MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

MPENDE JIRANI YAKO KAMA NAFSI YAKO.

Luka 10: 25 “Na tazama, mwana-sheria mmoja alisimama amjaribu; akisema, Mwalimu, nifanye nini ili niurithi uzima wa milele?

26 Akamwambia, Imeandikwa nini katika torati? Wasomaje?

27 Akajibu akasema, Mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako.

28 Akamwambia, Umejibu vema; fanya hivi nawe utaishi. 

29 Naye akitaka kujidai haki, alimwuliza Yesu, Na jirani yangu ni nani?

30 Yesu akajibu akasema, Mtu mmoja alishuka toka Yerusalemu kwenda Yeriko, akaangukia kati ya wanyang’anyi; wakamvua nguo, wakamtia jeraha, wakaenda zao, wakimwacha karibu ya kufa.

31 Kwa nasibu kuhani mmoja alishuka kwa njia ile; na alipomwona alipita kando.

32 Na Mlawi vivyo hivyo, alipofika pale akamwona, akapita kando.

33 Lakini, Msamaria mmoja katika kusafiri kwake alifika hapo alipo; na alipomwona alimhurumia,

34 akakaribia, akamfunga jeraha zake, akizitia mafuta na divai; akampandisha juu ya mnyama wake, akampeleka mpaka nyumba ya wageni, akamtunza.

35 Hata siku ya pili akatoa dinari mbili, akampa mwenye nyumba ya wageni, akisema, Mtunze huyu, na cho chote utakachogharimiwa zaidi, mimi nitakaporudi nitakulipa.

36 Waonaje wewe, katika hao watatu, ni yupi aliyekuwa jirani yake yule aliyeangukia kati ya wanyang’anyi?

37 Akasema, Ni huyo aliyemwonea huruma. Yesu akamwambia, Enenda zako, nawe ukafanye vivyo hivyo”.

Kuna kitu kidogo cha kujifunza katika hichi kisa…Mwanasheria mmoja alisimama kumwuliza swali la kumjaribu Bwana Yesu…kumwangalia atajibuje! Lakini Bwana alimjibu kwa kumrudisha kwenye Torati na kumwuliza imeandikwaje! Akamjibu “mpende Bwana Mungu wako kwa moyo wako wote, na kwa roho yako yote, na kwa nguvu zako zote, na kwa akili zako zote; na jirani yako kama nafsi yako”.

Bwana akampongeza akamwambia afanye hivyo naye utaupata huo uzima wa milele. Lakini Yule mwanasheria hakuishia hapo…akataka kuendelea kumpima ufahamu Bwana Yesu kwa kumwuliza jirani yake ni nani??.

Sasa kumbuka huyu mtu hakuwa na lengo la kutaka kujifunza bali kwa lugha ya sasa hivi tunaweza kusema ni mtu aliyekuwa anajifanya mjuaji…Kwasababu alikuwa anajua kabisa vigezo vya kuupata uzima wa milele ni kumpenda Mungu kwa moyo wote na akili zote na pia kumpenda jirani kama nafsi yake, lakini bado alikuwa anamwuliza Bwana kwa kumjaribu…Na hapa anamwuliza tena Bwana jirani yangu ni nani…Na wakati Bwana ameshamjibu kuwa anapaswa ampende jirani yake kama nafsi yake..Kwahiyo alikuwa anajua kabisa jirani yake ni nani lakini alitaka kumwonyesha Bwana yeye ni mjuaji zaidi….

Na hicho kiburi alikipata kutokana na kusoma kwingi, alifahamu mambo mengi ya torati na dini yake kwasababu hapo juu biblia inasema alikuwa ni mwanasheria…Sasa hakuwa mwanasheria kama hawa wanasheria tunaowajua sasahivi wanaotumia katika ya nchi kuhukumu…Hapana bali yeye alikuwa ni mwanasheria aliyesoma sheria zote za Mungu kupitia Torati za Musa…Kwahiyo alikuwa anajua kufumbua maswali yote yanayohusiana na torati…kukitokea jambo Fulani anaweza kukupatia ufumbuzi kamili kwa kurejea kwenye Torati…atakwambia Aya Fulani ya torati, kipengele Fulani kinasema hivi na hivi…Kwahiyo ni watu ambao ulikuwa huwezi kuwadanganya kitu chochote kinachotoka kwenye Torati, walikuwa wanaijua yote.

Ndio maana alikuja kwa ujasiri kumjaribu Bwana akiwa tayari na majibu sahihi ya maswali yake kichwani.

Wakati yeye anadhani anajua kumbe mbele za Mungu alikuwa anaonekana hajui chochote.

Sasa katika mfano huo hapo juu Bwana Yesu alioutoa, alikuwa anataka kumwonyesha Yule mwanasheria kuwa “dhana ya kufikiri kuwa wayahudi ndio majirani zao pekee ni uongo”..Kama Torati ilivyowafundisha kuwa… “jirani yako ni Mwisraeli mwenzako”..Mtu mwingine tofauti na mwisraeli (Myahudi) sio jirani yako. Hivyo mtu unayepaswa kumpenda kama nafsi yako ni mwisraeli mwenzako tu!…Ndivyo huyu mwanasheria alivyokuwa anajua kichwani mwake na ndivyo torati ilivyokuwa inasema. Lakini ashukuriwe Mungu Bwana Yesu ndiye ukamilifu wa Torati Haleluya!!. Ndio maana Biblia inatuonya tutoke katika kamba za madhehebu kwasababu zinatufungia mlango wa kumjua Mungu…kamba za madhehebu zinatufanya tusimwelewe Mungu wala tusimsikie Mungu kwa kisingizio tu! Dini yetu inasema hivi, dhehebu letu linasema hivi. Zinatufanya tujione tunajua kila kitu kumbe hatujui chochote kama huyu mwanasheria hapa!.

Sasa tukirudi kwenye Torati ya Musa, Baada ya Mungu kuwatoa wana wa Israeli Misri na kuwaingiza nchi ya Kaanani aliwaambia…wapendane wao kwa wao, yaani wayahudi kwa wayahudi kama nafsi zao, pia walionywa wasichangamane na watu wa mataifa, hata wasioe watu wa mataifa. Na waliambiwa pia wasitozane riba wao kwa wao, wanaweza kuwatoza riba watu wa mataifa lakini sio wao kwa wao. Hivyo ilikuwa inaaminika na kufahamika kuwa sheria hiyo Musa aliyoitoa ya kumpenda jirani yako kama nafsi yako, inawahusu tu wayahudi kwa wayahudi, kwamba wao tu watapendana kama nafsi zao, kwamba mtu mwingine tofauti na Taifa lao ni ruksa kutokumjali..ni ruksa kutojishughulisha naye. Lakini mwisraeli mwenzako ndio unapaswa umpende kama nafsi yako. Ukisoma kitabu cha Mambo ya Walawi utaweza kuelewa jambo hilo vizuri kwa undani, lakini moja ya mstari unaozungumzia upendo kwa wayahudi tu ni huu..

Walawi 19:18 “Usifanye kisasi, WALA KUWA NA KINYONGO JUU YA WANA WA WATU WAKO; bali umpende jirani yako kama nafsi yako; Mimi ndimi Bwana”.

Umeona?..Biblia inasema hapo “juu ya watu wako”..ikiwa na maana watu wengine (yaani watu wa mataifa) ni ruksa kuwawekea kinyongo endapo wamefanya jambo la kukwaza.

Kwahiyo ndivyo ilivyokuwa inaeleweka miaka na miaka…Na huyu mwanasheria ndivyo alivyokuwa anajua…Lakini tunaona Bwana alimwambia kitu kipya..kuhusu JIRANI YAKE KUWA NI NANI?…Alitegemea aambiwe kuwa jirani yake ni myahudi mwenzake, (aidha mlawi au kuhani au mwisraeli wa kawaida tu)..lakini Bwana alimwonyesha Msamaria ndiye ndugu yake.

Sasa WASAMARIA wakati huo hawakuwa watu wa Taifa la Israeli, walikuwa ni watu wa mchanganyiko na watu wa mataifa…Kwahiyo hawakuwa uzao wa Ibrahimu hata kidogo..Lakini Bwana alitoa mfano huo kuonyesha kuwa watu wa mataifa wanaweza kuwa majirani wa kweli kuliko hata hao waisraeli wanaojiona wamestahili kupendana wao kwa wao tu!.

Katika mfano ule tunaona…Alikuja kwanza kuhani ambaye alikuwa myahudi lakini alipita kando hakutaka kumsaidia myahudi mwenzake mtu wa Taifa moja na yeye…Baadaye kidogo alipita Mlawi ambaye alikuwa myahudi pia lakini hakutaka kumsaidia myahudi mwenzake aliyekuwa amepatwa na matatizo…Lakini alipopita Msamaria ambaye hakuwa hata myahudi wala hamjui Mungu wa Israeli, alimsaidia kwa msaada mkubwa Myahudi ambaye alikuwa hata hamjui..Na hivyo huyo Bwana ndiye akasema ni JIRANI mwema anayepaswa kupendwa kama nafsi yake.

Bila shaka baada ya mfano huo, Yule mwanasheria aliondoka kwa hasira kwasababu ni kama aliambiwa amri mpya awapende pia watu wa mataifa aliokuwa anaishi nao, (makafiri) kama nafsi yake.

Na sisi kuna jambo tunaweza kujifunza hapo….Udini na Udhehebu ni mbaya sana, unaweza kutufanya tudhani tunampendeza Mungu kumbe hatumpendezi hata kidogo…Ni mara ngapi umeona watu wanaojiita wakristo wakiwachukia watu wasio wa Imani yao?…Utaona wanatoa mpaka maneno ya laana kwasababu tu sio wakristo kama wao…Wakati hao wanaowashutumu ndio Mungu anawaona ni MAJIRANI ZAO WAZURI kuliko hata wakristo wenzao..

Kama umefanya utafiti, utagundua kuwa fursa nyingi au msaada mwingi, Mungu anawatumia watu wasio wa Kristo au watu wa kiulimwengu kutusaidia kuliko watu wa ki-Mungu, Utaona watu ambao ni wakidunia wakati mwingine ni wakarimu na wanaojali kuliko hata watu wanaomjua Mungu. Hao Bwana anatuambia tuwapende kama nafsi zetu..hao ndio wasamaria wema..ndio majirani zetu, sio wakuwachukia na kuwasema bali kuwapenda kama nafsi zetu….

Sio kwasababu hamjui Mungu wako basi ndio awe sababu ya kuwa adui yako na kusema watu wa imani yangu tu ndio marafiki zangu, wakati mwingine Bwana anawatumia hao watu wasiomjua Mungu wako kukuletea wewe msaada kama ilivyokuwa kwa huyu myahudi aliyeangukia katikati ya wanyanganyi badala asaidiwe na watu wa dini yake na imani yake anakwenda kusaidiwa na watu hata wasioijua Torati..

Biblia imetuonya tu tusichangamane kufuata njia zao zisizofaa, kama ni walevi hatuenendi katika njia zao, kama ni waasherati vivyo hivyo, kama ni wacheza dansi, kama ni waabudu sanamu tusishirikiane nao hata kidogo…lakini sio tusiwapende na kuwachukia, wakitaka kukopa kwako usiwape kisogo, wakikuaribisha kwao usikatae, wakikupa zawadi pokea, wakiumwa uwatembelee… ili kwa matendo yetu mazuri na upendo wetu tuwavute waje upande wetu, na tuonekane tumeweza kuyafanya mapenzi ya Baba yetu aliye mbinguni.

Hivyo jawabu la mambo yote ni upendo, kwetu sisi kwa sisi na kwa wale walio nje.

Bwana atusaidie sote .jiunge na channel yetu Kwa kubofya hapa >> WHATSAPP

UPENDO

UMETEKWA NA UPENDO WA KRISTO?

BIBLIA ITUAMBIA TUSALIMIANE KWA BUSU TAKATIFU. HILI BUSU NDIO LIPI?

HAWA ALIPOLAANIWA ALIAMBIWA “TAMAA YAKO ITAKUWA KWA MUMEO”.NI TAMAA IPI INAYOZUNGUMZIWA HAPO?


Rudi Nyumbani

 

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments