Title 2020

MKESHA WA KUINGIA MWAKA MPYA KILA MWAKA NI WA KUUTHAMINI SANA.

Leo  tutaona kibiblia ni kwanini uuthamini mkesha wako wa kuingia mwaka mpya. Wengi wetu tunapuuzia, tunaona ni jambo la kawaida tu, na hivyo tunautumia msimu huu pengine kulala, au kwenda kufanya anasa, au kwenda kufanya part na ndugu au marafiki n.k.. Ni heri upange kwenda kusheherekea nao siku inayofuata kuliko siku ya mkesha wa kuukaribisha mwaka mpya.

Lipo jambo kubwa sana la kiroho katika usiku wa siku hiyo.

Ukisoma biblia utaona Mungu alipokuwa anawatoa wana wa Israeli Misri, siku hiyo  kwao ndio ilikuwa siku ya kwanza ya mwaka wao mpya.. Lakini utaona Mungu hakuwatoa mchana, au jioni, au alasiri bali aliwatoa usiku wa manane,  Sio kwamba mchana wasingeweza kusafiri, hapana, lakini siku ya kutengwa na maadui zako, na siku ya kuukaribisha mwaka mpya sikuzote ni lazima maandalizi yaanzie angali bado kuna giza nene.

Utasoma usiku ule kabla ya kuamkia tarehe moja, walimla yule pasaka(mwanakondoo), wakiwa wamevaa viatu vyao chini, kiashirio kuwa wapo mbali na vitanda vyao, na huku wamefunga mikanda yao viunoni, kuashirio kuwa wapo tayari kwa safari, kisha wamejifungia ndani wakimtafakari Mungu na kumwimbia, wakisubiria tu muda ufike wa kuondoka..

Kutoka 12: 11 “Tena mtamla hivi; mtakuwa mmefungwa viuno vyenu, mmevaa viatu vyenu miguuni, na fimbo zenu mikononi mwenu; nanyi mtamla kwa haraka; ni pasaka ya Bwana.

12 MAANA NITAPITA KATI YA NCHI YA MISRI USIKU HUO, NAMI nitawapiga wazaliwa wa kwanza wote katika nchi ya Misri, wa mwanadamu na wa mnyama; nami nitafanya hukumu juu ya miungu yote ya Misri; Mimi ndimi Bwana”.

Kwasababu walifahamu wanaingia katika mwaka wao mpya wa kufanywa huru mbali na maadui zao. Sasa embu fikiria kama wangekuwa wamelala, halafu asubuhi ndio wanaamka watake kuondoka Misri, hali  ingekuwaje? Ni wazi wasingetoka kwa ushindi mnono kama walivyotarajia.

Vivyo hivyo na sisi, siku kama ya leo, ndio tunavuka kuingia mwaka mpya. Usiku ambao tunayaacha mambo ya mwaka huu, na kuyakaribisha mambo ya mwaka mwingine mpya, Hivyo kama tunataka  Mungu ampige adui yetu shetani kwelikweli, ili mwaka wetu mpya tunapouanza uwe wa kuwa huru, na wa Baraka nyingi na wa mafanikio, hatuna budi leo kukesha nyumbani mwake, katika kuomba, kumwabudu na kumfanyia ibada.

Yaani tarehe moja ya mwaka mpya isikukute upo kitandani, isikukute unaangalia MUVI, isikukute unacheza gemu, isikukute unazurura zurura mtaani, isikukute unapiga piga stori na marafiki zako n.k., bali ikukute nyumbani mwa Bwana unamshukuru na kumtukuza.

Hata kama upo katika nchi ambazo, ibada zimekatazwa makanisani, bado unayo nafasi ya kujifungia mwenyewe nyumbani na familia yako ukawa unaomba na kumshukuru Mungu, kama wana wa Israeli walivyofanya. Hakikisha kuwa mwaka wako mpya unaukaribisha ukiwa macho kwa Bwana.

Itakuwa ni ajabu sana, kama mwaka huu utashindwa kumshukuru Mungu kwa wema wake aliokutendea mwaka mzima..Wewe mwenyewe unajua mambo tuliyoyapitia mwaka huu jinsi yalivyokuwa mazito , lakini umepewa neema ya kuyavuka, ujue sio kwa nguvu zako,wala fedha zako, wala afya yako wala chochote ulicho nacho.

Hivyo utumie mkesha huu, vema kwasababu hakutakuwepo tena na mwingine kama huu, kwa miezi mingine 12 ijayo. Bwana akubariki

Pia wakumbushe na wengine, jambo hilo. Na shea kwa wengine.

Mwisho kabisa, nikutakie HERI YA MWAKA MPYA WENYE MAFANIKIO YOTE YA MWILINI NA ROHONI KATIKA JINA LA BWANA YESU KRISTO.

AMEN.

Mawasiliano/ Whatsapp: +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NAKUTAKIA HERI YA MWAKA MPYA!

UNAMALIZAJE MWAKA WAKO, JE NA MUNGU AU SHETANI?

NJIA MUNGU ALIYOIWEKA KWA KILA JAMBO:

THAWABU ZA SIRI, ZA WATAKATIFU MBINGUNI.

Rudi nyumbani

Print this post

IFAHAMU HUZUNI NA FURAHA YA MALAIKA.

Shalom, karibu tena tuyatafakari maneno ya Bwana wetu Yesu, biblia inasema manabii wengi na wenye hekima walitamani sana kusikia tunayoyasikia na kuyaona tunayoyaona lakini hawakupata neema hiyo, Lakini mimi na wewe tumepewa neema ya kuyasikia maneno ya Bwana wetu Yesu. Ni furaha iliyoje?

Yesu ambaye aliiumba dunia kwa Neno lake, leo hii inakaa na sisi kutufundisha hilo hilo Neno lake, unadhani ni rahisi sisi kuacha kuyatafakari maneno yake kwa kuyarudia rudia kila siku? Tutafanya hivyo kwa msaada wake.

Leo tuutafakari tena kwa pamoja mfano huu alioutoa. Unaweza ukawa umeusoma mara 100, lakini tuutafakari tena, Neno la Bwana huwa haliishi ubora.

Luka 15:3 “Akawaambia mfano huu, akisema,

4 Ni nani kwenu, mwenye kondoo mia, akipotewa na mmojawapo, asiyewaacha wale tisini na kenda nyikani, aende akamtafute yule aliyepotea hata amwone?

5 Naye akiisha kumwona, humweka mabegani pake akifurahi.

6 Na afikapo nyumbani kwake, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimekwisha kumpata kondoo wangu aliyepotea.

7 Nawaambia, Vivyo hivyo kutakuwa na furaha mbinguni kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye, kuliko kwa ajili ya wenye haki tisini na kenda ambao hawana haja ya kutubu.

8 Au kuna mwanamke gani mwenye shilingi kumi, akipotewa na moja, asiyewasha taa na kufagia nyumba, na kutafuta kwa bidii hata aione?

9 Na akiisha kuiona, huwaita rafiki zake na jirani zake, akawaambia, Furahini pamoja nami, kwa kuwa nimeipata tena shilingi ile iliyonipotea.

10 Nawaambia, Vivyo hivyo kuna furaha mbele ya malaika wa Mungu kwa ajili ya mwenye dhambi mmoja atubuye”.

Katika maneno hayo, tunaweza kujifunza jambo moja, kwa hawa watu wawili, kwanza, furaha yao haijaja katika kukipata kitu kipya, bali ni katika kitu kile kile cha zamani walichokuwa nacho.  Lingekuwa ni jambo la heri kama wangekuwa wamezalisha kitu jipya na kwa hicho kikawapatia faida, hapo ndio tungesema furaha yao inamaana, lakini tunaona ni vilevile walivyokuwa navyo hapo mwanzo ndivyo wanavyovifurahia.

Furaha hii sio ya kawaida, bali ni furaha inayojificha ndani ya uthamani wa kitu. Inazuka pale kitu hicho kinapoathiriwa na kupata suluhisho.

Furaha ya namna hii inaweza kujengeka hata kwako, kwamfano unaweza ukawa na simu yako nzuri, lakini ghafla kibaka akapita mbele yako akakupokonya akakimbia nayo..Ni wazi kuwa hilo jambo litakuudhi sana kama sio kukuhuzunisha. Lakini baada ya wiki moja pengine wakati unafikiria labda kwenda kununua simu  nyingine, unashangaa unapigiwa simu na polisi, unaambiwa simu yako tumemshika nayo mtu mmoja mwizi alikuwa anakwenda kuiuza.. Hivyo njoo chukua simu yako.

Ni wazi kuwa taarifa hizo zitauchangamsha moyo wako, na kukufurahisha sana kana kwamba ni jambo fulani la maana sana umelipata, kumbe ni kitu kile kile. Furaha hii inakuja yenyewe tu ndani, haulazimishwi, unasema daah! Afadhali nimeipata simu yangu, asante Mungu. Tena ukikutana na Yule mtu aliyekusaidia utataka hata umpe chochote cha kumpongeza au kumfuta jasho kwa kukuhangaikia.

Sasa huzuni na  furaha ya namna hiyo, ndiyo Mbingu yote na malaika wa Mungu wanayoipitia kila siku, pale mwenye haki mmoja anapoicha imani, mbinguni wanahuzunika, na kukasirika, lakini pale mwenye dhambi aliyeiacha imani anapotubu , Malaika wanamshukuru Mungu,wanasema afadhali fulani kapatikana, siku yao huwa inakwenda vizuri sana, wanamshukuru Mungu sana kwa hilo. Hivyo na sisi tusichoke kuwahubiria wenye dhambi wamgeukie Mungu hata kama hapo mwanzo walikuwa wameokoka wakapotea, Unaweza kudhani wakitubu na kumgeukia Mungu,ndio basi, mbinguni wanalichukulia hilo jambo kawaida tu, fahamu kuwa huko mbinguni ni shangwe tu.

Biblia inatuonyesha hilo jambo huwa linawafurahisha na kuwachangamsha sana malaika. Wapo kondoo wa Mungu wengi sana leo hii wamepotea, wengine wamerudi nyuma, ule moto waliokuwa nao umezima,

Idadi ya wakristo walioacha imani ni kubwa kuliko idadi ya watu ambao hawakuijua imani kabisa kwasasa hivi..tafakari tu mpaka Yesu mwenyewe  anasema mwenye dhambi MMOJA TU, atubupo, hajataka wengi, bali mmoja tu, inaipa furaha mbingu. Itakuwaje wakitubu mia, au mia mbili au elfu, Hivyo kwa pamoja tusimame katika karama zetu, kuwarejesha wale waliopotea katika imani tena, na Bwana atusaidie.

Vilevile ikiwa na wewe unayeusoma ujumbe huu, hapo mwanzo ulikuwa kwa Mungu lakini sasa umeurudia ulimwengu, hapo Mwanzo ulikuwa moto lakini sasa umekuwa baridi tena, fahamu kuwa umemuhuzunisha Mungu sana kwa maamuzi yako hayo mabaya. Mungu anasikitika gharama alizoingia kukukomboa na leo hii unamwacha na kwenda kuunufaisha ulimwengu. Hilo jambo linamsikitisha kweli kweli ndugu, yangu pamoja na malaika wake.

Mungu anataka leo hii umrudie tena, ujumbe huu unakuhusu wewe, mwana mpotevu, leo mrudie muumba wako, hizi ni siku za mwisho, dunia hii haina muda mrefu mpaka iishe, na hata kama bado itakuwepo, wewe hauna garantii ya kuiona kesho.Au unayo? Vifo vinakujaga ghafla tu bila hodi, ziwa la moto halishibi watu, na kila sekunde maelfu ya watu wanashuka huko. Wanajuta kwa majuto ambayo hayaelezeki, mfano wake ni Yule tajiri wa Lazaro, habari yake unaifahamu.

Huko walipo sasahivi wanatamani wewe utii injili uokoke, ili usifike hizo sehemu za mateso walizopo. Dakika moja tu ya uhai uliyopewa, usiichee rafiki yangu, itathamini, shetani anaiwinda roho yako, kwa namna isiyo ya kawaida. Hivyo tubu mgeukie Kristo upokee ondoleo la dhambi. Na yeye mwenyewe atakutia muhuri kwa Roho wake mtakatifu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

Mungu anaposema “nitaliweka jina langu” ana maana gani?

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

OLE WAKO KORAZINI NA BETHSAIDA.

Rudi nyumbani

Print this post

KWANINI UNAPASWA UWE BIBI ARUSI NYAKATI HIZI ZA MAJERUHI?

Shalom, biblia inasema..

Yohana 3:29 “Aliye naye bibi arusi ndiye bwana arusi;..”

Huu ni wakati wa kupigania kwa bidii kuwa bibi arusi wa Kristo kwelikweli, kwasababu kama ukifa leo hii na sio bibi-arusi au unyakuo umekukuta na bado hujafanyika kuwa bibi arusi ujue kuwa unyakuo hautakuhusu hata kidogo, haijalishi utasema mimi ni mkristo wa miaka mingi, hutakwenda popote. kumbuka si wakristo wote ni bibi-arusi, jambo ambalo wengi wetu hatulijui, Wakati huu wa mwisho maandiko yanatuonyesha wazi kuwa kutakuwa na makundi makuu mawili ya watu wanaojiita wakristo.

Na hao wamezungumziwa kwa marefu sana katika kile kitabu cha Mathayo 25, kama wanawali werevu na wapumbavu.  Hao kwa jina lingine ndio wanaojulikana kama bibi arusi na masuria. Suria ni mwanamke aliyetwaliwa tu na kuwekwa ndani, hana mkataba wala urithi wowote kwa mume wake, isipokuwa kupewa tu zawadi na kuondoka,  lakini bibi arusi yeye ni mke, ambaye si tu kupokea zawadi, na urithi, kutoka kwa mume wake, bali pia anakuwa na kitu kingine cha zaida, ambacho leo tutajifunza kwasababu ndio kiini cha somo letu la leo.

Na kitu chenyewe ni “Kufahamu ya sirini ya Bwana wake”. Kama vile tunavyojua mtu pekee anayeweza kumfahamu mtu ndani nje, ni mke wa mtu, au mume wa mtu. Kwasababu watu hawa walishaunganishwa na kuwa mwili mmoja, hivyo usishangae kuona mke au mume anajua mambo mengi ya mwenzi wake kuliko hata ndugu zake alioishi nao kwa miaka mingi tangu utotoni.

Ndivyo ilivyo katika wakati huu wa mwisho. Bwana Yesu analiandaa kundi lake dogo sana, ambalo linajulikana kama bibi-arusi, kumbuka hili sio suria, yaani sio watu tu wanaojiita ni wakristo lakini wanaishi maisha yao ya kidunia wanayoyajua wao, hapana bali ni kundi lingine kabisa. Ambalo tutaona tabia zake kidogo mbeleni.

Sasa Watu hawa ndio Kristo atakaowafunulia  baadhi ya siri ambazo si watu wote watazifahamu. Kwasababu  Biblia inatabiri wakati dunia inakwenda kukaribia kuisha, zipo siri ambazo Mungu alizihifadhi wala hakutaka ziandikwe kwa wazi kwenye biblia, siri hizo atakuja kuwafunulia watu wake.

Ufunuo 10:4 “Hata ngurumo saba zilipotoa sauti zao, nalikuwa tayari kuandika. Nami nalisikia sauti kutoka mbinguni ikisema, YATIE MUHURI MANENO HAYO YALIYONENWA NA HIZO NGURUMO SABA, USIYAANDIKE”.

Kama tunavyosoma hapo, yapo maneno ambayo yalitiwa muhuri, lakini hayakuandikwa.. Yalisikiwa tangu zamani lakini hayakuandikwa. Unaweza ukajiuliza ni kwanini yasiandikwe kama tayari yalishasikiwa? Ni kwasababu sio kila jambo ni la kila mtu. Mengine ni ya siri, ya Kristo na bibi arusi wake tu.

Na siku hizo ambazo siri hizi zitakapomalizika kuachiliwa mioyoni mwa kundi hili dogo la watakatifu, ujue kuwa tayari mstari wa neema umeshavukwa, na makundi mawili yameshajinga.

Hivyo Wakati huu tunaoishi,ni wa kumaanisha sana ndugu yangu, kwasababu ukijidanganya mwenyewe umeokoka, na huku nyuma unafanya matendo yako maovu sirini, kwa kisingizio wewe ni mchungaji, au mwalimu, au mwana kwaya, au nabii n.k…ukweli ni kwamba unajidanganya tu mwenyewe, wala usipoteze  muda wako mwingi kujisiri sitiri. Kwasababu Kristo anawajua walio wake, anamjua bibi arusi wake wa kweli yupoje, tangu kuwekwa misingi ya ulimwengu. Hana mzaha mzaha katika kuchagua.

Na tabia inayomtambulisha Bibi arusi wa kweli ni mataendo yake ya haki (yaani utakatifu). basi

Ufunuo 19:7 “Na tufurahi, tukashangilie, tukampe utukufu wake; kwa kuwa arusi ya Mwana-Kondoo imekuja, na mkewe amejiweka tayari.

8 Naye amepewa kuvikwa kitani nzuri, ing’arayo, safi; KWA MAANA KITANI NZURI HIYO NI MATENDO YA HAKI YA WATAKATIFU”.

Je! Na wewe utakatifu upo ndani yako?. Kama jibu ni hapana, basi anza kutengeneza taa yako sawasawa iwe na mafuta ya kutosha,. Kwasababu Bwana arusi wetu Kristo yupo mlangoni kuja kulinyakua kanisa lake. Na hakuna anayejua itakuwa ni lini, lakini kila dalili inatuonyesha ni hivi karibuni pengine ni leo usiku. Hivyo usiishi maisha ya kubahatisha. Maanisha kweli kumfauta Yesu.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

NA ROHO NA BIBI-ARUSI WASEMA, NJOO!

KARAMU YA MWANA-KONDOO.

UTAWALA WA MIAKA 1000.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

NITAUPATAJE UPENDO WA KI-MUNGU NDANI YANGU?

Rudi nyumbani

Print this post

Chuo cha vita vya Bwana ni kipi?(Hesabu 21:14)

SWALI: Naomba kufahamu hichi “Chuo cha vita vya Bwana” kinachozungumziwa katika Hesabu 21:14  ni kipi?.


Hiki ni moja ya vitabu ambavyo vinatajwa katika biblia lakini leo hii havipo, vinginevyo ikiwemo kitabu cha Yashari,(2Samweli 1:18), Kitabu cha tarehe cha wafalme wa Yuda(1Wafalme 14:29), Kulikuwa pia na  kitabu cha tarehe ya Nathani nabii, halikadhalika kitabu cha tarehe ya Gadi mwonaji, Na kitabu cha tarehe cha Samweli mwonaji, (1Nyakati 29:29); Vitabu hivi vyote havipo kwenye biblia hadi hii leo, japokuwa vimezungumziwa.

Kama vile jina lake linavyojieleza kinadhaniwa kuwa ni kitabu kilichokuwa kinarekodi matukio yote ya vita ambavyo Bwana aliwapigania watu wake, na kuwaokoa kwa mkono mkuu.

Japo, habari zote za kitabu hicho hazijawa wazi hadi leo, ni mambo gani na gani yalizungatiwa kuandikwa ndani yake. Lakini enzi za agano la kale, kitabu hichi kilikuwa ni kitabu maarufu kati ya vitabu vya kihistoria vya kiyahudi.

Habari ya kitabu hichi utaipata sehemu moja tu katika biblia,

Hesabu 21:13 “Kutoka huko wakasafiri, wakapanga upande wa pili wa Arnoni, ulio jangwani, utokao katika mpaka wa Waamori; maana, Arnoni ndio mpaka wa Moabu, kati ya Moabu na Waamori.

14 Kwa hiyo imesemwa katika chuo cha Vita vya Bwana, Wahebu katika Sufa, Na bonde za Arnoni,”

Lakini ni kwanini Mungu hakukiruhusu kiwepo hadi leo?

Kama Biblia ingerekodi matendo yote makuu Mungu aliyowafanyia watu wake tangu kuumbwa kwa ulimwengu hadi sasa, vitabu vyote duniani visingetosha kwa habari zake. Kama tu habari za matukio ya Yesu aliyoyafanya hapa duniani biblia inasema vitabu havitoshi kuelezea itakuwaje yaanzie tangu agano la kale.

Hivyo habari hizo chache zilizoandikwa kwenye biblia, Mungu ameona walau zitamtosha kila mtu azisome na kumsaidia,. Sasa ikiwa tumerahisishiwa habari njema hizi njema, kwa bahari chache sana, halafu tutakataa kusoma, basi hapo tunaonyesha ni jinsi gani tulivyo wavivu.

Ni lazima ujiulize ni kwanini hadi wakati huu uliofikia hujawahi kuisoma biblia yote? Lakini wakati huo huo magazeti uliyoyasoma, pamoja na vitabu shuleni, na mtaani umemaliza hata kurasa milioni 5, lakini biblia hujamaliza. Jiulize tatizo ni nini? Au urahisishiwe nini tena ndio usome.?

Kusoma biblia ni kutia bidii kidogo tu, Paulo alimwambia Timotheo maneno haya;

1Timotheo 4:13 “Hata nitakapokuja, ufanye bidii katika kusoma…”

Hivyo jijengee utaratibu wa kusoma biblia kila siku.

Shalom.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Kitabu cha YASHARI kinachozungumziwa katika 2Samweli 1:17-18, ni kitabu gani?

NGURUMO SABA

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

Pomboo ni nini katika biblia?(Kutoka 25:5, Ezekieli 16:10)

Rudi nyumbani

Print this post

KAMA MKRISTO FAHAMU ZIPO HATUA UTAPIGISHWA NA MUNGU.

Wakati ule Mbingu inafungwa Israeli mvua isinyeshe miaka mitatu na nusu, tunaona Mungu alimwagiza Eliya aende akakae karibu na kijito cha Maji cha Kerithi, anywe maji ya mto ule, na pamoja na hayo, kunguru watatumwa kumletea chakula na nyama asubuhi na jioni.

Lakini tunasoma, upo wakati kijito kile kilikauka.. pengine yeye alidhani ataendelea kufaidika hivyo hivyo kwa muda wote mpaka Mungu atakapoileta tena mvua juu ya nchi, lakini haikuwa hivyo, Ni kweli yalikuwa ni maagizo ya Mungu yeye abaki pale, lakini Mungu hakukusudia abaki pale milele. Ingekuwa labda ni mimi wakati huo naona kijito ambacho Mungu alichoniagiza nikinywee kimekauka mawazo ya kuwa nimeashaachwa na Mungu yangeshaniingia.

Lakini baada ya tukio lile tunaona Mungu akampa maagizo mengine, ya kuelekea Sarepta akalishwe na mwanamke mjane, na sio tena kunguru.

1Wafalme 17: 2 “Neno la Bwana likamjia, kusema,

3 Ondoka hapa, geuka, uende upande wa mashariki, ujifiche karibu na kijito cha Kerithi kinachokabili Yordani.

4 Itakuwa utakunywa maji ya kile kijito; nami nimewaamuru kunguru wakulishe huko.

5 Basi akaenda akafanya kama alivyosema Bwana; kwa kuwa akaenda akakaa karibu na kijito cha Kerithi, kinachokabili Yordani.

6 Kunguru wakamletea mkate na nyama asubuhi, na mkate na nyama jioni, akanywa maji ya kile kijito.

7 Ikawa, baada ya siku kupita, kile kijito kikakatika, kwa sababu mvua haikunyesha katika nchi.

8 Neno la Bwana likamjia, kusema,

9 Ondoka, uende Sarepta, ulio mji wa Sidoni, ukae huko. Tazama, nimemwagiza mwanamke mjane wa huko akulishe.

10 Basi, akaondoka, akaenda Sarepta; hata alipofika langoni pa mji, kumbe! Mwanamke mjane alikuwako akiokota kuni; akamwita, akamwambia, Niletee, nakuomba, maji kidogo chomboni nipate kunywa.

Nachotaka tujifunze leo ni kuwa, ni tabia ya Mungu kutuvusha madarasa, si desturi yake sisi tuendelee katika darasa lile lile la ukristo kwa miaka yetu yote tuliyopo hapa duniani, ni lazima akikatishe kile kimoja, ili afungue mlango wa kutuletea kingine, na anafanya hivyo sio kutukomoa, bali ni kutukuza kiimani, tufikie utimilifu wa yeye anaoutaka kwetu.

Ikiwa wewe ni mkristo wa muda mrefu, utaelewa ninachokisema,ile  neema uliyokuwa unaipata kutoka kwa Mungu wakati unaokoka, sio neema ambayo unatembea nayo sasa hivi. Pengine siku za mwanzoni mwanzoni ulizookoka, ulihisi kama vile Mungu kakukumbatia kwa kila kitu, ni sawa na unalishwa na kunguru kama vile Eliya, lakini majira unafika unaona, kama neema hiyo imetoweka au imepungua kwako. Kile kijito kimekauka.

Sasa kama wewe ni mkristo ambaye umesimama, ukifikia katika hatua kama hiyo, usianze kufikiri kuwa Mungu amekuacha, kwasababu tu huoni yale mema uliyokuwa unayapata siku za mwanzoni. Badala yake fahamu kuwa, ni hatua nyingine Mungu anataka kukupigisha, ambayo hiyo itakufanya uwe imara zaidi kiimani kuliko ile uliyokuwa nayo hapo kabla.

Ukifikia hatua kama hiyo usikumbatie sana yale ya mwanzoni, kwasababu hata ukijaribu kuyaishi hutaweza tena, uvuli wake umeshapita, unachopaswa kufanya ni  kukaa katika utulivu mpya wa Mungu, omba, kisha pale Mungu anapokufungulia neema ya kuanzana napo, bila kukawia nenda napo..Wala usiogope, kwasababu Mungu atakuwa pamoja na wewe. Huku ukizingatia kuutunza tu utakatifu na Imani, viwango vyake vilevile vya kumcha Mungu.

Kwasababu ni Mungu Yule Yule aliyekuwa na wewe kukupigania, ndiye atakayekuwa na wewe, kukushindania katika darasa lingine jipya ambalo anakupeleka. Jambo unalopaswa kufanya ni wewe tu, kuongeza umakini wako kwa Mungu, na kutoruhusu kurudi nyuma kwa namna yoyote ile.

Kwamfano hapo nyuma ulikuwa katika mazingira tulivu sana ya kumtafakari Mungu, lakini unaona kama yamebadilika, mazingira mengine yamekuja, ambayo yanakulazimu kuwafundisha wengine zaidi, au kuwahubiria, ujue kuwa ni Mungu ndiye anayekuvusha darasa hilo, hawezi miaka yote, akufanye mtoto tu wa kulishwa, utafika wakati na wewe atakulazimisha uwalishe na wengine.

Pengine Mungu atakuhamisha hapo unapoishi na kukupelekea mahali pengine, Na kule unapata changamoto kidogo ya kukipata chakula cha kiroho, kama ilivyokuwa hapo mwanzoni, sasa  Unapoona hivyo, usifikiri kuwa Mungu amekuacha, bali ni wewe, kuishindania zaidi Imani, kutengeneza tena ratiba zako, Na Mungu atakufikisha mahali ambapo anataka ufike.

Hivyo ni jukumu letu kukumbuka kuwa tunapokuwa wakristo ni lazima Mungu atatupitisha  katika madarasa tofauti tofauti, atatuvikisha katika vipindi mbalimbali na katika madarasa hayo, tunapaswa tuwe wepesi wa kuyajua mapenzi yake ni nini, ili tuweze kuelewa ujumbe wa darasa hilo. Na faida yake ni kuwa yeye mwenyewe aliahidi kuwa hatatuacha, bali atakuwa pamoja nasi.

Eliya hakuachwa na Mungu alipoondolewa pale mtoni, na kupelekwa kwenye nyumba ya mjane, Baraka zile zile alizipata isipokuwa zilikuja tu katika maumbile tofauti. Huo ndio uzuri wa Mungu wetu.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Wale mamajusi walikuwa ni wakina nani?

JINSI ROHO MTAKATIFU ANAVYOWAFUNULIA WATU MAANDIKO.

RAHABU.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

NI SAA KUMI NA MBILI (12) TU, ZA KRISTO KWAKO.

TAZAMA, NASIMAMA MLANGONI.

