KARAMA ILIYO KUU.

KARAMA ILIYO KUU.

Jina la Bwana wetu Yesu Kristo lihimidiwe!

Karibu tujifunze pamoja Neno la Mungu ambapo leo tutajifunza juu ya KARAMA ILIYO KUU. Kama maandiko yanavyosema katika kitabu cha wakorintho..

1 Wakorintho 12: 28 “Na Mungu ameweka wengine katika Kanisa, wa kwanza mitume, wa pili manabii, wa tatu waalimu, kisha miujiza, kisha karama za kuponya wagonjwa, na masaidiano, na maongozi, na aina za lugha.

29 Je! Wote ni mitume? Wote ni manabii? Wote ni waalimu? Wote wanatenda miujiza?

30 Wote wana karama za kuponya wagonjwa? Wote wanena kwa lugha? Wote wafasiri?

31 TAKENI SANA KARAMA ZILIZO KUU. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”.

Tukisoma hapo juu tunaona maandiko yanasema kuna karama zilizo kuu, na kama kuna karama zilizo kuu ina maana kuwa kuna karama moja iliyo kuu zaidi ya nyingine zote. Na hiyo endapo mtu akiipata atakuwa mwenye huduma kubwa kuliko ya wote.

Tukirudi kwenye huo mstari hapo juu tunaona Mtume Paulo akitaja karama kadha wa kadha hapo, mfano Mitume, waalimu, miujiza, karama za uponyaji,karama za lugha, karama za kufasiri lugha,karama za masaidiano, karama za maongozi, karama za kinabii, karama za masaidiano n.k…Ametaja nyingi sana lakini tunaona hajataja karama iliyo kuu zaidi ya yote.

Sasa kwa akili zetu za kibinadamu tunaweza kufikiri kati ya hizo karama Mtume Paulo alizozitaja hapo juu kuna moja au mbili zilizo bora zaidi ya nyingine..au kuna moja kati ya hizo iliyo kuu kuliko zote..mwingine anaweza akafikiri karama ya uponyaji hapo ndio karama kuu Paulo aliyokuwa anaizungumzia…mwingine anaweza akafikiri karama ya kitume hapo ndio karama kuu Paulo aliyokuwa anaizungumzia kwamba tuitake.. Mwingine anaweza akasema karama ya kinabii ndio kuu kati ya hizo zote, mwingine karama ya lugha n.k Kila mtu anaweza kusema ya kwake kati ya hizo hapo juu.

Lakini je! Paulo aliposema takeni sana karama zilizo kuu alikuwa analenga moja wapo ya hizo alizozitaja hapo juu?.. Ili kuelewa ni karama ipi iliyo kuu kuliko zote ambayo Mtume Paulo alikuwa anailenga katika kifungu hicho cha mistari hebu tusome tena ule mstari wa 31..

31 TAKENI SANA KARAMA ZILIZO KUU. Hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”.

Umeona hapo? Anasema “hata hivyo nawaonyesha njia iliyo bora”…au kwa lugha rahisi na nyepesi Mtume Paulo alichokuwa anamaanisha ni kwamba “ hata hivyo nawaonyesha karama iliyo bora”

Sasa hiyo njia iliyo bora au karama hiyo iliyo bora ni ipi Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia?

Tukiendelea kusoma mstari unaofuata baada ya huo wa 31,tunaona Mtume Paulo ameizungumzia hiyo njia iliyo bora au karama iliyo kuu, ambayo tunapaswa tuitafute sana..

1 Wakorintho 13:1 “ Nijaposema kwa lugha za wanadamu na za malaika, kama sina upendo, nimekuwa shaba iliayo na upatu uvumao.

2 Tena nijapokuwa na unabii, na kujua siri zote na maarifa yote, nijapokuwa na imani timilifu kiasi cha kuweza kuhamisha milima, kama sina upendo, si kitu mimi.

3 Tena nikitoa mali zangu zote kuwalisha maskini, tena nikijitoa mwili wangu niungue moto, kama sina upendo, hainifaidii kitu.

4 Upendo huvumilia, hufadhili; upendo hauhusudu; upendo hautakabari; haujivuni;

5 haukosi kuwa na adabu; hautafuti mambo yake; hauoni uchungu; hauhesabu mabaya;

6 haufurahii udhalimu, bali hufurahi pamoja na kweli;

7 huvumilia yote; huamini yote; hutumaini yote; hustahimili yote.

8 Upendo haupungui neno wakati wo wote; bali ukiwapo unabii utabatilika; zikiwapo lugha, zitakoma; yakiwapo maarifa, yatabatilika”.

Umeona! Biblia inasema nijaposema kwa lugha za wanadamu na malaika; hii ikiwa na maana kuwa nijapokuwa na karama ya kuweza kunena lugha za malaika na za wanadamu wote kama sina karama hiyo kuu ya UPENDO mimi sio kitu. Anaendelea kusema nijapokuwa na karama ya KINABII kama sina UPENDO ni bure!..kwahiyo karama ya kinabii si kitu mbele ya karama ya upendo..Mtume Paulo anazidi kueleza nijapokuwa na karama ya Imani timilifu hata kuweza kuhamisha milima kama sijaipata hii karama iliyo kuu ya UPENDO mimi si kitu kabisa. Na karama nyingine zote nijapokuwa nazo lakini nikikosa karama moja iliyo kuu yaani ya UPENDO basi mimi sio kitu kabisa.

Kwahiyo karama iliyo kuu Mtume Paulo aliyokuwa anaizungumzia hapo ni UPENDO. Unaweza ukauliza kwanini UPENDO na si karama nyingine kama unabii, utume, lugha, imani, ualimu n.k kwanini upendo?

Karama ya UPENDO imekuwa ni karama KUU kuliko zote kwasababu NI KARAMA YA MUNGU MWENYEWE. Biblia inasema MUNGU NI UPENDO(1 Yohana 4:8 “Yeye asiyependa, hakumjua Mungu, kwa maana Mungu ni upendo”.)..Mungu sio MTUME, wala MWINJILISTI, wala MUHUBIRI, wala MNENAJI WA LUGHA wala kitu kingine chochote Mungu ni UPENDO..Hiyo ndio sababu UPENDO umekuwa ni karama kuu kuliko zote.

Mungu hakutuumba sisi kwasababu yeye ni nabii, hakutupatia pumzi kwa sababu yeye ni mponyaji, hatusamehi makosa yetu kwasababu yeye ni mwinjilisti, wala hatutimizii mahitaji yetu kwasababu yeye ni mtenda miujiza..Hapana Mungu ametuumba na kutupa pumzi na kutuokoa na kututimizia mahitaji yetu kwasababu yeye ni UPENDO wenyewe ni kama ni hivyo basi ni mwingi wa UPENDO.

Kwahiyo ndugu katika huu mwaka unaoanza pamoja na kwamba tumemwomba Mungu mambo mengi atutimizie, tumwombe pia tuwe kama yeye mwenye UPENDO alivyo, Ambao upendo huu unakuja kwa kujifunza Neno la Mungu, na pia kuchukua hatua ya kujifunza kupenda, kujifunza kusamehe kama yeye alivyotusamehe sisi, mwaka huu usianze na kinyongo na mtu, au na kisasi na mtu, mwaka huu uwe mwaka wako wa kupenda na kufadhili, wasamehe wote waliokuudhi huko nyuma, ili Mungu naye apate nafasi ya kukusamehe mambo yote maovu uliyomtendea mwaka wote wa jana ulioisha, bariki wengine kutoka moyoni kabisa ili na wewe uende kubarikiwa mwaka huu, Kwasababu biblia inasema kipimo kile kile upimacho ndicho na wewe utakachopimiwa..

Umefungua ukurasa mpya, basi uwe mpya kweli kweli katika roho yako pia,hapo utakuwa umemjua Mungu, naye Mungu mwenyewe atakupenda na kukutunza na kukuhifadhi kwasababu yeye mwenyewe ni UPENDO..

Ni maombi yangu kuwa Bwana atatujalia mambo hayo yote na zaidi ya hayo katika mwaka huu, Nakutakia Kheri ya Mwaka mpya 2019, Bwana akakutunze na kukuhifadhi dhidi ya yule mwovu wewe na watu wako na nyumba yako,na familia yako, akakulinde na kukupa afya njema, tangu mwanzo wa mwaka huu hadi mwisho wa mwaka, Bwana akakufanikishe katika mambo yote unayoyafanya yanayompendeza yeye katika JINA LA YESU KRISTO.

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

3 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Deborah
Deborah
1 year ago

Nimelia asubuhi ya Leo .na Mungu anipe kuanza upya😭😭

Emmanuel Kitengule
Emmanuel Kitengule
2 years ago

Amina mwalimu, nimebarikiwa sana.