ILI TUONEKANE WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU.

ILI TUONEKANE WAKAMILIFU MBELE ZA MUNGU.

Kama unamchukulia mtu ni adui yako kwasababu amekusengenya, au amekudharau, au amekutukana, au amekuibia, au amekurusha, au amekuaibisha, au amekata mazungumzo na wewe ghafla, au amejisifia mbele zako na kukuona kama wewe si kitu kwasababu yeye pengine anaye mtoto na wewe huna. Hivyo umekuwa ukitamani Mungu amlipize kisasi, aanguke, au ashushwe au ikiwezekana afe kabisa, basi ni dhahiri kabisa dua hizo unazomtakia huyo adui yako kwa namna moja au nyingine zitakurudia wewe mwenyewe..

Kwasababu, kwa mambo kama hayo hayo yanakufanya na wewe kuwa adui kwa mtu mwingine(usiyemtarajia), inawezekana ulishawahi kumkwaza mtu pasipo wewe kujua, au kumuumiza hisia zake pasipo kukusudia kwa maneno yaliyowahi kutoka kinywani mwako, au uliacha kuzungumza naye pengine kwasababu za msingi kabisa pengine huna simu, hivyo yeye akalichukulia jambo lile kwa namna nyingine tofauti, pengine ulijifisia mtoto wako mbele zake kwa nia ya kutokujiinua, na yeye akaona kama vile umewadharau wa kwake, n.k..

Yeye pia atakuona wewe kama adui yake, na pengine yeye naye anaomba mbele za Mungu kama wewe ulivyokuwa unaomba, asambaratishwe, anamwomba Mungu amwinue ili uone mafanikio yake, anamwomba Mungu vikwazo vikukute, upate hasara, au udhaifu pengine hata ufe, anakutaja kila siku kwenye dua zake mbele za Mungu ushushwe chini..Lakini je! ni kweli wewe unastahili kufanyiwa hivyo vitu??. Na kama sio kwanini wewe unamfanyia mwingine? Biblia inasema “Msilaumu, msije mkalaumiwa,” Kwasababu kipimo tutakachopima ndicho hicho hicho tutakachopimiwa.(Luka 6:37)

Cha kuhuzunisha haya ndiyo yamekuwa maombi ya wakristo wengi katika siku hizi za mwisho. Kupelekea maombi mbele za Mungu, ..“Mungu mpige Adui yangu”…Kadhalika na mwenzako anakuombea na wewe upigwe!! Vile vile , hivyo yanakuwa ni maombi ya siri kila mmoja kwa mwenzake. Maombi ya namna hiyo mbele za Mungu huwa hayana matunda yoyote kinyume chake ni kumuhuzunisha Mungu.

Jambo mojawapo ambalo lilimfanya Ayubu aonekane ni MKAMILIFU na MWELEKEVU mbele za Mungu, ni kutokufurahia pale adui zake walipoanguka. Tukisoma katika Ayubu 31,

Ayubu 31: 29 “KAMA NILIFURAHI KWA KUANGAMIA KWAKE HUYO ALIYENICHUKIA, AU KUJIKUZA ALIPOPATIKANA NA MAOVU;

30 (NAAM, SIKUKIACHA KINYWA CHANGU KUFANYA DHAMBI KWA KUUTAKA UHAI WAKE KWA KUAPIZA);”

Unaona hapo?. Ayubu aliogopa hata kumwapiza adui yake mbele za Mungu, kwamba Mungu autoe uhai wake.Walikuwepo watu waliomdharau sana na kumchukia, waliomnenea vibaya, waliokuwa wanamtukana pengine kwa ajili ya haki yake, wapo waliokuwa wanamwonea wivu kwa kufanikiwa kwake, lakini hao hao Ayubu alipoona wameanguka, au wamepatikana na shida, au wamepata madhara au misiba. Ayubu hakusema sasa huu ni wakati wa kusheherekea, kwasababu Bwana amewalipiza kisasi wale waliokuwa wananichukia, maadui zangu wote,.kinyume chake yeye aliwahurumia, na kuwaombea, na kuwatakia heri siku zote, na ndio sababu iliyomfanya Ayubu alionekana kuwa mtu wa kipekee sana mbele za Mungu..mpaka Bwana akamwambia shetani “Je! Umemwangalia huyo mtumishi wangu Ayubu? Kwa kuwa hapana mmoja aliye kama yeye duniani, MTU MKAMILIFU na MWELEKEVU, mwenye kumcha Mungu na kuepukana na uovu. (Ayubu 1:8)”.

Kadhalika pia tukimwangalia Bwana wetu YESU, hakuna mtu yoyote duniani aliyekuwa na maadui wengi kama yeye, Wewe unasema unao maadui, lakini hao maadui zako hawana hata mpango wowote wa kutoa maisha yako kwa gharama zozote, lakini Bwana wetu Yesu alikuwa na maadui ambao baadaye walifanikiwa kuja kumshika na kumtukana,kumdhihaki, kumtemea mate,kumvua nguo, kumpiga, kumwaibisha hadharani na hatimaye kumuuwa,,Lakini je! Aliwatakia laana mbele za Mungu?. Jibu ni Hapana kinyume chake tunaona aliwaombea, na kusema..”Ee Baba uwasamehe, kwa kuwa hawajui walitendalo”.Aliwaombea rehema badala ya Laana..Aliwaombea amani badala ya misiba.

Mahali pengine alifika maadui zake wakamkataa, na wanafunzi wake walipomshauri ashushe moto awaangamize kama Nabii Eliya alivyofanya lakini yeye aliwaambia,

Luka 9: 54 “Wanafunzi wake Yakobo na Yohana walipoona hayo, walisema, Bwana, wataka tuagize moto ushuke kutoka mbinguni, uwaangamize; [kama Eliya naye alivyofanya]?

55 Akawageukia, akawakanya. [Akasema, Hamjui ni roho ya namna gani mliyo nayo.]

56 Kwa maana Mwana wa Adamu hakuja kuziangamiza roho za watu, bali kuziokoa. Wakaondoka wakaenda mpaka kijiji kingine”.

Unaona hapo?. Swali ni lile lile na wewe leo ni roho gani ipo ndani yako?. Kuangamiza au kuokoa,? Biblia inatumbia “Upendo huvumilia yote”, Upendo HAUHESABU MABAYA,(1Wakorintho 13) , Unachopaswa kufanya ni kumwomba Mungu amwokoe na sio kumwangimiza kwa dua zako, Tunachopaswa kuomba, ni Mungu atuepushe na madhara yao, na sio Mungu awaangamize, na ndio maana Bwana Yesu alisema ili sisi tuwe WAKAMILIFU kama Ayubu, ili sisi tuwe WAKAMILIFU kama BABA yetu wa mbinguni tunapaswa tulizingatie Neno hilo…Alisema:

Mathayo 5: 43 “Mmesikia kwamba imenenwa, Umpende jirani yako, na, Umchukie adui yako;

44 lakini mimi nawaambia, Wapendeni adui zenu, waombeeni wanaowaudhi,

45 ili mpate kuwa wana wa Baba yenu aliye mbinguni; maana yeye huwaangazia jua lake waovu na wema, huwanyeshea mvua wenye haki na wasio haki.

46 Maana mkiwapenda wanaowapenda ninyi mwapata thawabu gani? Hata watoza ushuru, je! Nao hawafanyi yayo hayo?

47 Tena mkiwaamkia ndugu zenu tu, mnatenda tendo gani la ziada? Hata watu wa mataifa, je! Nao hawafanyi kama hayo?

48 Basi ninyi mtakuwa WAKAMILIFU, kama Baba yenu wa mbinguni alivyo MKAMILIFU”.

Hivyo ndugu Mungu hapendezwi kila siku tunapompelekea mashtaka mabaya dhidi ya maadui zetu, hiyo inatufanya tunaonekana kuwa hatujakamilika mbele zake, sio kila mara tuzunguke huku na huku, tukisema ..Adui yangu apigwe!..Adui yangu afe!! Adui yangu ashushwe!!…Kwanini tusiseme Adui yangu Bwana ambadilishe!!..Kwanini tusiseme ..Mungu mpe rizki Adui yangu”…kwanini tusiseme Mungu mrehemu adui yangu, hajui alitendalo??… Badilika sasa, Acha kumgeuza mtu kuwa adui yako pale anapokusengenya, pale anapokutukana, pale anapokudharau, au anapojitukuza juu yako.. Kumbuka maisha yako ndiyo yatakayougeuza moyo wa huyo ndugu yako, Fuata ule ushauri wa Bwana, mwombee. Na ndivyo tutakavyoonekana kuwa WAKAMILIFU mbele za Mungu.

Ubarikiwe.

Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine.


Mada Nyinginezo:

MADARAKA YA WAKATI MKAMILIFU.

LULU YA THAMANI.

NINI MAANA YA ELOHIMU?


Rudi Nyumbani

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest
1 Comment
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments
Anonymous
Anonymous
2 years ago

Amen