Si kila wakati maombi yatakuwa ni mazungumzo ya utulivu na amani, wakati mwingine maombi hugeuka kuwa mapambano, na ung’ang’anizi, na usumbufu. Kuna nyakati Mungu anabadilika tabia, kuonyesha kama hakujali hivi, hakusikii hivi, Sio kwamba anakuonea, au anafurahia wewe kuendelea kuteseka katika hali hiyo, hapana bali anafanya hivyo ili kukutengeneza wewe, kwa namna usiyoijua.
Ni lazima ufahamu, Mafanikio ya maombi si lazima yawe majibu, bali mafanikio ya maombi ni mabadiliko yako. Mungu akitaka kukutengeneza, ili tegeo lako lote liwe kwake, hukawia kutimiza ombi Fulani, ili uongeze tegemeo lako lote kwake.
Imani, tumaini, ukomavu, na Upendo wa ki-Mungu, mara nyingi hujengwa katika namna hiyo ya maombi ambayo yanakugharimu kumtaabisha Mungu.
Yakobo alipomtaka Mungu ulinzi, Mungu hakuonyesha kujali hata kidogo, Hivyo mazungumzo yao, yakabadilika kutoka kuwa ya amani, hadi mapambano, wakapigana mweleka usiku kucha mpaka akajeruhiwa uvungu wa paja, ijapokuwa maombi yalikuwa ni ya ung’ang’anizi sana, ya kuumwa, ya kudhoofika, ya kuchakaa, ya kukonda, ya njaa, lakini hakujua anakwenda kubadilisha hali yake ya ndani, alikuwa anaandiliwa kuwa ISRAELI, na sio Yakobo tena mdhaifu.(Mwanzo 32:24-28)
Fahamu kuwa maombi hufanya jambo la ziada juu ya majibu. Wakati mwingine unaweza usijibiwe kabisa hata hilo ombi unaloliomba lakini fahamu kuwa hutabaki kuwa yule yule.. Mtume Paulo, alimlilia sana Mungu (maombi ya ung’ang’anizi), kuhusu mwiba uliokuwa ubavuni mwake uondolewe, ukweli ni kwamba haukuondolewa, lakini alitoka na ufunuo mpya wa “Neema ya Mungu” ukambadilisha mtazamo wa maisha yake moja kwa moja kuhusu Mungu, Maana yake ni kuwa kama mwiba ule usingemtesa na kumlilia sana Mungu asingeielewa neema ya Mungu, ambayo mpaka leo hii tunajifunza kupitia masumbufu yake.
2Wakorintho 12:7-10
7 Na makusudi nisipate kujivuna kupita kiasi, kwa wingi wa mafunuo hayo nalipewa mwiba katika mwili, mjumbe wa Shetani ili anipige, nisije nikajivuna kupita kiasi.8 Kwa ajili ya kitu hicho nalimsihi Bwana mara tatu kwamba kinitoke.9 Naye akaniambia, Neema yangu yakutosha; maana uweza wangu hutimilika katika udhaifu. Basi nitajisifia udhaifu wangu kwa furaha nyingi, ili uweza wa Kristo ukae juu yangu.10 Kwa hiyo napendezwa na udhaifu, na ufidhuli, na misiba, na adha, na shida, kwa ajili ya Kristo. Maana niwapo dhaifu ndipo nilipo na nguvu.
Hii ni siri ambayo wengi hawaijui, Uonapo upo kwenye Wakati mgumu na umeomba kwa namna ya kawaida huoni dalili yoyote ya kujibiwa, anza maombi ya kung’ang’ana, funga zaidi, lia zaidi, kemea zaidi, zama zaidi …Fanya hivyo kwasababu ipo kazi ya ziada Mungu anataka kuitenda ndani yako zaidi ya majibu unayoyataka,. Usiridhike tu na maombi ya utulivu, shindana na Mungu wako, ng’ang’ana sana, ikiwa hujajibiwa jana, endelea leo, tena kwa nguvu zaidi, ukiona hali imekuwa mbaya, usipoe, shughulika na Mungu zaidi na zaidi, hakuna kukata tamaa, hakuna kurudi nyuma, kwasababu Maombi hufanya kazi nyingine ya ndani zaidi ya majibu tu..
Mwisho utauna uzuri wa Mungu, jinsi atakavyokuleta katika matokeo bora zaidi, ambayo utamshukuru Mungu maisha yako milele. Hivyo fahamu kukawia kwake ni kwa faida yako.
Maombolezo 3:31-33
31 Kwa kuwa Bwana hatamtupa mtu Hata milele.32 Maana ajapomhuzunisha atamrehemu, Kwa kadiri ya wingi wa huruma zake.33 Maana moyo wake hapendi kuwatesa wanadamu. Wala kuwahuzunisha
Mungu akubariki.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
NGUVU YA MAOMBI
MWONGOZO WA MAOMBI YA FAMILIA
MWONGOZO WA MAOMBI YA KUJIKUZA KIROHO.
Print this post
Save my name, email, and website in this browser for the next time I comment.
Δ