Jina la Bwana na Mwokozi wetu YESU KRISTO libarikiwe, karibu tujifunze biblia Neno la Mungu wetu, lililo Taa ya njia zetu na Mwanga wa njia yetu (Zab. 119:105).
Zipo aina tatu (3) za sanamu zinazoabudiwa na watu.
1.Sanamu zenye mfano wa Mtu
2.Sanamu-watu
3.Sanamu-vitu
Tutazame moja baada ya nyingine.
1.SANAMU ZENYE MFANO WA MTU.
Hivi ni vitu vyote visivyo na uhai vyenye mfano wa mtu, ambavyo vinatengenezwa na watu kwa lengo la kuabudiwa.
Tabia ya hizi sanamu kulingana na biblia ni kwamba zina midomo lakini hazisemi, zina macho lakini hazioni, zina masikio lakini hazisikii, zina pua lakini hazinusi..na wanaoziabudu wanafanana na hizo kiroho.
Zaburi 115:4 “Sanamu zao ni fedha na dhahabu, Kazi ya mikono ya wanadamu.
5 Zina vinywa lakini hazisemi, Zina macho lakini hazioni,
6 Zina masikio lakini hazisikii, Zina pua lakini hazisikii harufu,
7 Mikono lakini hazishiki, miguu lakini haziendi, Wala hazitoi sauti kwa koo zake.
8 Wazifanyao watafanana nazo, Kila mmoja anayezitumainia”
Hizi ndio zile zote zinazoabudiwa na wapagani, pamoja na baadhi ya madhehebu yajiitayo ya kikristo. Utakuta sanamu imewekwa ndani ya nyumba ya ibada, na watu wanakwenda kuiangukia na kuisujudia, hata kuitolea sadaka na kuiomba, jambo ambalo ni machukizo makubwa..
Ni dhambi kubwa kusujudia sanamu yoyote ile, Kasome Kutoka 20:1-6.
2. SANAMU-WATU.
Hii ni aina ya pili ya sanamu ambayo ni tofauti kidogo na ile ya kwanza… ile ya kwanza ina midomo lakini haisemi, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii…. Hii ya pili nayo ni hivyo hivyo, ina macho lakini haioni, ina masikio lakini haisikii, ina macho lakini haioni..tofauti tu ni kwamba ile ya kwanza ile ya kwanza haipumui ila hii ya pili inapumua, ile ya kwanza imetengenezwa kwa miti, udongo, chuma, fedha au dhahabu lakini hii ya pili ni Wanadamu.
Sasa tunaisoma wapi katika biblia…
Ezekieli 12: 1 “Neno la Bwana likanijia tena, kusema,
2 Mwanadamu, wewe unakaa kati ya nyumba iliyoasi, WATU AMBAO WANA MACHO YA KUONA, ILA HAWAONI, WANA MASIKIO YA KUSIKIA, ILA HAWASIKII; kwa maana ni nyumba iliyoasi”.
Umeona? Kumbe sanamu sio tu mawe na udongo vinavyoweza kuwa sanamu bali hata watu..
Kama hujamaanisha kumfuata YESU wewe ni SANAMU.. Kwasababu una macho lakini huoni mambo ya rohoni, una masikio lakini husikii sauti ya MUNGU, Una kinywa lakini hakineni mambo ya Mungu, Hivyo wewe ni sanamu pamoja na viungo vyako vyote.
“KICHWA” chako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unakitumikia kwa vitu vya kidunia kama YEZEBELI..
“MASIKIO” yako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unayatumikia kwa kubadilisha vipuli kila siku.
“MACHO” yako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unayatumikia usiku na mchana kupaka uwanja, na kupadilisha kope pamoja na kuchonga nyusi.
“MDOMO” wako ni sanamu/mungu wako, ndio maana unautumika kwa rangi na kila aina ya lipstick
“MIKONO” yako na “MIGUU” ni sanamu/mungu wako, ndio maana unaitumika kwa bangili na kucha za bandia..
“TUMBO” lako ni mungu wako ndio maana unalitumikia kwa kulinywesha pombe na kuliburudisha kwa kila linachohitaji usiku na mchana… Huna muda wa kufunga na kuomba walau kwa wiki mara moja, kwako kufunga ni adhabu kubwa!!..
Wafilipi 3:19 “mwisho wao ni uharibifu, MUNGU WAO NI TUMBO, utukufu wao u katika fedheha yao, waniao mambo ya duniani”.
Ikiwa hujamaanisha kumfuata YESU kila kiungo katika mwili wako ni sanamu/mungu.. Ndio maana biblia inasema tuvifishe viungo vyetu vilivyo katika nchi, maana kwa hivyo huzaa dhambi na NDIO ibada ya sanamu.
Wakolosai 3:5 “Basi, vifisheni viungo vyenu vilivyo katika nchi, uasherati, uchafu, tamaa mbaya, mawazo mabaya, na kutamani, ndiyo ibada ya sanamu;
6 kwa ajili ya mambo hayo huja ghadhabu ya Mungu”.
3. SANAMU-VITU.
Hizi ni sanamu zote zisizo na mwonekano au maumbile ya mwanadamu lakni zinaabudiwa.
Mfano wa hizi ni kazi, fedha, umaarufu, Elimu, Mali kama nyumba, magari, ardhi n.k. Mtu akiwa na hivi na hana KRISTO maishani mwake ni mwabudu sanamu tu!
KUMBUKA: Usipomwabudu MUNGU WA KWELI, basi unaabudu sanamu, na usipoabudu sanamu basi unamwabudu MUNGU WA KWELI, Hakunaga hapo katikati! Ni aidha uwe wa shetani au wa Mungu.
Kama kazi yako inaheshima kuliko Mungu kiasi kwamba unakosa hata siku moja ya wiki kumtolea Mungu wako, hiyo kazi ni sanamu/mungu kwako.
Kama elimu yako, au umaarufu wako au cheo chako kina nguvu kuliko Neno la MUNGU, basi hicho ulichonacho tayari ni mungu wako.
Je umeokoka?…Kumbuka wote wanaoabudu sanamu sehemu yao ni katika lilwe ziwa liwakalo moto na kiberiti kulingana na biblia.
Ufunuo 21:8 “Bali waoga, na wasioamini, na wachukizao, na wauaji, na wazinzi, na wachawi, NA HAO WAABUDUO SANAMU, na waongo wote, sehemu yao ni katika lile ziwa liwakalo moto na kiberiti. Hii ndiyo mauti ya pili”
Bwana akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kupofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx1
Kwa mawasiliano: +255789001312 au +255693036618
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
JIHADHARI NA UONGO WA SHETANI UNAOKARIBIANA NA UKWELI.
Biblia inamaanisha nini kusema Yeye aliye na sikio, na asikie?
About the author