MUNGU AKETIYE MAHALI PA JUU PALIPOINUKA.

MUNGU AKETIYE MAHALI PA JUU PALIPOINUKA.

Isaya 6:1

[1]Katika mwaka ule aliokufa mfalme Uzia nalimwona Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana, na pindo za vazi lake zikalijaza hekalu.

Je unayajua makao hasaa ya Mungu?

Ni kweli tunafahamu Mungu anaketi katika kiti chake cha enzi, lakini ni kiti kilicho wapi hasaa?

Je! handakini? Mabondeni? Mapangoni? Kichakani? hasha!

Maandiko yanatueleza “Bwana ameketi katika kiti cha enzi, kilicho juu sana na kuinuliwa sana”

Kwahiyo na sisi lazima tuyajue makao hayo, ili tumfikie, vinginevyo tutajikuta tunaabudu Mungu mahali Ambapo kiti chake hakipo.

Katika biblia sehemu yoyote unapokutana na hili Neno “mahali pa juu”, Moja kwa moja utaona palihusishwa Na ibada..Yaani madhahabu zilijengwa pale ili kumtolea Mungu dhabihu. (1Samweli 9:12-13, 1Wafalme 3:2)

Yalikuwa ni maeneo yote yaliyoinuka mfano milimani. Kwasababu huko ndiko Mungu alikuchagua kujidhihirisha, na sio mabondeni, au mapangoni.

Ni kwanini?

Kwasababu Mungu anakaa sehemu Bora kuliko zote, sehemu iliyozidi vyote, sehemu ya juu ya juu kuliko zote. Hakai penginepo, Mungu hawekwi chini, haabudiwi mabondeni..kamwe hiyo sio sifa yake.

Hivyo ni vema ukafahamu sifa yake hii, ili tujue namna sahihi ya kumwendea.

Sasa sehemu zake za juu, kiroho tutaziona katika makundi matano(5), kisha tutaona namna anavyopaswa kufikiwa.

1). Makazi:

(Mbinguni)

Kimakazi Mungu anaketi mbinguni.. Kwasababu Mbingu ni bora kuliko dunia hii.

Isaya 66:1

[1]BWANA asema hivi, Mbingu ni kiti changu cha enzi, na dunia ni mahali pa kuweka miguu yangu; mtanijengea nyumba ya namna gani? Na mahali pangu pa kupumzikia ni mahali gani?

Ndio maana tuna ujasiri na Mungu, akatie sehemu Bora zaidi ya hii, ambayo alisema atatukaribisha katika makao hayo baadaye.

Bwana Yesu alituambia tukisali tuseme Baba yetu uliye mbinguni.. (Mathayo 6:9). Hata alipoomba aliinua macho yake juu(Yoh 17:1), na sisi tumtakaripo Mungu, tuiweke picha hiyo akilini mwetu. Kwamba Baba yetu yupo mbinguni.

Na kutoka huko ndio tunatarajia mema yetu yaje, Na wenyeji wetu kushuka.(Yerusalemu mpya).

2) Viumbe.

(Mwanadamu).

Mwanadamu ametukuka kuliko viumbe vyote, amemvika uwezo na mamlaka (Zab 8:4-6). ndio maana amechagua kuketi ndani ya moyo wa mwanadamu na sio kiumbe kingine chochote. Mungu hakai ndani ya swala, au sungura, au simba.. amechagua makao yake kuwa ndani ya mwanadamu tu.

Na aliyetufungulia lango hilo ni Yesu Kristo mwokozi wetu, kama mwanadamu wa kwanza ambaye Mungu alikaa ndani yake kikamilifu. Pasipo yeye kamwe Mungu asingekaa ndani ya moyo wa mwanadamu.

Ukimkosa Kristo umemkosa Mungu ndani yako.

Hivyo wewe uliyeokoka, fahamu kuwa Mungu anakaa ndani yako, hivyo wajibu wa kujichunga sana na kumpa Mungu ibada ya kweli( Warumi 12:1)

Ndio maana anapouheshimu mwili wako umemuheshimu Mungu. Kama mwanadamu ogopa sana kujiharibu kwasababu wewe ni mahali pa juu sana palipoinuka pa Mungu.

1 Wakorintho 3:16-17

[16]Hamjui ya kuwa ninyi mmekuwa hekalu la Mungu, na ya kuwa Roho wa Mungu anakaa ndani yenu?

[17]Kama mtu akiliharibu hekalu la Mungu, Mungu atamharibu mtu huyo. Kwa maana hekalu la Mungu ni takatifu, ambalo ndilo ninyi.

3) Tabia

(Utakatifu)

Mungu ni mtakatifu, hivyo amechagua usafi zaidi ya uchafu, yeye ni Nuru si giza, ni mkamilifu si mwenye kasoro.

Hivyo tufahamu kuwa, tukimwendea yeye? kwa kupenda usafi? Lazima tutamwona.Lakini tukisema tunamtafuta na huku ni wachafu, hapo bado hatujamfikia Mahali pake pa juu anapoketi.

Isaya 57:15

[15]Maana yeye aliye juu, aliyetukuka, akaaye milele; ambaye jina lake ni Mtakatifu; asema hivi; Nakaa mimi mahali palipoinuka, palipo patakatifu; tena pamoja na yeye aliye na roho iliyotubu na kunyenyekea, ili kuzifufua roho za wanyenyekevu, na kuifufua mioyo yao waliotubu.

Sehemu nyingine anasema..

Zaburi 24:3-4

[3]Ni nani atakayepanda katika mlima wa BWANA? Ni nani atakayesimama katika patakatifu pake?

[4]Mtu aliye na mikono safi na moyo mweupe, Asiyeiinua nafsi yake kwa ubatili, Wala hakuapa kwa hila.

Soma pia, Zab 15

4) Uweza:

(Imani)

Mungu si dhaifu, hivyo jambo lolote linaloonekana lina Nguvu, lililotukuka, lipitalo uwezo au ufahamu wa kibinadamu ni lake.

Ndio maana mtu anayemwendea Mungu kuomba yasiyowezekana kibinadamu, amemfikia Mungu.

Anaitwa Mungu wa miungu, Ibrahimu alimwamini Mungu kwa yasiyowezekana akawa rafiki wa Mungu, watu wote walio wa Imani ndio wanaomwona Mungu, Akiwatendea miujiza. Fahamu kuwa Mungu anavutiwa zaidi na yale yasiyowezekana Kibinadamu kuliko yale yanayowezekana..Jifunze kuishi kwa Imani, maana hapo ni mahali pake pa juu.. ondoa mashaka Ndani yako. Utamfikia Bwana hakika.

5) Ibada:

(Heshima)

Katika eneo la ibada, Mungu hafanyiwi Ibada ilimradi ibada. akiabudiwa ni lazima iwe katika Roho na kweli. Tunamtolea ibada ya juu sana..ikiwa ni sadaka Hatumpelekei kilema, bali ile ya juu zaidi, ikiwa ni sifa tunamsifu kwa nguvu zetu zote, kama Daudi,bila kujali kitu, kama ni kumtukuza Basi tunamtukuza sana na kumwadhimisha kwa viwango vyote.

Kwasababu yeye ndiye Mungu wetu astahiliye sifa zote.

Hivyo yatupasa maeneo yote hayo, tuyatambue, kisha tumwabudu kiufasaha Mahali pake pa Juu palipoinuka.

Zaburi 113:5-6

[5]Ni nani aliye mfano wa BWANA,  Mungu wetu aketiye juu;  [6]Anyenyekeaye kutazama,  Mbinguni na duniani?

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments