Kama tukisoma biblia katika agano la kale, tunaona kuwa mambo yaliyokuwa yanamkasirisha sana Bwana Mungu na kumtia wivu, sio maovu yaliyokuwa yanatendeka katikati ya WATU WA MATAIFA, La! bali ni yale yaliyokuwa yanaendelea katikati ya watu wake (ISRAELI), watu alioingia nao agano. Na ndio maana zile amri 10 zilitolewa kwa wana wa Israeli tu! Na sio kwa watu wa mataifa yote ulimwenguni,.
Hivyo hao ndio watakaohusika na adhabu kwa Mungu endapo watakiuka mojawapo ya amri hizo. Kwa mfano mwanaume aliyemuoa mke wake kamwe hawezi kuona wivu kwa wanawake wengine wasiokuwa wake anapowaona wanafanya ukahaba, lakini akimwona mke wake aliyempenda na kumtolea mahari anafanya hivyo ni lazima aingiwe wivu na hasira na ghadhabu nyingi na ndivyo ilivyo hata kwa Mungu na Israeli.(Yeremia 3:14)
Kuna wakati ulifika maovu yalizidi sana katika nyumba ya Israeli ndipo Mungu akamuonyesha Ezekieli maono ya mambo yaliyokuwa yanaendelea kwa siri katikati ya watu wake. Alionyeshwa watu wakiabudu JUA katika ya nyumba yake, wengine walikuwa wanamlilia TAMUZI,(miungu ya wakaldayo), wengine wanaabudu vinyago kwa siri katika nyumba zao, na makuhani wanavukiza uvumba kwa miungu migeni,(Ezekieli 8:1-18), alionyeshwa dhuluma katika mji na umwagaji damu,na upotoshaji hukumu umejaa, na zaidi sana kulinyanyuka manabii wa uongo waliokuwa wanawatabiria watu amani wakati hamna amani. Yote haya yalimchukiza Mungu sana mpaka kuifikia kilele cha Mungu kuleta hukumu kwa watu wake wote.
Lakini kabla maangamizi hayajaja Mungu huwa anawatenga waovu na wema katikati ya watu wake kwa kuwatia ALAMA..kumbuka hawatengi hao watu katikati ya ulimwengu wote, hapana bali ni katikati ya watu wake(ISRAELI)..watu wa ulimwengu tayari Mungu alishawawekea hukumu yao katika siku ile. Na ndivyo alivyoonyeshwa Ezekieli katika habari hii..Tunasoma.
Ezekieli 9:1-11
“1 Kisha akalia kwa sauti kuu masikioni mwangu, akisema, Waamuru WALE WANAOUSIMAMI MJI wakaribie, kila mmoja na awe na kitu chake CHA KUANGAMIZA mkononi mwake.
2 Na tazama, watu SITA wakaja, wakitokea kwa njia ya lango la juu, lielekealo upande wa kaskazini, kila mmoja ana kitu chake cha kufisha mkononi mwake; na mtu mmoja kati yao amevaa bafta, naye ana kidau cha wino cha mwandishi kiunoni. Wakaingia, wakasimama karibu na madhabahu ya shaba.
3 Na huo utukufu wa Bwana wa Israeli ulikuwa umepanda juu kutoka kwa kerubi, ambaye ulikuwa juu yake, mpaka kizingiti cha nyumba; akamwita mtu yule aliyekuwa amevaa bafta, mwenye kidau cha wino cha mwandishi kiunoni.
4 Bwana akamwambia, Pita kati ya mji, kati ya Yerusalemu, UKATIE ALAMA KATIKA VIPAJI VYA NYUSO VYA WATU WANAOUGUA NA KULIA KWASABABU YA MACHUKIZO YOTE YANAYOFANYIKA KATI YAKE.
5 Na hao wengine aliwaambia, nami nalisikia, Piteni kati ya mji nyuma yake, mkapige; jicho lenu lisiachilie, wala msione huruma;
6 Waueni kabisa, mzee, na kijana, na msichana, na watoto wachanga, na wanawake; lakini msimkaribie mtu ye yote MWENYE HIYO ALAMA; TENA ANZENI KATIKA PATAKATIFU PANGU. Basi, wakaanza kwa wazee waliokuwa mbele ya nyumba.
