SIFA SITA (6), ZINAZOIKAMILISHA ILE SIKU YA BWANA ITISHAYO.

SIFA SITA (6), ZINAZOIKAMILISHA ILE SIKU YA BWANA ITISHAYO.

Nyakati tunazoishi ni za hatari kubwa, zaidi hizo zinazokuja wakati si mwingi ndio za hatari mno. Watu wengi hawajui kuwa mwisho umekaribia sana, dunia imekwisha, na kwamba SIKU YA BWANA, ipo mlangoni.

Siku ya Bwana ni nini?

Siku ya Bwana ni kipindi fulani maalumu ambacho Mungu amekiandaa ili kuuharibu huu ulimwengu pamoja na watu wote waovu waliopo duniani, na mifumo yao mibovu. Na hiyo itakuja baada ya kanisa la Kristo kunyakuliwa 

Tukisoma katika kitabu cha Sefania tunaelezwa kwa urefu juu ya sifa kuu za siku hiyo itakavyokuja. 

Ametaja sifa zake sita (6), kwa kuziita “siku ya”..”siku ya”…”siku ya”

Tusome..

Sefania 1:14-16

[14]Hiyo siku ya BWANA iliyo kuu i karibu; I karibu, nayo inafanya haraka sana; Naam, sauti ya siku ya BWANA; Shujaa hulia kwa uchungu mwingi huko!

[15]Siku ile ni siku ya ghadhabu, Siku ya fadhaa na dhiki, Siku ya uharibifu na ukiwa, Siku ya giza na utusitusi, Siku ya mawingu na giza kuu,

[16]Siku ya tarumbeta na ya kamsa, Juu ya miji yenye maboma, Juu ya buruji zilizo ndefu sana.

1) Anaanza kwa kusema ni Siku ya ghadhabu.

Ghadhabu ni zao la hasira, na hasira hufuatana na mapigo. ndio hapo tunaposoma kitabu cha ufunuo 16, tunaona kipindi hicho kikifika wale malaika saba watavimimina vile vibakuli vyao saba vya ghadhabu ya Mungu juu ya nchi. na kitakachofuata kwa tendo lile ni mapigo, ndio hapo utaona majipu mabovu, yanawatokea wanadamu, na tena jua linashushwa na kiwaunguza watu, mpaka wanafikia hatua ya kumtukana Mungu.

Ufunuo 16:8-9

[8]Na huyo wa nne akakimimina kitasa chake juu ya jua, nalo likapewa kuwaunguza wanadamu kwa moto. 

[9]Wanadamu wakaunguzwa maunguzo makubwa, nao wakalitukana jina la Mungu aliye na mamlaka juu ya mapigo hayo; wala hawakutubu wala kumpa utukufu. .

2) Siku ya fadhaa na dhiki.

Dhiki na fadhaa ni taabu ambazo mtu anazipata hususani kutoka katika mazingira ya nje. Ukiendelea kusoma sura ile ya 16, utaona mito, chemchemi na bahari zote zinageuzwa kuwa damu, wanadamu wanakosa maji. hofu na mashaka ya mabadiliko ya nchi. Duniani hatakuwa ni mahali penye utulivu, tengeneza picha unaishi katika dunia ya namna hii, utastahimili vipi. Bwana anasema wanadamu watafuta kifo, lakini kifo kitawakimbia.

Ufunuo 16:3  Na huyo wa pili akakimimina kitasa chake juu ya bahari, ikawa damu kama damu ya mfu, na vitu vyote vyenye roho ya uhai katika bahari vikafa.

