Title April 2020

OLE WA NCHI NA BAHARI.

Ufunuo 12:12 “Kwa hiyo shangilieni, enyi mbingu, nanyi mkaao humo. Ole wa nchi na bahari! Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu.

13 Na joka yule alipoona ya kuwa ametupwa katika nchi, alimwudhi mwanamke yule aliyemzaa mtoto mwanamume.

14 Mwanamke yule akapewa mabawa mawili ya tai yule mkubwa, ili aruke, aende zake nyikani hata mahali pake, hapo alishwapo kwa wakati na nyakati na nusu ya wakati, mbali na nyoka huyo.

15 Nyoka akatoa katika kinywa chake, nyuma ya huyo mwanamke, maji kama mto, amfanye kuchukuliwa na mto ule.

16 Nchi ikamsaidia mwanamke; nchi ikafunua kinywa chake, ikaumeza mto ule alioutoa yule joka katika kinywa chake.

17 Joka akamkasirikia yule mwanamke, akaenda zake afanye vita juu ya wazao wake waliosalia, wazishikao amri za Mungu, na kuwa na ushuhuda wa Yesu; naye akasimama JUU YA MCHANGA WA BAHARI”.

Shalom, Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe, kama ukisoma mistari iliyotangulia kabla ya hiyo, utaona kuwa shetani kuna majira alijaribu kufanya vita katika mbingu, lakini alishindwa kama biblia inavyotuambia akatupwa chini na mahali pake hapakuonekana tena mbinguni kuanzia huo wakati.

Lakini biblia inatuambia pia alipotupwa, hakukaa katika eneo la nchi peke yake, au hakwenda baharini moja kwa moja , hapana, bali alikwenda kusimama juu ya mchanga wa bahari….Kwa namna nyingine alikwenda kusimama ufukweni mahali ambapo nchi na bahari vinakutana.

Shetani alifahamu kuwa, hivyo ndivyo vitu viwili vinavyoikamilisha dunia, hakuegemea tu upande mmoja afanye makao yake huo hapana..badala yake alisimama pale ufukweni ili aweze kuyaona na kuyatawala yale yanayotoka katika nchi na yale yanayotoka katika bahari. Na ndio maana baada ya pale biblia inasema “Ole wa nchi na bahari”, Kwa maana yule Ibilisi ameshuka kwenu mwenye ghadhabu nyingi, akijua ya kuwa ana wakati mchache tu..

Unaona? haituambii nchi tu peke yake, au bahari peke yake, hapana bali vyote viwili, kwasababu ndipo alipopania kuwanasa wanadamu.

SASA NCHI NA BAHARI KIBIBLIA VINAWAKILISHA NINI?

BAHARI: au sehemu yenye maji mengi, biblia imeshatupa majibu yake,.Tusome.

Ufunuo 17:15 “Kisha akaniambia, Yale maji uliyoyaona, hapo aketipo yule kahaba, ni jamaa na makutano na mataifa na lugha”.

Kumbe maji yanawakilisha jamaa, na makutano na mataifa na lugha…Yaani kwa ufupi watu wengi.

Vilevile, tunaweza kuona jambo lingine, pale Bwana Yesu alipochagua mitume wake, wengi wao aliwachagua kutoka katikakati ya wavuvi, akifunua kuwa watakuja kufanya kazi ya uvuvi wa watu wengi, yaani jamaa, na mataifa la Lugha, kama alivyomwambia Petro na Andrea katika (Mathayo 4:19)..

Hivyo Bahari inawakalisha watu wengi, kwahiyo shetani tangu alipoona ameshindwa hawezi tena kupigana yeye kama yeye aliamua sasa kuelekeza macho yake katikati ya watu ili apate nguvu, na chombo kikubwa anachokitumia ili kupata ufuasi mkubwa wa watu ni kupitia kitu kinachoitwa DINI, penye dini ndipo palipo na watu wengi, sio katika siasa au makabila..

Hivyo mpaka sasa yupo katika kilele cha kuzikutanisha dini zote na madhehebu yake yote ambayo tangu zamani yalishautupilia mbali uongozo wa Roho Mtakatifu na kufuata mapokeo yao ya kibinadamu, ili zikubaliane katika kitu kimoja.

Na ndio maana ukisoma ile sura inayofuata ya 13, utaona Yule joka aliposimama tu pale kwenye mchanga wa bahari, wakati huo huo wanyama wawili walitokea, mmoja alitokea baharini, na mwingine akatokea nchi kavu (Soma ufunuo sura ya 13 yote utaona)..Sasa Yule aliyetokea habarini ndiyo huyu atakayepata nguvu ya kuwa na wafuasi wengi sana duniani kwa kupitia dini…

NCHI: NI Hifadhi ya kimwili, tangu mwanzo, Mungu alipomuumba Adamu alimpa ardhi ailime na kuitunza kwasababu huko ndipo alipomchipulia chakula chake kitakachomfanya aishi hapa duniani.

Ayubu 28:5 “Katika ardhi ndimo kitokeamo chakula;…”..

Hata sasa chakula na utajiri vipo katika ardhi..Hivyo kwa lugha ya sasa nchi tunaweza kusema inawakilisha Uchumi,..Fedha, biashara, hazina, vitu vinavyoweza kumpatia mwanadamu Rizki ili aishi hapa duniani n.k…

Kwahiyo shetani kuona hivyo, alisimama pia katika eneo hilo.. tangu huo wakati akajikita kudhibiti mihimili hiyo miwili mikuu, Watu, na uchumi.. nchi na bahari..

Kwanza Ili awapate Watu anatumia kivuli cha dini, ambapo hivi karibu anaenda kutimiza adhma yake ya kuzileta dini zote zilizopoteza uongozo wa Roho Mtakatifu pamoja, zikiongozwa na ile dini mama ya Rumi, na cha ajabu biblia inatuambia watu wote na mataifa yote ambao majina yao hayakuandikwa katika kitabu cha uzima cha mwanakondoo tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu wataufurahia huo utawala na mfumo mzima wa ibilisi ..

Na sasa ili kuwalazimisha watu wote waufuate huo mfumo wa mpinga-Kristo, shetani atamnyanyua mnyama mwingine ambaye atakuwa na nguvu ya kiuchumi sana,(taifa kubwa) ambalo hilo litayahimiza mataifa mengine yote yapokee maagizo kutoka kwa huo umoja wa dini duniani, na mtu yoyote atakayekataa kuupokea hataruhusiwa kununua wala kuuza, wala kufanya biashara yoyote, wala kuajiriwa mahali popote.. Unaona Jinsi hali itakavyokuwa mbaya.. Ni nani atapona hapo.

Haya ni mambo ambayo tunaweza kuyashuhudia siku za hivi karibuni wala tusidhani bado miaka mingi, jaribu kufikiria jinsi ugonjwa huu wa Corona ulivyozuka tu ghafla, na athari yake ndogo tu inawafanya watu wasiweze kutembea hata nje katika baadhi ya nchi, na imetokea tu ndani ya kipindi kifupi cha miezi mitatu tu, hakuna ambaye angeamini kuwa dunia ingeweza kuwa namna hii, dunia ambayo inashamra shamra za kila namna..Lakini mambo yamekuwa hivyo barabara zipo wazi..Hata matajiri na wana wa wafalme, na watu mashuhuri na fedha zao haziwasaidii wakati huu. Ndivyo mambo yatakavyobadilika ghafla tu wakati huo ukifika.

Shetani ameshajidhatiti vya kutosha, na ghafla tu, dini zote zitafikia muafaka mmoja zikiongozwa na dini ile mama ya Rumi, watafikia muafaka mmoja, watapata sapoti kutoka katika kila pembe ya dunia, watakuwa na kiongozi wao mmoja ambaye ndio atakuwa mpinga-Kristo..Huyo ataishawishi dunia iwe na ustaarabu mpya, Lakini lengo lake ni kuihimiza ile chapa ya mnyama ili awanase wanadamu wote.. Sasa kwa kuwa yeye amejikita katika masuala ya kiimani sana, kama tulivyosema atapata msaada mwingine kutoka katika taifa lenye nguvu ya kiuchumi duniani, ili kuyalazimisha mataifa mengine yote yamtii yeye kwa shuruti.

Mpaka wakati huo umefika ujue unyakuo tayari umeshapita ndugu yangu, sijui utakula nini wewe unayemkataa Yesu leo, wewe ambaye utakuwepo ulimwenguni wakati huo, pona yako itakuwa ni kufia njaa ndani, kama utakuwa hujakamatwa na kuuliwa kwa mateso yasiyokuwa ya kawaida.. Hakuna mtu yoyote atayevumiliwa na mtu au chombo chochote cha dola ambaye ataonekana hajapokea chapa hiyo ya mnyama.. usifikiri utapona..Ni ngumu sana ndugu, usidhani akaunti yako ya benki itakusaidia wakati huo, hilo jambo halitakuwepo, usidhani utakimbilia mafichoni, ondoa hayo mawazo, usidhani elimu yako itakusaidia kupata ajira wakati huo, acha kufikiria hivyo..Chapa utaipokea tu.

Hizi ni nyakati za hatari tunazoishi, ole wa nchi na bahari!…Kimbilio pekee ni Kristo tu saa hii..Ikiwa upo bado nje ya Kristo, basi fanya uamuzi wa Busara leo hii, tubu dhambi zako kwa kumaanisha kuziacha, omba toba kwa Mungu, nenda kabatizwe ikiwa bado hujafanya hivyo. huu ni wakati sasa wa kuamka usingizini.

Warumi 13:11 “Naam, tukiujua wakati, kwamba saa ya kuamka katika usingizi imekwisha kuwadia; kwa maana sasa wokovu wetu u karibu nasi kuliko tulipoanza kuamini”.

Bwana akubariki sana.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

UFUNUO: Mlango wa 13

UCHAWI WA BALAAMU.

CHUKIZO LA UHARIBIFU

DANIELI: Mlango wa 7

MWISHO WA DUNIA UTAKUJAJE?

Nini maana ya “Siku moja nyuani mwa Bwana ni bora kuliko miaka elfu”?

Rudi Nyumbani:

Print this post

UCHAWI WA BALAAMU.

Hesabu 23:23 “Hakika hapana uchawi juu ya Yakobo, Wala hapana uganga juu ya Israeli”

Wengi tunalifahamu hili andiko na tunalitumia, pale tunapohisi roho za kichawi zinatunyemelea…Na tunapolitumia kwa Imani linaleta majibu hakika kwasababu ni pumzi ya Mungu…Lakini hebu leo tuingie kwa undani kidogo kujifunza juu ya Neno hili ili tupate faida mara mbili Zaidi.

Siku zote tunashauriwa tujifunze biblia na sio tuisome tu…tukichukua tu kipengele cha mstari wa biblia na kukitumia hicho bila kutafuta maana ya mstari huo, kwanini mwandishi aliandika hivyo, na Mungu alikuwa anamaanisha nini juu ya mstari huo..hapo tutakuwa hatujajifunza bali tumesoma tu..ambapo matokeo yake ni madogo kuliko kama tungeketi chini na kujifunza kuanzia juu chanzo cha mstari huo na dhima, na maudhui ya huo mstari ukoje.

Sasa tukirudi katika mstari huo hapo juu, kama ukianza kusoma kitabu hicho cha Hesabu kuanzia sura zilizotangulia kabla ya hiyo ya 23, utaona inahusu safari ya wana wa Israeli (au wana wa Yakobo), walipokuwa wanatoka Misri kuelekea nchi yao ya Ahadi,

Wakiwa njiani jangwani walikutana na kikwazo, Ilikuwa kwamba ili waendelee na safari yao iliwapasa wakatize katika nchi ya watu fulani ambao walijulikana kama wamoabu.

Nchi hiyo ilikuwa na mfalme na huyo mfalme akawakatalia wasikatize katika nchi hiyo, na hakukuwa na njia nyingine ya karibu isipokuwa kukatiza katika nchi hiyo..Ijapokuwa waliwaomba sana na kuwaahidi kwamba watalipia gharama zote za uharibifu wowote kama ukijitokeza katika kukatiza kwao lakini wenyeji wa mji ule walikataa katakata wakiongozwa na mfalme wao..Na kwa hofu Mfalme wao hakuishia tu kuwazuia bali alipanga pia kwenda kupigana nao, hivyo akatafuta pia namna ya kuwalaani(au kwa lugha rahisi kuwaloga) ili atakapokwenda kupigana nao aweze kuwashinda kirahisi bila kutumia nguvu nyingi.

Katika harakati za kutafuta mtu mashuhuri wa kuloga, akampata mtu anayeitwa Balaamu mchawi (Hesabu 24:1), huyu alikuwa ni mchawi wa viwango vya juu sana na aliyejulikana kwa kuloga hata mataifa, ambaye alitumia nguvu za giza, na alikuwa anauwezo wa kuisikia pia sauti ya Mungu..na kabla ya kuloga alikuwa anauwezo wa kupima kiwango cha kiroho mtu alichopo kabla ya kumwangusha…na sio hilo tu, alikuwa anazo mpaka mbinu mbadala zisizo za kuweza kumwangusha mtu bila kutumia uchawi wowote…(na huo ndio mbaya Zaidi ambao ndio alioutumia kuwaangusha wana wa Israeli).

Sasa alipoitwa kama wengi wetu tunavyoijua habari…haraka sana aliwajua wana wa Israeli ni watu gani…alijua ni watu wa Mungu na wamezungukwa na ukingo wa Mungu pande zote…hakuna namna ya kuweza kuwaingia kwa njia ya uganga wala uchawi (hakuna namna yoyote vibuyu na dawa za miti shamba zinaweza kufanya kazi juu yao)..hata hivyo alinusurika kifo njiani wakati anajaribu kutaka kwenda kuwalaani…Ili litimie lile neno la kwanza (akulaaniye atalaaniwa, na akubarikiye atabarikiwa).

Hivyo Balaamu alilijua hilo na alipofika kwa mfalme wa MOABU akamwambia wazi kabisa kwamba “HAKIKA HAPANA UCHAWI JUU YA YAKOBO, WALA HAPANA UGANGA JUU YA ISRAELI”.

Hiyo ndiyo asili ya Neno hilo…Ni mchawi Balaamu ndiye aliyeyasema maneno hayo sio Mungu kama wengi wetu tunavyodhani. Balaamu alikiri kabisa..Hivyo akaacha kujaribu kuwaloga/kuwalaani Israeli ambaye ndiye Yakobo, kinyume chake akawabariki, kwasababu alijua endapo angetaka kuwaalaani ni kujitafutia laana na kifo..hivyo akaamua kuhamia kwenye Mbinu yake ya pili ambayo ndiyo KUBWA NA KUU.

Hesabu 24:1 “Basi Balaamu alipoona ya kuwa ilimpendeza Bwana kuwabariki Israeli, hakwenda, kama hapo kwanza, ili kutafuta uchawi, bali alielekeza uso wake jangwani”

Mbinu hiyo siyo ya kutumia vitunguli tena/wala vibuyu/ wala ya kuwatamkia maneno mabaya..Mbinu hii ya pili ambayo ndio UCHAWI HASAA ni ya kuwakosesha wana wa Israeli na Mungu wao..Ili Mungu awakasirikie na kuwaadhibu yeye mwenyewe…kwasababu kuwaangusha kwa njia ya uchawi imeshindikana sasa dawa ni kuwachonganisha na Mungu wao..Hivyo akamfundisha Mfalme wa Moabu namna ya kuwakosesha wana wa Israeli ili wapigwe na Mungu wao..

Akamfundisha na kumwambia wawaalike wana wa Israeli baadhi katika sadaka za miungu yao na kuwapa wanawake wao walio wazuri na warembo, hivyo Wana wa Israeli watakapoona hivyo wataingia tamaa na kuzini na wanawake hao katika karamu hizo za miungu na hasira ya Mungu itawaka juu ya wana wa Israeli..Tusome

Hesabu 25:1 “Basi Israeli akakaa Shitimu, kisha watu wakaanza kuzini pamoja na wanawake wa Moabu;

2 kwa kuwa waliwaalika hao watu waende sadakani, sadaka walizowachinjia miungu yao; watu wakala chakula, wakaisujudu hiyo miungu yao.

3 Ikawa Israeli kujiungamanisha na Baal-peori; hasira za Bwana zikawaka juu ya Israeli”.

Ukiendelea kusoma utaona Mungu aliwakasirikia na aliwaua kwa pigo watu elfu 24. Kama sio mtu mmoja kwenda kurekebisha Israeli wote wangeisha siku hiyo mbele ya ghadhabu ya Mungu..Hivyo japokuwa Yule mchawi balaamu hakuwaloga kwa uchawi wa uganga na vibuyu lakini aliwaloga kwa kuwakosesha na Mungu wao.

Jambo hilo hilo linaendelea hata sasa katika nyakati hizi za agano jipya. Ni kweli hakuna uganga wala uchawi juu yako, umelindwa na kuzungukwa na kingo za moto pande zote, katika afya yako, katika kazi zako, katika familia yako, mpaka una ujasiri wa kusema Bwana ndiye anisaidiaye sitaogopa mabaya, wala uchawi wala uganga..Ndio shetani analijua hilo na wala hawezi kukuloga kwa vitunguli, wanaokuendea kwa waganga ni kweli wanapoteza muda..nataka nikuambie shetani akishalijua hilo wala hapotezi muda wake kukutumia watu kutafuta kukuloga wewe…kwasababu hawezi kulaani kilichobarikiwa…hviyo acha kufikiri kwamba wachawi wanakuwinda wewe uliyeokoka kweli kweli, walishaacha siku nyingi wakati ule walipogundua tu unazungukwa na jeshi la mbinguni…

Shetani anachofanya sasa juu yako ni kutafuta njia ya kukukosesha wewe na Mungu wako, ili Mungu akuadhibu…na anatumia watu mfano wa Balaamu..wanaoonekana nje ni watu wa Mungu kumbe ndani ni mbwa-mwitu wa kali…Hao watakwambia kuoa mke wa pili si dhambi, watakwambia kuziangukia sanamu na kuzibusu na kuzipa heshima sio kuzisujudia.

Na biblia imeshatabiri nyakati hizi za mwisho watu wengi wataangukia katika kosa hili la Balaamu..

Yuda 1:11 “Ole wao! Kwa sababu walikwenda katika njia ya Kaini, na kulifuata kosa la Balaamu pasipo kujizuia, kwa ajili ya ujira, nao wameangamia katika maasi ya Kora”.

Watakwambia kufanya matambiko ya ukoo sio dhambi, watakuwambia kuishi na mwanamke/mwanamume ambaye hamjaoana hakuna tatizo, watakuwambia kuzini ni mapungufu ya kila mtu, watakuweka katika kila kishawishi cha wewe kufanya dhambi, , Zaidi sana watakufariji katika dhambi na watakukemea katika kuwa mtakatifu…lengo na madhumuni ni kukukosesha wewe na Mungu wako ili Mungu akukasirikie na kukuangamiza (Huo ndio uchawi mkubwa shetani anaowalogea watu wa Mungu kuliko hata ule wa vibuyu)..

Bwana Yesu alisema maneno hayo Dhahiri katika Ufunuo.

Ufunuo 2:14 “Lakini ninayo maneno machache juu yako, kwa kuwa unao huko watu washikao mafundisho ya Balaamu, yeye aliyemfundisha Balaki atie ukwazo mbele ya Waisraeli, kwamba wavile vitu vilivyotolewa sadaka kwa sanamu, na kuzini”.

Je! Na wewe umedanganyika na uchawi huo wa Balaamu? Nabii wa uongo?..Unadhani shetani anahangaika na bati lako usiku na kundi lake la wachawi?..usidanganyike!..anahangaika sasa kukukosesha na Mungu wako. Hataki ulifahamu neno na anafanya juu chini ufe katika dhambi zako ili siku ile uingia katika adhabu ya hasira ya Mungu katika ziwa la moto. Hivyo mwache aende peke yake huko yeye na mabalaamu wake, sisi tujitenge na yeye kwa kutubu leo na kushika amri za Mungu na Neno lake, kwa kujitenga na uasherati wote, wizi, rushwa, anasa, tamaa mbaya, wivu, matusi, na mambo yote machafu na kuzidi kujitakasa kila siku, na kuishi katika utakatifu ndipo tutakapojiepusha na ghadhabu ya Mungu na kupata baraka zote alizozikusudia katika Maisha yetu. Hatuna haja ya kuogopa wachawi wa vibuyu kwasababu huko waliko wanakiri kwamba hakuna uchawi wala uganga kwa waliokoka..

Sisi tupambane kujilinda na dhambi ndilo jukumu tulilolonalo sasa.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

KIFO CHA MTAKATIFU PERPETUA NA FELISTA.

WAKAMTUKANA MUNGU, WALA HAWAKUTUBU.

NENO NI LILE LILE, LAKINI UJUMBE NI TOFAUTI.

VITABU VYA BIBLIA: Sehemu ya 2

JINA LA MUNGU NI LIPI?

Rudi Nyumbani:

Print this post