USIONDOE ALAMA YA MPAKA ILIYOWEKWA NA MABABA.

USIONDOE ALAMA YA MPAKA ILIYOWEKWA NA MABABA.

Wana wa Israeli walipokuwa wanatoka Misri na kwenda katika nchi yao ya ahadi, walikuwa ni umati mkubwa sana wa kabila 12 za Israeli, Hivyo ili hayo makabila yote yaweze kukaa kila moja kivyake kwa amani iliwapasa waigawe ile nchi katika vipengele 12. Hivyo mipaka ikawekwa kama alama kwa kila kabila kwamba hiyo mipaka isivukwe na mtu yeyote yule kuingilia upande wa wenzake, Na atakaye jaribu kusogeza au kuondoa mpaka laana itamwangukia. Hivyo huo utaratibu uliendelea kujulikana kwa vizazi vyote vya wana wa Israeli kwamba mipaka iliyowekwa na wazee wa kale kwa kila kabila haitakiwi kuguswa kwa namna yeyote ile ibaki kama ilivyo.

Musa aliandika katika Kumbukumbu 19:14 “Usiiondoe alama ya mpaka wa jirani yako, waliouweka watu wa kale katika urithi wako, utakaorithi ndani ya nchi akupayo Bwana, Mungu wako, uimiliki.”

Na pia inasema..Kumbukumbu 27: 17 “NA ALAANIWE AONDOAYE MPAKA WA JIRANI YAKE. Na watu wote waseme, Amina.”

Hivyo hofu kubwa ilikuwepo kwa Israeli, kwa yeyote aliyejaribu kufanya tendo kama hilo.

Kadhalika hata katika Israeli ya Rohoni (KANISA) ambalo ndio sisi, nayo imewekewa mipaka na wazee wa zamani isivukwe wala isiondolewe, na kwa mtu yeyote atakayejaribu kufanya hivyo ataangukia laana nzito kutoka kwa Mungu mwenyezi. Mithali 22:28 inasisitiza… “ USIIONDOE ALAMA YA MPAKA WA ZAMANI, ULIOWEKWA NA BABA ZAKO.”

USIIONDOE ALAMA YA MPAKA WA ZAMANI, ULIOWEKWA NA BABA ZAKO

MIPAKA YETU KWA SASA NI NINI?..Mipaka yetu ni NENO LA MUNGU.

Na wazee wetu wa zamani ni wakina nani? . Ni MITUME NA MANABII.

Biblia inasema Waefeso 2:20 “Mmejengwa juu ya msingi wa mitume na manabii, naye Kristo Yesu mwenyewe ni jiwe kuu la pembeni.”. Sisi kama kanisa la Kristo tumejengwa juu ya mafundisho ya mitume na manabii, wale mitume wa Bwana Yesu Kristo na manabii wa agano la kale, hao ndio waliotuwekea mipaka ya IMANI yetu kwamba isivukwe zaidi ya hapo kwasababu maagizo waliyopokea yalikuwa ni moja kwa moja kutoka kwa Mungu mwenyewe na ndio maana Paulo kama mmoja wa mitume wa Kristo alisema..

Wagalatia 1: 8 “LAKINI IJAPOKUWA SISI AU MALAIKA WA MBINGUNI ATAWAHUBIRI NINYI INJILI YOYOTE ISIPOKUWA HIYO TULIYOWAHUBIRI, NA ALAANIWE.

9 Kama tulivyotangulia kusema, na sasa, nasema tena, mtu awaye yote akiwahubiri ninyi injili yo yote isipokuwa hiyo mliyoipokea, na alaaniwe.

10 Maana, sasa je! Ni wanadamu ninaowashawishi, au Mungu? Au nataka kuwapendeza wanadamu? Kama ningekuwa hata sasa nawapendeza wanadamu, singekuwa mtumwa wa Kristo.

11 Kwa maana, ndugu zangu, injili hiyo niliyowahubiri, nawajulisha ya kuwa siyo ya namna ya kibinadamu.

12 Kwa kuwa sikuipokea kwa mwanadamu wala sikufundishwa na mwanadamu, bali kwa ufunuo wa Yesu Kristo.”

Unaona hapo hatari iliyopo katika kuvuka mipaka ya Injili iliyohubiriwa na mitume?. (Mipaka iliyowekwa na mababa?). Laana imekwisha tamkwa.

NA KUVUKA MIPAKA NI KUPI?.

1) Injili inasema katika matendo 2:38 “Petro akawaambia, Tubuni mkabatizwe kila mmoja kwa jina lake Yesu Kristo, mpate ondoleo la dhambi zenu, nanyi mtapokea kipawa cha Roho Mtakatifu.” Tunafahamu katika maandiko hakuna sehemu yoyote mtoto mchanga alibatizwa, na ubatizo sahihi ni katika jina la YESU KRISTO, sawasawa na (matendo 8:16, mdo 10:48, mdo 19:5), sehemu zote hizi watu wote walibatizwa kwa jina la YESU KRISTO. Hivyo mtu yeyote anayefanya kinyume na hicho ni sawa na kuvuka mipaka iliyowekwa na mababa, haijalishi umemaanisha kiasi gani, ni makosa.

2) Biblia inaposema. Kutoka 20:4 “Usijifanyie sanamu ya kuchonga, wala mfano wa kitu cho chote kilicho juu mbinguni, wala kilicho chini duniani, wala kilicho majini chini ya dunia.

5 USIVISUJUDIE WALA KUVITUMIKIA; kwa kuwa mimi, Bwana, Mungu wako, ni Mungu mwenye wivu; nawapatiliza wana maovu ya baba zao, hata kizazi cha tatu na cha nne cha wanichukiao,”….Na pale mtu anapochukua sanamu ya mtakatifu fulani aliyekufa siku nyingi na kuiabudu huko ni kuvuka mipaka iliyowekwa na manabii na mtu yeyote anayefanya au kwenda kinyume ataangukia laana iliyoandikwa hapo juu.

3) Kadhalika mitume kwa maagizo ya Bwana walionywa wasiwaruhusu wanawake wafundishe katika kanisa. Mtume Paulo alisema..

 1Wakoritho 14:34 “Wanawake na WANYAMAZE katika kanisa, maana HAWANA RUHUSA YA KUNENA BALI WATII, kama vile inenavyo torati nayo.

35 Nao wakitaka kujifunza neno lo lote, na wawaulize waume zao wenyewe nyumbani mwao; maana ni aibu wanawake kunena katika kanisa.

36 Au je! Neno la Mungu lilitoka kwenu? Au kuwafikia ninyi peke yenu?

37 Mtu akijiona kuwa ni nabii au mtu wa rohoni, na ayatambue hayo ninayowaandikia, ya kwamba ni MAAGIZO YA BWANA.

38 Lakini mtu akiwa mjinga, na awe mjinga.”……Na pia alisema.

1Timotheo 2: 8 Basi, nataka wanaume wasalishe kila mahali, huku wakiinua mikono iliyotakata pasipo hasira wala majadiliano.

9 Vivyo hivyo wanawake na WAJIPAMBE KWA MAVAZI YA KUJISITIRI, pamoja na adabu nzuri, na moyo wa kiasi; si kwa kusuka nywele, wala kwa dhahabu na lulu, wala kwa nguo za thamani;

10 bali kwa matendo mema, kama iwapasavyo wanawake wanaoukiri uchaji wa Mungu.

11 Mwanamke na ajifunze katika utulivu, akitii kwa kila namna.

12 SIMPI MWANAMKE RUHUSA YA KUFUNDISHA,WALA KUMTAWALA MWANAMUME, bali awe katika utulivu.

13 Kwa maana Adamu ndiye aliyeumbwa kwanza, na Hawa baadaye.

14 Wala Adamu hakudanganywa, ila mwanamke alidanganywa kabisa akaingia katika hali ya kukosa.” Hivyo kama tunavyosoma maandiko mwanamke kufundisha kanisani kwenye mchanganyiko wa wanaume na wanawake hairuhusiwi, kufanya hivyo kwa kisingizio cha haki sawa, au kisa wote ni watu wa Mungu, huko ni kuvuka mipaka iliyotangulia kuwekwa.

 Kadhalika Kuvaa mavazi yoyote ya kutokujisitiri kwa wanawake, pia ni kuvuka mipaka.

4) Kuoa mke zaidi ya mmoja; angali Bwana Yesu alisema Hapo mwanzo Mungu alimuumba mtu mume na mtu mke, na hao wawili watakuwa mwili mmoja, na sio hao “wengi” watakuwa mwili mmoja(Mathayo 19:4-9). Hivyo mtu yeyote anayefanya hivyo ni kuvuka mipaka iliyowekwa na Mungu tangu zamani.

Biblia inasema katika Ayubu 24:2 “WAKO WAZIONDOAO ALAMA ZA MIPAKA; HUYACHUKUA MAKUNDI KWA JEURI NA KUYALISHA.”. Hawa ni wahubiri wanaondoa mipaka ya NENO LA MUNGU, na kuwafundisha watu mafundisho yasiyoendana na maagizo ya BIBLIA. Wapo wanaofundisha kuwa hakuna jehanamu ya moto, wapo wanaofundisha kuwa Dunia hii haiishi leo wala kesho tufurahie maisha, wapo wanaofundisha kuoa mke zaidi ya mmoja ni sawa, wapo wanaofundisha kusujudia sanamu katika ibada ni ishara ya unyenyekevu kwa Mungu hivyo hakuna shida. Wapo wanaofundisha Mungu huwa haangalii tena mambo ya mwilini tunaishi chini ya neema, hivyo kuvaa nguo za uchi ni sawa, ushoga ni sawa, Wapo wanaofundisha kuwa kunywa pombe ni sawa n.k. Na wengi wa hawa ni viongozi wakubwa wa dini wanaoheshimiwa na wengi.

Lakini Bwana anasema siku inafika atawamwagia ghadhabu yake kama maji. Hosea 5: 10 “WAKUU WA YUDA NI KAMA WATU WAONDOAO ALAMA YA MPAKA; nitawamwagia ghadhabu yangu kama maji.”

Hivyo ndugu kuwa makini na jinsi unavyoenenda katika ukristo wako, usije ukaangukia laana kwa kuyasikiliza mafundisho yaliyo nje ya NENO LA MUNGU, wanayoyafundisha manabii wa uongo. Dumu katika BIBLIA TU mipaka iliyowekwa na mababa wa kale(yaani Mitume na Manabii). Usiongeze wala usipunguze ili uwe na uhakika upo katika njia salama. Bwana alisema;

Ufunuo 22:

“18 Namshuhudia kila mtu ayasikiaye maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mtu ye yote akiyaongeza, Mungu atamwongezea hayo mapigo yaliyoandikwa katika kitabu hiki.

19 Na mtu ye yote akiondoa lo lote katika maneno ya unabii wa kitabu hiki, Mungu atamwondolea sehemu yake katika ule mti wa uzima, na katika ule mji mtakatifu, ambao habari zake zimeandikwa katika kitabu hiki.”.

Mungu akubariki sana.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

usiiondoe alama ya mpaka iliyowekwa na mababa


Mada Nyinginezo:

NAFASI YA MWANAMKE KATIKA KANISA

JE! UMEPOKEA KWELI ROHO MTAKATIFU?

MIHURI SABA

JE! MUNGU ANAUPENDELEO KWA WANAUME ZAIDI YA WANAWAKE?

NINI TOFAUTI KATI YA KARAMA, UTENDAJI KAZI NA HUDUMA.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments