Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi?

SWALI: Je tunapaswa tushiriki Meza ya Bwana mara ngapi kwa Mwezi, au kwa Mwaka?


Jina la Bwana wetu Yesu Kristo libarikiwe. Ni neema ya Mungu tumeiona siku mpya ya leo, hivyo nakukaribisha tujifunze Biblia pamoja.

Kutokana na mkanganyiko mkubwa wa kila mmoja kusema ratiba yake, na kuiona kuwa ndio ipo sahihi, imesababisha kuzalika kwa madhehebu mengi, na hivyo kuzidi kuufanya ukristo uwe mgumu kueleweka zaidi kwa wale walio nje. Lakini maandiko yanasema..

2Timotheo 2;19  “Lakini msingi wa Mungu ulio imara umesimama, wenye muhuri hii, Bwana awajua walio wake…”.

Hivyo haijalishi kuna mkorogo mkubwa kiasi gani duniani, lakini walio wa Mungu, hawatapotea kamwe.

Tukirudi katika Maandiko tunasoma mstari ufuatao…

Luka 22:19  “Akatwaa mkate, akashukuru, akaumega, akawapa, akisema, [Huu ndio mwili wangu unaotolewa kwa ajili yenu; fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.

Hapo biblia imesema “fanyeni hivi kwa ukumbusho wangu”.. Maana yake wafanye mara kwa mara ndio maana kaongezea neno “kwa ukumbusho wangu”, mbele yake. Sasa katika hali ya kawaida hata nikikupa picha yangu, nikakwambia ichukue hii kwa ukumbusho wangu..haimaanishi kwamba uichukue iangalie mara moja kisha ukaitupe.. la! Bali nimemaanisha uihifadhi, kila unaitazama unikumbuke..na hiyo inaweza kuwa kwa wiki mara moja, au kwa mwezi mara moja..lakini ni ngumu kuwa kwa mwaka mara moja..Kama ukiitazama picha yangu kwa miaka 3 mara moja, ni wazi kuwa mimi sipo moyoni mwako kwa kiwango kikubwa, ndio maana hata hamu ya kunikumbuka huna. Lakini kama nipo moyoni mwako kikweli kweli, ile picha haiwezi kupita siku mbili, au wiki hujaitazama.

Sasa katika kushiriki meza ya Bwana ni hivyo hivyo, Bwana hajaweka kwamba ni mara ngapi kwa wiki, au kwa mwezi au kwa mwaka tunapaswa tuishiriki. Lakini kwa mkristo kweli aliyezaliwa mara ya Pili, ambaye anajua umuhimu wa kuishiriki meza ya Bwana, hawezi kusubiria kulifanya hilo tendo mara moja kwa mwaka, au mara mbili au mara tatu?

Ni sawa na biblia ilivyosema katika Waebrania 10:25  “wala tusiache kukusanyika pamoja, kama ilivyo desturi ya wengine; bali tuonyane; na kuzidi kufanya hivyo, kwa kadiri mwonavyo siku ile kuwa inakaribia”.

Hapo biblia imesema “tusiache kukusanyika” lakini haijasema ni mara ngapi kwa wiki tukusanyike, au mara ngapi kwa mwezi au mwaka. Hivyo kwa mtu aliyezaliwa mara ya pili, na anayejua umuhimu hasa wa kukusanyika pamoja..haiwezi ikapita wiki bila kuhudhuria kwenye kusanyiko pamoja na wenzake. Kanisa la kwanza walijua umuhimu wa kukusanyika na hivyo wakaona kiwango cha chini cha kukusanyika pamoja angalau kiwe mara moja kwa wiki.Na sisi tunafuata utaratibu huo huo, angalau tukusanyike mara moja kwa wiki, ili kujinoa sisi kwa sisi. Lakini Bwana Yesu hakuwapa masharti wala ratiba ya siku za kukusanyika pamoja.

Kadhalika biblia inasema “ Ombeni bila kukoma (1Wathesalonike 5:17)”.  Haijatoa ratiba ya kwamba tuombe mara ngapi kwa wiki, au mwezi au mwaka.. Lakini kwa mtu aliyezaliwa kweli mara ya pili na ambaye Roho Mtakatifu anaugua ndani yake, hawezi kupitisha siku mbili hajaingia kabisa magotini…Lakini yule asiyejua umuhimu wa maombi katika maisha yake, anaweza kupitisha hata mwezi au miezi kadhaa bila kuomba kabisa.

Hivyo hata katika kushiriki meza ya Bwana, kama kweli umezaliwa mara ya pili, na unampenda Bwana, na umepata kujua umuhimu wa kushiriki meza ya Bwana, na jinsi gani tendo hilo lina madhara makubwa sana katika ulimwengu wa roho, huwezi kulifanya kwa mwaka mara moja au mara mbili.

Zipo dini ambazo ibada za kushiriki meza ya Bwana ni mara moja kwa mwaka. Na zinatumia andiko la kwamba Kristo alishiriki na wanafunzi wake mara moja tu, msimu ule wa pasaka. Hivyo na dini hizo zinasema kushiriki meza ya Bwana ni mara moja tu, na tena ni ile siku ya Pasaka.

Ndugu usidanganyike!, Meza ya Bwana tunaweza kushiriki mara kwa mara kwa kadiri tupatavyo nafasi ya kukutanika. Na sio tu meza ya Bwana ndio agizo la msingi.. Yapo na maagizo mengine yaliyo ya muhimu hivyo hivyo, kama KUTAWADHANA MIGUU. Ni lazima sisi kwa sisi tutawadhane miguu mara kwa mara tunapokusanyika pamoja, kama Bwana alivyotupa maagizo hayo. Na pia ni lazima tuwe waombaji wa mara kwa mara, angalau kila siku. Hayo yote ni kwa faida yetu wenyewe.

Bwana akubariki.

Tafadhali washirikishe na wengine habari hizi njema, na pia kama utapenda tuwe tunakutumia mafundisho ya Neno la Mungu ya mara kwa mara kwa njia ya email yako au Whatsapp basi tutumie ujumbe kwenye namba hii +255 789001312

Mada Nyinginezo:

MEZA YA BWANA, NA KUTAWADHANA MIGUU.

DAKIKA MOJA TU, INAKUFANYA UMWAMINI SHETANI?

Ni kwa nini tunasema tunamwabudu MUNGU aliye hai ,Je! wale wanaomwabudu shetani sio mungu wao aliye hai?

UPENDO WA KRISTO WATUBIDISHA;

Rudi Nyumbani:

Print this post

About the author

Admin administrator

Subscribe
Notify of
guest

0 Comments
Newest
Oldest Most Voted
Inline Feedbacks
View all comments