Je! Unaweza kubatizwa na usipokee Roho Mtakatifu?. Na Je! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono?

Je! Unaweza kubatizwa na usipokee Roho Mtakatifu?. Na Je! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono?

SWALI: Habari mtumishi…, ninaswali hapa naomba uniweke sawa.

Matendo ya mitume 8:14 “ na Mitume waliokuwako Yerusalemu, waliposikia ya kwamba Samaria imelikubali neno la Mungu,wakawapelekea Petro na Yohana,

15.ambao waliposhuka, wakawaombea wampokee Roho Mtakatifu,

16. kwa maana bado hawajashukia hata mmoja wao, ila wamebatizwa tu kwa jina la Bwana Yesu.

17.Ndipo wakaweka mikono yao juu yao, nao wakampokea Roho Mtakatifu”.. 

Sasa swali langu limegawanyika katika vipengele 3..a) Je! unaweza kubatizwa na usimpokee Roho Mtakatifu kama hawa watu wa Samaria ilivyokua?. b) Je! unaweza mpokea Roho Mtakatifu kwa kuombewa kama Petro na Yohana walivyofanya?. c) Kwa jamii yetu ya kawaida ni kigezo gani kinatumika kwa mtu kuwabatiza wengine au awe na sifa zipi huyo mbatizaji ili tupate ubatizo sahihi?


JIBU: Shalom, Bwana akubariki kwa swali zuri, Kwanza ni muhimu kufahamu umuhimu wa ubatizo sahihi, Ubatizo sahihi ni kama Leseni ya Roho Mtakatifu kukaa ndani ya mtu, yaani mtu anapobatizwa katika ubatizo sahihi, amemhalalisha Roho Mtakatifu kuingia ndani yake na kuwa wake. 

Hivyo Roho Mtakatifu anaweza kushuka juu ya mtu kabla au baada ya kubatizwa, lakini uhalali wa kukaa moja kwa moja ndani ya mtu unakuja baada ya mtu kubatizwa. Sasa tukirudi kwenye swali la kwanza linalouliza “a) Je! unaweza kubatizwa na usimpokee roho mtakatifu kama hawa watu wa Samaria ilivyokua?” Jibu ni ndio! Kama umeamini na kutubu dhambi zako kwa kudhamiria kuziacha, na ukaenda kubatizwa, lakini hujawahi kusikia lolote juu ya Roho Mtakatifu, hapo hawezi kuingia ndani yako, kwasababu Roho hawezi kuja juu ya mtu ambaye hajawahi kabisa kuzisikia habari zake, ni sharti kwanza mtu huyo ahubiriwe Roho Mtakatifu ni nini, ndipo ashuke juu yake, Hata Bwana Yesu hawezi kuingia ndani ya moyo wa Mtu kama mtu huyo hajahubiriwa kabisa, au hajawahi kusikia kabisa habari za Yesu…. hivyo Kwa mtu aliyeamini na kutubu na kubatizwa ipasavyo, Roho Mtakatifu mwenyewe atahakikisha anamletea mhubiri ambaye atamweleza kuwa kuna kitu kinachoitwa Roho Mtakatifu ndipo ashuke ndani yake. Ndicho kilichotokea kwa hawa watu wa Samaria na wale Wakorintho Paulo aliokutana nao..

Matendo 19:1 “Ikawa, Apolo alipokuwa Korintho, Paulo, akiisha kupita kati ya nchi za juu, akafika Efeso; akakutana na wanafunzi kadha wa kadha huko;

2 akawauliza, Je! Mlipokea Roho Mtakatifu mlipoamini? Wakamjibu, La, hata kusikia kwamba kuna Roho Mtakatifu hatukusikia.

3 Akawauliza, Basi mlibatizwa kwa ubatizo gani? Wakasema, Kwa ubatizo wa Yohana.

4 Paulo akasema, Yohana alibatiza kwa ubatizo wa toba, akiwaambia watu wamwamini yeye atakayekuja nyuma yake, yaani, Yesu.

5 Waliposikia haya wakabatizwa kwa jina la Bwana Yesu.

6 Na Paulo, alipokwisha kuweka mikono yake juu yao, Roho Mtakatifu akaja juu yao; wakaanza kunena kwa lugha, na kutabiri.

7 Na jumla yao walipata wanaume kumi na wawili”.

 Na pia Roho Mtakatifu anaweza kushuka juu ya mtu kabla hajabatizwa endapo tu atakuwa ameshasikia kuwa kuna kitu kinachoitwa ROHO MTAKATIFU, kama mtu ameshasikia kuwa kuna kitu kinaitwa Roho Mtakatifu na jinsi anavyotenda kazi, basi Roho anaweza kushuka juu ya huyo mtu kabla hata hajabatizwa, lakini ili awe na uhalali wa kukaa ndani ya huyo mtu ni lazima mtu huyo akabatizwe ili kukamilisha wokovu wake…Ndicho kilichotokea kwa Kornelio akida wa Kirumi wakati Petro amekwenda nyumbani kwake.. 

Matendo : 10:44 “Petro alipokuwa akisema maneno hayo Roho Mtakatifu akawashukia wote waliolisikia lile neno

45 Na wale waliotahiriwa, walioamini, wakashangaa, watu wote waliokuja pamoja na Petro, kwa sababu Mataifa nao wamemwagiwa kipawa cha Roho Mtakatifu.

46 Kwa maana waliwasikia wakisema kwa lugha, na kumwadhimisha Mungu. Ndipo Petro akajibu,

47 Ni nani awezaye kuzuia maji, hawa wasibatizwe, watu waliopokea Roho Mtakatifu vile vile kama sisi?

48 Akaamuru wabatizwe kwa Jina lake Yesu Kristo. Ndipo wakamsihi azidi kukaa siku kadha wa kadha”. 

Swali la pili linasema “Je! unaweza mpokea Roho Mtakatifu kwa kuombewa kama Petro na Yohana walivofanya?” Jibu ni ndio! Unaweza kupokea Roho Mtakatifu kwa kuwekewa mikono, lakini sio wakati wote!.. mara nyingi watu wanapokea Roho pasipo hata kuwekewe mikono, mfano siku ya Pentekoste mitume hawakuwekewa mikono na mtu yeyote, na hata wakati Petro yupo nyumbani kwa Kornelio kama tulivyosoma hapo juu, wale watu hawakuwekewa mikono na mtu yeyote lakini Roho alishuka juu yao..hivyo Roho anaweza kushuka juu ya mtu aidha kwa kuwekewa mikono na watiwa Mafuta wake au bila kuwekewa mikono. Ni kwa jinsi Roho atakavyopenda!..Na kwa jinsi Roho atakavyomuongoza yule anayehudumu. Swali la tatu … “kwa jamii yetu ya kawaida ni kigezo gani kinatumika kwa mtu kuwabatiza wengine au awe na sifa zipi huyo mbatizaji ili tupate ubatizo sahihi?” 

Jibu: Vigezo vinavyotumika vya mtu kuwabatiza wengine ni vigezo vile vile vya mtu anayetaka kuwa mhubiri!..Mtu akitaka kuwa mhubiri, au mwalimu kwa wengine ni sharti kwanza awe mwanafunzi wa Kristo, pili awe na uwezo wa kufundisha wengine kitu ambacho yeye mwenyewe anakiishi, na awe na uelewa wa kutosha wa kitu anachokwenda kukifanya, Awe Ameitwa na Mungu kweli na anafahamu kuwa anafanya kazi ya Mungu na si ya mwanadamu…

Kadhalika mtu anayetakiwa kubatiza wengine anapaswa na yeye mwenyewe kwanza awe amebatizwa katika ubatizo sahihi, na awe na uelewa wa kutosha kuhusu ubatizo yaani faida za kubatizwa na hasara za mtu kutokubatizwa ili aweze kuwafundisha vyema wale ambao watakuja kubatizwa naye!. Mtu mwingine yoyote asiyekuwa na vigezo hivyo haruhusiwi kifanya kitendo hicho kitakatifu. 

Bwana akubariki!


Mada Nyinginezo:

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOKUJA JUU YA MTU.

UPEPO WA ROHO.

JE! NI LAZIMA WATU WOTE WANENE KWA LUGHA?

FAIDA ZA MAOMBI.

ROHO ZILIZO CHINI YA MADHABAHU:

AMIN! NAWAAMBIA KIZAZI HIKI HAKITAPITA.

 


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments