MTOLEE BWANA KWA UFUNUO KAMA HANA

MTOLEE BWANA KWA UFUNUO KAMA HANA

Jina la Bwana YESU libarikiwe, karibu tujifunze Biblia, Neno la MUNGU wetu lililo Taa na Mwanga wa njia zetu (Zab. 119:105).

Katika Biblia tunajifunza jambo kubwa sana kwa mwanamke “Hana” ambaye alikuwa tasa lakini baadae Bwana alimfungua tumbo lake na kuzaa watoto.

Katika usomaji wa kitabu cha 1Samweli mlango wa kwanza na wa pili, ni rahisi kufikiri kuwa Hana alimwekea MUNGU nadhiri ya kumtoa mtoto wake wa kwanza atumike kwenye nyumba ya MUNGU daima, bila kuwa na ufunuo au sababu yoyote (ni rahisi kufikiri hilo).

Lakini tukijifunza kwa undani, tunaona wazi kuwa sababu kuu ya Hana kumtoa mtoto wake wa kwanza (Samweli) atumike kwenye nyumba ya MUNGU daima, ni matatizo aliyoyaona  ndani ya nyumba ya MUNGU, kwa wakati ule.

Kwani walikuwepo wana wawili wa kuhani Eli, walioitwa Hofni na Finehasi, vijana hawa hawakuwa waaminifu katika nyumba ya MUNGU,

Kwani walikuwa wanatumia vibaya dhabihu na sadaka zilizokuwa zinaletwa nyumbani mwa Bwana, na zaidi sana walikuwa wakizini na wanawake waliokuwa wakihudumu ndani ya nyumba ya MUNGU, na sifa zao hizo mbaya ziijulikana na watu wote, na hata mwanamke “Hana” aliwajua kwa sifa hiyo.

1 Samweli 2:22 “Basi Eli alikuwa mzee sana; naye alisikia habari za mambo yote ambayo wanawe waliwatenda Waisraeli; na jinsi walivyolala na wanawake waliokuwa wakitumika mlangoni pa hema ya kukutania.

23 Akawaambia, Mbona mnatenda mambo kama hayo? Maana nasikia habari za matendo yenu mabaya kwa watu hawa wote.

24 Sivyo hivyo, wanangu, kwa maana habari hii ninayoisikia si habari njema; mnawakosesha watu wa BWANA.

25 Mtu mmoja akimkosa mwenzake, Mungu atamhukumu; lakini mtu akimkosa BWANA, ni nani atakayemtetea? Lakini hawakuisikia sauti ya baba yao, kwa sababu BWANA amekusudia kuwaua”.

Kwasababu hiyo basi Hana, aliona shukrani pekee ambayo anaweza kumpa MUNGU endapo Mungu atamfungua tumbo lake si kutoa pesa, kwasababu hata akizipeleka madhabahuni  nyumbani mwa MUNGU zitatumiwa vibaya na wale vijana wawili wa Eli (Hofni na Fineasi), wala si dhabihu kwasababu pia zinatumika vibaya.

Ndipo alipotafakari na kuona nadhiri bora na sadaka maalumu itakuwa ya kumtoa mwanae wa kwanza kwa Bwana akawe Mtumishi wa madhabahuni,

Hiyo aliona inaweza kuwa sadaka njema kwake kwa BWANA, Kwani mtoto yule atakuwa katika misingi sahihi ya kiMungu, na atasimama katika kazi ya nyumba ya Bwana kwa uaminifu na kuwa baraka kwa Israeli yote.

Ndivyo Hana alivyofanya, na kupitia sadaka yake hiyo ya kiufunuo, Mungu alisikia maombi yake na kumpa mtoto Samweli, ambaye ndiye aliyekuja kuwaa nabii mkuu Israeli kwa wakati ule.

Ni hivyo hivyo kwa MUNGU wetu, aliona baraka kubwa atakayoibarikia dunia si kuleta mvua nyingi yenye kustawisha nafaka ili matatizo ya njaa yaishe duniani, wala si kumfanya kila mtu kuwa milionea, bali ni kwa kumtoa mwanae pekee YESU KRISTO, Kama dhabihu iliyo hai na sadaka kuu, na kupitia sadaka hiyo leo hii tunabarikiwa kwa baraka zote.

Na sisi tunajifunza mambo hayo hayo, kutazama katika roho ni nini cha kumtolea BWANA, si kila wakati fedha au mali zitakuwa ni sadaka sahihi kwa MUNGU au kwa Nyumba yake au kazi ya MUNGU, wakati mwingine wewe mwenyewe unaweza kuwa sadaka bora kwa kujitoa mwili wako na muda wako kutumika.

Warumi 12:1 “Basi, ndugu zangu, nawasihi, kwa huruma zake Mungu, itoeni miili yenu iwe dhabihu iliyo hai, takatifu, ya kumpendeza Mungu, ndiyo ibada yenu yenye maana.

Au si wewe bali mwanao anaweza kuwa bora zaidi na akawa sadaka yenye kumpendeza Bwana. (Kwa wewe kumuandaa kuwa mtumishi, kwa kumfundisha, kumwombea na kumtolea sadaka kwa MUNGU).

Kuna wakati ardhi inaweza kuwa sadaka nzuri kwa Bwana zaidi ya fedha, kuna wakati, kununua kitu na kukipeleka nyumbani mwa Bwana inaweza kuwa bora zaidi kuliko kutoa tu fedha, na kuna wakati fedha ni muhimu zaidi kuliko kitu utakachopeleka, hivyo ni muhimu kuwa na jicho la kiroho na kujua ni kipi kinafaa kutoa kwa wakati huo.

Na kumbuka siku zote, ni heri kutoa kuliko kupokea (Matendo 2:35).

Bwana YESU atusaidie katika  kumtolea yeye matoleo yenye kumpendeza.

Shalom.

Washirikishe na wengine habari hizi njema kwa kushea

Ikiwa utapenda kupata msaada wa kumpokea Yesu maishani mwako bure, Basi wasiliana nasi kwa namba uzionazo chini ya makala hii.

Pia kwa kupokea mafundisho ya kila siku kwa njia ya WHATSAPP, jiunge na channel yetu kwa kubofya link hii >> https://whatsapp.com/channel/0029VaBVhuA3WHTbKoz8jx10

Kwa mawasiliano: +255693036618 au +255789001312

Bwana akubariki.

Mafundisho mengine:

Print this post

About the author

Nuru ya Upendo administrator

Leave a Reply