Rudi nyumbani

Print this post

Wale mamajusi walikuwa ni wakina nani?

Jibu: Tofauti na inavyodhaniwa na wengi kuwa wale mamajusi walikuwa ni wasoma nyota au watu wenye elimu na nyota (wanajimu)..lakini ukweli ni kwamba hawakuwa wanajimu wala wachawi, wala wasoma nyota.

Mamajusi ni watu ambao hawakuwa wayahudi (yaani waisraeli) biblia inasema walitoka Mashariki,. Katika Nyakati za biblia, likizungumzwa neno mashariki lilikuwa linalenga maeneo ya Babeli au mbali zaidi ya hapo mpaka maeneno ya Hindi, hivyo hawakuwa Wayahudi, bali watu kutoka nchi ya Mashariki.

Lakini pamoja na hayo, walikuwa na juhudi nyingi sana za kumjua Mungu wa Israeli. Ni sawa na yule Malkia wa Sheba aliyetoka mbali sana huko Kushi, kwenda kuisikiliza hekima ya Sulemani,(Mathayo 12:42), au ni sawa na yule Towashi,mkushi aliyetoka huko Kushi kupanda Yerusalemu kumwabudu Mungu wa Israeli.(Matendo 8:26-40).

Hivyo na hawa mamajusi walikuwa ni hivyo hivyo. Hawakuwa waisraeli, lakini walitoka mbali kumtafuta Mungu wa Israeli.

Sasa ni kawaida ya Mungu kuwapa ishara mbali mbali na za ajabu watu wale wanaomtafuta hususani wale ambao sio wa uzao wa Israeli.  Kwamfano utaona huyu mkushi  (yani Mu-Ethiopia), alitoka huko Afrika akasafiri kwenda Yerusalemu, yeye alikuwa anaijua tu torati na vitabu baadhi vya manabii wa Israeli, na wakati anasoma vitabu hivyo akafika kwenye kitabu cha Nabii Isaya, mlango ule wa 53, ambao unazungumzia kuhusu unabii wa ujio wa Masihi (yaani Yesu). Lakini kwasababu hajui chochote, Mungu akamhurumia akamtumia mtumishi wake Filipo aweze kumfafanulia unabii huo, na baada ya kufafanuliwa ili Mungu alithibitishe neno lake ndipo akamwonyesha huyo towashi ishara ile ya KUTOWEKA ghafla kwa Filipo.

Tusome..

Matendo 8:26 “ Malaika wa Bwana akasema na Filipo, akamwambia, Ondoka ukaende upande wa kusini hata njia ile itelemkayo kutoka Yerusalemu kwenda Gaza; nayo ni jangwa.

27  Naye akaondoka, akaenda; mara akamwona mtu wa Kushi, towashi, mwenye mamlaka chini ya Kandake malkia wa Kushi, aliyewekwa juu ya hazina yake yote; naye alikuwa amekwenda Yerusalemu kuabudu,

28  akawa akirejea, ameketi garini mwake akisoma chuo cha nabii Isaya.

29  Roho akamwambia Filipo, Sogea karibu na gari hili, ukashikamane nalo.

30  Basi Filipo akaenda mbio, akamsikia anasoma chuo cha nabii Isaya; akanena, Je! Yamekuelea haya unayosoma?

31  Akasema, Nitawezaje kuelewa, mtu asiponiongoza? Akamsihi Filipo apande na kuketi pamoja naye.

32  Na fungu la Maandiko alilokuwa akilisoma ni hili, Aliongozwa kwenda machinjoni kama kondoo, Na kama vile mwana-kondoo alivyo kimya mbele yake amkataye manyoya, Vivyo hivyo yeye naye hafunui kinywa chake.

33  Katika kujidhili kwake hukumu yake iliondolewa. Ni nani atakayeeleza kizazi chake? Kwa maana uzima wake umeondolewa katika nchi.

34  Yule towashi akamjibu Filipo, akasema, Nakuomba, nabii huyu; asema maneno haya kwa habari ya nani; ni habari zake mwenyewe au za mtu mwingine?

35  Filipo akafunua kinywa chake, naye, akianza kwa andiko lilo hilo, akamhubiri habari njema za Yesu.

36  Wakawa wakiendelea njiani, wakafika mahali penye maji; yule towashi akasema, Tazama, maji haya; ni nini kinachonizuia nisibatizwe?

37  Filipo akasema, Ukiamini kwa moyo wako wote, inawezekana. Akajibu, akanena, Naamini ya kwamba Yesu Kristo ndiye Mwana wa Mungu.] 8.38  Akaamuru lile gari lisimame; wakatelemka wote wawili majini, Filipo na yule towashi; naye akambatiza. 8.39  Kisha, walipopanda kutoka majini, Roho wa Bwana akamnyakua Filipo, yule towashi asimwone tena; basi alikwenda zake akifurahi.

40  Lakini Filipo akaonekana katika Azoto, na alipokuwa akipita akahubiri Injili katika miji yote, hata akafika Kaisaria”.

Sasa huyu Towashi, Mkushi hakuwa na elimu yoyote ya kuhusu “watu kutoweka”, wala hakuwa mchawi mpaka akaiona ile ishara… Hapana ni Mungu tu alipenda kumpa ile ishara ili aamini kiwepesi. Mungu angeweza kumwonyesha ishara nyingine yoyote, lakini alichagua kumwonyesha hiyo, angeweza kumpa ishara hata kama ile ya Musa mkono wake kugeuka kuwa wenye ukoma na kurudia tena hali yake, au Mungu angeweza kuchagua ishara ya jua kusimama,  lakini Mungu aliichagua hiyo ya Filipo kupotea kwa makusudi yake, ili aamini kirahisi.

Vivyo hivyo na wale mamajusi, walikuwa ni watu wa kusoma sana maandiko na vitabu vya manabii wa Israeli, hivyo wakiwa katika “njia panda” ya kutamani kumjua Masihi ni nani, ndipo Mungu akachagua kuwapa ishara ya kuwapa ili kuwathibitishia na kuwaonyesha Masihi ni nani, ndio akawapa hiyo ishara ya  “Nyota”..Wangeweza kupewa ishara ya mwezi, au bahari au chochote kile, kwasababu Mungu hana mipaka anaweza kutumia chochote kile kupitisha ujumbe wake, kipindi fulani aliweza kumtumia Punda kumwonyesha Balaamu dhambi yake, lakini Mungu akawachaguli ishara hiyo, sasa sio kwamba kwa ishara ile walikuwa ni wachawi, au wasoma nyota, la! Walikuwa ni watu wa kawaida kabisa, kama tu wale wachungaji makondeni waliotokewa na malaika na kupewa habari za kuzaliwa kwa Masihi.(Luka 2:8)

Hivyo Mungu anaweza kutumia chochote, alitumia kijiti wakati wa Musa, alitumia Punda wakati wa Balaamu, alitumia milima wakati wa wana wa Israeli jangwani, alitumia jua wakati wa Yoshua, alitumia bahari wakati wa wana wa Israeli, na anaweza kutumia chochote kile hana mipaka..

Biblia inasema katika…

 Zaburi 97: 6 “Mbingu zimetangaza haki yake, Na watu wote wameuona utukufu wake”.

Kwahiyo mamajusi hawakuwa wachawi, wala wanajimu..Walikuwa ni watu wenye kutafuta kwa bidii habari za Mungu na hivyo Mungu akazungumza nao kwa ishara ya kipekee kama ile.

Hivyo na sisi leo Mungu anaweza kuzungumza na sisi kwa ishara yoyote ile aipendayo, lakini ishara hiyo ni lazima iturudishe kwa Yesu na si kwa mwingine yeyote. Ikitupeleka kwa mwingine hiyo ni ishara kutoka kwa yule adui yetu shetani.

Na pia ni muhimu kujua kuwa Leo hii kuna mafundisho ya kusoma nyota kwa kigezo cha hawa mamajusi, hayo ni mafundisho ya Adui, ni vizuri kuwa nayo makini, ni mafundisho ya mashetani, ndani yake kuna roho zidanganyazo na za kuwafunga watu badala ya kuwafungua.

Bwana azidi kutupa macho ya kuyaona hayo.

Maran atha.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312


Mada Nyinginezo:

WAENDEE WANA WA ISAKARI, UWE SALAMA.

UFUNUO: Mlango wa 12

Je ni wanyang’anyi wawili waliomtukana Bwana Yesu au mmoja?

YESU ANA KIU NA WEWE.

KUSUDI LA MIMI KUWEPO DUNIANI NI LIPI?

Rudi nyumbani

Print this post

Noeli ni nini, na je! Neno hili linapatikana katika biblia?

Noeli kwa lugha ya kilatini ni neno linalomaanisha, “siku ya kuzaliwa” , lakini linalenga mahususi siku ya kuzaliwa kwa mfalme wa ulimwengu duniani (yaani Yesu Kristo). Na kwa lugha ya kifaransa neno hili  linaweza kumaanisha aidha “habari njema” au “msimu  wa Krisimasi” kwa ujumla.

Pengine Neno hili umeshawahi kulisikia sana likiitwa kwa jina la watu, au likitajwa katika nyimbo moja maarufu ijulikanayo kama “Noeli ya kwanza”; Kama hujawahi kuufahamu, unataka Kusikiliza nota zake bofya link hii;

https://www.youtube.com/watch?v=mawwURNqPC0

Hivyo kwa maneno mafupi, hili ni neno linalomaanisha kusheherekea au kutangazwa kwa habari njema za kuzaliwa kwa Bwana Yesu duniani. Popote unapolisikia likitajwa basi ujue hizo ni habari za kuzaliwa kwa Yesu au msimu wote wa sikukuu ya Krisimasi kwa ujumla, Disemba 25

Kumbuka Neno hili halipo mahali popote katika biblia, Utalisikia sana sana katika madhebehu makongwe kama vile Katoliki, Anglikana na Lutheran.

Lakini Je ni takwa sisi wakristo kusheherekea Noeli /Krisimasi? Je! Ni kweli Yesu alizaliwa Disemba 25?.. Ili kufahamu fungua hapa >> KRISIMASI NI NINI?

Bwana akubariki.

Tazama maana nyingine ya maneno ya kibiblia chini;

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

SIFONGO NA SIKI NI NINI?

Sadaka ya kuinuliwa ni sadaka ya namna gani?

Herode aliliwa na chango, Je, chango ni nini kibiblia?

Mruba ni mdudu gani kwenye biblia?(Mithali 30:15)

Rudi nyumbani:

Print this post

INJILI YA MANENO LAINI ITAKUGHARIMU.

Ukiona unahubiriwa juu ya hukumu ya Mungu, au juu ya habari ya siku za mwisho halafu unachukia au unakwazika, lakini wakati huo huo ukiambiwa habari za mafanikio na mema ndio unafurahia, basi fahamu kuwa upo karibu sana kupotea.

Kwasababu kitengo hicho ndicho kitengo-mama cha shetani kuwadanganyia watu, Embu fikiria pale Edeni Mungu hakuwaficha chochote bali aliwaeleza Adamu na hawa madhara ya dhambi, akawaambia mkila matunda la ujuzi wa mema na mabaya hakika MTAKUFA..

Lakini shetani akaibuka na mahubiri yake laini, kinyume na yale Mungu aliyowaangiza, na kuwaambia hakika HAMTAKUFA,…Unaona? Hawa aliposikia habari za mema zimekuja, habari za mafanikio, habari za uzima wakati wote, habari za kuwa juu tu, haijalishi kuwa utamkasirisha Mungu kiasi gani, haijalishi kuwa utazini kiasi gani, atatoa mimba nyingi namna gani,  maadamu ni ya kutakiwa mema, basi akayachukua tu na kuyadharau yale ya Mungu, akayashilia yale ya shetani akayaamini kwelikweli kuwa hatakufa, bali ataishi naye atayasimulia matendo ya Bwana.

Ndugu yangu hizi ni siku za mwisho, ambazo biblia ilizitabiri kuwa kutatokea wimbi kubwa la manabii wa uongo, ambao kimsingi kazi yao kubwa itakuwa ni hiyo..kuwahubiria watu maneno laini, haijalishi watakuwa hawajaokoka, au la, hilo haliwahusu, kazi yao ni kuwatabiria mafanikio tu na uzima, na mema, lakini madhara ya dhambi hawataambiwa.. Kama alivyofanya shetani kwa Hawa pale Edeni.

Isaya 30:9 “Kwa maana watu hawa ni watu waasi, watoto wasemao uongo, watoto wasiotaka kuisikia sheria ya Bwana;

10 wawaambiao waonaji, Msione; na manabii, Msitoe unabii wa mambo ya haki, TUAMBIENI MANENO LAINI, HUBIRINI MANENO YADANGANYAYO;

Kwa  hawa manabii, na waalimu wa uongo kamwe hutasikia Neno ‘ukizini hakika utakufa’, na kwenda jehanamu, huwezi kusikia maneno kama hayo, kwasababu shetani anataka wewe uendelee kubakia hivyo hivyo katika ujinga, ili ufe ghafla ujikute kuzimu uanze kujuta kwanini sikufahamu haya yote.

Angalia shida tunazozipitia duniani leo hii, ni kwasababu ya wazazi wetu kusikiliza injili laini za shetani,  Inasikitisha kuona pale mtu unapoambiwa kuhusu dhambi zako, unaona kama vile unahukumiwa. Mama yetu  Hawa aliona kama Mungu anamtamkia mabaya, akafanya makosa yale..Na sisi vivyo hivyo tukipuuzia injili ya kuambiwa ukweli, injili za kukemewa dhambi, injili za ziwa la moto. Tujue kuwa tunajiandaa kwa majuto ya milele.

Mara nyingi wana wa Israeli waliingia katika makosa kama haya mpaka wakapelekwa utumwani Babeli kwasababu ya kuwasikiliza manabii wa uongo waliokuwa wanawatabiria amani tu muda wote, bila kushughulika na dhambi zao, ambazo ndio kiini cha matatizo yao.

Soma vifungu hivi;

Ezekieli 13:16 “yaani, manabii wa Israeli, watabirio habari za Yerusalemu, na kuona maono ya amani katika habari zake; wala hapana amani, asema Bwana MUNGU”.

