Mavuno ni mengi, lakini watenda kazi ni wachache.
Jina la Bwana Yesu libarikiwe. Karibu tujikumbushe baadhi ya mambo muhimu katika safari ya Imani.
Tukiwa kama wakristo ni wajibu wetu kuifanya kazi ya Mungu, kulingana na karama tulizopewa. Faida ya kuifanya kazi ya Mungu ni kubwa kuliko kutoifanya kabisa. Kwa jinsi tunavyozidi kuukaribia ule mwisho wa dunia, kazi ya Mungu inazidi kurahisishwa Zaidi lakini inazidi kuongezeka kiwango.
Kwamfano mtu anaweza kupewa alime shamba lenye kichaka la hekari mbili, aanze kwa kuondoa nyasi na miti yote na kisha alilime kwa jembe la mkono, na baada ya hapo apande mbegu, na mwingine anaweza kupewa kazi ya kuvuna hekari 10.
Sasa huyo wa kwanza amepewa kazi ngumu lakini kwa hekari chache..lakini huyo wa mwisho amepewa kazi nyepesi tu! Ya kuvuna lakini hekari nyingi. Na ndio hivyo hivyo siku hizi za mwisho, kazi ya Mungu si ngumu kwasababu haihusishi kulima, kupanda wala kumwagilia…bali inahusisha tu kuvuna!…Lakini hiyo haitoshi…mashamba ya mavuno ni mengi sana, hivyo inaifanya kazi iwe kubwa sana..
Bwana Yesu alisema…
Yohana 4:35 “ Hamsemi ninyi, Bado miezi minne, ndipo yaja mavuno? Tazama, mimi nawaambieni, INUENI MACHO YENU MYATAZAME MASHAMBA, ya kuwa yamekwisha kuwa meupe, tayari kwa mavuno.
36 Naye avunaye hupokea mshahara, na kukusanya matunda kwa uzima wa milele, ili yeye apandaye na yeye avunaye wapate kufurahi pamoja.
37 Kwa maana hapo neno hilo huwa kweli, Mmoja hupanda akavuna mwingine.
38 Mimi naliwatuma MYAVUNE YALE MSIYOYATAABIKIA; wengine walitaabika, nanyi mmeingia katika taabu yao”
Anaendelea kwa kusema…
Mathayo 9:36 “Na alipowaona makutano, aliwahurumia, kwa sababu walikuwa wamechoka na kutawanyika kama kondoo wasio na mchungaji.
37 Ndipo alipowaambia wanafunzi wake, MAVUNO NI MENGI, LAKINI WATENDA KAZI NI WACHACHE.
38 Basi mwombeni Bwana wa mavuno, apeleke watenda kazi katika mavuno yake”.
Ndugu katika Kristo, zama hizi sio zama za kanisa la kwanza ambalo utakwenda mahali ambapo utakuta watu ambao hawajawahi kumsikia kabisa Yesu..(hao watu wapo ila ni wachache sana) asilimia kubwa ya watu tayari wameshawahi kumsikia Yesu mahali Fulani, wawe nii wakristo au wasio waKristo, tayari wameshawahi kumsikia Yesu..fanya utafiti mwenyewe, mfuate mtu yeyote muulize Je! Unamfahamu Yesu..utasikia jibu atakalokuambia..Hiyo ni kwasababu tayari wengine walishapanda na kutia maji, tayari yanao msingi Fulani ndani ya Maisha yao…kazi iliyobaki ni mavuno tu!.
Na kazi ya mavuno sio ngumu! Ni nyepesi sana isipokuwa ni kubwa sana!..Kwahiyo tunategemewa kufanya kazi sana kuliko watu wa kanisa la kwanza. Wengi wameshamjua Kristo tayari, lakini bado wapo mashambani (ulimwenguni) kazi inayohitajika ni kuwatoa mashambani na kuwaingiza ghalani mwa Bwana, wakibaki huko mashambani wapo ngedere, wapo wezi kuiba, wapo ndege, wapo wadudu wanaoharibu mazao n.k..
Lakini wakiwekwa ghalani kwa Bwana watakuwa salama..mbali na wadudu na Wanyama, na wezi…watakuwa wamefichwa mbali na kuhifadhiwa na kila aina ya uharibifu.
Ghalani mwa Bwana ni wapi?
Mtu aliyemtii Kristo na kuamua kuacha uovu na kumgeukia Yeye kikamilifu na kubatizwa, katika ulimwengu wa roho anakuwa tayari kashaingia ghalani mwa Mungu, kafichwa na Mungu…ataonekana kwa macho lakini katika roho hataonekana, uhai wake unakuwa umefichwa kama biblia inavyosema katika..
Wakolosai 3:3 “ Kwa maana mlikufa, NA UHAI WENU UMEFICHWA PAMOJA NA KRISTO KATIKA MUNGU. 4 Kristo atakapofunuliwa, aliye uhai wetu, ndipo na ninyi mtafunuliwa pamoja naye katika utukufu”.
Hivyo Ghala la Mungu linaanzia hapa hapa duniani!..Wokovu unaanzia hapa hapa duniani. Kama upotevu unaanzia hapa hapa duniani, na wokovu ni hivyo hivyo…Huwezi kumwona mtu ambaye anafanya uovu wa kupitiliza na kusema bado hajapotea kwamba atapotea akishakufa hapana!..katika uovu wake tayari kashapotea, labda ageuke tu! Lakini pale alipo tayari kashapotea!…hali kadhalika huwezi kusema mtu mwenye haki bado hajaokoka..na kwamba ataokoka akifika kule…huo ni uongo wa shetani…katika haki yake tayari kashaokoka!!
Wokovu unaanzia hapa hapa duniani…GHALA LA MUNGU LINAANZIA HAPA HAPA ULIMWENGUNI…Mavuno yanaingizwa ghalani hapa hapa ulimwenguni…mbingu ni mwendelezo wa ghala, ambalo tayari limeshaanzia kazi zake duniani.
Kwahiyo ni wajibu wetu kuitenda kazi ya Mungu…Tayari wameshamsikia Yesu akitajwa katika Maisha yao, pengine tangu utoto wao? Wamebakia tu kuwa wakristo-jina, wakristo wa-kidini tu lakini Yesu hayupo ndani ya mioyo yao….hivyo hatua iliyobaki ni kuwaeleza kwa maarifa yote umuhimu wa Yesu katika Maisha tofauti na walivyosikia huko nyuma. Jinsi Yesu anavyoweza kuwabadilisha watu mioyo.
Lakini likumbuke pia hili neno la Bwana “Mavuno ni mengi ila watenda kazi ni wachache”. Maana yake kazi bado ni kubwa sana…na hivyo ni wa kujitoa sisi na pia kumwomba Bwana anyanyue watenda kazi wengi duniani kote. Kipengele hicho cha maombi ni muhimu sana katika Maisha na kinapuuziwa na wengi…lakini ni kipengele cha muhimu sana cha kuomba Bwana apeleke watenda kazi. Na sisi pia kila mmoja wetu akisimama katika nafasi yake.
Bwana atusaidie na kutushika mkono, na Zaidi sana atubariki wote.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
KWA HIYO NDUGU, VUMILIENI, HATA KUJA KWAKE BWANA.
KAMA MHUBIRI NI WOKOVU UPI UNAUPELEKA KWA WATU?
UTAFIKA WAKATI WA WEWE KUACHWA NYIKANI.
MJUMBE ASIYEKUWA NA UJUMBE.
HUIJUI KAZI YA MUNGU, AFANYAYE MAMBO YOTE.
CHUKIZO LA UHARIBIFU
About the author