MKAMCHUKUE SALAMA.

MKAMCHUKUE SALAMA.

Je unajua sababu kuu ya Yuda kujinyonga?.. Jibu ni kwasababu alishuhudia jambo ambalo lilikuwa ni tofauti na mategemeo yake!

Matazamio ya Yuda hayakuwa kumtoa Bwana Yesu auawe!.. Yuda lengo lake kuu lilikuwa ni KUPATA PESA!, Hivyo alichojua ni kwamba katika kumsaliti Bwana Yesu, Makuhani watamchukua na kisha watamwadhibu kwa viboko tu! Na kisha watamwonya asiendelee kuhubiri na hatimaye watamwachia, na yeye ataendelea kuwa mtume wa Bwana Yesu, hakujua kuwa USALITI WAKE utampelekea Bwana KUHUKUMIWA AFE!. Alijua hata kama Bwana atakuja kufa, lakini si kwa kupitia usaliti wake!, alijua atakuja kufa kwa njia nyingine. Ndio Maana utaona baada tu ya hukumu kupita ya Bwana kuuawa!, alijuta majuto makuu..

Mathayo 27:1 “Na ilipokuwa asubuhi, wakuu wa makuhani wote na wazee wa watu wakafanya shauri juu ya Yesu, wapate kumwua;

2 wakamfunga, wakamchukua, wakampeleka kwa Pilato aliyekuwa liwali

3 Kisha Yuda, yule mwenye kumsaliti, ALIPOONA YA KUWA AMEKWISHA KUHUKUMIWA, ALIJUTA, akawarudishia wakuu wa makuhani na wazee vile vipande thelathini vya fedha, akasema, NALIKOSA NILIPOISALITI DAMU ISIYO NA HATIA.

4 Wakasema, Basi, haya yatupasani sisi? Yaangalie haya wewe mwenyewe.

5 Akavitupa vile vipande vya fedha katika hekalu, akaondoka; akaenda, akajinyonga”.

Umeona?.. Wazee wa makuhani walimficha Yuda nia yao hiyo ya kumwua!, walikuja kuiweka wazi baada ya kumkamata Bwana Yesu!, kwasababu walijua endapo wangemfuata Yuda na kumwambia moja kwa moja kwamba wanataka kumwua!, Yuda angekataa!!!..kamwe asingeweza kumtoa Bwana Yesu auawe!!

Sasa ili tuzidi kulithibitisha hilo kuwa lengo la Yuda si kumpeleka Bwana asulubiwe!, bali aadhibiwe tu na kuachiwa.. tusome mistari ifuatayo…

Marko 14:42 “Ondokeni, twendeni zetu; tazama, yule anayenisaliti amekaribia.

43 Basi alipokuwa katika kusema, mara Yuda alifika, mmoja wa wale Thenashara, na pamoja naye mkutano, wana panga na marungu, wametoka kwa wakuu wa makuhani, na waandishi, na wazee.

44 Na yule anayemsaliti alikuwa amewapa ishara, akisema, Nitakayembusu, huyo ndiye; MKAMATENI, MKAMCHUKUE SALAMA.

45 Basi alipokuja, mara akamwendea, akasema, Rabi, akambusu.

46 Wakanyosha mikono yao wakamkamata”.

Hapo mstari wa 44, unasema.. “MKAMATENI, MKAMCHUKUE SALAMA”.. Maana yake halikuwa lengo lake Bwana apate madhara Makubwa kama yale!, ya kusulubiwa!.. Lakini ilikuja kinyume na matarajio yake!.. Badala wale wakuu wa makuhani wamwonye tu na kumwachia, wakahimiza asulubiwe!.. Ikawa ni kinyume na makubaliano yao na YUDA!, Na Yuda kuona vile akajuta kuchukua fedha zao, akawarudishia, kwasababu hawakukubaliana hayo!.

Ni kitu gani nataka tuone hapo?

Kuna mambo au maamuzi ambayo unaweza kuyachukua sasa, ambayo utaona kama madhara yake ni madogo mbeleni, lakini kumbe ni makubwa sana!.

Siku zote unapoingia mkataba na dhambi, madhara yake ni makubwa sana mbeleni!.. Leo hii dhambi inaweza kukushawishi kuwa ulifanyalo ni dogo tu!, halitakuletea shida kubwa mbeleni.. lakini siku itakapofika litakuletea matokeo makubwa tofauti na ulivyotegemea.

Maandiko yanasema kuwa “..mshahara wa dhambi ni mauti (Warumi 6:23)” na si “mshahara wa dhambi ni huzuni”.. maana yake Unapoingia mkataba na dhambi leo, fahamu kuwa mwisho wake ni Mauti!.

Umeshaokoka halafu unasema ngoja “nikazini tu mara moja” kwa matarajio kwamba utatubu tu! na hakutakuwa na madhara yoyote!.. Nataka nikuambie hata Yuda, alisema hivyo hivyo, alijua bado anazo siku nyingi sana za kuendelea kuwa mtume wa Bwana Yesu, hakujua ile siku ndio ilikuwa siku ya mwisho ya utume wake! Na lile busu ndio lilikuwa busu lake la mwisho!, milele hatamwona Bwana!.. mwisho wake ulikuwa ni MAUTI (Kujinyonga)..

Ndugu usiyapime matokeo ya dhambi kwa uzoefu!.. ile dhambi ambayo unaona kama haina matokeo makubwa.. maandiko yanasema matokeo yake ni MAUTI!

Leo hii unapomsaliti Bwana na kwenda kufanya uasherati, au kujiuza mwili wako, au kuiba au kutapeli, au kufanya anasa, au kuua, au kujilipiza kisasi, ukiwa na mategemeo kuwa utatubu tu! Na utarudiana na Bwana kama kawaida!!..nataka nikuambie “KUWA MAKINI SANA!!”.. Huo uzinzi unaopanga kwenda kuufanya pengine ndio unaweza kuwa mwisho wa mahusiano yako wewe na Bwana!, pengine ndio njia panda yako ya kuzimu!.. Laiti! Yuda angelijua masaa machache mbele ni nini kitakwenda kutukia, asingelimbusu Bwana!, laiti Samsoni angejua masaa machache mbele hatakaa amwone tena mama yake na Baba yake kwa macho yake, asingemfunulia siri Delila!

Kamwe usiipime nguvu ya dhambi kwa uzoefu!.. Mhubiri mmoja alisema “kamwe usimwogope shetani bali iogope dhambi” hiyo ni kweli kabisa!!.. Kwasababu maandiko hayajasema mshahara ya shetani ni mauti, bali yalisema “mshahara wa dhambi ni Mauti”

Bwana Yesu atusaidie, kila siku tuweze kujitenga na dhambi.

Maran atha!

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema,

Kwa maombezi/Ratiba za ibada/ Ushauri/ Maswali.
Piga namba hizi: +255693036618 au +255789001312

pia kama utapenda uyapate mafundisho haya kwa njia ya Whatsapp au email basi tutumie ujumbe kwenye namba hizo hizo.


Mada Nyinginezo:

Kwanini Yesu aliwaambia wale wakoma wakajionyeshe kwa makuhani?

UTAONA MAMBO MAKUBWA KULIKO HAYA.

KITABU CHA YUDA: SEHEMU YA 1

DHAMBI YA MAUTI

Rudi nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
2 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Marwa muniko chacha
Marwa muniko chacha
2 months ago

Nilianza kujisomea mafundisho haya tangu mwezi wa nne mwaka huu,kwa kweli yamenijenga mno, nakiri kumfahamu Mungu zaidi ya nilivyokuwa,Kila mara nifunguapo simu yangu huwa nakimbilia kuangalia Leo Kuna somo gani limetumwa? Nimefurahi sana,uchambuzi ni WA kina na lugha inayotumika ni nyepesi,Bwana Mungu wa Mbinguni Awabariki sana,kwa Baraka za rohoni na mwilini pia,awapiganie na kuwatia nguvu ili huduma hii iwafikie wengine