Jina la Mfalme Mkuu Yesu Kristo libarikiwe. Karibu tujifunze maneno yake ambayo ni mwanga wa njia zetu, na taa iongozayo miguu yetu (Zab. 119:105)
Leo tutajifunza kwa ufupi, umuhimu wa kutubu dhambi kabla ya kumaliza haya maisha, yapo mafundisho mengi yanayohubiri kuwepo kwa nafasi ya pili ya kusamehewa moto wa milele baada ya kufa…Miongoni mwa mafundisho hayo ni mafundisho ya kupitia Toharani. Lengo kuu la mafundisho haya ni kuwapa watu wanaoishi katika dhambi matumaini kwamba hata wakifa katika dhambi zao bado watakuwa na nafasi ya kutolewa kwenye mateso hayo ya milele na kuingia paradiso, na maombi ya watakatifu waliopo duniani yanaweza kupunguza mateso ya kule.
Haya ni moja ya mafundisho ya shetani yaliyobuniwa kuzimu kwa ujuzi wa hali ya juu yanayowapa watu matumaini na faraja za uongo…shetani anajua watu wanapenda faraja….Alijua Hawa anapenda faraja ndio maana uongo wa kwanza alioutumia ni uongo wa faraja…alimwambia Hawa kwamba “hakika hamtakufa” wakati Bwana alishawaambia wakila tu “watakufa”
Hivyo shetani ni Yule Yule aliyoyatumia Edeni kuwaangusha watu wa kwanza kuumbwa (Adamu na Hawa) ndio hayo hayo anayoyatumia kuwaangusha watu siku za mwisho (yaani mimi na wewe) hivyo tusipokuwa makini kidogo tu! Ni rahisi kwenda na maji!
Mahubiri ya Toharani yatawafanya watu wengi sana wajute siku ile, watakapokwenda huko na kugundua kuwa hakuna kitu kama hicho cha kupata nafasi ya pili. Walidanganywa!
Hebu chukua muda kutafakari kwa Makini sana mstari ufuatao ambao Bwana Yesu aliusema kisha useme mwenyewe kama kweli kutakuwa na nafasi ya pili..
Yohana 8:24 “Kwa hiyo naliwaambieni ya kwamba mtakufa katika dhambi zenu; kwa sababu msiposadiki ya kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu”.
Itafakari hiyo sentensi kwa makini, usiisome tu juu juu kwa mazoea, kwamba ulishawahi kuusoma huo mstari na hivyo huwezi kuurudia tena, hebu ingia ndani zaidi kuutafakari!…Bwana Yesu anasema msiposadiki kuwa mimi ndiye, mtakufa katika dhambi zenu…Ikiwa na maana kuwa kuna tatizo “katika kufa ukiwa na dhambi”…Hiyo ndiyo maana yake!…Na madhara hayo ni baada ya kifo! Kwamba mtu akifa mifupa itakwenda kuchimbiwa kaburini, nguo zitachimbiwa, ardhini nyama ya mwili wake itachimbiwa na kuoza lakini dhambi zake alizonazo atavuka nazo upande wa pili…Na hivyo hiyo dhambi inapaswa ichujwe kabla ya kifo, iachwe hapa hapa duniani..kwasababu ukivuka nayo kule hakuna nafasi tena ya kuitua.
Ingekuwa hakuna tatizo katika kufa ukiwa na dhambi na kwamba kuna nafasi nyingine ya kuokoka ukiwa kule…Bwana Yesu asingesema hivyo…jiulize sana kwanini ahusishe “kifo” na “dhambi” maana yake ukishakufa na dhambi ndio basi tena…ndio maana alikuwa anakazana kuwaambia watubu kabla ya kufa! Kwasababu hakuna tena toba, wala injili baada ya kifo..kinachofuata baada ya hapo ni hukumu..
Ndugu Kama ulikuwa unaamini hivyo kwamba kuna nafasi ya pili ya kuokoka baada ya kifo, ambayo mafundisho haya yanafundishwa sana katika kanisa Katoliki au pengine ulisikia kwa mchungaji wako au kiongozi wako wa dini..fahamu kuwa ulidanganywa! Kama tu Hawa alivyodanganywa kwamba hatakufa!…Umesoma mwenyewe maneno ya Bwana Yesu hapo juu, jinsi alivyokuwa anakazana kuwafanya watu wamwamini kabla ya kufa… na wewe kama hutatubu leo na kumwamini Bwana Yesu utakufa katika dhambi zako..Na baada ya kifo ni hukumu!, kama ni mlevi, mwasherati, mtukanaji, mfanyaji masturbation, mtazamaji wa picha za uchafu, mlawiti, msagaji, msengenyaji, mtoaji mimba, mvaaji mavazi ya kikahaba n.k ukifa leo bila kutubu…utakwenda jehanamu! Hakuna nafasi ya pili…
Bwana anatuonya hapo juu! Kwamba tusipomwamini tutakufa katika dhambi zetu! Je! Na wewe unataka kufa katika dhambi zako? Kama sio basi ni vema ukakata shauri leo la kumgeukia Bwana Yesu, akusafishe dhambi zako na akuoshe kabisa…unachotakiwa kufanya ni kutii msukumo uliopo ndani yako unaokusukuma kuacha dhambi na kumgeukia mwokozi, ujumbe huu unaweza ukawa ni wa kwako kukubadilisha ..
Hivyo unautii huo wito kwa kuamua kwa dhati kwamba kuanzia leo mimi na dhambi basiii, disko ndio mwisho leo, kuchat chat ovyo katika mitandao kwenye vitu visivyo na maana ndio mwisho, kutukana ndio mwisho, kusikiliza miziki ya kidunia ndio mwisho, na unaifuta yote sasahivi bila kuacha wimbo hata mmoja, na unakata kila mnyororo, unasema mimi na uasherati basi, na wale wanawake au wanaume unaotembea nao sasa inatosha, unawapigia simu na kuwaeleza maamuzi yako, na unawaacha kabisa…na unachukua msalaba wako unamfuata Yesu wewe kama wewe..
Baada ya hapo ile nguvu ya Roho itakuvaa itakayokuwezesha kutokutamani hayo mambo tena…utakuwa hujilazimishi kujizua kutukana, au kuiba, au kuzini, n.k itakuwa ni kitu kinachotoka ndani chenyewe (kama vile usivyotumia nguvu yoyote kusukuma damu kwenye moyo wako)…na utaona amani Fulani ya ajabu imekuingia Ukiona hali kama hiyo imekuja ndani yako fahamu kuwa ni Roho Mtakatifu huyo..Lakini ukikaidi sauti yake na kuendelea na ulimwengu huu wa kitambo utakufa katika dhambi zako na hakutakuwa na nafasi ya pili tena huko uendako. jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Bwana akubariki sana, Tafadhali share na wengine
Mada Nyinginezo:
Kati ya Unyakuo,dhiki kuu, utawala wa miaka 1000 kipi kinaanza
About the author