WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.

WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO.

Shalom. Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe daima. Karibu tuyatafakari maneno mazuri ya uzima.

Ulishawahi kuutafakari vizuri huu mstari?

Isaya 35: 8 “Na hapo patakuwa na njia kuu, na njia, nayo itaitwa, Njia ya utakatifu; wasio safi hawatapita juu yake; bali itakuwa kwa ajili ya watu hao; wasafirio, WAJAPOKUWA WAJINGA, HAWATAPOTEA KATIKA NJIA HIYO”.

Sana sana hapo mwishoni anaposema “ wajapokuwa wajinga, hawatapotea”?…. Maana yake ni kuwa kuna uwezekano kweli wa kuwepo watu wa Mungu baadhi, wanaotembea katika wokovu, lakini kwa namna moja au nyingine wanaoujinga fulani ndani yao.

Na ujinga huo unaweza kusababishwa na aidha kutoyaelewa vizuri maandiko, au kushindwa kuulewa uweza wote wa Mungu, na njia zake, Lakini pamoja na kuwa watu hao watakuwepo, lakini biblia bado inasema, maadamu wapo katika NJIA KUU, njia ya uzima,NJIA YA UTAKATIFU, kamwe hawatapotea.

Leo hii sehemu nyingi utapita na kukutana na kundi la watu linasema, “kama ulokole ndio ule ni heri nibaki katika dhambi zangu”, walokole ni wavivu, wenyewe kazi yao ni kukaa muda wote kusali tu na kufunga makanisani hawana shughuli nyingine yoyote ya kufanya.. Utakutana na wengine wanasema, walokole kazi yao ni kujinyima tu, kupendeza hawapendezi, wapo rafu rafu, kama Mungu ndio hivyo heri nibakie katika  udunia wangu tu..

Ndugu, biblia inasema, hata kama wanachokifanya ni kutokana na ujinga wao.. Lakini maadamu wameupokea wokovu, wamekusudia kumfuata Mungu wao, kamwe hawatapotea, hata iweje, hilo ni hakikisho kutoka kwa Mungu. Hata wakiwa wamekataa kwenda shule, hata wakiwa wanalala maporini, hata wakiwa wanafunga mwaka mzima, hata wakiwa hawajui vizuri kusoma na kuandika, kamwe usitazamie watu kama hao watapotea..Hilo ondoa akilini.

Lakini kama wewe ni rafiki wa dunia. Unajiona njia zako ndio zipo sawa, unaona njia za watu wa kidunia ndio sahihi, jinsi wanavyoishi kwa raha, wanavyostawi, wanavyoruka ruka, wanavyopiga makeup, na kutembea uchi barabarani, na kuvaa milegezo, wewe ndio unapendezwa nao, nataka nikuambie hata kama utakuwa na akili vipi, mwisho wa siku utaishia pabaya tu. Kwasababu biblia inasema hivyo.

Mithali 14:12 “Iko njia ionekanayo kuwa sawa machoni pa mtu, Lakini mwisho wake ni njia za mauti”.

Wewe unayejiona, maisha ni anasa, na huku Kristo yupo mbali na wewe, mwisho wako utakuwa jehanamu, wewe unayejiona maisha ni kujiachia na kuzini, na kufanya kila aina ya dhambi kama unavyojisikia, yaani kwa ufupi unaupa moyo wako kila kitu unachopenda, na huku unaona wokovu ni mzigo mzito. Jiandae kukutana na mauti.

Umekuwa ukiwadhihaki wakristo, na kusema wale ni wajinga, wamerukwa na akili, Mungu gani wanayemuabudu anawafanya kuwa vile, wanaomba usiku na mchana, na hakuna muujiza wowote unaotendeka. Ndugu hata kama ni wajinga, lakini ufahamu kuwa ujinga wao wanaufanyia wakiwa katika gari ambalo lipo safarini.

Na wewe akili zako unazionyesha ukiwa nje ya gari. Hiyo ndio tofauti kati ya wewe na wao.. Hizo akili zitakusaidi nini ukifa leo, itakufaidia nini upate ulimwengu mzima, halafu unapata hasara ya nafsi yako?. Kama unadhani ni  wapumbavu, basi ingia ndani ya Kristo, na wewe uwepo ndani ya gari hilo salama, ndipo uutoe huo upumbavu ulio ndani yao. Lakini kama upo nje ya Kristo, ujue wewe ndio mjinga wa mwisho kabisa.

Haya maisha ni mafupi sana, nakushauri umpe Yesu maisha yako ndugu yangu. Leo unayo pumzi, lakini siku ya kesho hujui utakuwa wapi, hata kama utakuwepo kumbuka Maisha ni fumbo hakuna anayejua siku ya kuondoka kwake, hivyo yatupasa kila siku tujichunguze, Je! Bado tupo ndani ya gari la mbinguni au tulishashuka siku nyingi?

Bwana atusaidie sote.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.

Mada Nyinginezo:

NJIA KUU YA KUINGIA KATIKA ULE MJI.

BIBLIA INAITAJA NJIA KUU YA MFALME, NJIA HII NI IPI?

JISHUSHE ILI MUNGU AKUHUDUMIE.

NJIA YA KUPATA WOKOVU.

KWANINI KRISTO AFE?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments