Shetani hapo nyuma alikuwa na mamlaka na hii dunia hata kufikia hatua ya kuweza kujiamulia kufanya jambo lolote na kufanikiwa, kiasi cha kuweza hata kuzuia majibu ya maombi ya watu yasiwafikie kwa wakati haijalishi mtu huyo atakuwa ni mcha Mungu kiasi gani, bado atayazuia tu, Tunaona mambo hayo yalitokea kwa Danieli, pale alipokuwa amefunga majuma matatu akiutafuta uso wa Mungu, Na kama tunavyosoma, biblia inasema mkuu wa ufalme wa Uajemi (Pepo la uajemi ), alimzuia malaika wa Bwana kwa muda wa wiki tatu ili tu asifikishe majibu ya maombi ya Danieli, Unaona hapo vita vya kiroho vilikuwa ni vikali sana wakati ule mpaka Danieli kufikia kusema, NI VITA VIKUBWA (Danieli 10:1) haikiwa ni kazi ndogo, aliiona taabu yake.
Zaidi ya hayo Shetani alikuwa na uwezo hata wa kuwaendea watakatifu wa Mungu waliokuwa wamelala, huko sehemu za wafu na kuzungumza nao, alifahamu mahali walipo na kwenda huko,kwani funguo za mauti na kuzimu zilikuwa bado mikononi mwake.
Hivyo Shetani aliendelea, kulitawala hili anga la kiroho kwa muda mrefu sana, vitu vyote vilikuwa mikononi mwake, na ndio maana alimwambia Bwana Yesu kule nyikani “Nitakupa wewe enzi hii yote, na fahari yake, kwa kuwa imo mikononi mwangu, nami humpa ye yote kama nipendavyo”.
Unaona? Wayahudi waliliona hilo tangu zamani, hivyo walikaa katika matumaini wakingojea siku ambazo ile Nuru kuu, nyota ya Alfajiri itakapozuka Israeli na kuangaza tena katikati yao na katika ulimwengu mzima, Walikuwa wanalisubiria hilo kwa hamu, siku ambazo Mungu atawarejeshea tena lile tumaini lao lililokuwa limepotea tangu Edeni..
Maneno haya yaliwatia faraja walipoyasoma:
Isaya 49: 6 “naam, asema hivi, Ni neno dogo sana wewe kuwa mtumishi wangu [Azungumza habari za YESU] ili kuziinua kabila za Yakobo, na kuwarejeza watu wa Israeli waliohifadhiwa; zaidi ya hayo nitakutoa uwe NURU YA MATAIFA, UPATE KUWA WOKOVU WANGU HATA MIISHO YA DUNIA”.
Isaya 9:2 “Watu wale waliokwenda katika giza WAMEONA NURU KUU; Wale waliokaa katika nchi ya uvuli wa mauti, Nuru imewaangaza.”
Nuru hiyo kuu, waliitazamia wakimwomba Mungu kila siku bila kukoma.
Na ndio hapo tunakuja kuona miaka 2000 iliyopita Nuru hiyo inakuja kutokea duniani, Nuru ambayo hata wanajimu waliuona utukufu wake kwa jinsi ilivyokuwa inang’aa sana gizani, Siku ambazo alizaliwa mwokozi duniani, ni wakati ambao shetani alipatwa na wakati mgumu sana, kuliko nyakati nyingine zote ambazo alishawahi kuwa nazo. Na tunaona siku ile Bwana alipokufa na kufufuka ndipo hali yake ilipozidi kuwa mbaya zaidi, akiona kuwa ameshanyang’anywa mamlaka yote na nguvu zote, na funguo zote za mauti na kuzimu alizokuwa nazo juu ya huu ulimwengu hapo kabla.
Tunayathibitisha hayo kwa maneno yaliyotoka katika kinywa cha Kristo mwenyewe akisema:
Mathayo 28: 18 “Yesu akaja kwao, akasema nao, akawaambia, Nimepewa mamlaka yote mbinguni na duniani.”
Unaona hapo? Kauli hiyo inaonyesha kuwa kumbe hapo kabla mamlaka hayakuwa kwake, bali yalikuwa mikononi mwa mtu mwingine, na huyu si mwingine zaidi ya shetani. Sasa kuanzia huu wakati, na kuendelea vitu vyote, mamlaka yote na chochote kile unachokifahamu kilianza kumilikiwa na YESU KRISTO, Bwana wetu.Haleluya!!…Vita alishavipigana na kushinda, kama kutupwa chini basi shetani alishatupwa chini tangu siku ile pale Kalvari, hana lake tena duniani.
Na kama ni hivyo basi, hapa juu yetu mkuu wa anga anapaswa awe YESU Kristo na si pepo tena, shetani hapaswi kuamua chochote juu ya miili yetu, hapaswi kuzuia maombi yetu, hapaswi kutuamulia mbaraka wetu kutoka kwa Mungu, yeye hana uwezo wa kututajirisha wala kutufukarisha, kwa ufupi hapaswi kuonekana katika dira ya maisha yetu popote pale, kwani alishashindwa vita na anayemiliki sasa ni mwingine, hivyo yeye hastahili kuwepo duniani, atafute sehemu yake nyingine ya kumiliki, lakini si katika dunia hii,
Lakini swali linakuja kama ni hivyo basi, ni kwanini, shetani bado anaendelea kuwatesa watu?, ni kwanini bado kuna vita, ni kwanini bado tunamwona shetani akizurura zurura katikati ya maisha yetu, ni kwanini bado anatuletea matatizo kana kwamba hakuna chochote kilichofanyika pale Kalvari, Na bado Biblia bado inatuambia maneno haya:
Waefeso 6:11-18 “Vaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kuzipinga hila za Shetani.
12Kwa maana kushindana kwetusisi si juu ya damu na nyama; bali ni juu ya falme na mamlaka, juu ya wakuu wa giza hili, juu ya majeshi ya pepo wabaya katika ulimwengu wa roho.
13 Kwa sababu hiyo twaeni silaha zote za Mungu, mpate kuweza kushindana siku ya uovu, na mkiisha kuyatimiza yote, kusimama.
14 Basi simameni, hali mmejifunga kweli viunoni, na kuvaa dirii ya haki kifuani,
15 na kufungiwa miguu utayari tupatao kwa Injili ya amani;
16 zaidi ya yote mkiitwaa ngao ya imani, ambayo kwa hiyo mtaweza kuizima mishale yote yenye
moto ya yule mwovu.
17 Tena ipokeeni chapeo ya wokovu, na upanga wa Roho ambao ni neno la Mungu;
18 kwa sala zote na maombi mkisali kila wakati katika Roho, mkikesha kwa jambo hilo na kudumu katika kuwaombea watakatifu wote;
Ni kwanini haya yote?. Sasa Kama utakuwa ni mfuatiliaji mzuri wa habari zinazaoendelea duniani, utakuwa umeshawahi kusikia mara nyingi juu vita vinavyoendelea katikati ya mataifa Fulani, mfano jeshi la nchi la husika pamoja na vikosi vya umoja wa mataifa utasikia vimefanikiwa kudhibiti maficho yote, na maeneo yote yaliyokuwa yanamilikiwa na waasi na hivyo waasi wametawanywa na kukimbilia katika mataifa jirani, hivyo nchi sasa ipo katika amani. Lakini utaona taifa litadumu katika amani kwa kipindi kifupi tu, halafu ghafla utasikia mapambano yamezuka tena, waasi wamevamia kambi za wanajeshi na kuwaua, au sehemu nyingine utasikia waasi wamekivamia kijiji Fulani na kukichoma moto.
Na hali hiyo hiyo utaona itaendelea kwa muda mrefu sana, japo hiyo nchi ni kweli imefanikiwa kuwatokomeza waasi wote, lakini ile roho ya uasi bado ipo ndani ya nchi, na ndio hapo utaona leo kumetulia kesho mapambano, hivyo hivyo itaendelea kwa miaka na miaka . Na ndio hapo utaona majeshi yanalazimika kuweka makao ya kudumu katika nchi husika, muda wote yanakuwa macho, yanakesha kulinda usalama wa raia,na mali zao yanazunguka huku na huko, kuangalia kama upo usalama katikati ya vijiji vyake, na kuvuruga vikundi vyote wanavyovihisi vitakuwa vinahusika na shughuli za uasi.
Kwasababu wanajua mfano wakizembea tu, au wakipunguza nguvu kidogo, wanafahamu kabisa wale waasi bado wana hasira na serikali, japo wameshindwa lakini chini kwa chini bado wanaunda mbinu za kuupindua ufalme. Hivyo vile vikosi vya kulinda amani haviwezi kustarehe japo kweli vinaimiliki nchi yote.
Na ndivyo ilivyo kwetu sisi wakristo vita bado vinaendelea. Ni kweli ushindi tuliupata pale Kalvari, Tulifanikiwa kumnyang’anya shetani mamlaka yote kwa Damu ya Yesu Kristo iliyomwagika pale msalabani, shetani hana uwezo tena wa kuzuia maombi yetu, wala kufanya kitu chochote juu ya miili yetu au katika maisha yetu. Lakini kama na sisi hatutakuwa macho, kuilinda enzi yetu tukilala, tuwe na uhakika kuwa kama vile Bwana Yesu alivyosema katika
1Petro 5:8 “mshitaki wenu Ibilisi, kama simba angurumaye, huzunguka-zunguka, akitafuta mtu ammeze”. Basi tujue kuwa yale mambo aliyokuwa anaweza kuyafanya zamani bado ataendelea kuyafanya hata sasa hivi kama hatusimama.
Tusijifariji na kusema sisi ni wakristo maombi yetu hayawezi kuzuiwa kwasababu sisi tupo katika agano lililo bora zaidi ya lile agano la kale, na huku hatuzingatii kusimama kama wanajeshi wa Kristo, hatujajifunga kweli viunoni mwetu, Neno la Mungu hatulijui,halipo ndani yetu, chepeo ya wokovu ipo mbali nasi, habari za wokovu hatutaki kusikia, hatuna Roho ndani yetu, ambaye kwa huyo anatupa uhakika kuwa sisi ni watoto wa Mungu, na kutuongoza katika kweli yote. Dirii ya haki hatujaivaa yaani, mambo maovu ya rushwa, ulaguzi, biashara haramu vimekuwa ni sehemu ya maisha yetu na bado tunajiita wakristo. Hatuna muda wa kusali wala kudumu katika maombi kama biblia inavyotuagiza kila wakati tunawaza mambo ya ulimwengu huu, , unategemea vipi tutayakwepa majaribu ya Yule mwovu?.
Bwana mwenyewe alituambia tukeshe tuombe tusije tukaingia majaribuni, sasa kama sisi hatuna desturi hizo, unategemea vipi tutamkwepa Yule mwovu maishani mwetu? Yeye Bwana Yesu mwenyewe alifunga na kusali, sisi inatupasaje? Na ndio maana wakati mwingine tunaomba tunaona kama hatujibiwa, au majibu yanachukua muda kufika ni kwasababu Yule mkuu ya anga (Pepo) ambaye alishashindwa tangu siku nyingi, sisi tunamrudisha katika nafasi yake ya kale kwa mienendo yetu, na ndio maana matokeo yanakuwa ni hafifu au wakati mwingine kuchukua muda mrefu kujibiwa.
Vita bado vinaendelea. Kazi yako wewe ni kuilinda enzi uliyopewa na YESU, kila wakati kuhakikisha je! Zile silaha zote zinazozungumziwa katika Waefeso 6, umezivaa?. Kama umezivaa basi shetani atabakia kuwa mbali na wewe, na dunia yako itakuwa chini ya milki ya Bwana Yesu na vyote utakavyomwomba utapata, kwasababu shetani hatapata mlango wa kuzua mambo yake kwenye njia zako.
Mpaka siku itakapofika ambayo sasa, UASI wote utaondolewa duniani, Yaani siku ambayo shetani, pamoja na mapepo yake, pamoja na watu wake waovu watakapoondolewa duniani sasa siku hiyo ndiyo, hakutakuwa na haja ya kulinda enzi yoyote ile na siku hiyo haipo mbali ndugu, mwisho wa kila kitu umekaribia. Hakutakuwa na kukesha huko, hakutakuwa kusoma biblia, hakutakuwa na majaribu,ni wakati wa mambo mapya, ni wakati ambao mema yote Mungu aliyokuwa ameyakusudia watu wake kabla hata ya kuwekwa msingi ya ulimwengu ndipo yatakapofunuliwa, mambo ambayo jicho halijawahi kuona wala sikio kusikia. Tusitamani kukosa.
Lakini kwasasa hatuna budi kuyathibishwa mamlaka tuliyopewa, kwa kuzingatia kukesha, kuzivaa SILAHA ZOTE tulizopewa ili tuweze kuyafurahia matunda yote ya Bwana wetu Yesu aliyotushindia siku ile pale Kalvari.
Kama hujampa Bwana maisha yako, huu ndio wakati usingoje kesho, Mwamini kwamba yeye ni Mwana wa Mungu, na alikuja kwa ajili ya kukuosha dhambi zako, na kukupa uzima wa milele. Na kisha utubu dhambi zako zote naye ni mwaminifu atakusamehe na kukupa uzima wa milele.
Bwana akubariki sana.
Tafadhali “share” ujumbe huu kwa wengine, Na Bwana atakubariki.
Pia unaweza ukapata mafundisho haya Kwa njia ya Whatsapp yako, jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP
Mada Zinazoendana:
TUKAZE MWENDO ILI TUUFIKILIE UTIMILIFU
VITA VYA KIFIKRA BAADA YA KUZALIWA MARA YA PILI
About the author