Ni nini tunajifunza katika maisha ya Nuhu, ambaye Mungu alimshuhudia kuwa mwenye haki katika kizazi chake? Lakini baadaye akaja kunaswa katika ulevi uliomletea aibu kubwa nyumbani mwake?
Mwanzo 9:20 Nuhu akaanza kuwa mkulima, akapanda mizabibu; 21 akanywa divai, akalewa; akawa uchi katika hema yake.
Ulishawahi kujiuliza kama Nuhu asingekuwa mkulima wa mizabibu, angekuwa na wazo la kutengeneza divai? Na hatimaye kuanguka kwenye makosa?
Jibu ni la! Kwasababu bila shaka Nuhu alikuwa mkulima, ili ajipatie rizki, na sio ili atengeneze divai. Lakini hakujua kuwa nyuma ya kazi yake ya halali upo mtego wa dhambi. Na hivyo akauridhia na ndio ikamshawishi mpaka kutoa bidhaa isiyopasa katika maisha yake kwa kazi hiyo.
Hata sasa watoto wengi wa Mungu wanashindwa kujua kuwa “shughuli za ulimwenguni zilizo za halali kabisa” zina udanganyifu Fulani nyuma yake, unaolewesha ambao unaweza mpelekea mtu anguko kubwa sana, kama asipokuwa makini.
Bwana Yesu alisema..
Marko 4:18 Na hawa ndio wale wapandwao penye miiba; ni watu walisikiao lile neno, 19 na SHUGHULI ZA DUNIA, NA UDANGANYIFU WA MALI, na tamaa za mambo mengine zikiingia, hulisonga lile neno, likawa halizai.
Kwamfano labda ni kijana, ameokoka, hapo mwanzo alikuwa amesimama vizuri tu, katika Bwana, anapata muda wa kuomba, kushuhudia, kujisomea Neno n.k. lakini akapata kazi nzuri, na ile kazi ikawa inamlazimu, awe bize wiki nzima, isipokuwa jumamosi na jumapili. Sasa katika miezi ya mwanzo, alikuwa anatimiza majukumu yake ya ushuhudiaji/ kuhudhuria mikusanyiko ya nyumbani na maombi, bila shida siku ya jumamosi, na jumapili anahudhuria ibadani , kama kawaida. Lakini baada ya miezi kadhaa, alivyozidi kufanikiwa, uvivu na udanganyifu wa mali ukaanza kumuingia, akasema, huu muda wangu wa jumamosi, nifanye kitu kingine cha kuniingizia kipato, (jambo ambalo si baya), lakini hajui kuwa analisogeza mahali ambapo sio sahihi. Na kweli akajiongezea kitu cha kufanya, matokeo yake jumamosi yake yote ikawa ni kazi zake za miradi. Hakuna ushuhudiaji tena, hakuna ibada za jumuiya tena, hakuna maombi.
Na inapofika jumapili, anaamka amechoka, anasema, aa wiki hii napumzika, wiki ijayo nitaenda..anaanza kuwa mdokoaji-dokoaji wa ibada, hivyo baada ya miezi miwili, anapokea mialiko ya marafiki zake, kwenda kwenye party, picnic, vikao vya kirafiki, sinema, n.k. vyote hivyo vinapaswa vifanyike siku ya jumapili ambayo yupo free. Matokeo yake anahudhuria kanisani mara moja kwa mwezi au miezi miwili. Hilo linaendelea mwaka mzima. Hajui kuwa mwili unafurahia kweli, lakini roho yake inadhoofika siku baada ya siku. Sasa baada ya kipindi kirefu hapo ndipo anashangaa haoni tofauti yake ni watu wa kidunia, kila jambo la ki-Mungu anaona ni mzigo kulifanya, yeye ambaye alikuwa anawaombea wengine anakuwa wa kuombewa, yeye ambaye alikuwa anawaokoa wengine, anafikiwa kuokolewa tena.Hana nguvu tena, ameshaleweshwa, shetani kamweka chini.
Sasa huyu ndio mfano wa Nuhu, Amelewesha na kazi yake. Na utumishi wake. Kwasababu hakujiwekea mipaka,.
Ndio maana maandiko yanatutaka tuwe na kiasi, katika huu ulimwengu.
1Wakorintho 7:31 Na wale wautumiao ulimwengu huu, kama hawautumii sana; kwa maana mambo ya ulimwengu huu yanapita.
Kuwa buzy kupita kiasi, si afya ya kiroho au kimaisha. Ni lazima upate nafasi ya kutosha kujijenga nafsi yako kwa Mungu. Ni vema utumie siku za tano, usiku na mchana kama ni hivyo kuwekeza na kupangilia ratiba yako, lakini upate pia nafasi nyingi ya kumwabudu na kumkaribia Mungu bila masumbufu. Umeajiriwa katika kazi ambayo siku zote saba za wiki, upo kazini, hupewi muda wa kupata ibada yako na Mungu, fahamu hiyo si kazi itokayo kwa Mungu. Fikiria kutafuta kazi nyingine.
Kama ubize, basi Mungu angekuwa buzy zaidi yetu sisi, kwasababu yeye ndio aliyeumba ulimwengu mzima, lakini alijipa pumziko Siku ya saba, akaiweka wakfu, akatuambia na sisi. Tufanye hivyo. Kumbuka hizi ni siku za mwisho, na wengi wataikosa mbingu kwa ubize usiokuwa na tija wa mambo ya ulimwengu huu, yanayopita.
Ni heri ukose vya dunia, lakini nafsi yako itajirike, kuliko kutajirika duniani na huku nafsi yako unaangamia. Uzima wako upo katika mambo ya rohoni, Jinsi unavyojitenga na Mungu ndivyo unavyojiua mwenyewe.
Kamwe usiyaige ya Nuhu mabaya ya ajira yake, bali yale mema aliyoyafanya kabla ya Gharika.
Shalom.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >>https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
KWANINI MTINI KATIKATI YA MIZABIBU?
UMUHIMU WA KUBATIZWA.(Opens in a new browser tab)
NUHU WA SASA.(Opens in a new browser tab)
(Opens in a new browser tab)KWANINI NI NUHU, AYUBU NA DANIELI?(Opens in a new browser tab)
Rudi Nyumbani
Print this post