Swali: Katika Ayubu 14:12 tunasoma kuwa wafu hawafufuliwi, lakini katika 1Wakorintho 15:51 tunaona tena biblia inasema wafu watafufuliwa, sasa tuchukue ipi tuache ipi?.. au je biblia inajichanganya yenyewe?
Jibu: Biblia kamwe haijichanganyi, wala haijawahi kujichanganya, isipokuwa tafakari zetu ndizo zinachojichanganya au kuchanganyikiwa.
Turejee mistari hiyo na kisha tuone majibu yake kupitia biblia hiyo hiyo..
Ayubu 14:10 “Lakini mwanadamu hufa, huifariki dunia; Naam, mwanadamu hutoa roho, naye yupo wapi?
11 Kama vile maji kupwa katika bahari, Na mto kupunguka na kukatika;
12 Ni vivyo MWANADAMU HULALA CHINI, ASIINUKE; Hata wakati wa mbingu kutokuwako tena, hawataamka, Wala kuamshwa usingizini.”
Ni kweli hapa maandiko yanasema kuwa MWANADAMU HULALA CHINI, ASIINUKE TENA… lakini hebu turejee agano jipya katika kitabu kile cha Wakorintho tuangalie biblia inatuambiaje..
1Wakoritho 15:51 “Angalieni, nawaambia ninyi siri; hatutalala sote, lakini sote tutabadilika,
52 kwa dakika moja, kufumba na kufumbua, wakati wa parapanda ya mwisho; maana PARAPANDA ITALIA, NA WAFU WATAFUFULIWA, wasiwe na uharibifu, nasi tutabadilika”.
Na hapa maandiko yanatuambia, parapanda italia na wafu waliolala katika Kristo watafufuliwa. Sasa swali tuchukue lipi tuache lipi?, maneno kama hayo hayo yanarudiwa tena katika 1Wathesalonike 4:16.
Jibu ni Dhahiri kuwa “Wafu watafufuliwa siku ya mwisho”.. sawasawa na Yohana 5:25.
Kwanini maandiko hayo ya 1Wakoritho 15:51 yana nguvu kuliko yale ya Ayubu 14:12, yanayosema kuwa “wafu hawafufuliwi”?… Ni kwasababu Agano jipya ni ukamilifu wa agano la kale.
Manabii waliotangulia walifahamu mambo kwa sehemu, lakini Roho Mtakatifu katika agano jipya, amekamilisha yote na kufunua yote… Na kawaida ni kwamba unapokuja ule ufunuo mkamilifu, bali ule uliokuwa unajilikana kwa sehemu unabatilika ndivyo maandiko yasemavyo..
1Wakorintho 13:9 “Kwa maana tunafahamu kwa sehemu; na tunafanya unabii kwa sehemu;
10 lakini ijapo ile iliyo kamili, iliyo kwa sehemu itabatilika”.
Manabii wengi wa agano la kale hawakujua mengi kuhusiana na ufufuo, au mbingu mpya na nchi mpya, ingawa walikuwa wanafahamu siku moja watajua mambo yote..hivyo walitoa unabii kwa sehemu waliyopimiwa…lakini mwisho wa nyakati Roho Mtakatifu anakamilisha ufunuo wote sawasawa na hiyo 1Wakorintho 13:9-10.
Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Wafu watafufuliwa siku ya mwisho, na watahukumiwa.
Yohana 5:28 “Msistaajabie maneno hayo; kwa maana saa yaja, ambayo watu wote waliomo makaburini wataisikia sauti yake.
29 NAO WATATOKA; WALE WALIOFANYA MEMA KWA UFUFUO WA UZIMA, na wale waliotenda mabaya kwa ufufuo wa hukumu”.
Na kumbuka hoja hii ya kufufuliwa kwa wafu ndiyo iliyoleta mgawanyiko mkubwa katikatika ya wayahudi hata kuzaliwa makundi (madhehebu) mawili ambayo ni MAFARISAYO NA MASADUKAYO, ambapo Mafarisayo waliamini ufufuo na masadukayo hawakuamini ufufuo kwa kutumia andiko hilo la Ayubu 14:12 pamoja na maandiko mengine machache..
Lakini Bwana YESU alikuja kuondoa huo utata kama tunavyosoma katika Mathayo 22:23-32..
Mathayo 22:23 “Siku ile Masadukayo, watu wasemao ya kwamba hakuna kiyama, wakamwendea, wakamwuliza,
24 wakisema, Mwalimu, Musa alisema, Mtu akifa, akiwa hana watoto, ndugu yake na amwoe yule mkewe, ili ampatie nduguye mzao.
25 Basi, kwetu kulikuwa na ndugu saba; wa kwanza akaoa, akafariki, na kwa kuwa hana mzao, akamwachia nduguye mke wake.
26 Vivyo hivyo wa pili naye, na wa tatu, hata wote saba.
27 Mwisho wa wote yule mwanamke akafa naye.
28 Basi, katika kiyama, atakuwa mke wa yupi katika wale saba? Maana wote walikuwa naye.
29 Yesu akajibu, akawaambia, Mwapotea, kwa kuwa hamyajui maandiko wala uweza wa Mungu.
30 Kwa maana katika kiyama hawaoi wala hawaolewi, bali huwa kama malaika mbinguni.
31 Tena kwa habari ya kiyama ya watu, hamjalisoma neno lililonenwa na Mungu, akisema
32 Mimi ni Mungu wa Ibrahimu, na Mungu wa Isaka, na Mungu wa Yakobo? Mungu si Mungu wa wafu, bali wa walio hai”
Kwahiyo wafu watafufuliwa, lakini swala la msingi ni je!.. sisi tutakuwepo upande upi wakati huo wa ufufuo?.. Je tutafufuliwa ili tukavikwe taji na kuurithi uzima wa milele, au kwaajili ya hukumu ya ziwa la Moto?
Kumbuka wote walio nje ya Kristo, ambao hawajampokea Bwana YESU na kuoshwa dhambi zao kwa damu yake, wametabiriwa kuwa miongoni mwa watakaohukumiwa katika hukumu ya milele. Je umeokoka?..umebatizwa katika ubatizo sahihi?.. umejazwa Roho Mtakatifu?.
Kama bado unangoja nini?… Ni heri ukafanya maamuzi leo ya kubadili maisha yako.
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
UTALIPWA KATIKA UFUFUO WA WENYE HAKI.
About the author