JE UTAKATIFU NI MATENDO YA SHERIA?

JE UTAKATIFU NI MATENDO YA SHERIA?

Ipo elimu kwamba kuishi maisha ya utakatifu ni kuishi kwa sheria, na biblia inafundisha kuwa “hatuishi chini ya sheria bali tunaishi chini ya Neema” na tunahesabiwa haki bure kwa imani si kwa matendo.

Dhana hii inazidi kwenda mbali  kwa kusisitiza kuwa maisha ya utakatifu ni ngumu kuishi, na ni vigumu kuishi maisha hayo kwasababu ni  sawa na kujifunga kwa sheria.

Ndugu kama na wewe ni mmoja ya watu wanaoamini hivi kwamba…“utakatifu ni kifungo kigumu cha sheria”…bali leo soma ujumbe huu mpaka mwisho, utapata kuelewa jambo.

Hebu tafakari mfano huu:

》 Upo jikoni unaandaa chakula kwa bahati mbaya ukagusa sufuria ya moto, bila shaka kitakachofuata baada ya hapo, ni wewe kutoa mkono wako sehemu hiyo ya moto kwa haraka sana..

》Au labda umeketi mahali na ghafla ukaona kuna kitu/uchafu unakaribia macho yako, ni wazi kuwa utafumba macho ghafla na kwa kasi.

》Au linapotokea jambo la kushtusha na mapigo ya moyo kuongezeka kasi na mwili kutetemeka

Sasa matendo hayo yote ya kuondoa mkono kwa kasi kutoka kwenye sufuria yenye moto na kufumba macho ghafla pale hatari inapoyakaribia macho yako, na mapigo ya moyo kuongezeka kasi, na mwili kutetemeka huwezi kusema ni matendo ya sheria uliyojiwekea wewe yanayokuongoza…

La! bali ni sheria mwili uliojiwekea isiyohusisha hiari yako wala maamuzi yako, unajikuta tu unafanya hayo matendo bila kupenda au kuamua au hata kutafakaro… yaani ni matendo yanayotokana na mwitikio wa mwili kutokana na mazingira ya nje yanayoendelea.

Na Lengo ni kuulinda mwili wako usidhurike au usiendelee kudhurika..

Hali kadhalika matendo ya utakatifu ni mwitikio wa nje wa imani iliyopo ndani ya mtu na si matendo ya sheria..

Mtu aliyeipokea imani kweli kweli na kubatizwa na Roho Mtakatifu, anajikuta tu kuna mambo anayafanya pasipo hiari yake.

Anapokaribia mazingira ya dhambi amani inatoweka yenyewe pasipo yeye kuamua na hivyo anayaepuka hayo mazingira haraka sana.

Akisikia masengenyo ni kama vile mtu aliyeketi kwenye mazingira ya takataka na akapata kichefuchefu katika mazingira yale, kile kichefuchefu hakupanga wala kuamia kije, bali kinakuja chenyewe tu, ili utoke katika yale mazingira, ni kwa namna hiyo hiyo mazingira ya usengenyaji, au mazungumzo mabaya ni kichefuchefu kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili kweli kweli.

Na hilo sio jambo linalompa shida sana kulitekeleza, bali linatoka tu lenyewe ndani, dunia nzima inaweza kumwona kama hayupo sawa kiakili au yupo kwenye utumwa mzito wa sheria alizojiwekea, lakini kumbe ni kinyume chake, mambo anayoyafanya yanabubujika yenyewe ndani yake na si sheria alizojiwekea.

Kwahiyo kwa hitimisho ni kwamba. Matendo ya utakatifu si sheria bali ni matendo yanayotendeka ndani ya mtu pasipo sheria, hata kama yanaonekana kama yamekaa kisheria, na hayo ni mambo ya rohoni yanayotambulika na watu wa rohoni kama maandiko yanavyosema..

1 Wakorintho 2:14 “Basi mwanadamu wa tabia ya asili hayapokei mambo ya Roho wa Mungu; maana kwake huyo ni upuzi, wala hawezi kuyafahamu, kwa kuwa yatambulikana kwa jinsi ya rohoni.

15 Lakini mtu wa rohoni huyatambua yote, wala yeye hatambuliwi na mtu”.

Mtu kamwe hawezi kuuishi utakatifu kama hatakuwa na ujazo wa Roho Mtakatifu..

Na hiyo inahitaji Maamuzi mazito, yaani kumwamini Bwana YESU, kutubu dhambi na kubatizwa kwa maji mengi na kwa Roho Mtakatifu.

Kwahiyo kama utaamua kufanya mageuzi ya kweli kweli ya kuamua kumfuata YESU kwa kutubu dhambi kabisa na kujikana nafsi na kujitwika msalaba wako na kumfuata na kujazwa Roho Mtakatifu, nakuhakikishia suala la kuutimiza utakatifu kwako halitakuwa sheria bali mwitikio wa hiari.

Hutakuwa unakunywa pombe kwasababu imeandikwa usilewe, bali utakuwa hunywi pombe kwasababu hiyo kiu wala shauku itakuwa haipo ndani yako.

Hutazini kwasababu maandiko yamesema usizini, bali hutazini kwasababu hiyo kiu au msukumo utakuwa haupo ndani yako

Hutasengenya kwasababu maandiko yanasema usisengenye bali hutasengenya kwasababu mazingira hayo kwako ni kichefuchefu.n.k

Sababu kubwa uminayomfanya mtu asipokee hii nguvu ya kuishi maisha masafi?..ni jinsi alivyopokea na alivyoamini.

Kama mtu ameamini au ameaminishwa kuwa hawezi kuishi maisha ya utakatifu duniani, na pia ukienda kwa YESU hakuna haja ya kujitoa wote (kujikana nafsi)..hapo ndipo tatizo linapoanzia..

Utatakaje matunda ya mtu na bado humtaki yule mtu,..utatakaje matunda ya Roho Mtakatifu na bado humtaki YESU??..Unampa asilimia moja ya maisha yako na asilimia nyingine 99 ipo kwa ibilisi na ulimwengu!…hapo kwanini matendo ya utakatifu yasiwe sheria ngumu kwako??.

Jikane nafsi, (hilo jambo usilikwepe)..Dhamiria kumfuata YESU kwa moyo wako wote…. Ingia gharama kubwa kuacha vingi katika maisha yako, jitoe wote halafu uone nguvu itakayoingia ndani yako.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

CHAGUA UTAKATIFU MWAKA HUU.

IFAHAMU NGUVU YA MAOMBI (Sehemu ya pili)

Wabadili fedha ni watu gani kwenye biblia? (Mathayo 21:21)

MGAWANYIKO WA ISHARA ZA UJIO WA BWANA YESU KRISTO.

Kwa mpotovu utajionyesha kuwa mkaidi, maana yake nini? (Zab.18:26)

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments