SHUKURU, ITA NA JULISHA.

SHUKURU, ITA NA JULISHA.

Labda unaweza kujiuliza maana yake nini maneno haya, tusome Zab.105:1

Zaburi 105:1 “Haleluya. Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake, Wajulisheni watu matendo yake”.

“Kumshukuru Mungu” na “Kuliitia jina lake” na “ Kuwajulisha watu matendo yake” Ni mambo ya msingi sana kuyafanya.

Haya ni mambo makuu matatu (03) yaliyo ya muhimu na msingi sana, hebu tuyasome tena mahali pengine katika maandiko..

Isaya 12:4 “Na katika siku hiyo mtasema, Mshukuruni BWANA, liitieni jina lake; Yatangazeni matendo yake kati ya mataifa, Litajeni jina lake kuwa limetukuka”.

Soma pia 1Nyakati 16:8.

   1. MSHUKURU MUNGU

Kumshukuru Mungu ni agizo la Mungu!.. Kumshukuru Mungu kwaajili ya uzima aliokupa, pumzi, ulinzi, Rehema, Fadhili na mambo mengine yote ni jambo linalompendeza MUNGU sana.

     2. LIITE JINA LA YESU

Vivyo hivyo, KULIITIA JINA LA MUNGU ni agizo!.. Tunapopitia vitisho, majaribu au mapito mengine yoyote ni lazima tuliitie jina la Mungu wetu, kwasababu hata waabuduo miungu huita majina ya miungu yao, ndivyo maandiko yanavyotuonesha..

1 Wafalme 18:25 “Eliya akawaambia manabii wa Baali, Jichagulieni ng’ombe mmoja, mkamtengeze kwanza; maana ninyi ndio wengi; mkaliitie jina la mungu wenu, wala msitie moto chini”

Nasi tunapaswa tuliitie kila wakati jina la YESU, ambalo ndilo pekee lituokoalo ( Matendo 4:12).

Watu wa MUNGU tunapoliita jina la YESU, vifungo vinakatika na mbingu na nchi zinatetemeka, tangu Siku za Sethi mpaka leo jina la MUNGU lina nguvu ile ile ya kuokoa.

Mwanzo 4:26 “Sethi naye akazaa mwana; akamwita jina lake Enoshi. Hapo ndipo watu walipoanza kuliitia Jina la BWANA”.

Soma pia Mwanzo 12:8, Mwanzo 13:4, Mwanzo 21:33,  Mwanzo 26:25,  Utaona ilikuwa ni desturi ya watu wote wa Mungu enzi za Biblia.

Na tunapoliitia jina la Bwana, anaitika.

Zaburi 99:6 “Musa na Haruni miongoni mwa makuhani wake, Na Samweli miongoni mwao waliitiao jina lake, Walipomwita Bwana aliwaitikia”

Lakini pia kama hatujamaanisha kumfuata Mungu na tukaliitia jina lake tunajiletea matatizo badala ya msaada, soma ile habari ya wana  watano wa Skewa utaelewa vizuri. (Matendo 19:13-15).

Kwahiyo ili tujidhi vigezo vya kuliita jina la MUNGU, ni lazima tumaanishe kumfuata MUNGU na kuacha dhambi (huo ndio Msingi).

2 Timotheo 2:19 “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake. Na tena, Kila alitajaye jina la Bwana na auache uovu”.

         3.WAJULISHE WATU MATENDO YA MUNGU.

Kumshuhudia Mungu mbele za watu, kwa kazi zake ni nguzo ya tatu ya msingi…

Na ushuhuda wa kwanza tunaopaswa kushuhudia ni kufufuka kwa YESU, Hilo ni tendo kuu la kwanza Mungu alilolifanya, kumfufua YESU kutoka katika mautini… na kwa kupitia huyo tunapata ondoleo la dhambi.

Shuhuda nyingine kama kuponywa magonjwa, kuokoka na ajali na majanga na kubarikiwa zinasimama kuthibitisha ushuhuda mmoja mkuu wa kufufuka kwa YESU na ondoleo la dhambi kwa wote wanaomwamini.

1 Yohana 5:11 “Na huu ndio ushuhuda, ya kwamba Mungu alitupa uzima wa milele; na uzima huu umo katika Mwanawe”.

Je wewe uliyempokea YESU kama mwokozi, je unafanya hayo?…je Una Desturi ya kumshukuru MUNGU kila wakati, au mambo yote anayokutendea wewe unaona ni kawaida tu?.

Na je una desturi ya kuliitia jina la MUNGU, kama huna desturi hiyo anza sasa utaona matokeo yake..

Na mwisho unayo desturi ya kushuhudia matendo makuu ya MUNGU?..Kama bado anza leo.

Kwa mambo hayo matatu, tutaweza kuangusha Ngome na kumpendeza MUNGU.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply