JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

JE! UMEYABATILISHA MAMBO YA KITOTO?

1Wakoritho 13: 11 “Nilipokuwa mtoto mchanga, nalisema kama mtoto mchanga, nalifahamu kama mtoto mchanga, nalifikiri kama mtoto mchanga; tokea hapo nilipokuwa mtu mzima, nimeyabatilisha mambo ya kitoto”.
 
Katika maisha ya kawaida, mwanadamu ni lazima apitie katika hatua hizi mbili; UTOTO na UTU UZIMA. Na kila hatua ni lazima iwe na uongozi juu yake, Kwamfano mtoto mdogo hawezi kujiongoza mwenyewe kwasababu akili yake haijakomaa kuweza kutambua jema na baya au kupambanua kanuni za maisha hivyo ni lazima aandaliwe na mzazi wake au mlezi wake kanuni fulani za kufuata aidha apende au asipende kwake huyo zinakuwa ni sheria na amri, na ndio maana tunaweza kuona mtoto anapofikisha umri fulani labda miaka 6/7, anapelekewa shule sio kwa mapenzi yake, hapana, pia analazimishwa kuamshwa asubuhi kila siku ili aende shule na tunafahamu hakuna mtoto anayependa kuamshwa asubuhi apige mswaki na kwenda shule, yeye atatamani tu acheze cheze na kurukaruka,
 
Kadhalika akirudi baadaye nyumbani, atalazamishwa alale mchana, atalazimishwa aoge, atalazimishwa afanye homework,atachaguliwa nguo za kuvaa, na wakati mwingine atachaguliwa mpaka na marafiki wa kucheza naye, n.k. Hivi vyote atafanya tu hata kama hataki, na wakati mwingine akikosea mojawapo ya hizo kanuni alizowekewa itamgharimu adhabu. Hivyo ukichunguza kwa undani utaona kuwa sio kwamba Yule mtoto anatimiza zile sheria kwa kupenda la! Bali anafanya vile kwa kutimiza tu matakwa ya baba / mama yake basi, laiti angepewa uhuru kidogo tu! Asingedhubutu kufanya mojawapo ya hayo, angeenda kufanya mambo yake mengi kuzurura zurura tu.
 
TABIA YA MTU MZIMA.
 
Lakini Yule mtoto atakapokuwa mtu mzima kidogo kidogo mabadiliko yataanza kutokea ndani yake, ataanza kuona umuhimu wa yeye kuamka asubuhi na mapema na kupiga mswaki mwenyewe, na umuhimu wa kwenda shule , ataona umuhimu wa kuoga, ataona umuhimu wa kuwa na marafiki wazuri, n.k. Lakini ni kwasababu gani anafanya hivyo?. Ni kwasababu ameshakuwa mtu mzima na anajua kufanya hivyo ni kwa faida yake mwenyewe na sio kwa faida ya mzazi. Na hiyo ndiyo dalili kubwa ya kuonyesha kuwa mtu huyo amekuwa. Kwasababu ile sheria na maagizo aliyopewa na wazazi wake sasa anayatimiza mwenyewe ndani ya moyo wake pasipo kushurutishwa. Na ndipo mzazi anapoona sababu ya kumwamini na kumwacha huru kabisa kabisa ayaongoze maisha yake mwenyewe.
 
Mfano mwingine tunaweza tukajifunza kwa mwanafunzi: alipokuwa shule ya msingi ni tofauti na atakapokuwa chuo kikuu, kule nyuma alikuwa analazimishwa kuwepo shule kila siku alfajiri, ahudhurie kila kipindi cha darasani, alilazimshwa avae sare, alichapwa alipokosea, alikaguliwa notes alizoandika n.k.. Lakini alipofika chuo hakuna tena sheria ya kumwambia aamke alfajiri kila siku aende chuo, ni kwasababu gani? Ni kwasababu chuo kinatambua kwamba Yule mtu anajielewa, hivyo hata asipohudhuria leo atakuwa na sababu za msingi za kutokufanya hivyo tofauti na alipokuwa shule ya msingi, mfano angepewa uhuru tu! Angeutumia katika michezo na utoro, kadhalika pia akiwa chuo hapewi sare, hashikiwi kiboko kulazimishwa kusoma, hakaguliwi notes n.k. lakini japokuwa hakuna sheria zote hizo, mwisho wa siku utakuta Yule mwanafunzi anafaulu. Unaona hapo? hayo yote haimaanishi kuwa chuo hakikuwa na sheria hapana, kilikuwa nayo sana tu, bali kimemweka huru mbali na ile sheria kwasababu kilitambua aliyefika chuo ameshajitambua vya kutosha na anajua jukumu lake kama mwanafunzi.
 
Kadhalika na katika KANISA LA MUNGU nalo pia limepitia katika hatua zote mbili: UTOTO na UTU UZIMA. Hatua ya utoto ni pale Mungu alipolizaa kanisa kwa mara ya kwanza kule jangwani, hivyo kama lilikuwa ni changa ni dhahiri kuwa lingehitaji kupewa sheria ya kuliongoza kwasababu halijaweza bado kupambanua mema na mabaya. Na ndio tunaona sheria/ Torati ilikuja na zile amri zote kutolewa kwa mkono wa Musa na kupewa watu, kwamba waishi katika hizo. Na kama tunavyojua sheria kwa mtoto inakuwa ni AMRI na sio OMBI, kadhalika na hawa nao (kanisa-jangwani waisraeli) ilikuwa ni AMRI kuzitimiza sheria za Mungu zilizotolewa, ndio maana ilikuwa ni amri mtu asiibe, asizini, asiue, aishike sabato, asiabudu sanamu n.k.na kwa yeyote asiyefanya aliadhibiwa vikali. Na kwasababu walikuwa ni watoto walifanya vile kwaajili ya kumridhisha tu baba yao (MUNGU), Walitimiza zile sheria sio kwasababu wanapenda hapana, ni kwasababu baba yao hapendi dhambi, laiti wangeachiwa uhuru kidogo wasingezishika.
 
Lakini ulipofika wakati wa KANISA LA MUNGU KUKUA, Ilipasa zile sheria ziingizwe ndani ya moyo wa kanisa ili zitimizwe kwa mapenzi ya mtu mwenyewe na sio mapenzi ya Mungu na bila shuruti. Kama biblia ilivyotabiri zamani za manabii tukisoma.
 
Yeremia 31: 31 “Angalia, siku zinakuja, asema Bwana, nitakapofanya agano jipya na nyumba ya Israeli, na nyumba ya Yuda.
32 Si kwa mfano wa agano lile nililolifanya na baba zao, katika siku ile nilipowashika mkono, ili kuwatoa katika nchi ya Misri; ambalo agano langu hilo walilivunja, ingawa nalikuwa mume kwao, asema Bwana.
33 Bali agano hili ndilo nitakalofanya na nyumba ya Israeli, baada ya siku zile, asema Bwana; NITATIA SHERIA YANGU NDANI YAO, NA KATIKA MIOYO YAO NITAIANDIKA; nami nitakuwa Mungu wao, nao watakuwa watu wangu.
34 Wala hawatamfundisha kila mtu jirani yake, na kila mtu ndugu yake, wakisema, Mjue Bwana; kwa maana watanijua wote, tangu mtu aliye mdogo miongoni mwao hata aliye mkubwa miongoni mwao, asema Bwana; maana nitausamehe uovu wao, wala dhambi yao sitaikumbuka tena”.
 
Jambo hili lilikuja kutimia siku ya PENTEKOSTE, pale ROHO wa Mungu alipomiminwa juu ya mioyo ya watu kwa mara ya kwanza na kuwafanya wavuke daraja la utoto na kuingia katika daraja la UTU UZIMA. Sasa kuanzia huo wakati Roho alipomshukia mtu, kitu cha kwanza alichokuwa anafanya ni kuiingiza ile sheria ndani ya moyo wake, kiasi kwamba Yule mtu ile sheria anakuwa anaitimiza kwa mapenzi yake mwenyewe na sio kwa mapenzi ya Mungu. Kama vile mwanafunzi aliyeko chuo anasoma kwa mapenzi yake na sio kwa mapenzi ya Baba yake au mama yake tofauti na alivyokuwa akifanya shule ya msingi. Hicho ndicho alichokifanya Roho Mtakatifu siku ya Pentekoste. Na ndio anachoendelea kukifanya mpaka sasa hivi.
 
Sasa kuanzia ule wakati wote walioshukiwa na Roho wa Mungu, wakawa hawazini, sio kwasababu Mungu kawakataza bali ni kwasababu waliona ni kwa faida yao wenyewe, wakawa hawaabudu sanamu sio kwasababu Mungu kawakataza hapana bali ni kwasababu wanajua Mungu pekee ndiye anayestahili kuabudiwa, wakawa wanaomba sio kwasababu Mungu kawaagiza lakini kwasababu waliona umuhimu wa kuomba kama Mkristo ili kuepukana na majaribu, hawakuishika sabato kama amri, kwamba tumwabudu Mungu tu katika siku fulani, hapana bali sabato yao ilikuwa kila siku, kwasababu walijua Mungu haabudiwi katika siku Fulani bali katika Roho na Kweli.Kadhalika na zile sheria zote walizopewa walipokuwa wachanga walikuwa wanazitimiza pasipo AMRI bali kwa moyo na kwa uelewa. Kwasababu hiyo basi Mungu akawacha huru kabisa mbali na SHERIA na TORATI. Na ndio maana biblia inasema:
 
Wagalitia 5: 18 “Lakini mkiongozwa na Roho, hampo chini ya sheria”. Na pia inasema…
Warumi 8: 2 “Kwa sababu sheria ya Roho wa uzima ule ulio katika Kristo Yesu imeniacha huru, mbali na sheria ya dhambi na mauti”.
Warumi 8: 4 “ili maagizo ya torati yatimizwe ndani yetu sisi, tusioenenda kwa kufuata mambo ya mwili, bali mambo ya roho”.
 
Kwahiyo unaona hapo? Umuhimu wa kuwa na Roho Mtakatifu?..Ni kukufanya wewe utoke katika hali ya utoto wa kiroho(utumwa) na uingie katika hali ya utu uzima(Uhuru) na hiyo ndiyo neema. Ukiona mtu pale unapomuuliza ni kwanini huzini, au huibi? Na anakwambia ni kwasababu Mungu kanikataza, moja kwa moja unajua huyo bado ni mtoto yupo chini ya Sheria hata kama atajifanya yupo chini ya neema. Ukiona mtu anakwambia mimi nashikilia siku moja ya kuabudia sabato, unajua huyo naye yupo chini ya sheria ya utoto, au mtu akikuambia mimi sivai vimini, sinywi pombe, sivuti sigara kwasababu Mungu kakataza, ujue huyo pia ni mtoto bado hajawekwa huru na sheria ya dhambi, Ukiona mtu anasema mimi siabudu sanamu kwasababu amri ya 2 inasema hivyo, unajua kabisa huyo bado ni mtoto Roho wa Mungu bado hajamfanya kuwa huru nk….
 
Lakini wale wote waliowekwa huru na ROHO, hawataona mzigo wowote kuishi maisha ya utakatifu wataona kutokuzini, kutokuvaa vimini, kutokuweka make-up, kutokuvaa suruali, kutokusengenya, kutoiba, kutokwenda disco, n.k. wataona kuwa hayo ni majukumu yao na ni kwa faida ya Roho zao na sio kwa faida ya Mungu, au sio kwasababu Mungu kawaambia. Watafanya yote yawapasayo kufanya iwe ni Mungu kawaagiza, au hajawaagiza.. Na hiyo ndio DALILI ya mtu kuwa amepokea kweli kweli Roho Mtakatifu…Utakatifu anautimizwa kwa kupenda na sio kwa maagizo Fulani.
 
Warumi 8: 9 “Lakini ikiwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu, ninyi hamwufuati mwili; bali mwaifuata roho. Lakini mtu awaye yote asipokuwa na Roho wa Kristo, huyo si wake”.
 

Hivyo ndugu, na wewe upo katika uchanga au utu uzima?. Umejazwa Roho Mtakatifu au bado unaongozwa na dini?. Tafuta Roho Mtakatifu kumbuka Roho Mtakatifu ndio muhuri wa Mungu (Waefeso 4:30) pasipo huyo hakuna UNYAKUO.

Ubarikiwe sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada Nyinginezo:

JIRANI YAKO NI NANI?

UMUHIMU WA KUISHI MAISHA YAMPENDEZAYO MUNGU SASA.

JIHADHARI NA ROHO ZIDANGANYAZO

JE! SISI NI WAFALME NA MAKUHANI KWA NAMNA GANI?

PETRO ALIAMBIWA NA BWANA YESU UKIONGOKA WAIMARISHE NA NDUGU ZAKO. JE! KUONGOKA MAANA YAKE NINI?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments