliye kusifiwa, Hivyo nitaokoka na adui zangu.”
Zaburi 18: 31 “Maana ni nani aliye Mungu ila Bwana? NI NANI ALIYE MWAMBA ILA MUNGU WETU”.
Tumpende Bwana wetu, tumtii yeye, tuvumilie, tulale juu ya ule mwamba salama, tunywe maji yale kwa utulivu, naye pekee ndiye atakayetuweka mbali na maadui zetu.
Zaburi 40:1 “Nalimngoja Bwana kwa saburi, Akaniinamia akakisikia kilio changu.
2 Akanipandisha toka shimo la uharibifu, Toka udongo wa utelezi; AKAISIMAMISHA MIGUU YANGU MWAMBANI, AKAZIIMARISHA HATUA ZANGU”.
Bwana akabariki sana.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
About the author