Kufuatana na ile habari ya Tajiri na Lazaro, ingewezekanikaje Nabii Samweli kupandishwa juu?

Kufuatana na ile habari ya Tajiri na Lazaro, ingewezekanikaje Nabii Samweli kupandishwa juu?

Swali: Katika ile habari ya Tajiri na maskini Lazaro (katika Luka 16: 27-31) tunasoma kuwa haikuwezekana kwa Lazaro kurudishwa duniani kuwahubiria ndugu watano wa yule Tajiri, ijapokuwa yule Tajiri alimsihi sana baba Ibrahimu amtume Lazaro, lakini haikuwezekana…

Lakini tukirudi nyuma katika 1Samweli 28:12-14….. tunasoma kuwa iliwezekana kumrudisha nabii Samweli aliyekuwa amekufa na kusema na Mfame Sauli ambaye alikuwa anaishi..je hii imekaaje, na ili hali tunajua Ibrahimu alikuwepo kabla hata ya Samweli na Sauli?.


Jibu: Awali turejee habari ya maskini Lazaro na Tajiri.

Luka 16:27 “Akasema, Basi, baba, nakuomba, umtume nyumbani kwa baba yangu,

28 kwa kuwa ninao ndugu watano, ili awashuhudie, wasije wao pia wakafika mahali hapa pa mateso.

29 Ibrahimu akasema, Wanao Musa na manabii; na wawasikilize wao.

30 Akasema, La, baba Ibrahimu, lakini kama akiwaendea mtu atokaye kwa wafu, watatubu.

31 Akamwambia, Wasipowasikia Musa na manabii, hawatashawishwa hata mtu akifufuka katika wafu”

Hapa biblia inaonyesha kuwa ni kweli haikuwezekana Lazaro kutumwa duniani na kusema na ndugu watano wa yule Tajiri…

Lakini tusome tena ile habari ya nabii Samweli na Sauli alipokwenda kwa yule mwanamke mwenye pepo la utambuzi.

1 Samweli 28:12 “Hata yule mwanamke alipomwona Samweli alilia kwa sauti kuu; na yule mwanamke akamwambia Sauli, akasema, Mbona umenidanganya? Kwa kuwa wewe ndiwe Sauli.

13 Mfalme akamwambia Usiogope; waona nini? Yule mwanamke akamwambia Sauli, Naona mungu anatoka katika nchi.

14 Naye akamwuliza, Ni mfano wa nini? Akajibu, Ni mzee anazuka; naye amefunikwa vazi. Basi Sauli akatambua ya kwamba ndiye Samweli mwenyewe, akainama uso wake mpaka nchi, akasujudia

15 Ndipo Samweli akamwambia Sauli, Mbona umenitaabisha mimi, hata kunipandisha juu? Sauli akajibu, Mimi nimetaabika sana; kwa kuwa hao Wafilisti wananifanyia vita, naye Mungu ameniacha; hanijibu tena, wala kwa manabii, wala kwa ndoto; kwa hiyo nimekuita wewe, ili wewe unijulishe nifanyeje”

Hapa tunaona Samweli aliyekufa akipandishwa juu, sasa swali la msingi ni hili; ingewezekanikaje jambo hilo na ilihali ile habari ya Lazaro na Maskini inakataa uwezekano wa jambo hilo?..je biblia inajichanganya?

Jibu ni la! biblia haijichanganyi, kwani maneno yake yote yamethibitika na wala haijakosewa mahali popote..

Sasa iliwezekanikaje nabii Samweli kuzungumza na Sauli aliye hai na ishindikane kwa Lazaro kurudi kuwahubiria walio hai?.

Fumbo lipo kwa huyo mwanamke mwenye pepo, alichokifanya mwanamke mwenye pepo si kumfufua nabii Samweli na kumrudisha juu, hiko kitu kisingewezekana….alichokifanya mwanamke mwenye pepo ni kuwasiliana na wafu.. na kutoa taarifa za wafu na kuwapa walio hai.

Hivyo Sauli hakumwona Samweli kwa macho, ndio maana alimwuliza yule mwanamke; anayezuka anaonekanaje na yule mwanamke akamtajia kuwa ni mzee mwenye mvi, ikimaanisha kuwa Sauli hakuwa anamwona Samweli, bali alikuwa anasubiria taarifa kutoka kwa yule mwanamke.

Kwahiyo kilichokuwa kinaendelea pale ni kwamba Sauli alikuwa anaongea na Samweli kupitia kinywa cha yule mwanamke, (kama tu vile mtu anavyoongea na roho za mapepo, kupitia kinywa cha yule aliyepagawa na pepo).

Lakini katika ile habari ya Luka, yule Tajiri alitaka Lazaro atoke kule kwa wafu (yaani afufuke) arudi katika mwili aseme na walio hai, jambo ambalo lisingewezekana..

Sasa utauliza je mpaka leo inawezekana mtu kuwasiliana na wafu kama huyu mwanamke mwenye pepo alivyofanya?.

Jibu ni La! Baada ya Bwana YESU kufufuka alizitwaa funguo za mauti na kuzimu, na kuwamiki wote walio hai na walio kufa, kwahiyo hakuna yoyote hata shetani mwenye uwezo wa kuwasiliana na mfu, au kutoa habari za wafu.

Mwenye uwezo huo ni BWANA YESU PEKE YAKE!!.

Mapepo yanaweza kujigeuza na kuchukua sauti na umbile la mtu aliyekufa na kuigiza kama yule mtu, na kuwatokea watu yakidai ni watu halisi waliokufa… yanaweza kufanya hivyo kwani maandiko yanathibitisha hilo.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba Nabii Samweli hakumtokea Sauli na kusema naye, bali alizungumza naye kupitia kinywa cha yule mwanamke mwenye pepo, na jambo hilo kwasasa haliwezekani tena kwani Kristo ndiye mwenye funguo hizo peke yake.

Kwa urefu kuhusiana na roho za waliokufa na mizimu fungua hapa 》》》Mizimu ni nini?

Bwana akubariki…

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments