Swali: Katika Matendo 20:15, tunasoma Mtume Paulo akirejea kauli ya Bwana kwamba akisema “Heri kutoa kuliko kupokea”.. Je ni wapi katika Injili nne, Bwana YESU alisema maneno hayo?
Jibu: Tuanzie kusoma ule mstari wa 33..
Matendo 20:33 “Sikutamani fedha wala dhahabu, wala mavazi ya mtu.
34 Ninyi wenyewe mnajua ya kuwa mikono yangu hii imetumika kwa mahitaji yangu na ya wale waliokuwa pamoja nami.
35 Katika mambo yote nimewaonyesha ya kuwa kwa kushika kazi hivi imewapasa kuwasaidia wanyonge, NA KUYAKUMBUKA MANENO YA BWANA YESU, JINSI ALIVYOSEMA MWENYEWE, NI HERI KUTOA KULIKO KUPOKEA”.
Katika vitabu vyote vinne vya injili (yaani kitabu cha Mathayo, Marko, Luka na Yohana) hakuna mahali popote pameandikwa maneno hayo ya Bwana kama yalivyo kwamba “heri kutoa kuliko kupokea”. Lakini ni wazi kuwa aliyasema mahali fulani ila hayakuandikwa katika vitabu vinne vya injili.
Tunalithibitisha vipi hilo?.. Turejee kitabu cha Yohana 21:24..
Yohana 21:24 “Kuna na mambo mengi aliyoyafanya Yesu; ambayo yakiandikwa moja moja, nadhani hata ulimwengu usingetosha kwa vile vitabu vitakavyoandikwa”.
Hapa Mtume Yohana anasema, yapo mambo mengi aliyoyafanya Bwana YESU ambayo hayakuandikwa katika vitabu hivyo..maana yake yapo maneno mengi aliyoyafundisha na mifano mingi na ishara nyingi alizozifanya ambazo laiti kama zingeandikwa moja baada ya nyingine, dunia isingetoshea kwa vitabu..
Kwa mantiki hiyo basi tunaanza kuelewa kuwa maneno hayo ya “heri kutoa kuliko kupokea” ni kweli Bwana YESU aliwahi kuyasema mahali fulani, isipokuwa tu hayakunukuliwa na waandishi wa vitabu vinne vya injili.
Lakini pamoja na hayo, yapo maneno aliyoyasema yenye mlengo huo huo wa “uheri wa kutoa kuliko kupokea”
Luka 6:38 “Wapeni watu vitu, nanyi mtapewa; kipimo cha kujaa na kushindiliwa, na kusukwa-sukwa hata kumwagika, ndicho watu watakachowapa vifuani mwenu. Kwa kuwa kipimo kile kile mpimacho ndicho mtakachopimiwa”.
Hii ni kauli ya Bwana YESU akitufundisha faida za kuwapa watu vitu, kwani tunapotoa ndivyo tutakavyopokea, na si tupokee kwanza na ndipo tutoe.. hiyo ikithibitisha kuwa ni kweli Bwana alifundisha uheri wa kutoa kuliko kupokea, na pia alituonya tujilinde na “uchoyo”.
Luka 12:15 “Akawaambia, Angalieni, jilindeni na choyo, maana uzima wa mtu haumo katika wingi wa vitu vyake alivyo navyo”.
Je umempokea YESU?.. Je una uhakika akirudi leo utakwenda naye?
Kama bado tengeneza maisha yako kwani majira tunayoishi ni ya hatari na parapanda ya mwisho imekaribia sana kulia.
Bwana atusaidie.
Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea
Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.
Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10
Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312
Bwana akubariki.
Mafundisho mengine:
Print this post