KALAMU YA CHUMA.

KALAMU YA CHUMA.

Kitabu cha Ayubu kinasemekana kuwa ni kitabu kikongwe kuliko vitabu vyote katika biblia, ni ngumu kutabiri kiliandikwa mwaka gani au wakati gani, kwasababu habari zilizopo ndani yake hazihusiani hata kidogo na Taifa la Israeli, wala Ayubu mwenyewe hakuwa Mwisraeli. Tofauti na vitabu vingine ambavyo hata kama waandishi wake walikuwa hawajulikani lakini ukisoma maandishi yake ndani ni rahisi kugundua kiliandikwa wakati gani, aidha wakati wa waamuzi, au wafalme, au wakati wa agano jipya ndio maana ilikuwa ni rahisi wanatheolojia wengi kutabiri viliandikwa wakati gani, lakini kitabu cha Ayubu ni cha kitofauti kidogo…Inakadiriwa kuwa Ayubu aliishi kabla ya Taifa la Israeli kuundwa vizazi vichache tu mbeleni baada ya Nuhu, au vizazi vichache nyuma kabla ya Ibrahimu..
 
Lakini tunapaswa tujiulize ni kwanini tunakiona hichi kitabu cha Ayubu miongoni mwa vitabu vitakatifu?,
Tukisoma maisha ya Ayubu aliyopitia, hakuna asiyejua alipitia majaribu mazito, lakini mwisho wa siku Mungu alikuja kumrudishia kila kitu alichopoteza na kumpa utajiri mara mbili, lakini pia habari zake zingepaswa zifahamike na watu wa kizazi chake tu, au hata kama zingeandikwa basi zingekuja kusomwa na watu wa vizazi vichache mbeleni, au hata kam zingedumu basi kingewekwa na kuwa ni moja vya vitabu vya kihistoria tu za imani na mashujaa, ambavyo hata sasa vipo vingi ambavyo vilivyorekodi matukio ya mashujaa waliyoyafanya zamani za kale, kama vile kitabu cha YASHARI ambacho tunakiona katika (2Samweli 1:18)..
 
Lakini jambo moja tunalisoma, Ayubu alipokuwa katika hali ile ya shida, alitamani sana moyoni mwake mateso anayoyapitia yaandikwe kwa kalamu ya chuma, yadumu milele ili yasomwe na vizazi vyote mbeleni, pengine yeye alivyotamani vile alidhani kuwa Mungu anaweza asimsikie lakini Mungu alimsikia na maneno yake yote aliyokuwa anayazungumza yakaandikiwa kweli kwa kalamu ya Chuma..Na ndio maana hadi leo hii tunayasoma yamewekwa miongoni mwa vitatu vitakatifu.
 
Ayubu 19:23 “Laiti maneno yangu yangeandikwa sasa! Laiti yangeandikwa kitabuni!
24 Yakachorwa katika mwamba milele, Kwa kalamu ya chuma na risasi.
25 Lakini mimi najua ya kuwa Mteteaji wangu yu hai, Na ya kuwa hatimaye atasimama juu ya nchi.
26 Na baada ya ngozi yangu kuharibiwa hivi, Lakini, pasipokuwa na mwili wangu nitamwona Mungu;”
 
Kama tunavyofahamu kalamu ya chuma sikuzote ni tofauti na kalamu za kawaida, kalamu ya kawaida inatumika kuandika tu, na pale mtu anapohijita kufanya marekebisho ni rahisi kwani anafuta tu au anayapaka maandishi yale rangi, na kisha anaandika mengine tena..lakini kalamu ya chuma, yenyewe haina wino, bali yenyewe huwa inaandika kwa kuchonga, hususani kwenye mbao ngumu sana, au mwamba…wale ambao wapo katika sanaa ya uchoraji wanafahamu, inafanana na driller, kama ni Neno Fulani linaandikwa basi ile kalamu inapitishwa kwenye mbao inaichimba mbao ile kulingana na umbo la Neno lile, na ukikosea kidogo tu basi mbao hiyo inatupwa haifai tena, ukiandika umeandika maandishi yale yatadumu milele pale, na kufuta kwake ni kuharibu mbao hiyo yote au mwamba huo, hakuna njia nyingine…
Na ndio maana leo hii tunayasoma maneno ya Ayubu.. Hii ni kuonyesha kuwa hata rohoni ipo kalamu ya chuma ambayo Mungu anaitumia kuandika fadhili au mema ya Mtu anayoyoafanya hapa duniani..
 
Lakini kinyume chake pia ni kweli, kalamu hiyo hiyo ya chuma, inaandika dhambi na makosa ya watu wanayoyafanya hapa duniani.. Na hiyo nayo ikishaandikwa haifutiki tena milele hata iweje, kufutika kwake ni mtu huyo kuangamizwa basi, hakuna njia nyingine.
 
Tukisoma biblia enzi za wafalme wana wa Israeli walikuwa wanamkosea Mungu kwa kiwango cha hali ya juu sana, lakini Mungu kwa rehema zake alikuwa akiwapelekea manabii wake wengi kuwaonya waache dhambi zao na ibada za sanamu, wamrudie Mungu wao, lakini badala yake walikuwa wanawapuuzia, wengine wanawaua, wengine wanawapiga kwa mawe, mpaka ikafakia wakati Mungu akaiandika dhambi yao kwa kalamu ya Chuma..kukawa hakuna tena msamaha..Ndipo Wakati ulipofika walivamiwa na maadui zao ambao ni Mungu mwenyewe aliwaleta wakauliwa sana, wengine wakachukuliwa mateka Babeli wengine Ashuru, wengine walikufa kwa njaa, ndipo walipomlilia Mungu na kuombolezea lakini Mungu hakuwasikia…mji mzima ulichomwa kukawa hakuna tena kitu kinachoitwa Taifa la Israeli, na adhabu hiyo iliwaathiri mpaka watoto wao vizazi na vizazi, kwa muda wa zaidi ya miaka 2500, kulikuwa hakuna taifa linaloitwa Israeli,..Ni mwaka 1948 ndio limekuja kuundwa tena, na kuwa taifa huru kama zamani..
Unaona Siku ya uharibifu wao ilipofika hawakuamini kuwa ndio wao wanachukuliwa mateka tena kama ilivyokuwa kule Misri..
 
Yeremia 17:1 “Dhambi ya Yuda imeandikwa kwa kalamu ya chuma, na kwa ncha ya almasi; imechorwa katika kibao cha moyo wao, na katika pembe za madhabahu zenu;”
 
Hayo ndio madhara ya dhambi ya mtu kuandikwa kwa kalamu ya chuma, inawezekana na wewe, umesikia injili mara nyingi, Mungu amekuonya kupitia njia nyingi, uache hiki auche kile, umgeukie yeye ayatakase maisha yako, lakini hutaki, unaipuuzia hiyo sauti, unaona kama bado unao muda, kumbuka dhambi zako leo zinasameheka sasa, lakini kama utendelea kuukataa wokovu, ujue kuwa umeukataa mwenyewe na umechagua kwa akili zako mwenyewe kudumu katika dhambi. Mungu akishakuona upo hivyo anaiandika dhambi yako kwa kalamu ya chuma, ikishafika hiyo hatua ujue kuwa hakuna kugeuka tena..wewe ni ibilisi milele.
 
2Nyakati 36: 14 Na zaidi ya hayo wakuu wote wa makuhani, na watu, wakakosa mno sawasawa na machukizo yote ya mataifa; wakainajisi nyumba ya Bwana aliyoitakasa katika Yerusalemu.
 
15 Naye Bwana, Mungu wa baba zao, akatuma kwao kwa mikono ya wajumbe wake, akiondoka mapema, na kutuma; kwa sababu aliwahurumia watu wake, na makao yake;
 
16 lakini waliwadhihaki wajumbe wa Mungu, na kuyadharau maneno yake, na kuwacheka manabii wake, hata ilipozidi ghadhabu ya Bwana juu ya watu wake, hata kusiwe na kuponya.
 
17 Kwa hiyo akaleta juu yao mfalme wa Wakaldayo, aliyewaua vijana wao kwa upanga nyumbani mwa patakatifu pao, asiwahurumie kijana wala mwanamwali, mzee wala mkongwe; akawatia wote mkononi mwake”
 
Ndugu Neema si ya kuchezea kabisa…usijaze uovu juu ya uovu..Dunia hii tunayoishi, ipo siku itafika, Kutakuwa hakuna kuponywa tena! Unyakuo ukishapita, hata watu watubu vipi, kutakuwa hakuna msamaha.
 
Tubu angali unao muda, mlango wa neema upo wazi kwa ajili yako, mbingu inakuita, fungua moyo wako sasa.
 
Ubarikiwe sana. Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine. Ili nao waisikie injili.

Mada Nyinginezo:

DHAMBI YA MAUTI.

NGUVU YA UPOTEVU.

MIISHO YA ZAMANI.

MATUMIZI YA DIVAI.

MUNGU KUSEMA NA WEWE PEKEE, HAITOSHI KUKUPA USHINDI.

NABII ELISHA ALIKUWA ANA MAANA GANI KULIA NA KUSEMA”GARI LA ISRAELI NA WAPANDA FARASI WAKE”?


Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments