Jina la Bwana na Mwokozi wetu Yesu Kristo, lihimidiwe daima.
Karibu katika darasa hili fupi la biblia?
Je unajua imani inafananishwa na nini? Na je unajua ni kitu gani kinachoikuza Imani?.
Majibu ya maswali haya tutayapata ndani ya biblia…
Bwana Yesu aliifananisha imani na chembe ndogo ya Haradali, Chembe ya Haradali au kwa lugha nyingine punje ya Haradali ni mbegu inayotoa mmea unaoitwa Haradali.
Luka 17:6 “Bwana akasema, Kama mngekuwa na imani KIASI CHA CHEMBE YA HARADALI, mngeuambia mkuyu huu, Ng’oka, ukapandwe baharini, nao ungewatii”
Hapa Bwana anaifananisha imani na chembe ya Haradali, na anasema mtu akiwa nayo kwa kiasi hicho tu!, Tayari anaweza kufanya makubwa.
Sasa mtu anawezaje kufanya makubwa akiwa na chembe hiyo ya Haradali?. Hilo ndio swali la kujiuliza.
Wengi tunaishia kuitafakari tu ile chembe ya Haradali kwa udogo wake basi na si kwa upana wake,
Lakini hebu leo hebu tutafakari kwa undani hii chembe ya Haradai na muujiza uliopo ndani yake.
Lakini awali ya yote tuweke msingi kwa kuutafakari mfano ufuatao…Tengeneza picha mkulima anakwambia ukiwa na punje moja ya indi, waweza kulisha watu mia.. Je kwa kusema hivyo atakuwa amemaanisha lile indi moja laweza kushibisha watu wote hao?.
Jibu ni la! Ni wazi kuwa indi moja haliwezi kushibisha umati wa watu mia, bali atakua amemaanisha kuwa endapo ukiiichukua ile mbegu moja ya indi, ukaipanda yaweza kuzaa mahindi mengi ambayo yaweza kushibisha umati mkubwa wa watu.
Vivyo hivyo Bwana Yesu aliposema “Imani kama chembe ya Haradali yaweza kuhamisha milima na mikuyu” ..hakumaanisha ile mbegu kama mbegu bali matokeo ya ile mbegu, ndio maana hakuifananisha imani na chembe ya mchanga isiyozaa bali chembe ya Haradali iliyo hai na inayozaa..
Sasa ili tuelewe vizuri, tusome maandiko yafuatayo…
Marko 4:30 “Akasema, Tuulinganishe na nini ufalme wa Mungu? Au tuutie katika mfano gani?
31 NI KAMA PUNJE YA HARADALI, ambayo ipandwapo katika nchi, ingawa ni ndogo kuliko mbegu zote zilizo katika nchi,
32 lakini ikiisha kupandwa hukua, ikawa kubwa kuliko miti yote ya mboga, ikafanya matawi makubwa; hata ndege wa angani waweza kukaa chini ya uvuli wake”.
Umeona muujiza uliopo ndani ya punje ya Haradali?…kwamba inaanza kama mbegu ndogo tena dhaifu na kisha inapokua kubwa huzidi mboga zote na miti yote na kufanya matawi makubwa ambayo ndege waweza kukaa chini yake.
Kwahiyo kumbe Imani inayofananishwa na chembe ya Haradali, inahitajika kupandwa kwanza katika nchi, na kupaliliwa na kumwagiwa maji, ili iweze kuwa mti mkubwa utakaoweza kutoa matunda na hata kuwa tegemezi kwa viumbe wengine, lakini ikibaki katika hali ile ile haizai kitu, ni sawa na imekufa..kama maandiko yanavyosema…
Yakobo 2:17 “Vivyo hivyo na imani, isipokuwa ina matendo, imekufa nafsini mwake”.
Sasa swali Imani inapaliliwaje na inamwagiwaje maji, ili ikue na kuleta matokeo makubwa.
Tusome Mathayo 17:20-21.
Mathayo 17:20 ” Yesu akawaambia, Kwa sababu ya upungufu wa imani yenu. Kwa maana, amin, nawaambia, Mkiwa na imani kiasi cha punje ya haradali mtauambia mlima huu, Ondoka hapa uende kule; nao utaondoka; wala halitakuwako neno lisilowezekana kwenu.
21 [LAKINI NAMNA HII HAITOKI ILA KWA KUSALI NA KUFUNGA.]”
Umeona mwisho hapo?.. anasema, namna hii haitoki isipokuwa kwa KUSALI na KUFUNGA.
Kumbe KUSALI na KUFUNGA ndio kanuni ya kukuza Imani,…..kumbe Kufunga na kusali ndiko kuipalilia na kuinyeshea Imani ili Ikue, na mtu akiendelea kwa kanuni hiyo, kwa kitambo fulani basi ile imani ndani yake itakua yenyewe na baadaye atatoa matokeo makubwa kwa kila anachokihitaji.
Mtu aliyeipalilia imani yake hatatumia nguvu nyingi kupata jambo, kwa maana Imani yake ni imara na thabiti.. Ile punje ya Haradali ndani yake imegeuka kuwa mti mkubwa usiotikisika.
Ndio maana watu waliojaa maombi na mifungo, wachawi hawawatesi wala hawana hofu na hatari yoyote, kwanini??..Kwasababu tayari imani yao imejengeka ndani yao.
Je na wewe unataka imani yako ikue?…basi usikwepe Mifungo, vile vile usikwepe maombi..Ikiwa utahitaji mwongozo wa maombi ya kukua kiroho ya kila wiki basi wasiliana nasi inbox na tutakusaidia kwa hilo, na vile vile kama utapenda kuungana nasi katika ratiba zetu za mifungo waweza kuwasiliana nasi inbox ili tuweze kukupa utaratibu.
Bwana akubariki.
Maran atha!
Tafadhali shea na wengine ujumbe huu;
Pia Kwa maombezi/ Ushauri/ Maswali/ Whatsapp:
Tuandikie katika BOXI la Maoni hapo chini au
Piga namba hizi: +255789001312 au +255693036618
Mada Nyinginezo:
UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA.
About the author