Je! Ni sahihi kwa mkristo kufundishwa na AI mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.

Je! Ni sahihi kwa mkristo kufundishwa na AI mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.

SWALI: Je! Ni sahihi kwa mkristo kujifunza, au kufundishwa na AI (Artificial Inteligence), mfano wa Chatgpt, deepseek n.k.


JIBU: Ili kujibu swali hili ni vema, kutambua mashine hizi za akili bandia (AI), zinafanya kazi gani.

Kwa ufupi ni kuwa AI, inafanya kazi ya kuchakata taarifa nyingi, kutoka katika vyanzo vingi vilivyopo mitandaoni, mfano vitabu, makala, sauti, machapisho n.k, na hivyo inazichanganya taarifa hizo zote kwa kuangalia muktadha unaofanana na kuzifupisha, na kukujibu.

Hivyo kimsingi, ni chombo ambacho kinatoa msaada mkubwa katika ulimwengu wa sasa, na ndio ukweli usiopingika..Kwasababu kinarahisisha utafutaji wa taarifa. Lakini pamoja na hayo haimaanishi kuwa kinatoa kwa ufasaha wote.

Sasa tukija kwenye eneo la kiroho. Je ni vema mkristo kwenda kuuliza AI, au kuandaa maombi au masomo kupitia hiyo, n.k.

Ukweli ni kwamba Imani, sio taarifa, ni zaidi ya taarifa.. Hizi AI, zinatoa tu taarifa lakini hazitoi mafunuo. Hazina pumzi ya Roho Mtakatifu ndani yake.

Ikiwa unataka kuongeza maarifa kwa sehemu fulani zinaweza kukusaidia, lakini sio kukujenga nafsi, kwani inahitaji pumzi ya Mungu na miongozo ya Mungu wewe kujengwa nafsi, na sio taarifa.

Kwamfano ikiwa wewe ni mchungaji halafu, kila inapokaribia jumapili unachowaza ni kwenda chatgpt, kuiambia ikuandalie somo la kufundisha jumapili,  ndugu hapo hesabu kuwa umepotea kama sio kukengeuka… Tumia hiyo kwenye biashara zako, masomo yako,  projekti zao lakini sio kwenye mambo ya kiroho. Hilo liepuke kabisa.

Kufundisha Neno inahitaji ‘Neno’ mwenyewe (Yesu) akae ndani yako, kwasababu ni UHAI sio taarifa (Waebrania 4:12) ndio hapo itakupasa kupiga magoti kwanza uombe, kwa muda mrefu, utafakari moyoni mwako, ukae kwenye utulivu wa kutosha, ndipo Mungu alipande somo lake moyoni mwako. Ambalo yeye mwenyewe anajua litakuwenda kuwagusa vipi watu wake, wenye changamoto mbalimbali, kwamfano, pengine mtu mmoja alikuwa anakaribia kwenda kujinyonga kwasababu ya ugumu wa maisha na mateso fulani, na Mungu kamwona anataka amsaidie, kwa kuliweka somo linalohusiana na mapito ya Ayubu ili ainuliwe imani. Kinyume chake kwasababu ya uvivu wako wewe unakwenda kuiambia chatgpt (akili bandia), ikuandalie somo. Halafu jumapili utakwenda na taarifa zao sio mafunuo. Badala uokoe roho inayokwenda kujinyonga, unaiambia, “leo tunajifunza kanuni kumi za kudumisha ndoa na mahusiano kibiblia”. Hapo unafanya nini sasa?

Au Neno fulani Bwana anataka kukupa la wakati wako, sasa ikiwa unakimbilia AI ikusaidie, hutaki kuchukua muda wako binafsi kutafakari na kuomba ‘jiandae kukutana na ukame wa kiroho.

Visaidizi hivi, hatupaswi kuvifanya ndio sehemu ya imani yetu, kwamba kila kitu tutegemee kule, hivi ni tone dogo sana kati ya bahari kubwa. Roho Mtakatifu alishatuandalia njia zake, kuu za kujengwa na yeye.

Wekeza zaidi, kuomba msaada kwa wakufunzi wako, viongozi wako, ndugu zako katika Kristo, wekeza katika maombi, mifungo, tafakari, na kujisomea mwenyewe Neno.  kwa njia hizi hakika Bwana atasema nawe na kujengwa zaidi kuliko visaidizi. Lakini pia ikiwa pana umuhimu wa kujiongezea taarifa kwa vile unavyovijua, visaidizi hivi vitakufaa (Katika uangalizi maalumu), vinginevyo utajidumaza kiroho.

Bwana akubariki.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >>  https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Karismatiki ni nini?

Uinjilisti kama agizo kuu la Bwana.

Vita vya kiroho, na mwamini Mpya.

Print this post

About the author

Devis administrator

Subscribe
Notify of
guest
0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments