(Kwanini Mungu hatumuoni?)….Hili ni swali ambalo karibu kila mtu anajiuliza au alishawahi kujiuliza pengine kipindi Fulani nyuma, kwanini Mungu hajidhihirishi wazi wazi tukamwona kama tunavyoonana sisi kwa sisi?, au kwanini Mungu hatumsikii kama tunavyosikilizana sisi tunavyoongea?….Watu wanasema Ni rahisi kumwona Mungu kwa kazi zake lakini yeye mwenyewe ni ngumu sana ni kwanini kaamua kuwa hivyo? Na hiyo imewafanya watu wengi kuishia kutoamini kabisa kama kuna Mungu na wengine wameishia kusema Mungu amekufa..
Lakini Je! kutokumwamini Ndio kutaleta suluhisho la yeye kutokuonekana?, Jibu ni hapana, yeye atabakia kuwa Mungu tu haijalishi tunamfikiriaje au tunamzungumziaje,..Jambo la pekee tunaweza kufanya ni kujiuliza ni kwanini Mungu aonyeshe tabia kama hiyo
Ukweli ni kuwa Mungu hayupo hivyo wakati wote, upo wakati biblia inatuambia tutamwona, uso kwa uso, upo wakati tutakaa naye, upo wakati tutazungumza naye uso kwa uso, (Mathayo 5:8, 1Wakorintho 13:11-12), Ufunuo 21:3 inasema..
“Nikasikia sauti kubwa kutoka katika kile kiti cha enzi ikisema, Tazama, maskani ya Mungu ni pamoja na wanadamu, naye atafanya maskani yake pamoja nao, nao watakuwa watu wake. Naye Mungu mwenyewe atakuwa pamoja nao.”
Lakini kwasasa yeye ametuweka tuishi katika hali hii ya kutomwona tujifunze kitu, Na siku tukilifahamu vizuri hilo wazo la Mungu, hatutafikiri kitoto tena..Embu jaribu kufikiria, wewe ulipokuwa mtoto, au kijana ambaye upo chini ya wazazi wako, jaribu kuwaza ingekuwa mzazi wako kila mahali ulipo au unapokwenda yupo nyuma yako kukufuatilia, ukienda kula mgahawani yupo hapo anakuangalia ni chakula gani unakula, ukienda shule yupo hapo nyuma yako anakuangalia, ukiingia darasani yupo pale nyuma ya darasa na yeye anakuangalia kuakikisha ni kitu gani unasoma au unaandika, ukiwa unazungumza na marafiki zako yupo hapo anakusikiliza mazungumzo yako na kukuambia zungumza nao hivi, au usizungumze nao vile, ukiwa upo kwenye michezo yupo pembeni yako kukuchunga usiumie, ukienda uwani, yupo hapo nje anakusubiria utoke,..kila kitu unachokifanya yupo hapo pembeni yako anakuangalia, anasema ni kwasababu anakupenda na anakujali na ndio maana hataki akae mbali na wewe hata sekunde moja..anataka kila wakati umuone na yeye akuone..
Sasa jiulize wewe kama mtoto utajisikiaje, cha kwanza ni kuwa japo mzazi wako anakupenda sana na kukujali sana, lakini kule kuwa na wewe kila sekunde kila dakika kunakufanya upoteze uhuru Fulani wa kufanya mambo yako hata yale ya msingi.., pili kunakufanya uboreke kwa sehemu Fulani, haijalishi nia ya mzazi ni nzuri kiasi gani..Kuna mahali utahijitaji uhuru wako sehemu Fulani ili ufanye mambo yako kwa ufasaha zaidi.
Na kwa Mungu ndivyo ilivyo, tunasema Ee Mungu naomba kila saa nikuone, naomba kila saa nisikie sauti yako, naomba kila saa unitokee, tunasema hivyo ni kwa vile tu hutujui tunachokiomba,..Wewe unaweza kuona ni jambo jema na zuri kumwona Mungu au kusikia kila dakika anasema na wewe, lakini katika upande wa pili utakuwa unamtumikia Mungu kwa presha na bila UHURU ambao Mungu anataka utembee nao, na hilo ndilo jambo ambalo Mungu hapendi.
Wengi tunatamani Mungu akishatuokoa tu, basi saa hiyo hiyo tuanze kumsikia akizungumza ndani yetu na kutupa maelekezo karibu ya kila kitu cha kufanya..hata tukitaka kupiga hatua tunataka tumsikie Mungu akituambia piga hatua tano kisha kunja mbili kulia, fanya hivi, fanye vile, sema hiki, usiseme kile..kama vile GPS, ambayo hiyo inakuongoza kama vile Roboti kugeuka kulia na kushoto ili kufika pale ulipoelekezwa…
Mungu hayupo hivyo, yeye anachofanya ni kutugawia sisi ramani mkononi, ambayo inatuonyesha mwanzo hadi mwisho wa safari yetu, na katika ramani hiyo hiyo anatuonesha na mwisho wa njia mbaya zote, na katika ramani hiyo hiyo ndani yake kaweka mashauri ya njia sahihi ya kuiendea, Hivyo hapo ni wewe kuchagua njia ipi inayokufaa, kama utachagua njia ya uzima hapo ni wewe, kama utachagua njia ya mauti hapo ni wewe mwenyewe, lakini ramani inaelekeza kila kitu na ramani yenyewe ni BIBLIA TAKATIFU.
Lakini leo hii ukimpa Kristo maisha yako na ukaufahamu ukweli usitazamie utasikia sauti inakuambia usiende disko, au usizini au usiibe, au usiabudu sanamu, au kula hichi au usile kile, au ukaanza kutokewa na Mungu kila siku, kwenye ndoto, ikitokea jambo kama hilo basi ufahamu kuwa ni Mungu anataka kukufundisha kitu lakini usidhani itakuwa ni jambo la sikuzote. Ni wajibu wako wewe kuishi kulingana na njia za uzima inavyoelekeza ili ufikie mwisho mwema, na ndivyo utakavyoishi kwa uhuru ambao Mungu anataka auone kwetu..Ni sawa na mwanamke mwerevu aliyeolewa, ambaye akishaingia tu ndani ya nyumba ya mumewe hasubirii kusikia mumewe akimwambia nipikie chai, au nenda sokoni, yeye mwenyewe tu atajua majukumu yake kama mwanamke na kuanza kujitumia sawasawa na alivyoitiwa vivyo hivyo na mwanamume mwenye akili ambaye ameona, hatangojea siku mkewe amwambie mume wangu nenda katafute ugali wa nyumbani, yeye mwenyewe tu atatoka na kwenda kupambana ili kuakikisha kuwa familia yake inakula na kufurahi.
Hivyo ikiwa wewe ni mkristo, usisibiri Bwana akupe maagizo Fulani ya kufanya, utafunga sana, utaomba sana na usipate majibu yoyote, lakini tambua majukumu yako kama mkristo na uishi kulingana na ramani uliyopewa mkonono mwako yaani biblia!, na huko huko mbele ya safari ikiwa kuna kitu cha kuongezea au kina mapungufu ndipo Bwana atakuambia rekebisha hapa au rekebisha pale.
Kwamfano kama mkristo unajua kabisa tunapaswa kumzalia Mungu matunda ya aina zote (yaani ya haki na ya kazi), sasa tusisubirie kumngojea Mungu atuambie tukawashuhudie wengine waje kwake Hilo hutakaa ulisikie, Kwasababu Mungu anataka tuifanye kazi yake kwa uhuru..Hivyo tumia uhuru uliopewa kuifanya kazi ya Mungu pale ulipo kabla siku zako hazijaisha hapa duniani…Wapo wengi wanahitaji kumjua Mungu kama wewe ulivyo, lakini ukisubiria uone maono, hutafika popote.
2Wakorintho 3:17 Basi ‘Bwana’ ndiye Roho; walakini alipo Roho wa Bwana, hapo ndipo penye uhuru.
Hizi ni siku za mwisho, Bwana wetu yupo mlangoni kurudi, hivyo tuzidi kuongeza nguvu katika kumtafuta yeye.
Bwana akubariki.
Mada Nyinginezo:
HATARI YA KUTOKUITAFAKARI BIBLIA VIZURI?
KWANINI BWANA YESU ALISEMA PALE MSALABANI NAONA KIU?
BIBLIA INAMAANA GANI KUSEMA “VILIVYOTAKASWA NA MUNGU, USIVIITE WEWE NAJISI”?
About the author