Mathayo 12:36 “Basi, nawaambia, KILA NENO LISILO MAANA, watakalolinena wanadamu, watatoa hesabu ya neno hilo siku ya hukumu.
37 Kwa kuwa kwa maneno yako utahesabiwa haki, na kwa maneno yako utahukumiwa”.
Mfano wa maneno yasiyo na maana ni maneno yote ya kukufuru, kulaani, kutukana, mizaha, mashindano, mazungumzo machafu, nyimbo za kidunia na mengine yanayofanana na hayo.
1. Mizaha
Unapotumia baadhi ya mistari ya kwenye Biblia au matukio kwaajili ya kufanya utani, au mzaha au vichekesho…maneno hayo utayatolea hesabu siku ile. Biblia sio kitabu cha comedy.
Zaburi 1:1 “Heri mtu yule asiyekwenda katika shauri la wasio haki; Wala hakusimama katika njia ya wakosaji; Wala hakuketi barazani pa wenye mizaha”.
2. Dhihaka.
Unapotoa dhihaka juu ya Neno la Mungu, au Watumishi wa Mungu ambao unajua kabisa ni wa kweli, siku ya mwisho utatoa hesabu..
3. Mabishano na Mashindano.
Unapobishana na ukweli, kwasababu tu unataka uonekane unajua au unatafuta ushindi wa maneno.. basi fahamu kuwa siku ya mwisho utatoa hesabu ya maneno yako yote… Biblia inasema mashindano ya dini yote ni maneno yasiyo na maana..
1Timotheo 6:20 “Ee Timotheo, ilinde hiyo amana; ujiepushe na maneno yasiyo ya dini, yasiyo na maana, na mashindano ya elimu iitwayo elimu kwa uongo”
4. Kufuru
Unapotoa kufuru na kashfa juu ya kazi ya Mungu, na moyoni unajua kabisa ni kazi kamili ya Mungu, mbeleni kuna kutoa hesabu ya maneno yaliyotoka kinywani.
Mafarisayo walinena maneno ya kumkufuru Roho Mtakatifu katika kitabu hiko cha Mathayo 12, na ndio sababu ya Bwana YESU kusema maneno hayo kuwa “kila neno lisilo maana watu watatoa hesabu yake siku ya mwisho”.
5. Nyimbo za kidunia.
Maneno yaliyopo kwenye nyimbo za kidunia hayana maana na yanamtukuza shetani, na hivyo hata maneno ya nyimbo hizo yatatolewa hesabu.
Amosi 6:5 “ninyi mnaoimba nyimbo za upuzi pamoja na sauti ya vinanda, na kujifanyizia vinanda vya namna nyingi, kama vile Daudi”.
6. Mazungumzo machafu.
Mazungumzo machafu ni yale yote ya kijiweni au ya mtu na mtu, ambayo ni mazungumzo ya uasherati, ushabiki, uhuni, na mipango mibaya, matusi na mambo mengine yote mabaya.. yote hayo mtu atayatolea hesabu siku ya mwisho.
Sasa nini maana ya kutoa hesabu?
Kutoa hesabu maana yake ni kutoa “maana au tafsiri ya kina ya kile kilichotoka kinywani”. Kwamfano kama mtu umemtukana mtu na kumwita yeye ni Mbwa, basi siku ile utaeleza sababu za kumwita vile, na kama kweli yeye ni mbwa kama ulivyosema… kwaufupi maneno ambayo sisi tuliyatamka kwa utani tu na ufupi, kule yatarefushwa na kuwa mada ndefu mno.
Hivyo hatuna budi kuwa makini na yanayotoka kinywani mwetu.. kwamaana yanarekodiwa yote, na pia ni vizuri kama tumekosea kwa vinywa vyetu kuwahi kurudi kutubu kwa tuliyemtolea maneno mabaya, au tuwahi kurudi kwa Mungu kutubu ili tusiangukie hukumu.
Hukumu inakuja, hukumu inakuja, tumwamini YESU na kutubu na tuyashike sana maungamo yetu.
Ubarikiwe.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
KILA MTU ATATOA HABARI ZAKE MWENYEWE.
About the author