Wokovu wa kweli ni upi?
Je unaposema umeokoka, ni nini kinakupa uhakika huo?
Fahamu ni nini Bwana anataka kuona kwako, pindi tu unapookoka.
Ni kweli katika Warumi 10:9 biblia inasema;
“Ukimkiri Yesu kwa kinywa chako ya kuwa ni Bwana, na kuamini moyoni mwako ya kuwa Mungu alimfufua katika wafu, utaokoka”.
Lakini kukiri kunakozungumziwa hapo, sio sawa na inavyotafsiriwa sasa. Zamani, kukiri kulimaanisha kutangaza vita na ulimwengu, Pamoja na kuhatarisha Maisha yako pia . Kwani ukristo ulijulikana kama ni dini asi, dhidi ya Imani za kipagani.
Soma,
Yohana 9:22 “.. kwa maana Wayahudi walikuwa wamekwisha kuafikiana kwamba mtu akimkiri kuwa ni Kristo, atatengwa na sinagogi”.
Hivyo watu wengi walikuwa wanauliwa, wengine wanafukuzwa mbali na jamii, kwa jambo hilo tu moja, la kumkiri Yesu hadharani. Kwahiyo mtu yeyote kabla ya kwenda kumtangaza Yesu hadharani kuwa ndiye mwokozi wake, alijifikiria mara mbili kwanza.
Sasa jambo kama hili linatokea kweli sehemu baadhi ulimwenguni, lakini sio kote. Kwani sisi tuliopo katika mazingira mchanganyiko kama haya. Neno kukiri tu kwa kinywa, sio kipimo tosha kwamba wewe umemfuata Yesu, kwasababu mtu yeyote anaweza kufanya hivyo hata mpagani, kwasababu hakuna hatari yoyote inaweza kumtokea kama akifanya hivyo. Kwasababu anakuwa ni kama tu kaongea.
Na ndio maana leo hii kuna idadi kubwa sana ya watu wanajiita wakristo wanasema wameokoka. Ukiwauliza wameokokaje watakuambia, kwasababu walimkiri Yesu kwa vinywa vyao, hilo tu.Na huku ukiangalia Maisha yao, hayana tofauti na watu wa kidunia.
Ndugu usidanganyike, wokovu wetu ili ufanane na ule wa watu wa zamani, hatuna budi tumkiri Yesu KWA MATENDO YETU. Tunaukataa ulimwengu na mambo yake yote, kivitendo.
Bwana Yesu alitabiri kuwa siku za mwisho, wengi watamwita ‘Bwana, Bwana’, kwa midomo tu, lakini matendo yao yapo mbali naye, lakini anasema atawafukuza Dhahiri.
Mathayo 7:21 “Si kila mtu aniambiaye, Bwana, Bwana, atakayeingia katika ufalme wa mbinguni; bali ni yeye afanyaye mapenzi ya Baba yangu aliye mbinguni.
22 Wengi wataniambia siku ile, Bwana, Bwana, hatukufanya unabii kwa jina lako, na kwa jina lako kutoa pepo, na kwa jina lako kufanya miujiza mingi?
23 Ndipo nitawaambia dhahiri, Sikuwajua ninyi kamwe; ondokeni kwangu, ninyi mtendao maovu.
Umeona? Ikiwa hao atakaowafukuza wanafanya miujiza mikubwa, na kutoa ishara nyingi, jiulize wewe ambaye hutendi lolote, na bado unatenda dhambi, unadhani utamwonga Mungu, kisa uliongozwa sala ya toba?
Ndugu, ni kuwa makini sana nyakati hizi, Ukisema umeokoka, uthibitishe wokovu wako kwa matendo kwamba umeuacha ulimwengu kweli kweli. Unaacha hivyo vimini, hizo suruali uvaazo binti,Uzinzi, anasa, punyeto, picha za ngono utazamazo mitandaoni.
Kuongozwa sala ya toba mara nyingi, sio tiketi ya kwenda mbinguni, bali badiliko lako ndilo litakalokuoa.
Bwana atufumbue macho yetu tulione hilo.
About the author