Yeremia 6:14 “Wameiponya jeraha ya watu wangu kwa juu juu tu, wakisema, Amani, Amani, wala hapana amani”.

Unaona yaliyokuwa yanaendelea kale ndiyo yanayoendelea sasa.

Leo swali linakuja kwako, Je unaufungaje mwaka wako?, mwaka huu wa 2020 ndio unapita, unakuja mwingine mpya wa 2021, kumbuka kwa jinsi miaka inavyosogea ndivyo tunavyoyakaribia mambo mawili makuu mbele yetu, la kwanza Ni Unyakuo. Na la pili ni Kifo chako. Maelfu ya watu kila sekunde wanakufa duniani, vilevile na wewe hujui siku yako itakuwa ni lini, pengine ni kesho, au mwanzoni mwa mwaka ujao, Jiulize ukifa leo ghafla huko utakapokwenda utakuwa ni upande gani?

Vilevile jiulize ikiwa unyakuo utapita leo usiku halafu ukaachwa, utakuwa kwenye hali ya namna gani..Kumbuka ni siku kama hizi  ndizo Bwana atakazorudi, watu watakuwa wakila na kunywa, wakipanda na kujenga, wakisherehekea, ndipo huo mwisho utakapokuja..Jiulize utakuwa wapi wakati huo ukikujia kwa ghafla.

Ukijifunza kuyatafakari hayo, hutaishi maisha ya ilimradi tu hapa duniani, bali utajiangalia sana mwenendo wako, ili siku ile isije ikakunasa kama mtego.

Hivyo, tubu dhambi zako mgeukie Muumba wako, usikubali uanze mwaka mpya na viporo vya dhambi vya mwaka huu, mgeukie Yesu Kristo leo hii, akusafishe dhambi zako.

Ikiwa upo tayari kutubu sasa, basi uamuzi huo utakuwa ni wa busara sana kwako. Mahali popote ulipo, tafuta sehemu ya utulivu, piga magoti, kisha kwa kumaanisha kabisa kutoka katika moyo wako sema sala hii kwa sauti.

EE MUNGU BABA, NAJA MBELE ZAKO, NIKIWA NINAJITAMBUA KUWA MIMI NI MKOSAJI NA NIMEKUTENDA DHAMBI NYINGI, NA KWAMBA NIMESTAHILI HUKUMU. LAKINI WEWE MUNGU WANGU ULISEMA KATIKA NENO LAKO KUWA WEWE NI MUNGU WA REHEMA UNAYEWAREHEMU  MAELFU ELFU YA WATU WANAOKUPENDA WEWE. NA LEO HII NINAKUJA MBELE ZAKO NAHITAJI MSAMAHA WAKO NA MSAADA WAKO MUNGU WANGU, NINATUBU DHAMBI ZANGU ZOTE KWA KUMAANISHA NA KWA MOYO WANGU WOTE, NINAKIRI KUWA YESU KRISTO NI BWANA, NA YEYE NDIYE MWOKOZI WA HUU ULIMWENGUNI. HIVYO NAOMBA DAMU YA MWANAO TAKATIFU INISAFISHE UOVU WANGU WOTE, NIFANYIKE KUWA KIUMBE KIPYA KUANZIA LEO NA HATA MILELE.

ASANTE BWANA YESU KWA KUNIPOKEA NA KUNISAMEHE.

AMEN.

Basi kwa sala hiyo fupi, Mungu ameshakusamehe, kilichobakia kwako ni kubatizwa, ikiwa hukubatizwa, na kudumu katika neema na utakatifu siku zote za maisha yako.

Ikiwa utahitaji msaada zaidi ya kiroho, basi tutafute kwa namba hizi +255693036618

Mungu akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

UNYAKUO.

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

Rudi nyumbani

Print this post

JE! JICHO LAKO LINAONA NINI KATIKATI YA MAJARIBU?

Shalom.

Karibu tujifunze maneno ya uzima,

Biblia inatuambia, Bwana wetu Yesu alijaribiwa sawa sawa na sisi, katika mambo yote, lakini hakutenda dhambi wala kutetereka katika imani, Sio kwamba alikuwa mgumu sana kuliko sisi, hapana, yeye mwenyewe alisema..

Yohana 16:33 “Hayo nimewaambieni mpate kuwa na amani ndani yangu. Ulimwenguni mnayo dhiki; lakini jipeni moyo; mimi nimeushinda ulimwengu”.

Bwana anajua kabisa siku unapokuwa mkristo, si wakati wote mambo yatakuwa mteremko kama wengi wanavyodhani, utakutana na majira mengi tofauti tofauti, ya kucheka, mengine ya kulia, ya kuwa mpweke, mengine ya kuchangamka, ya kupata, ya kupoteza, ya kupungukiwa, ya kujaliwa, ya kuugua, ya kuwa na afya n.k. yote hayo ni majira, lakini sote tunajua hali inakuwa mbaya zaidi pale tunapopitia katika hali za majaribu. Au kujaribiwa. Hivyo ni vizuri kujua kuwa tunapopitia majira kama hayo tunapaswa tufanye nini.

Embu leo tuangalie, ni nini kilikuwa kinaendelea katika mazingira ya kujaribiwa kwa Bwana Yesu alipokuwa hapa duniani.

Marko 1:12 “Mara Roho akamtoa aende nyikani.

13 Akawako huko jangwani siku arobaini, hali akijaribiwa na Shetani; naye alikuwa pamoja na wanyama wa mwitu, na malaika walikuwa wakimhudumia”.

Kama tunavyosoma hapo, katika kujaribiwa na shetani, vipo vitu viwili viliambatana naye. Cha kwanza ni wanyama wa mwituni. Akiwa jangwani alikutana na wanyama ambao hajazoea kukutana nao  katika maisha ya kawaida, sehemu moja aliposogea alikutana na mbweha, mbele  kidogo pengine alikutana na simba wenye njaa, siku tatu tena mbeleni tena alikutana na dubu, kila siku usiku anawaona  chui wanakatiza, kwasababu yupo nyikani, wanyama wa nyikani kukutana nao, litakuwa ni jambo la kawaida.

Inafunua nini, wakati wa majaribu usishangae kukutana na mbwa mwitu wakali mbele yako, ambao pengine hapo nyuma hukuwahi kuwaona.., unapitia ugonjwa fulani mbaya, pengine unatarajia kuona faraja katika huo, kinyume chake ndio unaona watu wakikukimbia, wengine wanakusema vibaya, Umekuwa mkristo, ukitazamia familia yako ndio ikufurahie, kinyume chake ndio inakutenga na kukurushia maneno, wengine hawakudhara., Unakataa rushwa kazini, maboss wako ndio wana kuundia visa ufukuzwe kazi n.k.. Mambo kama hayo utakutana nayo kwa namna moja au nyingine.

Lakini pia tunaona Bwana Yesu katikati ya majaribu yale, lilikuwepo kundi lingine lisiloonekana ambalo lilikiwa likimuhudumia, na hao sio wengine zaidi ya malaika watakatifu.. Hapo ndipo kiini chetu cha somo kilipo..Ni faraja iliyoje. Wakati ambapo macho yake yanaona maadui waliomzunguka, lakini roho yake ilikuwa inawaona malaika wa Mungu wamemzunguka wakimuhudumia..kuhakikisha hadhuriki na maadui wake, kuhakikisha hafu, kuhakikisha analivuka lile jaribu haijalishi kuwa yupo katika wakati mgumu kiasi gani, kuhakikisha anapata faraja ya kweli kutoka kwa Mungu.

Hapa ndipo wengi wetu tunaposhindwa kupaona, na matokeo yake majaribu yanatuzidi nguvu mpaka kuiacha imani, au kurudi nyuma. Hilo ndio lililokuwa linataka kumtokea Yule mtumishi wa Elisha, siku ile walipozungukwa na majeshi ya maadui zao, jambo ambalo lilimpelekea  aogope sana na kupaniki, na kulia.. Alipoanza kufikiria jinsi atakavyokwenda kukatwa vipande pande, au jinsi atakavyoondolewa kichwa chake, hilo lilimfanya atamani hata ardhi ipasuke saa ile ile , azame.

Lakini jicho la Elisha lilikuwa linaona mbali zaidi, lilikuwa linaona upande wa pili yupo nani, lilikuwa linaona jeshi la mbinguni lililokuwa pamoja naye, pindi anapopitia majira ya majaribu kama hayo, Ndipo baadaye akamwomba Mungu, amfungue macho yule kijana, akafunguliwa na kuona idadi isiyohesabika ya malaika wa Mungu wakiwa karibu yao wamewazunguka, kwa lengo la kuwahudumia.

2Wafalme 6:15 “Hata asubuhi na mapema mtumishi wake yule mtu wa Mungu alipoondoka, na kwenda nje, kumbe! Pana jeshi la watu, na farasi na magari, wameuzingira mji ule. Mtumishi wake akamwambia, Ole wetu! Bwana wangu, tufanyeje?

16 Akamjibu, Usiogope; maana walio pamoja nasi ni wengi kuliko wale walio pamoja nao.

17 Elisha akaomba, akasema, Ee Bwana, nakusihi, mfumbue macho yake, apate kuona. Bwana akamfumbua macho yule mtumishi; naye akaona; na tazama, kile kilima kilikuwa kimejaa farasi na magari ya moto yaliyomzunguka Elisha pande zote”.

Hizo ndio siri zilizowafanya manabii wote wa kale, kuyashinda majaribu mazito, kwasababu waliacha kuwaangalia maadui zao, wakaliangalia jeshi la Mungu mwenyezi lililo pamoja nao. Vile vile utaona wakati ule walipomkamata Danieli na kwenda kumtupa katika lile tundu la Simba, Danieli hakupeleka mawazo yake  sana kwa wale simba, bali alimuawaza Mungu wa majeshi, akijua kuwa jeshi alilonalo la malaika watakatifu la kumuhudumia yeye ni kubwa sana. Na ndipo alipotupwa tu mule tunduni, wale simba hawakumdhuru, Na baadaye  mfalme alipomuuliza ni nini?, Danieli akamwambia maneno haya

Danieli 6:22 “Mungu wangu AMEMTUMA MALAIKA WAKE, naye ameyafumba makanwa ya simba, nao hawakunidhuru; kwa kuwa mbele zake mimi nalionekana kuwa sina hatia; tena, mbele yako, Ee mfalme, sikukosa neno”.

Hivyo na wewe pia fahamu kuwa, katikati ya majaribu, wapo malaika wa Mungu kukuhudumia usipatwe na dhara lolote, katikati ya shida zako, mateso yako na magonjwa upo muujiza wa Mungu mkononi mwa malaika zake. Hivyo usiwe na hofu, wala wasiwasi wala uoga.

Subiri tu, utaona mambo ya ajabu. Ni vile tu, Mungu huwa si kila jambo atatufumbua macho yetu  tuone, lakini kama angetaka iwe hivyo uone kila kitu, usingekaa uogope jaribu lolote lililo mbele yako. Hivyo tulia,utahudumiwa kwa namna ya kimbinguni, ondoa tu woga,mtazame Mungu. Acha kufikiria juu ya mateso na dhiki, mfikirie Mungu hilo tu. Utaona kazi za malaika wa Mungu wazi wazi mbele ya macho yako.

Shalom

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

MAJARIBU MATATU YA YESU KRISTO

KUMTUMIKIA MUNGU, KUNAWEZA KUWE KINYUME NA MATARIJIO YAKO.

NAWE UTAGEUZWA KUWA MTU MWINGINE.

KUNA MAJIRA MUNGU ATAIVURUGA MIPANGO YETU.

Ngome ni nini?  Kwanini Mungu anafananishwa na ngome?

Rudi nyumbani

Print this post

Nini maana ya neno ‘Kuabiri’ kama linavyotumika katika  biblia?

Kuabiri maana yake ni kupanga safari, husasani ile ya majini, Neno hilo ndilo lililozaa neno abiria, ikiwa na maana  wale wanaosafiri.

Utalisoma sana sana katika zile ziara za mtume Paulo, na ile safari yake ya kuelekea Rumi kama mfungwa.

Vifuatavyo ni vifungu ambavyo utakutana na neno hilo.

Matendo 20:13 “Lakini sisi tukatangulia kwenda merikebuni,TUKAABIRI kwenda Aso, tukikusudia kumpakia Paulo huko; kwa maana ndivyo alivyoagiza, yeye mwenyewe aliazimu kwenda kwa miguu”.

Hapo mtume Paulo anamaanisha walipotangulia kwenda merikebuni walipanga safari ya majini ya kwenda Aso.

Matendo 21:1 “Ikawa tulipokwisha kujitenga nao na KUABIRI, tukafika Kosi kwa tanga moja, na siku ya pili yake tukafika Rodo na kutoka huko tukafika Patara”,

Hapo Paulo anamaanisha , walipokwisha kujitenga nao wakapanga safari majini ya kuelekea Kosi.

Vifungu vingine ni hivi;

Matendo 27:1 “Basi ilipoamriwa TUABIRI hata Italia, wakamtia Paulo na wafungwa wengine katika mikono ya akida mmoja, jina lake Yulio, wa kikosi cha Augusto.

2 Tukapanda katika merikebu ya Adramitio iliyokuwa tayari kusafiri mpaka miji ya pwani za Asia, tukatweka; Aristarko, Mmakedonia wa Thesalonike, akiwa pamoja nasi”.

Matendo 28:10 “nao wakatuheshimu kwa heshima nyingi; BASI TULIPOABIRI wakatupakilia vitu vile tulivyokuwa na haja navyo.

11 Baada ya miezi mitatu tukasafiri katika merikebu ya Iskanderia iliyokuwa imekaa pale kisiwani wakati wa baridi; na alama yake ni Ndugu Pacha”.

Shalom.

Tazama maana ya maneno mengine ya biblia chini.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255693036618 au +255789001312

Mada Nyinginezo:

Mtu mwenye “kitango” ni mtu wa namna gani kibiblia?

Mruba ni mdudu gani kwenye biblia?(Mithali 30:15)

Pambaja ni nini katika Biblia kama tunavyosoma katika kitabu cha Wimbo ulio bora 1:2?

“Shinikizo” ni nini kibiblia, Na maana yake rohoni ni ipi?

Shekina ni nini? Na Je! Utukufu wa shekina unamaana gani?

Rudi nyumbani

Print this post