Kwanini kuna tafsiri nyingi za Biblia, na tafsiri ipi ni sahihi?

Kwanini kuna tafsiri nyingi za Biblia, na tafsiri ipi ni sahihi?

Jibu: Mpaka kufikia mwaka 2024 biblia imetafsiriwa kwa lugha 756, hivyo kuna tafsiri Zaidi ya 756 mpaka sasa duniani kote.

Sasa kwa asili biblia iliandikwa kwa lugha kuu tatu, ambazo ni KIEBRANIA (Agano la Kale), lugha ya KIARAMU (Sehemu za Agano la kale na jipya) pamoja na lugha ya KIYUNANI AU KIGIRIKI (Agano jipya), Hizo ndizo lugha kuu tatu zilizoandikia biblia ya kwanza, na haikuandikwa kwa lugha ya kiingereza wala Kiswahili, wala lugha nyingine yoyote tofauti na hizo tatu.

Sasa kuna tafsiri nyingi za biblia siku hizi za leo kwasababu kadhaa, na sababu hizo zipo tatu (3)..

1)Tofauti za lugha, 2) Maendeleo ya Lugha 3) Mitazamo ya kidhehebu.

Hizo ndizo sababu kuu tatu,.. hebu tutatame moja baada ya nyingine.

1. Tofauti za Lugha

Kwasababu biblia kwa asili iliandikwa kwa lugha ya Kiebrania, Kiaramu, na Kigiriki. Zipo jamii za watu zisizozungumza lugha hizo, na kwasababu ni lazima watu wote, ulimwenguni kote walisikie Neno la Mungu, ni lazima tafsiri iwepo,….na watalisikiaje na kulielewa wasipolisikia kwa lugha yao na kulisoma kwa lugha yao?..

Hiyo ndiyo ikawa sababu ya Biblia ya kwanza yenye lugha hizo tatu, kutafsiriwa kwa lugha nyingine mbali mbali ikiwemo lugha yetu ya Kiswahili, Hebu tafakari laiti isingetafsiriwa kwa lugha yetu, biblia kwetu ingekuwa ngumu kiasi gani leo?.. Hivi ilivyo tu tayari ni ngumu!… vipi kama tungekuwa tunaisoma kwa lugha nyingine?? Si hali ingekuwa mbaya Zaidi??…kwasababu ingetupasa tukajifunze kwanza lugha hizo tatu, jambo ambalo lingekuwa gumu sana kwa wengi!.

Kwasababu ya shida hiyo, ndipo Bwana MUNGU wetu kupitia Roho wake Mtakatifu alitangulia kuachilia uwezo wa lugha na tafsiri zake ile siku ya Pentekoste, (soma Matendo 2) kuonyesha kuwa sasa Neno linapaswa lihubiriwe kwa watu wote na lugha zote, na ndipo zikaja tafsiri hizo.

 2. Maendeleo ya Lugha.

Hii ni sababu ya pili ya uwepo wa tafsiri nyingi, utaona tayari kuna tafsiri moja ya lugha husika, tuchukue mfano lugha ya Kiswahili, halafu baada ya muda unaona kuna tafsiri nyingine zinaongezeka tofauti na hiyo ya kwanza na tena kwa lugha hiyo hiyo ya Kiswahili.

Sasa hiyo inatokana na kukua kwa lugha, kwani lugha siku zote inakuwa (inaongezeka misemo na maneno), na kwasababu hiyo basi tafsiri nyingi zinatokea na bado zitaendelea kutokea,

3. Mitazamo ya Kidhehebu na Theolojia

Kutokana na ongezeko la Madhehebu mengi yenye itikadi zinazotofautiana, imechangia pakubwa kutokea kwa tafsiri mpya kila siku kulingana na misimamo ya dhehebu husika. Kwani tafsiri nyingine zinaegemea mapokeo ya dhehebu hilo, kwamfano utaona dhehebu la katoliki linatumia biblia yenye vitabu vingine vya Deuterokanoni, ambavyo vinafanya jumla ya vitabu 72, tofauti na Biblia ya asili yenye vitabu 66.

Zipo na sababu nyingine ndogo ndogo ikiwemo mbinu za kutafsiri, kwamba wengine wanatafsiri neno kwa neno, na wengine wanatafsiri sentensi nzima na kuleta maana ya ujumla, na sababu nyingine ni mapendekezo ya lugha laini kwaajili ya watoto, zenye kutumia tafsida na zisizotumia lugha za ukali na kuogopesha. Hizi zote ndizo zinazochangia ongezeko la tafsiri za biblia kila siku.

Lakini swali je! Ni tafsiri ipi iliyo sahihi na isiyo na sumu kwa mkristo?

Mara nyingi kitu cha asili kinakuwa ni bora kuliko kile kilichochujwa Zaidi.. Tafsiri iliyo bora na yenye kufaa kuliko zote ni ile yenye lugha tatu (Kiebrania, Kiaramu na kiyunani), lakini kwasababu ni ngumu sisi kukijua kiyunani, na kiebrania kifasaha, basi tafsiri inayofuata kwa Ubora ni ile ya kwanza kabisa iliyotafsiriwa katika yetu lugha husika, kwamfano kwa sisi tunaozungumza Kiswahili, tafsiri ya kwanza kabisa na bora kwa lugha yetu ni ile ya SWAHILI UNION VERSION (SUV), ambayo ndiyo inayotumika sasa kwa wingi, inayoanza na…

Mwanzo 1:1 “Hapo mwanzo Mungu aliziumba mbingu na nchi.

2 Nayo nchi ilikuwa ukiwa, tena utupu, na giza lilikuwa juu ya uso wa vilindi vya maji; Roho ya Mungu ikatulia juu ya uso wa maji.”

Hiyo ndiyo tafsiri iliyo bora, tafsiri nyingine zinazofuata baada ya hapo faida yake inakuwa ni ndogo ukilinganisha na hasara…kwani zinabadilishwa maana na zinatengenezwa kwa kuegemea dini Fulani, na katika lugha nyingine ni hivyo hivyo, ile ya kwanza ni bora Zaidi kuliko zilizoendelea kufuata.

Kwahiyo kwa hitimisho, Tafsiri sahihi yenye kumfaa mtu ni ile ya kwanza (yenye kiebrania, kiyunani na kigiriki) ikiwa mtu atakuwa ana uwezo wa kuzielewa lugha hizo, lakini kama hana uwezo basi ile tafsiri ya kwanza kabisa iliyotafsiriwa kwa lugha yake, ni bora Zaidi.

Je umempokea Bwana YESU kikweli kweli?

Je unajua kuwa tunaishi katika siku za kurudi kwa pili kwa Bwana YESU na unyakuo upo karibu?, Je unajua kuwa kama huna Roho Mtakatifu huwezi kuiona mbingu (Warumi 8:9).. sasa kama bado hujaokoka unasubiri nini?,

Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini

12  Usiku umeendelea sana, mchana umekaribia, basi na tuyavue matendo ya giza, na kuzivaa silaha za nuru.

13  Kama ilivyohusika na mchana na tuenende kwa adabu; si kwa ulafi na ulevi, si kwa ufisadi na uasherati, si kwa ugomvi na wivu.

14  Bali mvaeni Bwana Yesu Kristo, wala msiuangalie mwili, hata kuwasha tamaa zake”.

Maran atha.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments