Udhihirisho wa Bwana Yesu kabla ya kufufuka, ulikuwa ni tofauti na baada ya kufufuka..Kabla ya kusulibiwa Bwana Yesu alikuwa anaonekana kila mahali na sehemu nyingi, hata watu waliotaka kumwona na kumfahamu, walikuwa wakimtafuta kwa bidii wanampata mahali popote..Alifanya huduma yake kwa wazi sana..Lakini haikuwa hivyo tena baada ya kufufuka kwake. Baada ya kufufuka kutoka katika wafu, hakuwa anajidhihirisha kwa kila mtu, isipokuwa kwa watu wachache sana, tena,sana sana wale wanafunzi wake…Wengine wote waliosalia ambao walikuwa hawafuatani naye wala hawajishughulishi na mambo yake, walibakia kuamini uongo kwamba Bwana hajafufuka ameibiwa na wanafunzi wake usiku, na kuzusha kwamba amefufuka.
Kwahiyo waliokuwa wana uhakika kwamba Bwana Yesu kafufuka kweli kweli ni wale wanafunzi wake tu, na ndugu zake Bwana pamoja na kikundi cha watu wachache sana waliokuwa wanafuatana naye, mamilioni ya watu waliokuwa pale Yerusalemu hawakujua chochote..Na siku ya unyakuo itakuwa hivyo hivyo watakaomwona Kristo mawinguni watakuwa wachache sana kati ya mabilioni ya watu wanaoishi duniani.
Wakati hata ule mti ambao ulimsulibishia Bwana haujaoza, Tayari Bwana alikuwa anazungumza na wanafunzi wake katika vyumba vya ndani vya siri. Wakati ambao bado watu walikuwa wanamwombolezea tayari yeye ameshawatokea wengi na kuzungumza nao.
Wakati Pilato, Herode,mafarisayo, masadukayo pamoja na wayahudi wamestarehe wakisheherekea na kudhani Bwana sasa ni marehemu, kumbe maili kadhaa tu hapo,si mbali na wao Bwana anawaaga wanafunzi wake na kuchukuliwa juu mbinguni..
Matendo 1: 4 “Hata alipokuwa amekutana nao aliwaagiza wasitoke Yerusalemu, bali waingoje ahadi ya Baba, ambayo mlisikia habari zake kwangu;
5 ya kwamba Yohana alibatiza kwa maji, bali ninyi mtabatizwa katika Roho Mtakatifu baada ya siku hizi chache.
6 Basi walipokutanika, wakamwuliza, wakisema, Je! Bwana, wakati huu ndipo unapowarudishia Israeli ufalme?
7 Akawaambia, Si kazi yenu kujua nyakati wala majira, Baba aliyoyaweka katika mamlaka yake mwenyewe.
8 Lakini mtapokea nguvu, akiisha kuwajilia juu yenu Roho Mtakatifu; nanyi mtakuwa mashahidi wangu katika Yerusalemu, na katika Uyahudi wote, na Samaria, na hata mwisho wa nchi.
9 Akiisha kusema hayo, walipokuwa wakitazama, akainuliwa, wingu likampokea kutoka machoni pao.
10 Walipokuwa wakikaza macho mbinguni, yeye alipokuwa akienda zake, tazama, watu wawili wakasimama karibu nao, wenye nguo nyeupe,
11 wakasema, Enyi watu wa Galilaya, mbona mmesimama mkitazama mbinguni? Huyu Yesu aliyechukuliwa kutoka kwenu kwenda juu mbinguni, atakuja jinsi iyo hiyo mlivyomwona akienda zake mbinguni.
12 Kisha wakarudi kwenda Yerusalemu kutoka mlima ulioitwa wa Mizeituni, ulio karibu na Yerusalemu, wapata mwendo wa sabato”.
Kwahiyo tunaweza tukaona kujidhihirisha kwa Bwana baada ya kufufuka kulikuwa ni kwa siri sana, sio wote waliokuwa wanajua kinachoendelea wakati ule.
Lakini jambo la kipekee tunaloweza kujifunza ni kwamba, Wakati Bwana anachukuliwa juu katika wingu..wale wanafunzi walikuwa wanamtazama kwa macho yao jinsi alivyokuwa anaondoka hatua kwa hatua..jinsi wingu lilivyomchukua mpaka kupotelea mawinguni…Lakini tunaona baada ya kudumu kwa muda mrefu wakiangalia mawinguni malaika wawili waliwatokea katikati yao na kuwahamisha akili zao wasibaki kuangalia mbinguni, kwa maana Kwa jinsi hiyo hiyo aliyoondokea ndio atakayorudia..hivyo waache kuangalia juu, wakaendelee na mambo mengine yanayohusiana na kuutangaza ufalme wa mbinguni..Mpaka wakati wa Bwana kurudi, wakawe mashahidi wa Yesu Kristo, wakiutangaza ufalme wa mbinguni kwa watu wengine.
Kwa wakati huo ulikuwa ndio ule wakati Bwana Yesu aliowaambia mafarisayo kwamba utafika wakati Bwana arusi ataondolewa na ndipo wanafunzi wake watafunga na kuomboleza.
Mathayo 9: 14 “Wakati ule wanafunzi wake Yohana wakamwendea, wakasema, Kwa nini sisi na Mafarisayo twafunga, bali wanafunzi wako hawafungi?
15 Yesu akawaambia, Walioalikwa arusini wawezaje kuomboleza, muda bwana arusi akiwapo pamoja nao? Lakini siku zitakuja watakapoondolewa bwana arusi; ndipo watakapofunga”.
Siku zote upo wakati ambao Bwana atatembea na Mtu, kama mtu na rafiki yake au mpenzi wake, na upo wakati ambao Bwana atatembea na mtu kama mtu na mtumwa wake..wakati huo Bwana ataondoka juu, na kukutuma kama mfanya kazi katika shamba lake.
Utakuwa ni wakati wa Bwana kugeuza hisia zako, na kukusukuma kwenda kuzaa matunda zaidi badala ya kukaa mwenyewe mwenyewe tu!..
Nakumbuka kipindi cha kwanza kwanza nampa Bwana maisha yangu, nilikuwa sitamani kitu kingine chochote zaidi ya kuondoka kwenye hii dunia na kwenda kwa Baba..Nilikuwa natamani leo Kristo arudi niondoke..(sio kwamba hata sasa bado sikitamani,nakitamani hicho kitu sana) na nilikuwa namwona Bwana akinifariji kwa namna ya kipekee kwa njia hiyo, nilikuwa naona maono, na ishara baadhi kuthibitisha njia hiyo..Lakini ilifika wakati mambo yalibadilika ndani…
Nilianza kuhisi kuna majukumu Fulani nayakwepa, Nilianza kusikia msukumo mwingine tofauti na ule wa kwanza, badala ya kukaa peke yangu na kujifunza tu Neno, na kusikiliza tu mahubiri na kusoma vitabu..huku nikitamani siku yoyote parapanda ilie niondoke…Nilianza kuhisi kuna umuhimu wa kwenda kusambaza habari za Yesu Kristo kwa watu wengine..Jambo hilo lilikuja ndani kwa nguvu sana kwa muda mrefu kidogo..mpaka ikafika wakati siku ikipita pasipo kufanya chochote katika kuisambaza kazi ya Mungu, nakosa amani, hata nguvu za mwili naona zinapungua kabisa..Kwahiyo nikahama kutoka kutazama tu mbinguni na kuanza kazi nyingine ya kuhubiri, ndio angalau unafuu ndani ya nafsi ukarudi.
Kwahiyo ikawa nikiona tu ndani amani imetoweka najua sehemu ya kwenda kuirudisha.. “ni kwenda kuwahubiria wengine habari njema”..amani inarudi kama kawaida na siku yangu inaenda vizuri, tofauti na hapo kwanza ambapo hata nisipofanya hivyo..nikisoma tu Neno na kusikiliza mahubiri na kusali basi Napata amani.
Nimetoa ushuhuda huu mfupi tu wa mimi binafsi kuonyesha kwamba kuna nyakati na majira, kuna wakati wa kukaa na Bwana arusi (Yesu Kristo) na kuna wakati wa Bwana arusi kuondolewa.. Waliooa au walioolewa wanafahamu kuwa kuna wakati wa mume na mke kukaa pamoja kwa raha na furaha, wakiwa wawili tu..na kuna wakati wa majukumu, wakati ambao watoto wamezaliwa wanahitajika kutunzwa, wakati huo upendo lazima ugawanyike kidogo, sehemu Fulani lazima uelekee katika kuwatunza watoto. Upendo unahamia kwa watoto.
Na katika Ukristo nako ni hivyo hivyo, upo wakati wa kufurahi na Bwana, kipindi cha mwanzo cha wokovu lakini pia upo wakati wa kwenda kuzaa matunda, kipindi ambacho Bwana arusi ataondolewa..wakati ambao unalazimika kujihusisha na watoto wa kiroho zaidi, kuliko kitu kingine zaidi…Kama ilivyokuwa kwa wanafunzi, walikaa na Bwana miaka mitatu na nusu kwa raha…na siku Bwana anaondoka walidhani wataendelea kutembea naye na kula naye kama hapo kwanza..walimwuliza Bwana huu ndio wakati wa kurejeshewa ufalme (Yaani wakati wa kutawala na Bwana wao kwa raha na furaha pasipo usumbufu)..Lakini Bwana aliwaambia huo ni wakati wa kupokea nguvu kuwa mashuhuda wake, na kupeleka injili duniani kote na kuleta mazao mengi katika ufalme wa mbinguni…huo sio wakati wa kustarehe tena, ni wakati wa kufunga,na kuombeleza, ni wakati wa kupambana vita.
Kwa kupitia ujumbe huu mfupi, naamini utakuwa umeongeza kitu katika vile Bwana alivyokujalia kuvijua, ni maombi yangu kuwa Bwana atakusaidia Katika hilo, utapofikia katika hiyo hatua au kama upo katika hiyo hatua Bwana akufanikishe sana na azidi kukutia nguvu katika kuifanya kazi yake.
Kama hujampa Bwana maisha yako, nakushauri ufanye hivyo leo, kabla mlango wa Neema haujafungwa, kwa Kristo atakuja na wala hatudanganyi..Yeye anatupenda ndio maana amejitoa maisha yake kwa ajili yako na yangu.Hivyo mgeukie leo ukatubu dhambi zako zote kwa kumaanisha kuziacha, na yeye atakupokea kama alivyoahidi, na pia haraka tafuta mahali ukabatizwe ikiwa haukubatizwa ipasavyo, ili upate ondoleo la dhambi zako, na utakuwa na uhakika wa Uzima wa milele na kuiona Mbingu.
Bwana akubariki, Tafadhali “share” Ujumbe huu kwa wengine,
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.
NINI MAANA YA KUHUBIRI INJILI KWA KILA KIUMBE?
About the author