Shalom,
Nakukaribisha tutafakari pamoja vifungu vifuatavyo vya maandiko, naamini lipo jambo utajifunza mwishoni mwa somo..
Matendo 16:6 “Wakapita katika nchi ya Frigia na Galatia, wakikatazwa na Roho Mtakatifu, wasilihubiri lile neno katika Asia.
7 Walipofika kukabili Misia wakajaribu kuenda Bithinia, lakini Roho wa Yesu hakuwapa ruhusa,
8 wakapita Misia wakatelemkia Troa.
9 Paulo akatokewa na maono usiku; alimwona mtu wa Makedonia amesimama, akimsihi, na kumwambia, Vuka, uje Makedonia utusaidie”.
Wengi wetu tunafahamu vipingamizi pekee mtume Paulo alivyokuwa anapitia vya kuhubiri injili vilitoka kwa shetani, lakini hatujui kuwa kuna wakati mwingine Mungu mwenyewe alikuwa anamzuia Paulo asihubiri injili japokuwa alitamani kufanya hivyo,.
Mungu anafanya hivyo sio kwamba hataki watu wahubiriwe injili kama ilivyo kwa shetani, hapana, bali ni kawaida yake kuwapa vipaumbele vya kwanza wale ambao wanaonyesha kiu ya kutaka kumjua yeye.
Ili kutimiza haya maandiko.
Mathayo 5:6 “Heri wenye njaa na kiu ya haki; Maana hao watashibishwa”.
Na haya..
Mathayo 5:3 “Heri walio maskini wa roho; Maana ufalme wa mbinguni ni wao”.
Kama ukichunguza hiyo mistari utaona, Mungu hakumkataza Paulo kufika kabisa katika hiyo miji iliyotajwa hapo juu, lakini aliifikia na kuipita, kuonyesha kuwa kama kungekuwa na utayari wa wenyeji wa pale kutamani kumjua Mungu basi wangeanzwa kwanza wao, kisha ndio wafuate wale wengine..
Jaribu kufikiria anafika pale Frigia, anataka tu kuanza kuhubiri Mungu anamzuia, anaondoka anaenda mji unaofuata Galatia huko nako Mungu anamzuia anaondoka tena anafikiria labda ashuke kwenye miji mingine ya Asia (ambayo ndio kama Efeso, Smirna, Pergamo, Laodikia n.k. ) lakini huko nako Mungu anamwambia asihubiri chochote aondoke…
Haishii hapo anaondoka tena Asia anafika mji ulioitwa Misia ili aanze kuhubiri bado Mungu anamkataza, anafika Troa bado Mungu hampi kibali, wakati sasa akiwa hapo Troa ukingoni kabisa mwa mji ndipo Mungu anamwonyesha maono ambayo yalikuwa yanaonyesha jinsi watu wa kule Ng’ambo ya bahari Makedonia walivyokuwa wanahitaji msaada mkubwa sana wa kiroho..
Ndipo hapo utaona inamgharimu Paulo kuvuka bahari sasa asafiri, mpaka kwenye hiyo miji ya Makedonia ambayo, ilikuwa ni Filipi, Thesalonike, na Beroya.. Ili kuihubiri injili.. Si jambo rahisi
Ili kuelewa vizuri jaribu kutengeneza picha labda mtumishi wa Mungu anatoka nchi ya mbali Afrika Magharibi labda tuseme Ghana, anafika nchi za Afrika ya kati kama vile Congo n.k., Mungu anamwambia pita usihubiri, anafika mpaka nchi zetu za Afrika mashariki, Anaanzia Uganda anaambiwa pita, anafika Kenya anaambiwa pita, anafika hapa Tanzania, bado Mungu anamwambia usihubiri hapo, sasa akiwa ameshavuka kote toka kigoma, akiwa pale Daresalaam, Mungu anamwambia panda Meli nenda taifa la India wapo watu wangu kule wanahitaji msaada wa kunijua mimi..
Ndivyo ilivyokuwa kwa Mtume Paulo na wenzake, walienda Makedonia na kweli kule walikutana na watu ambao kwanza walikuwa ni maskini, lakini walikuwa tayari kumtolea Mungu kwa moyo wao wote..na zaidi ya yote walikuwa tayari kulipokea Neno la Mungu, mfano watu wa Beroya ndio wale ambao walikuwa wapo tayari kuchunguza maandiko ya kujua ufasaha wa yote,
2Wakorintho 8:1 “Tena ndugu zetu, twawaarifu habari ya neema ya Mungu, waliyopewa makanisa ya Makedonia;
2 maana walipokuwa wakijaribiwa kwa dhiki nyingi, wingi wa furaha yao na UMASKINI WAO uliokuwa mwingi uliwaongezea utajiri wa ukarimu wao.
3 Maana nawashuhudia kwamba, kwa uwezo wao, na zaidi ya uwezo wao, kwa hiari yao wenyewe walitoa vitu vyao;
Hivyo mimi na wewe tunajifunza nini?
Mungu ni yeye ule jana na leo na hata milele, kama mengi ya makanisa ya Asia hayakustahili kupewa neema ya wokovu kwanza, atafanya na kwetu vivyo hivyo kama hatutakuwa tayari kuipokea.
Tupaswa tujiulize je! mioyo yetu ni kweli ina kiu ya kumjua Mungu, kiasi kwamba mpaka rohoni Mungu anatufananisha na watu wa Makedonia?.. Vuka, uje Makedonia utusaidie?. Je! ni kweli tunaonyesha tunahitaji msaada kutoka kwa Mungu? Je tunastahili msaada?.. Kama ni kweli tunaonyesha tunahitaji msaada, basi hapo ndipo Mungu atakapofungua njia ya kutusaidia, kwa namna ya ajabu.
Na tunaonyesha tunahitaji msaada kwa namna gani?.. Tunaonyesha kwa bidii yetu sisi ya kutafuta yeye kwa nguvu zetu zote, kwa akili zetu zote, kwa mioyo yetu yote na kwa Roho zetu zote.
Bwana akubariki.
Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia masomo haya kwa njia ya email yako au Whatsapp tutumie ujumbe kwenye box la maoni chini au piga namba hii +255 789001312
Mada Nyinginezo:
About the author