Utumwa siyo neno zuri, lakini pia ni neno zuri. Watu wa dunia hii wanao watumwa,lakini pia Yesu Kristo anao watumwa wake. Ndio maana alisema maneno haya..
Mathayo 11:28 ” Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha. 29 Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu, kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;30 kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”
Hapo hasemi kuwa tukishakwenda kwake ni kupumzishwa tu, basi na baada ya hapo hakuna kitakachoendelea..la! Hakusema hivyo, badala yake alisema “JITIENI NIRA YANGU” na tena anasema” mzigo wangu ni mwepesi “….Kumbe! Na yeye anayo nira!.. maana yake anatutoa kwenye utumwa mmoja na anataka kutuingiza kwenye utumwa mwingin!.. Tofauti ni kwamba nira yake yeye ni laini na pia mzigo wake ni mwepesi…
Lakini pamoja na hayo hasemi kwamba ” yeye atatutia nira yake,baada ya kutufungua hiyo nira ya adui ” badala yake anasema ” JITIENI NIRA YANGU ” huo ni kama “Ushauri” na siyo “amri”. Ingekuwa ni amri angesema ” njooni kwangu nami nitawapa pumziko na kuwatia nira yangu “..hapo ingeweza kuwa amri, lakini mpaka anasema sisi ndiyo tujitie nira yake… huo ni uchaguzi!!.. maana yake ukipenda kuwa huru sawa, au ukipenda kuichukua NIRA mpya ya YESU KRISTO ni vizuri zaidi…
Sasa kama hujui nira ni nini,..nira ni kifungo Fulani ambacho mnyama kama ng’ombe anavikwa shingoni, kama nyenzo ya kuvuta mzigo ulio nyuma yake..kadhalika na Kristo naye anayo nira ambayo anawafunga watu wake wale ambao kwa mapenzi yao wameamua kujitia katika UTUMWA WAKE. Na wanapofungwa Nira hiyo, wanageuka kuwa WAFUNGWA. Maana yake wanakuwa ni wafungwa wa YESU kwa ajili ya Injili. Mfano wa hao ni Mtume Paulo
Filemon 1:1 “Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemon mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi “
Waefeso 3:1 ” Kwasababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwaajili yenu ninyi Mataifa; 2 ikiwa mmesikia kwa habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu”
2Timotheo 1:8 ” Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi MFUNGWA WAKE, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwaajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu “
Wakolosai 4:3 ” Mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwaajili yake nimefungwa,
4 ili niidhihirihe, kama inipasavyo kunena”.
Unaweza kusoma zaidi kuhusu KUFUNGWA kwa Paulo katika misitari ifuatayo (Filemon 1:9, Waefeso 4:1, Filemon 1:23).
Zifuatazo ni tabia za Wafungwa wa Kristo, kwa ajili ya Injili.
Muda wote, masaa yote wapo katika mazingira ya kuifanya kazi ya Mungu.Mtume Paulo wa kwenye biblia na wengine baadhi, walijitoa katika Injili kiasi kwamba hawakuwa na muda wa kutafuta wake, akili zao zote zilikuwa katika kuifanya kazi ya Mungu, mambo ya ulimwengu huu waliyaona kama mavi (Wafilipi 3:8).
Hawaionei haya Injili.2Timotheo 1:8 ” Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake ,bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili,kwa kadiri ya nguvu ya Mungu.
Wamejikana nafsi kweli kweli.Hakuna mtumwa yeyote anayekuwa na uhuru asilimia zote, muda wote utamkuta eneo la kazi..kitu kinachompa hofu kuliko yote ni kuipoteza kazi yake au kuiharibu, na kitu pekee kilichomuunganisha yeye na Bwana wake ni kazi yake hiyo aliyopewa, ya Injili. Huwezi kumkuta mtumwa aliye makini, muda wa kufanya kazi yupo anazurura!.. kadhalika wafungwa wa Yesu, kwaajili ya Injili hawazururi zururi katika huu ulimwengu, shughuli shughuli na anasa za ulimwengu huu, zinawapita! Na wala hawazitamani.. macho yao ni kuifanya kazi ya Bwana na kuimaliza.. kuhubiri Injili kwao ni sharti! Sio ombi tena!
1Wakorintho 9:16 ” Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili.17 maana nikitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili”.
Je wewe ni mfungwa wa Yesu?.. umejitia NIRA ya Bwana Yesu shingoni mwako?.. Au bado unayo nira ya adui shetani?.. Nira ya adui shetani ni ulevi unaoutumainia ambao unakufanya kuwa mtumwa wa pombe na singara!.. Nira ya shetani ni uzinzi na ukahaba unaoufanya ambao huwezi kuishi bila huo.. Nira ya adui shetani ni ushabiki wa mpira unaokufanya uwe mtumwa wa huo mpira.. Nira ya adui shetani ni tamaa zote za macho ambazo zimekufanya kuwa mtumwa..Nira hiyo huwezi kujivua mwenyewe, kwasababu aliyekufunga hukuwa na nia ya wewe kukuacha huru siku moja!
Hivyo huwezi kujifungua, unamhitaji Yesu azivunje!… ndipo uwe huru!… kwasababu kwa nguvu zako haiwezekani.. na baada ya kukufungua!, anakupa shauri la wewe kujitia nira yake!.. hapo siyo yeye anakufungua hiyo nira! Ni wewe ndio unayeamua kujifunga nira yake.. na kama ukitii na kukubali kumtumikia Yesu kwaajili ya Injili yake, na kuwa mfungwa wake.. yeye alisema maneno haya..
Marko 10:28″ Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.
29 Yesu akasema, Amini,nawaambieni, Hakuna mtu aliyeach nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwaajili yangu,na kwaajili ya Injili, 30 ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, au ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele “
Kumbuka kama bado hujampokea Yesu, basi fahamu kuwa bado unayo nira ya adui shetani mwako, na upo kwenye utumwa wa dhambi hata kama hujijui, Hivyo mgeukie leo Kristo akuweke huru,Yeye mwenyewe alisema ” Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli ( Yohana 8:36)”,
Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote unazozitenda kwa siri na kwa wazi, na kisha tafuta ubatizo sahihi, ubatizwe kwaajili ya ondoleo la dhambi zao, ubatizo sahihi ni ule wa maji mengi na kwa jina la Yesu ( Matendo 2:38), Na baada ya hapo amua kujitia Nira ya Kristo, kwa kudhamiria kumtumikia yeye kwa gharama zozote zile, na Bwana mwenyewe atakufanya kuwa mtumwa wake.. na thawabu yako itakuwa kumbwa hapa duniani na utakapofika mbinguni.
Bwana akubariki.
+255693036618/ +255789001312
jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mafundisho mengin
Mada Nyinginezo:
About the author