Baada ya muda mfupi, kinachosikika huko nje ni kilio na mahangaiko ya watu, gesi ile ni mbaya kwasababu inaua oxgen yote, halafu inachoma mapafu mtu akiivuta anasikia kama moto unawaka kwenye kifua chake, damu zinaanza kutoka puani na midomoni, sasa kwa kuwa hakuna sehemu ya kutokea, basi watu kwa kujaribu kuokoa maisha yao wanarukiana huku na kule kama vile kuku aliyechinjwa wakijaribu kutafuta walau hata sehemu ya kuokoa maisha yao. Lakini kwa kuwa gesi ile ni kali sana mtu hafi kifo cha raha bali cha mateso makali na mahangaiko yasiyoelezeka, wengi wao wanakutwa wamekufa huku wametokwa na haja zote mbili. Na ndani ya muda wa dakika chache tu, kila mmoja anakuwa ameshakufa, kisha baadaye kidogo kama baada ya dakika ishirini hivi, askari wa ki-NAZI anakuja kufungua mlango wa ile chemba, na kuvuta miili yote nje. Na wakitoka hao wanaingizwa wengine.