Swali: Kusaga kunakozungumziwa katika Ayubu 31:10 ni kupi?..na maandiko hayo kwa ujumla yana maana gani?
Jibu: Turejee kuanzia mstari ule wa 9.
Ayubu 31:9 “Kama moyo wangu ulishawishwa kwa mwanamke, Nami nimeotea mlangoni pa jirani yangu;
10 Ndipo hapo mke wangu na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake.
11 Kwani hilo lingekuwa kosa kuu; Naam, lingekuwa ni uovu wa kuadhibiwa na waamuzi”
Maneno haya ni ya Ayubu kwa rafiki zake watatu, ambapo alikuwa anajaribu kuwaambia ukamilifu wake kuwa hajawahi hata kumtazama mwanamke kwa kumtamani (Ayubu 31:1) wala hajawahi kumchukua mke wa jirani yake… Hivyo majaribu yaliyompata si kwasababu ya dhambi au makossa.
Na hapo mstari wa 9 anazidi kujithibitisha kuwa kama “moyo wake ulishawishwa kwa mwanamke, Na ameotea mlangoni pa jirani yake; Ndipo hapo mke wake na asage kwa mwingine, Na wengine na wainame juu yake”.
Akimaanisha kuwa kama yeye aliotea mlango kwa jirani yake, maana yake alisubiri mume wa mke wa jirani yake aondoke kisha aingia na kulala na mwanamke huyo.. basi na yeye pia mke wake na achukuliwe na akasage kwa nyumba ya mwanaume mwingine.
Sasa kusaga kunakozungumziwa hapo ni “kule kusaga nafaka”.. Kumbuka shughuli maarufu ya wanawake wa zamani katika nyumba zao zilikuwa ni kusaga nafaka kama ngano au mtama..
Ndio maana utaona katika lile tukio la unyakuo limefananishwa na wanawake wawili kukutwa wakisaga, na si wanaume..
Luka 17:34 “Nawaambia, usiku huo watu wawili watakuwa katika kitanda kimoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
35 Wanawake wawili watakuwa wakisaga pamoja; mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.
36 Watu wawili watakuwa shambani, mmoja atatwaliwa, mmoja ataachwa.]
Kwahiyo kusagan ilikuwa ni shughuli ya siku zote ya wanawake wa nyumbani, Na walikuwa wanasaga kwa kutumia mawe maalumu yajulikanayo kama “Mawe ya kusagia”
Kwa maelezo ziadi kuhusiana na Jiwe/mawe ya kusagia fungua hapa >>>JIWE LA KUSAGIA
Kwahiyo Ayubu alimaanisha kama aliiba mke wa mtu mwingine, basi wake pia achukuliwe na kutumikia nyumba nyingine, (kwa shughuli hizo za kusaga na nyingine kama za mama wa nyumbani).. na si tu asage, bali pia na wengine wainame juu yake, (maana yake walale naye).
Lakini hayo yote Ayubu hayakumpata kwasababu alikuwa mkamilifu katika njia zake, na wala hakuwahi kulala na mke wa jirani yake, wala kudhulumu, wala kumnyima maskini mkate..njia zake zote zilikuwa ni kamilifu kama Bwana Mungu alivyomshuhudia..
Ayubu 1:1 “Palikuwa na mtu katika nchi ya Usi, jina lake alikuwa akiitwa Ayubu; mtu huyo alikuwa mkamilifu na mwelekevu, ni mmoja aliyemcha Mungu, na kuepukana na uovu”
Ni mambo gani tunajifunza kwa maisha ya Ayubu?
Jambo la kwanza: ni roho ya kumcha Mungu na kuepukana na Uovu.. Watu wanaomcha Mungu na kuepukana na uovu ndio wanaosifiwa naye..
pili: ni Uvumilivu wa Ayubu…Pamoja na majaribu yote yale, alimngoja BWANA, wala hakumwazia Mungu kwa upumbavu (Ayubu 1:22), na mwisho wa siku Bwana alimwokoa na majaribu yale yote.
Yakobo 5:11 “Angalieni, twawaita heri wao waliosubiri. Mmesikia habari ya subira yake Ayubu, mmeuona mwisho wa Bwana ya kwamba Bwana ni mwingi wa rehema, mwenye huruma.”
Je umempokea YESU?..kama bado unasubiri nini?.. Fahamu kuwa mlango wa wokovu hautakuwa wazi siku zote, ipo siku utafungwa, na siku hiyo imekaribia sana, huwenda ikawa leo?..Je parapanda ikilia na ikikukuta ukiwa katika hali hiyo, utakuwa mgeni wa nani?..au ukifa katika hali hiyo kule uendako utakuwa mgeni wa nani?.. Tafakari sana na ufanye maamuzi, kama bado hujaokoka.
Bwana YESU ANARUDI.
Waebrania 10:37 “Kwa kuwa bado kitambo kidogo sana, Yeye ajaye atakuja, wala hatakawia”.
Maran atha!.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Kwa maana kahaba ni shimo refu; Na malaya ni rima jembamba.
MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.
Biblia inamaana gani inaposema “Wewe uchukiaye sanamu, wateka mahekalu?”
About the author