Swali: Je Mungu ni mkaidi kulingana na Zaburi 18:26, au kwanini Mungu aseme maneno hayo?
Jibu: Tuanzie kusoma ule mstari wa 24, ili tupate maana kamili..
Zaburi 18:24 “Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
25 Kwa mtu mwenye fadhili UTAKUWA MWENYE FADHILI; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;
26 KWAKE AJITAKASAYE UTAJIONYESHA KUWA MTAKATIFU; Na KWA MPOTOVU UTAJIONYESHA KUWA MKAIDI”
Hapo anasema kwa mtu mwenye fadhili Bwana atajionyesha mwenye fadhili kwake, na kwa ajitakasaye Bwana atajionyesha ni mtakatifu kwake, vile vile na kwa mpotovu atajionyesha mkaidi.
Sasa kwa maneno hayo haimaanishi kuwa Bwana ni MKAIDI..La! yeye ni mwema siku zote na hawezi kufananishwa na sisi wanadamu…Lakini sasa swali ni kwanini aseme hivyo?
Ili tuelewe vizuri tafakari mfano huu; Unaye mtoto halafu ukaanza kuona anaonyesha tabia za kukosa nidhamu, na anafanya mabaya mengi, na ulipomwonya haonyeki, kisha ukaamua kumwambia kuwa endapo akiendelea kuwa na tabia hiyo, utakuwa mbaya kwake!..na akibadilika kuwa mzuri basi utakuwa mzuri kwake…
Je kwa kauli hiyo utakuwa umemaanisha kuwa wewe ni ni MTU MBAYA na MWOVU?.. bila shaka hutakuwa umemaanisha hivyo, bali utakuwa umemaanisha kuwa endapo akiendelea kufanya mabaya, basi utambadilikia na kumwadhibu, jambo ambalo ni baya machoni pa huyo mtoto, na ndicho Bwana Mungu alichomaanisha hapo kuwa kwa “mtu mpotovu atajionyesha kuwa Mkaidi”… Na si kwamba MUNGU ni Mkaidi.
Kwamba kwa mtu anayefanya mabaya Bwana na maovu na hakubali kuonyeka basi atapata mabaya kutoka kwa Mungu, kwani BWANA atamwadhibu,…Na adhabu za Bwana ni za lengo la kuonya, na kumfanya mtu aache njia mbaya, na si za kumpoteza mtu.
Waebrania 12:10 “Maana ni hakika, hao kwa siku chache waliturudi kama walivyoona vema wenyewe; bali yeye kwa faida yetu, ili tuushiriki utakatifu wake.
11 Kila adhabu wakati wake haionekani kuwa kitu cha furaha, bali cha huzuni; lakini baadaye huwaletea wao waliozoezwa nayo matunda ya haki yenye amani.
12 Kwa hiyo inyosheni mikono iliyolegea na magoti yaliyopooza,
13 mkaifanyie miguu yenu njia za kunyoka, ili kitu kilicho kiwete kisipotoshwe, bali afadhali kiponywe.
14 Tafuteni kwa bidii kuwa na amani na watu wote, na huo utakatifu, ambao hapana mtu atakayemwona Bwana asipokuwa nao”
Na kinyume chake ni kweli, kwa mtu ajitakasaye, yeye Bwana atajionyesha mtakatifu kwake, Maana yake ataona mema mengi kutoka kwa Bwana..
Hivyo hiyo ni tahadhari kwetu na pia ni faraja kwetu, kwamba tukae katika usafi na utakatifu, ili tuuone wema wa Mungu, na tusikae katika upotovu, tusije tukauona ukaidi wa MUNGU, kwani Bwana atajionyesha kwa kila mtu sawasawasa na matendo yake.
Zaburi 18:24 “Mradi Bwana amenilipa sawasawa na haki yangu, Sawasawa na usafi wa mikono yangu mbele zake.
25 Kwa mtu mwenye fadhili UTAKUWA MWENYE FADHILI; Kwa mkamilifu utajionyesha kuwa mkamilifu;
26 KWAKE AJITAKASAYE UTAJIONYESHA KUWA MTAKATIFU; Na KWA MPOTOVU UTAJIONYESHA KUWA MKAIDI”
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Kama ulimwengu ujao utakuwa na watakatifu tu, sasa hao watakaotawaliwa watatoka wapi?
TULITAFUTE KWA BIDII TUNDA LA ROHO.
Mwandishi na Uchambuzi wa kitabu cha Wakorintho wa pili (2Wakorintho)
About the author