Nakusalimu katika jina la mwokozi wetu Yesu Kristo. Karibu tuzidi kuyatafakari maneno ya uzima.
Je! Unahabari kuwa watakaonyakuliwa wameshaanza kuandaliwa? Je! Wewe upo katika hatua ipi?
Biblia inasema zipo hatua ambazo Bwana atatumia kushuka kabla haijaja siku ile yenyewe ya sisi kutwaliwa kwenda mbinguni. Hivyo haitakuwa tendo la kushtukiza kwa wale ambao tayari yameshaingizwa katika hatua hizo.
Angalia ni nini Bwana anasema hapa..
1Wathesalonike 4:16 “Kwa sababu Bwana mwenyewe atashuka kutoka mbinguni pamoja na MWALIKO, na SAUTI YA MALAIKA MKUU, na PARAPANDA YA MUNGU; nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. 17 Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu, ili tumlaki Bwana hewani; na hivyo tutakuwa pamoja na Bwana milele. 18 Basi, farijianeni kwa maneno hayo.”
Tafakari kwa makini hayo maneno, Bwana hasemi atashuka na “Parapanda” nao waliokufa katika Kristo watafufuliwa kwanza. Kisha sisi tulio hai, tuliosalia, tutanyakuliwa pamoja nao katika mawingu. Hapana Bali anasema, ataanza kwanza na MWALIKO, kisha SAUTI YA MALAIKA MKUU na ndipo Parapanda ya Mungu mwisho. Tofauti na sisi tunavyofikiri, kuwa ni parapanda tu ndio tutakaoisikia ndipo tunyakuliwe.
Ndugu, tafsiri ya hayo maandiko ni kuwa huwezi kuisikia parapanda ya Mungu, kama hujaitikia hatua ya mwaliko na hatua ya sauti ya malaika mkuu. Hivyo Embu tukautazame huo mwaliko ni upi na hiyo sauti ya malaika mkuu ni ipi?
Awali ya yote tukumbuke kuwa lengo la kunyakuliwa sisi ni ili kwenda kula karamu ya arusi ya mwanakondoo mbinguni, aliyoiandaa Yesu Kristo kwa ajili yetu, kama alivyosema katika Yohana 14:1-4 na Ufunuo 19:9. Hivyo kama tunavyojua hakuna sherehe yoyote isiyokuwa na mwaliko. Hakuna mtu anayejikuta tu kwenye arusi ya mtu bila kualikwa, hakujawahi kuwa na utaratibu huo. Na ndivyo Yesu naye, kabla ya kutupelekea huko mbinguni alipotuandalia vinono, ni sharti kwanza atualike. Hapo ndipo akatumia mfano mmoja wa Mfalme aliyemfanyia mtoto wake karamu kubwa. Lakini katika kuwaalika watu wake, kukawa na mwitikio tofauti tofauti,
Embu tuisome habari hiyo tupate kuielewa vizuri; (Soma kwa utulivu) kwasababu hapa ndipo palipo na msingi.
Mathayo 22:1 “Yesu akajibu, akawaambia tena kwa mithali, akisema, 2 Ufalme wa mbinguni umefanana na mfalme mmoja aliyemfanyia mwanawe arusi.
3 Akawatuma watumwa wake wawaite walioalikwa kuja arusini; nao wakakataa kuja.
4 Akatuma tena watu kwa wengine, akisema, Waambieni wale walioalikwa, Tazameni, nimeandaa karamu yangu; ng’ombe zangu na vinono vimekwisha kuchinjwa, na vyote vimekuwa tayari, njoni arusini.
5 Lakini hawakujali, wakaenda zao, mmoja shambani kwake, mmoja kwenye biashara yake;
6 nao waliosalia wakawakamata watumwa wake, wakawatenda jeuri, na kuwaua.
7 Basi yule mfalme akaghadhibika; akapeleka majeshi yake, akawaangamiza wauaji wale, akauteketeza mji wao.
8 Kisha akawaambia watumwa wake, Arusi i tayari, lakini wale walioalikwa hawakustahili.
9 Basi enendeni hata njia panda za barabara, na wote mwaonao waiteni arusini.
10 Watumwa wale wakatoka wakaenda njia kuu, wakakusanya wote waliowaona, waovu kwa wema; arusi ikajaa wageni.
11 Lakini alipoingia yule mfalme ili kuwatazama wageni wake, akaona mle mtu mmoja asiyevaa vazi la arusi.
12 Akamwambia, Rafiki, uliingiaje humu nawe huna vazi la arusi? Naye akatekewa.
13 Mfalme akawaambia watumishi, Mfungeni mikono na miguu, mchukueni mkamtupe katika giza la nje; ndiko kutakuwako kilio na kusaga meno.
14 Kwa maana waitwao ni wengi, bali wateule ni wachache.
Ukitafakari hapo, utajiuliza, iweje mfalme akualike kwenye sherehe yake halafu usiende?..Ni heri angekuwa mtu wa kawaida, lakini walioalikwa hawakulijali hilo, kwamba yule ni mfalme na sio mtu wa kawaida, hawana budi kuahirisha shughuli zao waende, kwani wamepewa heshima kubwa, lakini kwao mambo yalikuwa tofauti, wakapuuzia na kibaya zaidi wakawapiga na kuwaua baadhi ya watumwa wake.
Sasa hawa wanalinganishwa na wayahudi, ambao ndio waliokuwa wa kwanza kupewa mwaliko huu ya injili, lakini waliwaangamiza, manabii wengi wa Mungu, mpaka ikafikia hatua ya Kristo akawakataa kabisa, akawakatilia mbali (Soma Mathayo 23:37-39). Hivyo Mungu akahamishia mpango wake wa wokovu kwa watu wa mataifa, ambao ndio mimi na wewe.
Ambao tunalinganishwa sasa na hao waovu, na vilema, waliookotwa huko mabarabarani wakaalikwa kwenye karamu. Maandiko yanatuambia kundi hilo halikukataa mwaliko kama lile la kwanza. Bali lilikubali lote, Lakini sasa ndani ya ukumbi, akaonekana mmoja ambaye alikuwa tofauti na wenzake, yeye hakuwa na “vazi la arusi”. Utajiuliza ni kwanini akose vazi lile? Ni kwanini asifanane na wenzake? Utagundua kuna jambo alilipuuzia, ambalo angepaswa alifanye kabla ili akidhi vigezo vya yeye kuila karamu.
Sasa kabla hatujatazama vazi hilo ni nini? Maana ya mfano huo ni mwaliko wa wokovu ambao tunahubiriwa sisi sote. Ukweli ni kwamba leo hii lipo japo kubwa la watu katika kanisa “wanaokiri wokovu”, wengi wao wamebatizwa, wanashiriki ibada kama kawaida kanisani, wanatoa zaka, wote wanakiri kuwa wanamsubiria Yesu aje kuwanyakua. Lakini je! Ni wote watakaonyakuliwa? La! Bwana anasema..Siku ile Mmoja atanyakuliwa mmoja ataachwa!(Mathayo 24:40-41) .. Maana yake ni kwamba hupaswi kuridhika tu kuitwa mkristo, lipo jambo la ziada unapaswa ufanye ili ukidhi vigezo vya kuiila karamu ya mwanakondoo mbinguni. Usiridhike tu kusema mimi ni mshirika, mimi ni muumini, acha kabisa hayo mawazo, katika siku hizi za mwisho tunazoishi, yule mtu aliketi kabisa ukumbini, akaona vinono vyote lakini hakula hata kimoja..Sasa embu tuitazame hatua ya pili,
Bwana anasema atashuka na..”Sauti ya malaika mkuu”. Maana yake ni kwamba kabla ya kuisikia parapanda, ni sharti uisikie hii sauti ya malaika mkuu. Tukirudi katika hiyo habari, ni kwamba yule mtu ambaye hakuwa na mavazi ya arusi, hakuisikia/aliipuzia sauti ya mjumbe aliyesimama pale mlangoni kuwapa maelekezo ya namna ya kukubaliwa katika karamu. Wakati wenzake wanamsikiliza, walipoambiwa wakaoge, wabadili mavazi yao ya kihuni, ya ki-utupu, ya ki-zinzi, ya ki-dunia. Wavae mavazi meupe ya sherehe, yeye akaona ule ni mzigo mzito sana, anamnyima uhuru wake, akataka kwenda kipekee pekee na staili zake, maadamu ameshapewa heshima ya kualikwa na mfalme. Hawezi kuzuiliwa. Hivyo akaendelea kustarehe vilevile pale ukumbini, akimsubiria mfalme, kuja kuwapongeza wageni wake waliomtii. Lakini alipofika kwake, akidhani, sasa ni wakati wa kupongezwa, akashangaa amebadilikiwa uso, badala ya kupongezwa, ndio kwanza anafungwa Kamba kama vile vibaka, kisha anatupwa nje!
Unajua ni kwanini mpaka biblia inasema ndipo kutakuwa na kilio na kusaga meno, maana yake ni kuwa huyu mtu ambaye alikuwa ameshaweka mawazo yake katika kusheherekea, ghafla anajikuta yupo nje, ni wazi kuwa yeye ndio atakayeumia Zaidi kuliko wale ambao hawakuwahi kualikwa kabisa.
Hivyo kundi hili linafananishwa na watu wote, wanaoitwa wakristo walio kanisani, lakini hawana mavazi ya arusi. Na vazi la Arusi ni UTAKATIFU. Maandiko yanasema hivyo.
Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.
8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; kwa maana kitani nzuri hiyo ni MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU.
9 Naye akaniambia, Andika, Heri walioalikwa karamu ya arusi ya Mwana-Kondoo. Akaniambia, Maneno haya ni maneno ya kweli ya Mungu.
Ndio maana malaika wa kanisani letu la Mwisho lijulikanalo kama Laodikia. Alipewa ujumbe, unaotuhusu sisi. Ambao hautaki tuwe vuguvugu. Kwasababu tukiwa vuguvugu tutatapikwa. Kumbuka kila kipindi cha Kanisa kilikuwa na malaika wake, mtoa ujumbe, na huyo malaika, alisema kigezo cha kila mmojawao kukubaliwa na Kristo. Tangu kanisa la kwanza, hadi sasa tupo kanisa la mwisho la saba, lijulikanalo kama Laodikia.
Huyo ndio malaika wetu mkuu, ambaye kaachiliwa kutushushia ujumbe huo, hatuna budi kuisikia sauti yake. Kwamba tuwe moto tusiwe vuguvugu, vilevile tununue mavazi meupe, kwa Kristo. Yaani tuishi maisha matakatifu wasiokuwa na madoa, ili tukidhi vigezo vya kunyakuliwa kwasababu tukikosa maisha hayo, kamwe tusijidanganye sisi ni wakristo.
Tuusome ujumbe wetu;
Ufunuo 3:14 “Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto. 16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, NA MAVAZI MEUPE UPATE KUVAA, AIBU YA UCHI WAKO ISIONEKANE, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami.
21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi.
22 Yeye aliye na sikio, na alisikie neno hili ambalo Roho ayaambia makanisa”
Hivyo wewe kama mkristo, Epuka maisha ya uvuguvugu. Sababu ya wale wanawali watano wapumbavu kutoingia karamuni, ilikuwa ni hiyo hiyo ya uvuguvugu, hawana mafuta ya kutosha kuziwasha taa zao (Mathayo 25). Mungu anajua tabia ya kanisa la sasa, halipendi kukemewa dhambi linapenda mwonekano wa nje tu, lakini ndani ya uchafu. Bwana atusaidie roho hii isituvae.
Sasa ukishakidhi vigezo hivyo, maana yake unakuwa umepita kigezo cha “walioitwa” mpaka kuwa “mteule”. Unachongoja wewe ni unyakuo tu, parapanda itakapolia, utapaa mawinguni, na hata ukifa kabla Yesu hajarudi, utafufuliwa siku ile, kwasababu ulitii mwaliko na Sauti ya Malaika wako mkuu.
Lakini ukifa katika ukristo vuguvugu, kisha ukafa leo, siku ile ya unyakuo hutafufuliwa na watakatifu wengine, utaendelea kubaki makaburini mpaka siku ya hukumu. Ndugu, unasubiri nini, usiokoke? Na ikiwa umeokoka, maisha ya uvuguvugu utaendelea nayo mpaka lini? Leo upo kanisani, kesho disco, leo unamsifu Mungu, kesho unasikiliza nyimbo za kidunia, leo unatoa sadaka, kesho unakula rushwa, hayo maisha yatakufikisha wapi? Hujui kuwa tunaishi katika kizazi ambacho yamkini kinaweza shuhudia tukio la Unyakuo, kutokana na kutimia kwa dalili zote za siku za mwisho?
Embu tubu sasa umaanishe kumfuata Yesu, mambo aliyotuandalia Yesu ni mazuri yasiyoelekeza, mambo ambayo jicho haliwahi kuona wala sikio kusikia. Tusiyakose hayo. Kosa kila kitu, Usikose Unyakuo. Ikiwa upo tayari kutubu leo dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha.
Wasiliana nasi kwa namba hizi bure +255693036618/ +255789001312, tukupe mwongozo wa sala ya toba.. Fanya uamuzi wa haraka sasa, kwani kesho si yao.
Shalom.
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na kundi letu la mafundisho ya Biblia whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
KWANINI KUWE NA UTAWALA WA MIAKA 1000
MAPIGO YA VITASA SABA, NA SIKU YA BWANA.
Kutekewa maana yake nini?(Mathayo 22:12)
Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza
About the author