4  Na huyo wa tatu akakimimina kitasa chake juu ya mito na chemchemi za maji; zikawa damu. 5  Nami nikamsikia malaika wa maji akisema, Wewe u mwenye haki, uliyeko na uliyekuwako, Mtakatifu, kwa kuwa umehukumu hivi;

6  kwa kuwa walimwaga damu ya watakatifu na ya manabii, nawe umewapa damu wainywe; nao wamestahili

3) Siku ya uharibifu na ukiwa

Sio tu mapigo na dhiki, lakini pia kuharibiwa kwa huu ulimwengu na mifumo yake kutafuata, kwasababu biblia inasema siku hiyo kutatokea tetemeko kubwa la ardhi ambalo halijawahi kutokea tangu dunia kuumbwa, mpaka visiwa kuhama, inasema moto utatokea kuharibu huu ulimwengu, mfano wa sodoma na gomora na mfano wa kipindi cha gharika.

2 Petro 3:10-12

[10]Lakini siku ya Bwana itakuja kama mwivi; katika siku hiyo mbingu zitatoweka kwa mshindo mkuu, na viumbe vya asili vitaunguzwa, na kufumuliwa, na nchi na kazi zilizomo ndani yake zitateketea. 

[11]Basi, kwa kuwa vitu hivi vyote vitafumuliwa hivyo, imewapasa ninyi kuwa watu wa tabia gani katika mwenendo mtakatifu na utauwa, 

[12]mkitazamia hata ije siku ile ya Mungu, na kuihimiza; ambayo katika hiyo mbingu zitafumuliwa zikiungua, na viumbe vya asili vitateketea na kuyeyuka? 

4) Siku ya giza na utusitusi.

Giza na utusitusi unaozungumziwa hapa ni ule wa rohoni. ni kipindi ambacho watu watautafuta uso wa Mungu lakini hawatauona, ndio maana Yesu alisema imetupasa kuzifanya kazi zake yeye aliyetupeleka maadamu ni mchana, usiku waja asioweza mtu kufanya kazi. watu watamwita Mungu, lakini hakutakuwa na majibu yoyote.

Mithali 1:27 Hofu yenu ifikapo kama tufani, Na msiba wenu ufikapo kama kisulisuli, Dhiki na taabu zitakapowafikia.  28 Ndipo watakaponiita, lakini sitaitika; Watanitafuta kwa bidii, wasinione.  29 Kwa kuwa walichukia maarifa, Wala hawakuchagua kumcha Bwana.  30 Hawakukubali mashauri yangu, Wakayadharau maonyo yangu yote

5) Siku ya mawingu na giza kuu. 

Vilevile kwa jinsi dunia hii itakavyoharibiwa jua na mwezi na nyota vitazuiliwa.. duniani kutakuwa na giza ambalo halijawahi kutokea, na hayo ndio yatakuwa yale mapigo ya mwisho mwisho kabisa yatakayokuwa yanaukaribisha ujio wa pili wa Yesu duniani.

Vilevile wingu zito litatandaa angani, mawe mazito yatashuka duniani kama talanta, jiwe lenye uzito wa kg 34, hatujui itakuwa ni mvua ya namna gani, hiyo.

Ufunuo 16:18-21

[18]Pakawa na umeme na sauti na radi; na palikuwa na tetemeko la nchi kubwa, ambalo tangu wanadamu kuwako juu ya nchi hapakuwa namna ile, jinsi lilivyokuwa kubwa tetemeko hilo. 

[19]Na mji ule mkuu ukagawanyikana mafungu matatu, na miji ya mataifa ikaanguka; na Babeli ule mkuu ukakumbukwa mbele za Mungu, kupewa kikombe cha mvinyo ya ghadhabu ya hasira yake. 

[20]Kila kisiwa kikakimbia, wala milima haikuonekana tena. 

[21]Na mvua ya mawe kubwa sana, ya mawe mazito kama talanta, ikashuka kutoka mbinguni juu ya wanadamu. Wanadamu wakamtukana Mungu kwa sababu ya lile pigo la mvua ya mawe; kwa maana pigo lake ni kubwa mno.

6) Anasema pia ni siku ya tarumbeta na ya kamsa.

Kamsa ni kelele za vita. Maana yake katika kipindi hicho cha siku ya Bwana, vita vitakuwepo, ndio ile vita ya mwisho ijulikanayo kama Harmagedoni.Mataifa yote yatahusika. lakini Bwana awataua watu wengi sana. damu nyingi sana zitamwagika. ni nyakati ambayo hakutakuwa na shujaa, kila mtu ataomboleza mpaka mashujaa, wafalme na matajiri wote hao watalia sana, pesa zao hazitawasaidia wataomba milima iwaangukie wafe haraka, kuliko kushuhudia huo mfululizo wa mapigo ya Mungu mwenyezi.

Na ndio maana ukimalizia kusoma mistari inayofuata pale kwenye kitabu cha Sefania anasema

Sefania 1:17-18

[17]Nami nitawaletea wanadamu dhiki, hata watakwenda kama vipofu, kwa sababu wamemtenda BWANA dhambi; na damu yao itamwagwa kama mavumbi, na nyama yao kama mavi. 

[18]Fedha yao wala dhahabu yao havitaweza kuwaokoa katika siku ile ya ghadhabu ya BWANA; bali nchi yote pia itateketezwa kwa moto wa wivu wake; maana atawakomesha watu wote wakaao katika nchi hii, naam, ukomo wa kutisha. 

Ndugu yangu, ikiwa unyakuo ukipita leo, fahamu haya utayashuhudia, wakati huu si wa kumbelelezewa wokovu, ni kuamka na kuikimbilia neema, nyakati mbaya zimekaribia, haya mambo ya duniani yatakufikisha wapi? uhai wako umefichwa wapi? Ukifa leo huko uendako utakuwa mgeni wa nani.Kwasababu huko nako kuna mateso makali vilevile kama hapa.

Embu dhamiria kutubu na kumgeukia Bwana Yesu leo, akupe msamaha wa dhambi bure. Hukumu ya Mungu inatisha. 

Ikiwa upo tayari kumpokea Yesu maishani mwako. Na unatamani leo Yesu akutue hiyo mizigo ya dhambi. Basi waweza kusali sala hii kwa imani. Ukijua Kristo wakati wote yupo kutuokoa. Kumbuka kinachotangulia ni kuamini. Kisha ndipo kukiri.

Hivyo

Hapo ulipo piga magoti, kisha dhamiria moyoni mwako kuyasema maneno haya, na moja kwa moja leo, utapokea msamaha wa dhambi zako hapo hapo ulipo, 

Sema.

Ee Bwana Yesu asante kwa kuja kwako duniani, kutukomboa sisi wanadamu tuliokuwa tumepotea, kwa kifo chako pale msalabani na kufufuka kwako. Ninaamini kuwa wewe ndio Bwana na mwokozi, nami napokea neema uliyonipa bure ya ondoleo la dhambi, tangu leo ninakubali kufanyika mwana wako, na kugeuka kuacha njia mbaya za kale. Asante kwa kuwa unanipa nguvu hiyo na kuliandika leo jina langu katika kitabu cha uzima. Nami nafanyika kiumbe kipya. Asante kwa kunipokea, asante kwa kunisamehe, Asante kwa kunifanya mwana wako.  Ninaomba nikiamini katika jina la Yesu Kristo Amen.

Basi ikiwa umesema sala hiyo toka moyoni kwa imani. Tayari umeshaupokea wokovu. Na hivyo hatua zilizobakia kwako ili kuitimiza haki yote, ni wewe kubatizwa. Tafuta mahali wabatizwapo kwa maji tele, na kwa jina la Yesu Kristo.  Ikiwa utahitaji msaada pia waweza kuwasiliana nasi kwa namba zetu chini.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1

Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine

MBINGU MPYA NA NCHI MPYA. (Sehemu ya 1)

JE KANISA LITAPITIA DHIKI KUU?

SIKU YA UNYAKUO ITAKUKUTAJE?

Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments