JE! WEWE NI MFUNGWA WA BWANA?

JE! WEWE NI MFUNGWA WA BWANA?

Utumwa sio neno zuri, lakini pia ni neno zuri. Watu wa dunia hii wanao watumwa, lakini pia Yesu Kristo anao watumwa wake. Ndio maana alisema maneno haya..

Mathayo 11:28  “Njoni kwangu, ninyi nyote msumbukao na wenye kulemewa na mizigo, nami nitawapumzisha.

29  Jitieni nira yangu, mjifunze kwangu; kwa kuwa mimi ni mpole na mnyenyekevu wa moyo; nanyi mtapata raha nafsini mwenu;

30  kwa maana nira yangu ni laini, na mzigo wangu ni mwepesi”

Hapo hasemi kuwa tukishakwenda kwake ni kupumzishwa tu, basi na baada ya hapo hakuna kinachoendelea…la! Hakusema hivyo, badala yake alisema “JITIENI NIRA YANGU” na tena anasema “mzigo wangu ni mwepesi”…. Kumbe! Na yeye anayo nira!..maana yake ametutoa kwenye utumwa mmoja na anataka kutuingiza kwenye utumwa mwingine!… Tofauti ni kwamba nira yake yeye ni laini na pia mzigo wake ni mwepesi…

Lakini pamoja na hayo hasemi kwamba “yeye atatutia nira yake, baada ya kutufungua hiyo nira ya adui” badala yake anasema “JITIENI NIRA YANGU” huo ni kama “ushauri” na sio “amri”. Ingekuwa ni amri angesema “njooni kwangu nami nitawapa pumziko na kuwatia nira yangu”..hapo ingeweza kuwa amri, lakini mpaka anasema sisi ndio tujitie nira yake… huo ni uchaguzi!!…maana yake ukipenda kuwa huru sawa, au ukipenda kuichukua NIRA mpya ya YESU KRISTO ni vizuri zaidi..

Sasa kama hujui nira ni nini,…nira ni kifungo Fulani ambacho mnyama kama ng’ombe anavikwa shingoni, kama nyenzo ya kuvuta mzigo ulio nyuma yake… kadhalika na Kristo naye anayo nira ambayo anawafunga watu wake wale ambao kwa mapenzi yao wameamua kujitia katika UTUMWA WAKE. Na wanapofungwa Nira hiyo, wanageuka kuwa WAFUNGWA. Maana yake wanakuwa ni wafungwa wa YESU kwaajili ya Injili. Mfano wa hao ni Mtume Paulo.

Filemoni 1:1  “Paulo, mfungwa wa Kristo Yesu, na Timotheo aliye ndugu yetu, kwa Filemoni mpendwa wetu, mtenda kazi pamoja nasi”

Waefeso 3:1  “Kwa sababu hiyo mimi Paulo ni mfungwa wake Kristo Yesu kwa ajili yenu ninyi Mataifa; 2  ikiwa mmesikia habari ya uwakili wa neema ya Mungu niliyopewa kwa ajili yenu”

2Timotheo 1:8 “Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi MFUNGWA WAKE, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu”

Wakolosai 4: 3 “mkituombea na sisi pia, kwamba Mungu atufungulie mlango kwa lile neno lake, tuinene siri ya Kristo, ambayo kwa ajili yake nimefungwa,

4  ili niidhihirishe, kama inipasavyo kunena”.

Unaweza kusoma zaidi kuhusu KUFUNGWA kwa Paulo katika mistari ifuatayo. (Filemoni 1:9 , Waefeso 4:1, 2Timotheo 1:8,  Filemoni 1: 23 ).

Zifuatazo ni tabia za Wafungwa wa Kristo, kwaajili ya Injili.

  1. Muda wote, masaa yote wapo katika mazingira ya kuifanya kazi ya Mungu.

Mtume Paulo wa kwenye biblia na wengine baadhi, walijitoa katika Injili kiasi kwamba hawakuwa na muda wa kutafuta wake, akili zao zote zilikuwa katika kuifanya kazi ya Mungu. Mambo ya ulimwengu huu waliyaona kama mavi (Wafilipi 3:8).

  1. Hawaionei haya injili.

2Timotheo 1:8  “Basi usiuonee haya ushuhuda wa Bwana wetu, wala usinionee haya mimi mfungwa wake, bali uvumilie mabaya pamoja nami kwa ajili ya Injili, kwa kadiri ya nguvu ya Mungu”

  1. Wamejikana nafsi kweli kweli.

Wafungwa wote wa Kristo wanakuwa wamejikana nafsi kweli kweli, wapo tayari hata kufa kwaajili ya injili, wapo tayari kutukanwa, kuonekana wajinga na waliorukwa na akili kwaajili ya injili, wapo tayari kuacha hata kila kitu ilimradi tu, kutimiza kusudi la Bwana wao.

  1. Wamejitenga na Ulimwengu.

Hakuna mtumwa yeyote anayekuwa na uhuru asilimia zote, muda wote utamkuta eneo la kazi..kitu kinachompa hofu kuliko zote ni kuipoteza kazi yake au kuiharibu, na kitu pekee kilichomuunganisha yeye na Bwana wake ni kazi yake hiyo aliyopewa, ya Injili. Huwezi kumkuta mtumwa aliye makini, muda wa kufanya kazi yupo anazurura!..Kadhalika wafungwa wa Yesu, kwaajili ya injili hawazururi zururi katika huu ulimwengu, shughuli shunguli na anasa za ulimwengu huu, zinawapita! na wala hawazitamani.. Macho yao ni kuifanya kazi ya Bwana na kuimaliza… Kuhubiri injili kwao ni Sharti! Sio ombi tena!.

1Wakorintho 9:16  “Maana, ijapokuwa naihubiri Injili, sina la kujisifia; maana nimewekewa sharti; tena ole wangu nisipoihubiri Injili!

17  Maana nikiitenda kazi hii kwa hiari yangu nina thawabu; ila ikiwa si kwa hiari yangu, nimeaminiwa uwakili”.

Je wewe ni Mfungwa wa Yesu?.. Umejitia NIRA ya Bwana Yesu shingoni mwako?.. Au bado unayo nira ya adui shetani?..Nira ya adui shetani ni ulevi unaoutumainia ambao unakufanya kuwa mtumwa wa pombe na sigara!.. Nira ya shetani ni uzinzi na ukahaba unaoufanya ambao huwezi kuishi bila huo.. Nira ya adui shetani ni ushabiki wa mpira unaokufanya uwe mtumwa wa huo, Nira ya adui shetani ni tama zote za macho ambazo zimekufanya kuwa mtumwa… Nira hiyo huwezi kujivua mwenyewe, kwasababu aliyekufunga hakuwa na nia ya wewe kukuacha huru siku moja!

Hivyo huwezi kujifungua, unamhitaji Yesu azivunje!.. ndipo uwe huru!..kwasababu kwa nguvu zako haiwezekani.. na baada ya kukufungua!, anakupa shauri la wewe kujitia nira yake!.. hapo sio yeye anakufunga hiyo nira! Ni wewe ndio unayeamua kujifunga nira yake… na kama ukitii na kukubali kumtumikia Yesu kwaajili ya injili yake, na kuwa mfungwa wake..yeye alisema maneno haya…

Marko 10:28  “Petro akaanza kumwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata wewe.

29  Yesu akasema, Amin, nawaambieni, Hakuna mtu aliyeacha nyumba, au ndugu waume, au ndugu wake, au mama, au baba, au watoto, au mashamba, kwa ajili yangu, na kwa ajili ya Injili, 30  ila atapewa mara mia sasa wakati huu, nyumba, na ndugu waume, na ndugu wake, na mama, na watoto, na mashamba, pamoja na udhia; na katika ulimwengu ujao uzima wa milele”

  Kumbuka kama bado hujampokea Yesu, basi fahamu kuwa bado unayo nira ya shetani shingoni mwako, na upo kwenye utumwa wa dhambi hata kama hujijui, Hivyo mgeukie leo Kristo akuweke huru, Yeye mwenyewe alisema “Mwana akiwaweka huru, mtakuwa huru kweli kweli (Yohana 8:36)”.

Hivyo tubu leo kwa kumaanisha kuacha dhambi zako zote unazozitenda kwa siri na kwa wazi, na kisha tafuta ubatizo sahihi, ubatizwe kwaajili ya ondoleo la dhambi zako, ubatizo sahihi ni ule wa maji tele na kwa jina la Yesu (Matendo 2:38), na baada ya hapo amua kujitia Nira ya Kristo, kwa kudhamiria kumtumikia yeye kwa gharama zozote zile, na Bwana mwenyewe atakufanya mtumwa wake.. na thawabu yako itakuwa kubwa hapa duniani na utakapofika mbinguni.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Je watu ambao hawajasikia kabisa injili watahukumiwa?

Kuwiwa maana yake nini katika biblia?

UFUNUO: Mlango wa 14

MWANZO WA INJILI YA YESU KRISTO.

Vyombo vya uzuri ni vipi vinavyotajwa katika biblia?

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Inline Feedbacks
View all comments