UFUNUO: Mlango wa 20

UFUNUO: Mlango wa 20

Bwana wetu YESU KRISTO apewe sifa, karibu katika mwendelezo wa kitabu cha ufunuo, leo tukiwa katika ile sura ya 20, tunasoma..

Mlango 20.

1 Kisha nikaona malaika akishuka kutoka mbinguni, mwenye ufunguo wa kuzimu, na mnyororo mkubwa mkononi mwake.

2 Akamshika yule joka, yule nyoka wa zamani, ambaye ni Ibilisi na Shetani, akamfunga miaka elfu;

3 akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache.

4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.

5 Hao wafu waliosalia hawakuwa hai, hata itimie ile miaka elfu.

6 Huo ndio ufufuo wa kwanza. Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu.

Katika sura iliyotangulia tuliona jinsi Bwana Yesu Kristo alivyoyahukumu mataifa yote ya dunia katika ile vita kuu ya Har-magedoni, na kuharibu utawala wa dunia nzima, na tuliona pia zile roho mbili kati ya zile tatu chafu yaani roho ya yule mnyama na nabii wa uongo zilitupwa katika lile ziwa la moto, ikiwa imesalia roho moja ya lile joka ambalo ndiye shetani mwenyewe,

lakini katika sura hii tukisoma kuanzia mstari wa 1-3 tunaona shetani akikamatwa na kufungwa na kutupwa kuzimu, kwa muda wa miaka 1000, kumbuka huyu hakutupwa katika lile ziwa la moto kama wale wengine, huyu atafungwa kwa kitambo tu akingojea kuja kufunguliwa baadaye kwa kazi maalumu na kisha ndio aje kutupwa katika lile ziwa la moto aliyomo yule mnyama na nabii wa uongo.

Kuna vitu kadhaa vya kuzingatia hapo…

1) Malaika akishuka kutoka mbinguni. Huyu ni mmoja wa Malaika watakatifu, kumbuka kuna malaika walioasi ambao waliungana na shetani, na kuna waliobaki kuwa waaminifu kwa Mungu, na wametofautiana kimaumbile na uwezo, wapo malaika wa vita na wa sifa n.k na huyu ni mmoja wapo wa vita kwasababu tunaona ameshika mnyororo mkononi mwake..

2) mwenye ufunguo wa kuzimu na mnyororo mkubwa mkononi mwake…Kumbuka Bwana Yesu Kristo baada ya kushinda mauti alizitwaa funguo zote za mauti na kuzimu, kwahiyo watu wote walio hai na waliokufa wapo chini yake yeye…anao uwezo wa kumshusha mtu kuzimu na kumpandisha, huo uwezo anao ndio maana siku za mwisho atawafufua watu wote ambapo wengine atawapa uzima wa milele wengine atawafufua kwa hukumu, hivyo kama anao huo uwezo ni lazima atakuwa na uwezo pia wa kumshusha mtu au kiumbe chochote kuzimu, na ndio hapa tunaona anampa huyu malaika funguo hizo ambazo ni amri ya kumkamata shetani na kumtupa kuzimu. Kuzimu iliyozungumziwa hapa ni SHIMO REFU LISILOKUWA NA MWISHO ( Bottomless Pit).

Huko hakuna raha sana, ni sehemu mbaya ya uchungu ambayo iliwekwa maalumu kwa malaika walioasi sio wanadamu…wanadamu walioasi sasa wanaokufa wanakwenda sehemu yao (kuzimu yao ambayo hiyo na yenyewe ina mateso lakini sio makali kama ya hawa malaika walioasi…(Mapepo na yenyewe yanayokuzimu yao ambapo yakifanya jambo lisilopasa yanakwenda kutupwa huko).

Ndio maana wakati Fulani Mapepo yalimsihi Bwana yasipelekwe shimoni, baada ya kumtesa Yule mtu wa Pwani ya wagerasi…yalijua Bwana tayari alichukizwa na jambo lile la kumtesa Yule mtu anazo amri za kufunga na kufungua..na yalijua endapo Bwana angetamka Neno tu la wao kwenda shimoni, habari yao imeisha….huko shimoni ni mahali ambapo wanafungwa na kuna mateso yasiyoyakawaida.

Luka 8: 30 “Yesu akamwuliza, Jina lako nani? Akasema, Jina langu ni Jeshi; kwa sababu pepo wengi wamemwingia.
31 Wakamsihi asiwaamuru watoke kwenda shimoni.
32 Basi, hapo palikuwa na kundi la nguruwe wengi wakilisha mlimani; wakamsihi awape ruhusa kuwaingia wale. Akawapa ruhusa”.

Na mpaka sasa kuna baadhi ya mapepo yamefungwa huko biblia inasema hivyo…kwa maelezo marefu kuhusu roho za mapepo zilizopo kifungoni bonyeza hapa >>  ‘Vifungo vya Giza vya Milele”

Sasa shetani naye atakamatwa na kwenda kutupwa shimoni, mule mapepo yalipomwomba Bwana asiwapeleke. Atakaa kule kwa muda wa miaka 1000, akionja uchungu mkali kuliko wa wanadamu..Na hatakwenda peke yake bali na mapepo yote pamoja naye…duniani hakutabaki na roho yoyote chafu..watakaa kule kwa maumivu kwa miaka 1000..Kumbuka hilo sio ziwa la Moto…ziwa la Moto litakuja kuzinduliwa rasmi na yeye mwenyewe(shetani) baada ya hukumu ya kiti cheupe ambayo tutakuja kuiona huko mbeleni.

Ufunuo 20:3 “akamtupa katika kuzimu, akamfunga, akatia muhuri juu yake, asipate kuwadanganya mataifa tena, hata ile miaka elfu itimie; na baada ya hayo yapasa afunguliwe muda mchache”.

Baada ya kufungwa tunaona pia ukatiwa muhuri juu yake, Nia ya kutiwa muhuri ni “ili asiwadanganye tena mataifa hata itimie miaka elfu”…Muhuri kazi yake ni kuzuia kitu Fulani kisiendelee juu ya huyo mtu/kitu kwa kipindi Fulani cha muda…Hapa shetani baada ya kufungwa nguvu za upotevu zinaondolewa juu yake, anakuwa hana kitu tena..

Kadhalika na watu wa Mungu wana Muhuri wanaotiwa na Mungu ambao huo Mungu anawatia ili wasipotee au wasidanganywe tena mpaka siku ya ukombozi wao..Na huo Muhuri sio mwingine zaidi ya Roho Mtakatifu…
Waefeso 4:30 ” Wala msimhuzunishe yule Roho Mtakatifu wa Mungu; ambaye kwa yeye mlitiwa muhuri hata siku ya ukombozi.”

Baada ya hapo tunaona jambo lingine katika mstari wa nne,

“4 Kisha nikaona viti vya enzi, wakaketi juu yake, nao wakapewa hukumu; nami nikaona roho zao waliokatwa vichwa kwa ajili ya ushuhuda wa Yesu, na kwa ajili ya neno la Mungu, na hao wasiomsujudia yule mnyama, wala sanamu yake, wala hawakuipokea ile chapa katika vipaji vya nyuso zao, wala katika mikono yao; nao wakawa hai, wakatawala pamoja na Kristo miaka elfu.”

Hapa kuna makundi mawili ya kuyatazama: kundi la kwanza ni la wale waliopewa viti vya enzi na kuketi juu yake kisha kupewa hukumu, na watu hawa si wengine zaidi ya wale watakatifu(bibi-arusi safi) waliokwenda na Bwana katika unyakuo, kama biblia inavyosema watakatifu ndio watakaouhukumu ulimwengu na Bwana Yesu pia alisema katika..

Mathayo 19:27 “Ndipo Petro akajibu, akamwambia, Tazama, sisi tumeacha vyote tukakufuata; tutapata nini basi?

28 Yesu akawaambia, Amin, nawaambia ya kwamba ninyi mlionifuata mimi, katika ulimwengu mpya, atakapoketi Mwana wa Adamu katika kiti cha utukufu wake, ninyi nanyi mtaketi katika viti kumi na viwili, mkiwahukumu kabila kumi na mbili za Israeli.”

Sasa hukumu wanayopewa hapo sio hukumu ya kuwahukumu wengine hapana! Bali hukumu inayozungumziwa hapa ni Mamlaka ya kutawala…hiyo ndio hukumu watakayopewa…Kila mmoja atapewa mji wake wa kutawala (na atakuwa anahukumu juu ya huo mji atakaopewa)..yeye ndiye atakuwa kama mkuu wa huo mji…Hiyo ndio maana ya kupewa hukumu hapo katika mstari wa 4.

Luka 19:16 “Akaja wa kwanza, akasema, Bwana, fungu lako limeleta faida ya mafungu kumi zaidi.

17 Akamwambia, Vema, mtumwa mwema; kwa vile ulivyokuwa mwaminifu katika neno lililo dogo, uwe na mamlaka juu ya miji kumi.

18 Akaja wa pili, akasema, Bwana, fungu lako limeleta mafungu matano faida.

19 Akamwambia huyu naye, Wewe uwe juu ya miji mitano”.

Hapo ulimwengu mpya Bwana anaozungumzia ni ule utawala wa miaka 1000, Kristo atakapotawala na watakatifu wake,

Kundi la pili ni wale waliofufuliwa ambao waliuawa na mpinga-kristo katika ile dhiki kuu, kwa kukataa kusujudia sanamu yake na kupokea chapa katika vipaji vya nyuso zao, hapa watakuwa ni wayahudi na wakristo, hawa nao watafufuliwa na kupewa miili ya utukufu na kuingia katika ule utawala wa miaka 1000 pamoja na Kristo,huo ndio ufufuo wa kwanza, lakini wafu wengine wote waliosalia ikiwemo watu wote walioipokea ile chapa ya mnyama pamoja na watu wote waovu, hawatafufuliwa mpaka ile miaka 1000 itakapoisha, biblia inasema Heri, na mtakatifu, ni yeye aliye na sehemu katika ufufuo wa kwanza; juu ya hao mauti ya pili haina nguvu; bali watakuwa makuhani wa Mungu na wa Kristo, nao watatawala pamoja naye hiyo miaka elfu. Kumbuka hatutakaa mbinguni milele, bali biblia inasema makao yetu yatakuwa na Bwana hapa duniani milele.

Kuna hatari kubwa sana ya kukosa unyakuo, au kufa katika dhambi sasa, kutakuwa hakuna nafasi ya pili, inatisha sana!!

UTAWALA WA MIAKA 1000

Hivyo kwenye utawala wa miaka 1000 Bwana Yesu atairejesha dunia katika hali yake ya mwanzo kama ilivyokuwa pale Edeni, amani itarejea duniani, wanyama wakali hawatakuwa na madhara, simba atakula nyasi, mwanakondoo atachunga na simba. ukisoma

Isaya 11:6 inasema ” Mbwa-mwitu atakaa pamoja na mwana-kondoo, na chui atalala pamoja na mwana-mbuzi; ndama na mwana-simba na kinono watakuwa pamoja, na mtoto mdogo atawaongoza.

7 Ng’ombe na dubu watalisha pamoja; watoto wao watalala pamoja; na simba atakula majani kama ng’ombe.

8 Na mtoto anyonyaye atacheza penye tundu la nyoka, na mtoto aliyeachishwa atatia mkono wake katika pango la fira.

9 Hawatadhuru wala hawataharibu katika mlima wangu wote mtakatifu; maana dunia itajawa na kumjua Bwana, kama vile maji yanavyoifunika bahari.”

Kwahiyo Kifo hakitakuwa na nguvu, ingawa kwa watakaokaidi wachache na kwenda kinyume na utawala adhabu kama kifo zitakuwepo, kwamaana Bwana atawachunga mataifa yote kwa fimbo ya chuma maana biblia inasema ..

Isaya 65:

18 Lakini furahini, mkashangilie daima, kwa ajili ya hivi niviumbavyo; maana, tazama, naumba Yerusalemu uwe shangwe, na watu wake wawe furaha.

19 Nami nitaufurahia Yerusalemu, nitawaonea shangwe watu wangu; sauti ya kulia haitasikiwa ndani yake tena, wala sauti ya kuomboleza.

20 Hatakuwapo tena mtoto wa siku chache, wala mzee asiyetimia siku zake; kwa maana mtoto atakufa mwenye umri wa miaka mia; bali mtenda dhambi mwenye umri wa miaka mia atalaaniwa.

21 Nao watajenga nyumba, na kukaa ndani yake; watapanda mizabibu, na kula matunda yake.

22 Hawatajenga, akakaa mtu mwingine ndani yake; hawatapanda, akala mtu mwingine; maana kama siku za mti ndivyo zitakavyokuwa siku za watu wangu, na wateule wangu wataifurahia kazi ya mikono yao muda wa siku nyingi.

23 Hawatajitaabisha kwa kazi bure, wala hawatazaa kwa taabu; kwa sababu wao ni wazao wa hao waliobarikiwa na Bwana, na watoto wao pamoja nao.

24 Na itakuwa ya kwamba, kabla hawajaomba, nitajibu; na wakiwa katika kunena, nitasikia.

25 Mbwa-mwitu na mwana-kondoo watalisha pamoja, na simba atakula majani kama ng’ombe; na mavumbi yatakuwa chakula cha nyoka. Hawatadhuru wala kuharibu katika mlima wangu mtakatifu wote, asema Bwana.” 

Na Kristo pamoja na watakatifu wake ndio watakaotawala mataifa yote, kumbuka ni wale tu watakaoshinda,

ufunuo 2:26″Na yeye ashindaye, na kuyatunza matendo yangu hata mwisho, nitampa mamlaka juu ya mataifa,

27 naye atawachunga kwa fimbo ya chuma, kama vyombo vya mfinyanzi vipondwavyo, kama mimi nami nilivyopokea kwa Baba yangu.

28 Nami nitampa ile nyota ya asubuhi. ” na pia BWANA YESU anasema ufunuo 3:21 Yeye ashindaye, nitampa kuketi pamoja nami katika kiti changu cha enzi, kama mimi nilivyoshinda nikaketi pamoja na Baba yangu katika kiti chake cha enzi. “

Amen!.

Kwa maelezo marefu juu ya utawala huu bofya hapa ‘utawala wa miaka 1000”

VITA VYA GOGU NA MAGOGU.

Tukiendelea na mistari inayofuata tunasoma..

Ufunuo 20:7-15

“7 Na hiyo miaka elfu itakapokwisha, Shetani atafunguliwa, atoke kifungoni mwake;

8 naye atatoka kuwadanganya mataifa walio katika pembe nne za nchi, Gogu na Magogu, kuwakusanya kwa vita, ambao hesabu yao ni kama mchanga wa bahari.

9 Wakapanda juu ya upana wa nchi, wakaizingira kambi ya watakatifu, na mji huo uliopendwa. Moto ukashuka kutoka mbinguni, ukawala.

10 Na yule Ibilisi, mwenye kuwadanganya, akatupwa katika ziwa la moto na kiberiti, alimo yule mnyama na yule nabii wa uongo.

Nao watateswa mchana na usiku hata milele na milele.

Hapa tunaona baada ya ile miaka 1000 kuisha shetani sasa anafunguliwa tena ili awadanganye mataifa ambao hawakuwa wakamilifu katika njia zao wakati wa utawala wa AMANI wa BWANA wetu YESU KRISTO , ambao wingi wao ni kama mchanga wa bahari, kwahiyo hili ni kundi la watu waliozaliwa ndani ya ule utawala na ndio hao wataizingira kambi ya watakatifu kutaka kufanya vita nao lakini kabla hawajafanya hivyo biblia inasema moto utashuka kutoka mbinguni na kuwateketeza wote, na ndipo shetani akakamatwa na kutupwa katika lile ziwa la moto walipokuwepo yule mnyama na nabii wa uongo. Na kilichobaki itakuwa ni hukumu ya watu wote waovu ambao hawakuwepo katika ufufuo wa kwanza. Na ndio tunaendelea kusoma..

HUKUMU YA KITI CHEUPE

Ufunuo 20:11-15″

11 Kisha nikaona kiti cha enzi, kikubwa, cheupe, na yeye aketiye juu yake; ambaye nchi na mbingu zikakimbia uso wake, na mahali pao hapakuonekana.

12 Nikawaona wafu, wakubwa kwa wadogo, wamesimama mbele ya hicho kiti cha enzi; na vitabu vikafunguliwa; na kitabu kingine kikafunguliwa, ambacho ni cha uzima; na hao wafu wakahukumiwa katika mambo hayo yaliyoandikwa katika vile vitabu, sawasawa na matendo yao.

13 Bahari ikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake; na Mauti na Kuzimu zikawatoa wafu waliokuwamo ndani yake. Wakahukumiwa kila mtu kwa kadiri ya matendo yake.

14 Mauti na Kuzimu zikatupwa katika lile ziwa la moto. Hii ndiyo mauti ya pili, yaani, hilo ziwa la moto.

15 Na iwapo mtu ye yote hakuonekana ameandikwa katika kitabu cha uzima, alitupwa katika lile ziwa la moto. “

Hii ni hukumu ya mwisho ambayo wafu wote waliosalia makaburini watafufuka kila mmoja atahukumiwa kwa matendo yake, kumbuka hapo vilifunguliwa vitabu vya aina mbili.1)KITABU CHA UZIMA 2) VITABU VINGINE.

Sasa anaposema vitabu anamaanisha ni vingi, na hivi si vingine zaidi ya maisha ya kila mmoja wetu alivyoishi hapa duniani,na kile kitabu cha uzima kipo kimoja tu na si kingine zaidi ya NENO LA MUNGU(biblia), na kama unavyosoma hapo kama jina lako halikuonekana katika kile kitabu cha uzima ikiwa na maana kuwa kama MATENDO YAKO(ambayo ndio kitabu chako) hayaendani na kile KITABU CHA UZIMA(yaani biblia) sehemu yako itakuwa ni katika lile ZIWA LA MOTO. Kumbuka biblia inasema “sisi ni BARUA inayosomwa na watu wote” ikiwa na maana maisha yetu ni “KURASA ZINAZOANDIKWA” na kila siku tunafungua ukurasa mpya, siku utakapokufa kitabu chako kitakuwa kimeisha na kufungwa…kinasubiriwa kufunguliwa tena katika ile siku ya hukumu, sasa jiulize! je leo hii kitabu chako unakiandikaje? je maisha yako ya jana na ya leo yanaendana na kile kitabu (Neno la Mungu). Angalia muda unavyokimbia usije ukasema nitatubu siku nitakayokaribia kufa au nikiwa mzee, wakati huo pengine kitabu chako kitakuwa hakina maana tena au hakikidhi viwango vya kufanana na kile kitabu cha uzima, na hiyo ndio maana ya “KUKOSEKANA JINA LAKO KATIKA KILE KITABU CHA UZIMA”.

Na baada ya haya yote kuisha BWANA YESU atakuwa amekwisha waweka maadui zake wote chini na adui wa mwisho ni MAUTI, Kisha baada ya hapo UMILELE unafunguliwa usio kuwa na dhambi,wala vita,wala shida, wala waovu,wala maumivu,wala shetani wala mapepo. Ni MBINGU MPYA NA NCHI MPYA, tutaendelea kujifunza katika sura zilizosalia juu ya hayo.

Je! Leo hii bado unaendelea kuishi maisha ya kutokujali, unavaa vimini,unakuwa mzinzi,mlevi,mtu wa mizaha,msengenyaji, mpenda anasa, mtukanaji,n.k kumbuka biblia ilishaonya kuwa watu kama hao sehemu yao itakuwa katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti, hivyo ndugu maombi yangu ni utubu umgeukie Bwana Yesu angali bado unayo nafasi ya kukiandika kitabu chako vizuri.

Mungu akubariki.

Kwa mwendelezo >>UFUNUO: Mlango wa 21

Ikiwa utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara,  kwa njia ya whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255789001312. Na kama utapenda kwa njia ya E-mail basi tuandikie email yako katika boksi la maoni chini.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP


Mada zinazoendana..


KITABU CHA UZIMA

KITABU CHA UKUMBUSHO

UTAWALA WA MIAKA 1000.


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
NIYIKIZA
NIYIKIZA
1 year ago

ASANTE SANA KWA HUDUMA HII?