DANIELI: Mlango wa 7

DANIELI: Mlango wa 7

Jina la BWANA wetu YESU KRISTO lihimidiwe.

Katika sura zilizotangulia (yaani ya 1-6), tuliona zikielezea sana sana historia za maisha ya watakatifu waliyopitia zaidi kuliko unabii lakini kuanzia Mlango huu wa 7 na kuendelea tunaona Danieli akionyeshwa maono ya mambo yatakayokuja kutokea katika siku za mwisho. Tukisoma..

Danieli 7:1-8″ Katika mwaka wa kwanza wa Belshaza, mfalme wa Babeli, Danieli aliona ndoto, na maono ya kichwa chake, kitandani mwake; basi akaiandika ndoto, akatoa habari ya jumla ya mambo hayo.

2 Danieli akanena, akisema, Naliona katika maono yangu wakati wa usiku; na tazama, hizo pepo nne za mbinguni zilivuma kwa nguvu juu ya bahari kubwa.

3 Ndipo wanyama wakubwa wanne wakatoka baharini, wote wa namna mbalimbali.

4 Wa kwanza alikuwa kama simba, naye alikuwa na mabawa ya tai; nikatazama, hata mabawa yake yakafutuka manyoya, akainuliwa katika nchi, akasimamishwa juu kwa miguu miwili kama mwanadamu; naye akapewa moyo wa kibinadamu.

5 Na tazama, mnyama mwingine, wa pili, kama dubu, naye aliinuliwa upande mmoja, na mifupa mitatu ya mbavu ilikuwamo kinywani mwake katika meno yake; wakamwambia mnyama huyo hivi, Inuka, ule nyama tele.

6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.

7 Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.

8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake pembe tatu katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.

Tukirejea kwenye ile sura ya pili tunaona jinsi Mfalme Nebudreza akionyeshwa katika ndoto Falme nne zitakazotawala dunia mpaka hapo ALIYE JUU(YESU KRISTO) atakapochukua Falme zote za dunia, hivyo Danieli alimpa tafsiri yake, Ufalme wa kwanza ukiwa ni Babeli, wa pili ukiwa ni Umedi na uajemi, wa tatu ukiwa ni ufalme wa uyunani na wa nne ni Rumi. Jambo hili hili tunaona linajirudia tena katika sura hii ya 7, Danieli akifunuliwa zile zile Falme 4 zitakazotawala ulimwengu wote mpaka mwisho wa dunia isipokuwa hapa anaonyeshwa kwa undani zaidi.

Hapa aliona wanyama 4, wakitoka baharini, kumbuka bahari inawakilisha mikusanyiko ya watu wengi(makutano){ufunuo 17:15, } hivyo hizi falme zitanyanyuka kutoka katikakati ya watu.Kumbuka wanyama hawa 4 Danieli aliowaona ndio yule yule mnyama Yohana alioonyeshwa akitoka Baharini mwenye vichwa 7 na pembe 10, wa kwenye Ufunuo 13 isipokuwa hawa wameunganishwa wote pamoja..

“ufunuo 13:1 Kisha nikaona mnyama akitoka katika bahari, mwenye pembe kumi, na vichwa saba, na juu ya pembe zake ana vilemba kumi, na juu ya vichwa vyake majina ya makufuru.2 Na yule mnyama niliyemwona alikuwa MFANO WA CHUI, na miguu yake ilikuwa kama miguu ya DUBU, na kinywa chake kama kinywa cha SIMBA, yule joka akampa nguvu zake na kiti chake cha enzi na uwezo mwingi. “

Tutazame wanyama hawa.

MNYAMA WA KWANZA:

Kama tunavyosoma yule mnyama wa kwanza alionekana kama mfano wa SIMBA na akiwa na mabawa ya tai, kumbuka utawala wa kwanza Babeli ndio uliohusika kuwapeleka wana wa Israeli utumwani, ulifananishwa na simba ukisoma Yeremia 4:5-6 inaelezea kuwa watu walioichukua Israeli mateka na kuwapeleka Babeli walifananishwa na kama simba aangamizaye mataifa. Na pia kama anavyoonekana na mabawa ya tai hii inaashiria uharaka wake katika kuteka, kitu kinachopaa siku zote kina kasi kuliko vinavyokwenda kwa miguu hivyo Babeli ulikuwa mwepesi wa kuteka.

Habakuki 1:6″ Kwa maana, angalieni, nawaondokesha Wakaldayo {wakaldayo ni wa-babeli}, taifa lile kali, lenye haraka kupita kiasi; wapitao katikati ya dunia, ili wayamiliki makao yasiyo yao.”

7 Hao ni watu wa kutisha sana, wa kuogofya sana; hukumu yao na ukuu wao hutoka katika nafsi zao wenyewe.

8 Farasi zao ni wepesi kuliko chui, ni wakali kuliko mbwa-mwitu wa jioni; na wapanda farasi wao hujitapa naam, wapanda farasi wao watoka mbali sana; HURUKA KAMA TAI AFANYAYE HARAKA ALE. “

Kwahiyo tunaona hapo yule mnyama wa kwanza ni ufalme wa Babeli ambao ulikuja kuanguka baadaye na kunyanyuka mwingine wenye nguvu kushinda huo.

MNYAMA WA PILI:

Mnyama huyu anaonekana akifanana na Dubu, na pia anaonekana kama ameinuliwa upande mmoja ikiwa na maana kuwa anazo pande mbili na upande mmoja imezidi mwingine, na tunafahamu utawala huu si mwingine zaidi ya ufalme wa UMEDI na UAJEMI, na historia inaonyesha ufalme wa Uajemi ulikuwa na nguvu zaidi kuliko Umedi , hivyo zilipoungana zikaja kuundoa ufalme wa Babeli katika mamlaka yake na kuimiliki dunia upya, na pia yule Dubu anaonekana akiwa na MIFUPA MITATU ya mbavu kinywani mwake hizi ni ngome tatu walizoziangusha hawa wafalme wa Umedi na Uajemi, nazo ni Lidya, Misri na Babeli.

Ukisoma Isaya 13:15 ilishatabiri ukatili wake hata kabla ya utawala huo kunyanyuka.inasema ..

“15 Kila mtu atakayeonekana atatumbuliwa, na kila mtu atakayepatikana ataanguka kwa upanga.

 16 Na watoto wao wachanga watavunjwa-vunjwa mbele ya macho yao, nyumba zao zitatekwa nyara, na wake zao watatendwa jeuri.

17 Tazama, nitawaamsha WAAMEDI juu yao, ambao hawaoni fedha kuwa kitu, wala hawafurahii dhahabu.

18 Na nyuta zao zitawaangusha vijana; wala hawatahurumia mazao ya tumbo; jicho lao halitawahurumia watoto.

19 Na Babeli, huo utukufu wa falme, uzuri wa kiburi cha Wakaldayo, utakuwa kama Sodoma na Gomora hapo Mungu alipoiangamiza.”

ukizidi kusoma utaona huyu mnyama anaambiwa “ainuke ale nyama tele” ikiwa na maana kuwa atapewa uwezo wa kuteka mataifa mengi, na ndivyo ilivyokuja kuwa, katika historia inaonyesha Umedi na Uajemi uliteka na kutawala mataifa mengi Kuanzia India mpaka Ethiopia majimbo 127 (Esta 1:1) inaelezea vizuri.

MNYAMA WA TATU:

Mnyama huyu wa tatu Danieli alimwona akiwa mfano wa chui mwenye vichwa vinne, tukisoma..“6 Kisha nikatazama, na kumbe! Mnyama mwingine, kama chui, naye juu ya mgongo wake alikuwa na mabawa manne kama ya ndege; mnyama huyo alikuwa na vichwa vinne; akapewa mamlaka.”

Huu ni utawala wa UYUNANI (UGIRIKI) ambao ulikuja kunyanyuka baada ya mtawala wa Uyunani “Alexander the great” kuiangusha ngome ya Umedi na Uajemi, ni mtawala aliyekuwa na nguvu sana, kama chui alivyo mwepesi wa kushika mawindo yake, ndivyo ilivyokuwa kwa huyu mtawala mdogo, kila alipokwenda kupigana na maadui zake alifanikiwa, kwa muda wa miaka 12 tu alikuwa tayari amekwishafanikiwa kuiteka dunia nzima. Lakini naye pia hakudumu sana katika utawala wake, alipokuwa na miaka 31 alipata ugonjwa na kufa, hivyo hakuacha mtu wa kumrithi baada yake, Hivyo ikasabisha wale majemedari waliokuwa chini yake kupigania ufalme lakini hakufanikiwa kutokea mwenye nguvu kama za Alexander hivyo ufalme ule ukagawanyika katika pande NNE, Ambavyo ndio vile vichwa vinne vya yule mnyama; Cassander, Lysimachus ,Ptolemy na Seleucus

MNYAMA WA NNE:

 Danieli 7:7 “Baadaye nikaona katika njozi ya usiku, na tazama, mnyama wa nne, mwenye kutisha, mwenye nguvu, mwenye uwezo mwingi, naye alikuwa na meno ya chuma, makubwa sana; alikula na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake; na umbo lake lilikuwa mbali kabisa na wale wa kwanza, naye alikuwa na pembe kumi.

Mnyama huyu ni utawala wa RUMI, ndio ile miguu ya chuma kwenye yale maono aliyoyaona Mfalme Nebukadreza kwenye Danieli 2, na mnyama huyu hapa anaonekana akiwa na meno ya chuma, ikiashiria ana nguvu nyingi za kuharibu na kusagasaga, na pia hapa anaonekana na pembe 10, ambavyo ndio vile vidole 10 vya kwenye ile sanamu ya Nebukadreza. Kumbuka utawala huu ndio uliokuwa utawala katili kuliko yote iliyotangulia, na ndio unaotawala hata sasa katika roho,Lakini Katika historia, utawala wa Rumi ya magharibi ulikuja kugawanyika katika mataifa 10 yanayojitegemea AD 476, ambayo ni

1) Alemanni– kwa sasa ni Ujerumani

2) Franks – kwa sasa ni Ufaransa

3) Burgundians-Kwa sasa ni uswizi

4) Visigoths -Hispania

5) Lombards-Italia

6) Anglo-Saxons– Uingereza

7) Suevi- Ureno

8) Vandals -iling’ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka

9) Ostrogoths-ilingom’ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka

10) Heruli– iling’ofolewa na ile pembe ndogo iliyozuka

Lakini tukiendelea kusoma mstari wa 8 tunaona kuna PEMBE nyingine ndogo ikizuka

“Danieli 7:8 Nikaziangalia sana pembe zake, na tazama, pembe nyingine ikazuka kati yao, nayo ilikuwa ndogo, ambayo mbele yake PEMBE TATU katika zile za kwanza zikang’olewa kabisa; na tazama, katika pembe hiyo mlikuwa na macho kama macho ya mwanadamu, na kinywa kilichokuwa kikinena maneno makuu.

Hivyo baada ya Danieli kuona haya alitamani kufahamu ile pembe ndogo maana yake ni nini??, Kama tunavyosoma Danieli 7:19 Kisha nalitaka kujua maana ya yule mnyama wa nne, aliyekuwa mbali na wenziwe wote, mwenye kutisha sana, ambaye meno yake yalikuwa ya chuma, na makucha yake ya shaba; aliyekula, na kuvunja vipande vipande, na kuyakanyaga mabaki kwa miguu yake;

20 na habari za zile pembe kumi zilizokuwa kichwani mwake, na ile pembe nyingine iliyozuka, ambayo mbele yake zilianguka pembe tatu; yaani, pembe ile yenye macho, na kanwa lililonena makuu, ambayo kuonekana kwake kulikuwa hodari kuliko wenzake.

Kumbuka Pembe zinawakilisha ufalme au mfalme, Hivyo zile pembe 10 zinasimama kama wafalme wenye falme, vivyo hivyo na ile pembe ndogo ya 11 iliyoonekana kuzuka na kung’oa pembe nyingine tatu ni mfalme atakayenyanyuka na kuangusha wafalme wengine watatu. Historia inaonyesha mara baada ya utawala wa RUMI kugawanyika katika zile Falme 10, utawala wa KIPAPA ulizuka na kungusha tatu ya hizo ngome 10, pale zilipotaka kushindana na utawala wa PAPA aliziharibu kabisa na kuzishinda na hizo si nyingine zaidi ya Vandals, Ostrogoths na Heruli.

Na kama tunavyosoma pembe hiyo ilijitukuza sana na kunena maneno makuu ya makufuru, tunafahamu cheo pekee kinachosimama kama Mungu duniani ni cheo cha UPAPA, leo hii katika enzi yake yeye anasimama kama ” badala ya Kristo duniani”, anao uwezo wa kusamehe dhambi, anafahamika kama mtawala wa mbinguni, duniani, na chini ya nchi, N.K. hayo yote ni maneno ya makufuru mbele za Mungu. watu wanamtazama duniani yeye kama Mungu.

Lakini Mstari wa 21 unasema. ” Nikatazama, na pembe iyo hiyo ilifanya vita na watakatifu, ikawashinda; “ hakuishia tu katika kujitukuza lakini aliendelea hata kufanya vita na watakatifu Hili ni jambo limekuwa likijirudia katika historia tangu utawala wa KIPAPA chini ya Kanisa Katoliki uanze, wakristo wengi wamekuwa wakiuliwa kikatili pindi tu pale walipoonekana wanaenda kinyume na Dini hiyo. Wakristo zaidi ya milioni 68 waliuawa kikatili walipoonekana tu wanalishika Neno na kupinga mafundisho ya uongo ya kanisa hilo. Kumbuka wakatoliki sio wapinga-kristo isipokuwa ule mfumo wa lile kanisa na kile cheo anachokikalia kiongozi wa lile kanisa ndio cha MPINGA-KRISTO MWENYEWE.

Mstari wa 25 unasema Naye atanena maneno kinyume chake Aliye juu, naye atawadhoofisha watakatifu wake Aliye juu; naye ataazimu kubadili majira na sheria; nao watatiwa mikononi mwake kwa WAKATI, NA NYAKATI MBILI, NA NUSU WAKATI (Danieli 7:25)”. Hii inafunua siku mpinga-Kristo yule PAPA wa mwisho atakaposimama kutenda kazi.

Kumbuka hawa PAPA waliopo sasa hivi na waliopita wamekaa katika viti vya mpinga-kristo lakini yupo MMOJA atakayesimama na kubadilisha majira, na sheria, biblia inasema

( 1Yohana 2:18 “Watoto, ni wakati wa mwisho; na kama vile mlivyosikia kwamba MPINGA KRISTO YUAJA , hata sasa WAPINGA KRISTO WENGI wamekwisha kuwapo. Kwa sababu hiyo twajua ya kuwa ni wakati wa mwisho).

Na siku sio nyingi atasimama atawale na kuitesa dunia kwa nyakati na nyakati mbili na nusu wakati, ambayo ni miaka mitatu na nusu, kwasababu kibiblia nyakati moja ni mwaka mmoja.

Hivyo hiyo itakuwa ni miaka mitatu na nusu ya dhiki kuu,. labda anaweza akawa ndio huyu PAPA aliyepo sasa au mwingine muda utaeleza yote.. Huu ni wakati wa kujiweka tayari muda wowote mambo yanabadilika, Hauoni sasa hivi anavyozunguka kuleta DINI zote pamoja, akiwa kama mtu mwenye wafuasi wengi kuliko wote duniani. Kilio chake ni AMANI! AMANI! kwa kivuli hicho anatafuta ufalme ili baadaye aje kupambana na uzao wa Mungu.

Biblia inasema..1Wathesalonike 5:1-3″ Lakini, ndugu, kwa habari ya nyakati na majira, hamna haja niwaandikie. Maana ninyi wenyewe mnajua yakini ya kuwa siku ya Bwana yaja kama vile mwivi ajavyo usiku.Wakati wasemapo, KUNA AMANI NA SALAMA, ndipo uharibifu uwajiapo kwa ghafula, kama vile utungu umjiavyo mwenye mimba, wala hakika hawataokolewa. “

Ndugu wakati umeisha usidanganyike na watu wanaosema dunia haishi leo wala kesho, geuka weka mambo yako sawasawa yahusuyo wokovu.Huu ulimwengu unapita na mambo yake yote.

Mstari wa 9-10. unasema…” Nikatazama hata viti vya enzi vikawekwa, na mmoja aliye mzee wa siku ameketi; mavazi yake yalikuwa meupe kama theluji, na nywele za kichwa chake kama sufu safi; kiti chake cha enzi kilikuwa miali ya moto, na gurudumu zake moto uwakao.10 Mto kama wa moto ukatoka ukapita mbele zake; maelfu elfu wakamtumikia, na elfu kumi mara elfu kumi wakasimama mbele zake; hukumu ikawekwa, na VITABU VIKAFUNULIWA.

Hapa tunaona mwisho wa yote vitabu vitafunguliwa vihusuvyo maisha yetu, kila mtu na kitabu chake na utahukumiwa katika hicho, je! kitabu chako unakiandikaje? Biblia inasema sisi ni barua, na kila siku tunafungua kurasa mpya wa vitabu vyetu, na siku ile utakapokufa kitafungwa kikingojea kufunguliwa tena katika siku ile ya HUKUMU.

Hivyo tukiona mambo haya tunajua kabisa ule mwisho umekaribia UTAWALA USIOWEZA KUHARIBIKA wa mwokozi wetu ,hivi karibuni utakuja hapa ulimwenguni,.BWANA wetu YESU KRISTO MFALME WA WAFALME NA BWANA WA MABWANA, atamiliki pamoja na watakatifu wake milele tunasoma..

Danieli 7:27 Na ufalme, na mamlaka, na ukuu wa ufalme, chini ya mbingu zote, watapewa watu wa watakatifu wake Aliye juu; UFALME WAKE NI UFALME WA MILELE, na wote wenye mamlaka watamtumikia na kumtii.

2Petro 1:10” Kwa hiyo ndugu, jitahidini zaidi kufanya imara kuitwa kwenu na uteule wenu; maana mkitenda hayo hamtajikwaa kamwe.”

AMEN!

Kwa Mwendelezo >>> Mlango wa 8


Mada Nyinginezo:

UFUNUO: MLANGO WA 13

UFUNUO: MLANGO WA 17

JE! KUSHIRIKI AU KUJIHUSISHA KWENYE MICHEZO NI DHAMBI?

   WAPUNGA PEPO WANAOZUNGUMZIWA KWENYE BIBLIA NI WATU WA NAMNA GANI?

JE! BIKIRA MARIA NI MALKIA WA MBINGUNI?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Paul Aroka
Paul Aroka
4 years ago

Naomba kupata hizi falme na miaka walio tawala. Lkn pia Mtumishi wa BABA ubarikiee sana