7 Akawaambia, itieni nyumba unajisi, mkazijaze nyua mizoga ya hao waliouawa; haya, enendeni. Wakaenenda, wakapiga-piga katika mji.
8 Tena ikawa, walipokuwa wakipiga, nami nikiachwa, nalianguka kifudifudi, nikalia, nikasema, Ee Bwana MUNGU! Utaangamiza mabaki yote ya Israeli, wakati wa kumwaga ghadhabu yako juu ya Yerusalemu?
9 Ndipo akaniambia, Uovu wa nyumba ya Israeli na Yuda ni mwingi sana, nayo nchi imejaa damu, nao mji umejaa kupotosha hukumu; MAANA HUSEMA, BWANA AMEIACHA NCHI HII, NAYE BWANA HAONI.
10 Nami, jicho langu halitaachilia, wala sitaona huruma; lakini nitaleta njia yao juu ya vichwa vyao”.
11 Na tazama, mtu yule aliyevaa bafta, mwenye kidau cha wino kiunoni, akaleta habari, akisema, Nimefanya kama ulivyoniamuru.”
Hukumu hii iliyoletwa na hao malaika 6 ilikuja kutimia pale wa-babeli walipokuja kuuteketeza mji na kuwauwa wayahudi vijana, wazee na watoto, na kuiacha nyumba Israeli ukiwa isipokuwa kikundi kidogo sana kilichokuwa kinaugua na kulia juu ya maovu ya Israeli hao tu ndio waliosalimika(Ndio wale waliotiwa Alama katika roho) wengine wote walikufa na kuchukuliwa utumwani. Soma 2Wafalme 25:8-12, Sefania 3:11-13. utaona jambo.
Ndivyo ilivyo hata sasa hivi, Maovu makubwa yanayopelekea hasira ya Mungu kumwaga sio yatokanayo na watu wasiomjua Mungu.Hapana bali ni kwasababu ya maovu yanayoendelea katika nyumba ya Mungu (yaani kanisa), Katikati ya WAKRISTO aliowanunua kwa damu ya thamani nyingi wivu wake ndimo ulimo.
Kumbuka wana wa Israeli walidhani kuwa Mungu haoni waliyokuwa wanayafanya kwa siri, japo aliwapa muda mrefu wa kutubu lakini hawakugeuka mpaka kikombe cha ghadhabu kilipojaa hata kukawa hakuna kusamehewa tena, pale walipotengwa WEMA kati ya WAOVU.
Na katika kanisa la Kristo vivyo hivyo maovu yanayoendelea sasa hivi ni mengi mno vitu kama Siasa, ibada za sanamu ( sanamu za watakatifu waliokufa zamani mfano bikira Maria zikiabudiwa n.k.), kanisani kuna vichekesho na mizaha, mchungaji ni mlevi, mwasherati, na mpenda fedha, mtu anajiita mkristo lakini ni vuguvugu, leo yupo kwa Mungu kesho yupo kwa shetani, leo anaenda kanisani kesho disko, leo anavaa vizuri kesho kimini,.leo anamwimbia Mungu kesho anaimba nyimbo za kidunia, leo anasali kesho anasengenya. n.k.
Sasa mambo kama haya ndiyo yanayochochea ghadhabu ya Mungu, ni heri haya yangetendeka kwa mtu asiye mkristo kuliko mtu anayesema yeye ni mkristo na kakombolewa na damu ya Mungu na bado anatenda mambo kama hayo huko ni kumtia Mungu wivu mkubwa sana.
Lakini pamoja na hayo kabla Mungu hajashusha ghdhabu yake huwa anawatia ALAMA kwanza WATU WAKE waaminifu katikati ya wanaojiita wakristo, hawa anawatenga na kuwaepusha na mabaya yanayokuja mbeleni. Ndio kitu kinachoendelea sasahivi katika kanisa. Japo yanaonekana mambo ya ajabu na yasiyofaa katika Kanisa, Mungu anaendelea kuwatia muhuri wale waliojazwa Roho na waliowaaminifu na kuwaepusha na ile ghadhabu kwa KUWANYAKUA mbinguni kisha baadaye wale waliosalia wasiotiwa muhuri/alama wataangamizwa, katika siku ile kuu ya Bwana inayotisha.
Biblia inasema Nuhu na Luthu walikuwa ni watu wenye haki wakilia juu ya maovu yaliyokuwa yanaendelea katika nchi, hivyo Bwana akawaepusha na Hukumu iliyokuwa inakuja..Kadhalika Bwana YESU pia alisema kama ilivyokuwa katika siku za Nuhu na Luthu ndivyo itakavyokuwa kuja kwake mwana wa Adamu.
Hivyo ndugu, Kanisa tunaloishi sasa ndilo la mwisho linaloitwa LAODIKIA. Na ujumbe Bwana alioutoa kwetu sisi ni huu;
Ufunuo 3: 14-20
” Na kwa malaika wa kanisa lililoko Laodikia andika; Haya ndiyo anenayo yeye aliye Amina, Shahidi aliye mwaminifu na wa kweli, mwanzo wa kuumba kwa Mungu.
15 Nayajua matendo yako, ya kuwa hu baridi wala hu moto; ingekuwa heri kama ungekuwa baridi au moto.
16 Basi, kwa sababu una uvuguvugu, wala hu baridi wala moto, nitakutapika utoke katika kinywa changu.
17 Kwa kuwa wasema, Mimi ni tajiri, nimejitajirisha, wala sina haja ya kitu; nawe hujui ya kuwa wewe u mnyonge, na mwenye mashaka, na maskini, na kipofu, na uchi.
18 Nakupa shauri, ununue kwangu dhahabu iliyosafishwa kwa moto, upate kuwa tajiri, na mavazi meupe upate kuvaa, aibu ya uchi wako isionekane, na dawa ya macho ya kujipaka macho yako, upate kuona.
19 Wote niwapendao mimi nawakemea, na kuwarudi; basi uwe na bidii, ukatubu.
20 Tazama, nasimama mlangoni, nabisha; mtu akiisikia sauti yangu, na kuufungua mlango, nitaingia kwake, nami nitakula pamoja naye, na yeye pamoja nami. “
Wanaozungumziwa hapa ni wanaojiona kuwa ni wakristo, na sio watu wasiomjua Kristo, ule mfano wa magugu na ngano unawakilisha kundi lililopo kanisani..mfano wa wanawali 10, watano werevu na watano wapumbavu wote ni wanaojiona kuwa ni wakristo na sio watu wa wasiomjua Mungu. Hivyo Bwana alishatoa ONYO kwa wakristo wote wa kanisa hili tulilopo sasa wote walio vuguvugu kuwa ATAWATAPIKA, tena anasema ni HERI kuwa baridi kabisa au moto kuliko kuwa hapo katikati.
Huu ni wakati wa kufanya IMARA WITO wako na UTEULE wako. Kitu kinachoendelea sasahivi katika roho ni BWANA kuwatia alama wale wanaenenda katika ukamilifu na UTAKATIFU, wasiojitia unajisi na mambo ya ulimwengu huu, walioamua kumwishia Bwana tu na si kingine. Iogope ghadhabu ya Mungu inayokuja tubu sasa uyaweke mambo yako vizuri unyakuo usikupite.
Ubarikiwe.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp: Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312
Jiunge na magroup yetu ya whatsapp kwa kubofya hapa > Group-whatsapp
Mada Nyinginezo:
SABATO HALISI NI LINI, JE! NI JUMAPILI AU JUMAMOSI?, NI SIKU GANI ITUPASAYO KUABUDU?
Nini maana ya “Kandake” (Matendo 8:27)
MUNGU ALIKUWA ANAONGEA NA NANI ALIPOSEMA NA “TUMFANYE MTU KWA MFANO WETU”,(MWANZO 1:26)?
About the author